11-Madhara Ya An-Namiymah (Kufitinisha): Sababu za Kufitinisha, Sifa Za Mfitinishaji
Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) Na An-Namiymah (Kufitinisha)
11- An-Namiymah: Sababu za Kufitinisha, Sifa Za Mfitinishaji
Kufitinisha baina ya watu ni jambo ovu linalochukiza mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Ametuamrisha tuepukane nalo kama Anavyosema:
وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ
Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. [Al-Maaidah :2]
Vile vile Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلَا تَبْغِ الْفَسَادَ فِي الْأَرْضِ ۖ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ ﴿٧٧﴾
na wala usitake ufisadi ardhini. Hakika Allaah Hapendi mafisadi.” [Al-Qaswasw: 77]
Sababu zinazomfanya mtu afitinishe:
1. Ujinga wa kutokujua makatazo yake katika Qur-aan na hatari yake na adhabu zake kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
2. Nafsi kuwa na chuki na uhasidi kwa kuona ndugu wawili wanapendana na kushirikiana katika mambo yao. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameonya:
عن أبي هُريرةَ رضي اللهُ عنه قال: قال رسوُل الله صلى الله عليه وسلم : ((لا تَحَاسَدُوا، ولا تَنَاجَشُوا، ولا تَباغَضُوا، ولا تَدَابَرُوا، ولا يَبعْ بَعْضُكُمْ على بَيْعِ بَعْضٍ، وكُونُوا عِبادَ اللهِ إخْوَاناً، المُسْلمُ أَخُو المُسْلمِ: لا يَظْلِمُهُ، ولا يَكْذِبُهُ، ولا يَحْقِرُهُ، التَّقْوَى هاهُنا)) ويُشِيرُ إلى صَدْرِه ثَلاثَ مَرَّاتٍ – ((بِحَسْبِ امْرِىءٍ مِنَ الشَّرِّ أن يَحْقِرَ أخاهُ المُسْلِمِ، كُلُّ المُسْلِمِ على الْمسْلِم حَرَامٌ: دَمُهُ ومالُهُ وعِرْضُهُ)) رَوَاهُ مُسْلِمٌ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msioneane choyo, wala msizidishiane bei (za vitu), wala msichukiane, wala msipigane mapande (msitengane), wala msishindane kwa kupunguza bei. Lakini kuweni ndugu, enyi waja wa Allaah, Muislamu ni ndugu wa Muislamu mwenzake, hamdhulumu wala hamvunji, hamwambii uongo wala hamdharau. Taqwa ipo hapa (huku akiashiria kifuani kwa vidole vyake mara tatu) Ni uovu wa kutosha kwa mtu kumdharau ndugu yake Muislamu. Muislamu ameharamishiwa kwa Muislamu mwenzake: damu yake, mali yake na heshima yake [Imesimuliwa na Muslim]
Yaani: Haramu kuchukua mali ya mwenzako, kumuua na kumdhalilisha.
3. Kutaka kujikurubisha zaidi kwa mmoja kati ya watu wawili anaowafitinisha, huenda kwa sababu ya kuwa na wivu kuwa hapendwi kama anavyopendwa mwengine.
4. Kufuata maslahi yanayopatikana kwa mmoja wao ili afaidike naye baada ya kumfitinisha mwenzake.
Sifa za An-Nammaam (mwenye kufitinisha)
1. Ni mwenye kupenda kuapa sana kwani hakuna mwenye kupenda kuapa sana isipokuwa mtu asiye mkweli. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلَا تُطِعْ كُلَّ حَلَّافٍ مَّهِينٍ﴿١٠﴾
Na wala usimtii kila mwingi wa kuapa, dhalili.
هَمَّازٍ مَّشَّاءٍ بِنَمِيمٍ﴿١١﴾
Mwingi wa kukashifu, mpitaji huku na kule kwa kufitinisha. [Al-Qalam: 10-11]
2. Mwenye kupenda kusengenya na kuwatia aibu wenziwe aidha kwa kauli zake, au ishara wakiwa mbele yake au nyuma yake.
3. Mwenye moyo mchafu usiopendelea kheri kwa wenzake.
4. Huzidisha wema kwa wengine aonekane kuwa ni mwema, na kujifanya mwenye maneno matamu.
5. Mwenye kupenda kulaumu bure bure almuradi tu akutie katika aibu kuwa una makosa japo atafute sababu yoyote imridhishe tu kuwa yeye ni mkweli na mwenziwe ni mkosa.