12-Madhara Ya An-Namiymah (Kufitinisha): Vipi Kutibu An-Namiymah?

Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) Na An-Namiymah (Kufitinisha)

 

12- An-Namiymah: Vipi Kutibu An-Namiymah?

 

 

 

Mafunzo yafuatayo yataweza In Shaa Allaah kutibu An-Namiymah ikiwa yatatekelezwa na inampasa kila mwenye tabia hii haraka ajifunze ili kujiepusha na maouvu haya yanayosababisha ufisadi na chuki baina ya ndugu Waislamu. Tutambue kuwa hii ni moja wapo ya jihadi ya nafsi kwa kujiepusha na maovu yanayoamrishwa na nafsi, ambayo ni jihadi  bora kabisa na itamuweka Muislamu katika radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Amesema Rasuli wa Allaah  (Swalla-Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kupitia usimulizi wa Fadhwaalah bin ‘Ubaydullaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

((أَلَا أُخْبِرُكُمْ بِالْمُؤْمِنِ؟ مَنْ أَمِنَهُ النَّاسُ عَلَى أَمْوَالِهِمْ وَأَنْفُسِهِمْ ، وَالْمُسْلِمُ مَنْ سَلِمَ النَّاسُ مِنْ لِسَانِهِ وَيَدِهِ ، وَالْمُجَاهِدُ مَنْ جَاهَدَ نَفْسَهُ فِي طَاعَةِ اللهِ ، وَالْمُهَاجِرُ مَنْ هَجَرَ الْخَطَايَا وَالذَّنُوبَ))  أحمد والحاكم قال الألباني  "إسناد صحيح" سلسلة الأحاديث الصحيحة

((Je, nikujulisheni kuhusu Muumini? Anayeaminiwa na watu juu ya mali zao na nafsi zao. Na Muislmu anayeweka amani kwa watu kwa ulimi wake na mkono wake. Na mfanyaji jihadi ni yule anayefanya jihadi ya nafsi yake katika kumtii Allaah, na mhamaji (hijrah) ni anayehama makosa na madhambi)) [Ahmad,   Al Haakim  na amesema Al-Albaaniy katika Silisilatul-Ahaadiyth Asw-Swahiyhah:  “Hii isnaad Swahiyh”]

 

 

Mwenye kufitinishwa

 

1-  Inapasa mwenye kuletewa fitna kutahadhari na mfitinishaji kwani mfitinishaji ni fasiki na fasiki anahitaji kukhofiwa. Inampasa asipokee khabari za mfitinishaji hadi upatikane ushahidi kama asemayo ni kweli. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا أَن تُصِيبُوا قَوْمًا بِجَهَالَةٍ فَتُصْبِحُوا عَلَىٰ مَا فَعَلْتُمْ نَادِمِينَ﴿٦﴾

Enyi walioamini! Anapokujieni fasiki kwa habari yoyote, basi pelelezeni, msije mkawasibu watu kwa ujahili, mkawa kuwa wenye kujuta juu ya ambayo mmeyafanya. [Al-Hujuraat: 6]

 

 

 

2- Kutokuamini asemayo mfitinishaji na uwe na dhana nzuri na nduguyo unayepatana naye, badala ya kumwekea dhana mbaya kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ

Enyi walioamini!  Jieupusheni sana na dhana kwani hakika baadhi ya dhana ni

 

3- Usipendelee kuwa na urafiki na mfitinishaji na anapokuja  kukufitinsha ni vizuri kumpa nasaha, kumkataza asiwe anafanya hivyo hata kama ni kweli kamsikia mwenzako anakusengenya. Kufanya hivi, utakuwa umemfunza yeye kuepukana na tabia hiyo kwani akitambua kuwa wewe sio mtu wa kukubali kupokea ufitinishaji hatorudia tena kwako mara nyingine. Vile vile itakuwa ni kheri kwako kutokusikia tena ufitinishaji na utaepukana na kuwachukia marafiki na ndugu zako ambao una maelewano nao. Kwa ujumla utazuia ufisadi wa aina hii kutendeka. Na lau kila mmoja atakuwa anafanya hivi basi bila shaka jamii nzima itaokoka na ufisadi huu wa kufitinisha.

 

Mwenye kufitinisha

 

1. Ajishughulishe na kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kila aina ya dhikru-Allaah.

 

2. Afikirie na akhofu adhabu za kufitinisha.

 

3. Afikirie ubaya ulioje kuwafitinisha watu na kutia chuki katika nyoyo za watu, je, yeye mwenyewe atapendwa kufitinishwa na kipenzi chake?

 

4. Asome mada zote za Ghiybah ziliomo Alhidaaya.com ili atambue hatari ya kutouhifadhi ulimi.

 

 

Hitimisho: 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aaala) Atuhifadhi na Atuepushe na maovu haya na mengineyo ili tubakie katika radhi Zake. Aamiyn.

 

 

 

Share