06-Madhara Ya Ghiybah: Sababu Zinazopeleka Katika Ghiybah
Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) Na An-Namiymah (Kufitinisha)
06- Sababu Zinazopeleka Katika Ghiybah
1-Kuambatana na marafiki waovu:
Moja ya sababu ya Ghiyba ni kuambatana na marafiki waovu wasiomkhofu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwani rafiki muovu humuathiri mwenziwe kwa yale anayoyatenda. Mfano mzuri ametupigia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
عن أبي موسى الأشعري رضي الله عنه أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((إِنَّمَا مَثلُ الجَلِيسِ الصَّالِحِ وَجَلِيسِ السُّوءِ كَحَامِلِ المِسْكِ وَنَافِخِ الْكِيرِ، فَحَامِلُ الْمِسْكِ إمَّا أنْ يُحْذِيَكَ وَإمَّا أنْ تَبْتَاعَ مِنْهُ وَإمَّا أنْ تَجِدَ مِنْهُ ريحًا طَيِّبَةً، وَنَافِخُ الكِيرِ إمَّا أنْ يُحْرِقَ ثِيَابَكَ وَإمَّا أنْ تَجِدَ مِنْهُ رِيحًا مُنْتِنَةً )) متفق عليه
Abuu Muwsaa Al-Ash'ariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesimulia: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mfano wa rafiki mwema unayeambatana naye rafiki mbaya ni kama mfano wa mbebaji miski na mfua chuma (anayevuvia kipulizo). Mbebaji miski ima atakupa au utanunua kutoka kwake au utapata harufu nzuri kwake. Na mfua chuma (anayepuliza kipulizo), ima atachoma nguo zako au utapata harufu mbaya kutoka kwake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
2-Mwenye kusengenya kutokuzingatia aibu zake:
Ghiybah ni maasi yanayoleta madhara makubwa baina ya ndugu wa Kiislamu kwa kukashifiana na kutangaziana aibu zao. Tutambue kuwa hakuna mwana Aadam aliyekamilika, na kila mtu atakuwa na aibu zake; kama si aibu yake mwenyewe, basi huenda ikawa kuna aibu katika familia yake, na kama si familia yake basi huenda akawa ni mtu wa karibu yake n.k. Na hata kama hakuna aibu yoyote kwake au kwa watu wake, basi akhofu kuwa huenda ikamfikia yeye aibu hiyo au ndugu zake au watoto wake au yeyote katika jamaa zake, kwa sababu huenda Allaah Akalipizia hapa hapa duniani kwa wenye kusengenya kwa kuwasibu nao yatakayopelekea watu kuwasengenya.
3-Simu ni chanzo kikuu:
Chanzo kikuu kinachofanikisha kutendeke Ghiybah na uzushi kuenea katika jamii kwa siku hizi ni simu, hasa kwa kuweko mawasiliano ya bure kama mitandao ya kijamii. Lau kama simu zingelikuwa ni za kulipiwa basi bila shaka wangelifilisika wenye kupenda kusengenya na kuzusha.
4-Kudhani kwamba kusikiliza umbeya, uzushi, hakuhusiani na ghiybah:
Mara nyingi utamsikia mtu anasema: "Lakini mimi nasikiliza tu sitii langu!” Mwenye kusema hivi atambue kuwa mwenye kusengenya na mwenye kusikia wote wako katika ushirikiano wa maasi haya ya ghiybah. Na kila kiungo cha mwana Aadam kitamchongea mwenye kufanya maasi siku ya Qiyaamah, hivyo masikio yatakuchongea unaposikiliza umbeya au usengenyaji kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ﴿٣٦﴾
Hakika masikio na macho na moyo; vyote hivyo vitakuwa vya kuulizwa (Siku ya Qiyaamah). [Al-Israa: 36]
5-Kujishughulisha na upuuzi badala ya kutumia muda kwa mambo yenye manufaa ya Dini:
Kuwa na faragha (muda na wasaa) ni neema ambayo inampasa Muislamu ashukuru, kwani kila dakika ni muhimu kuitumia ipasavyo kwa kujichumia mema na sio kuipoteza kwa mambo ya upuuzi ambayo yanayoweza kumuamgamiza mtu motoni kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
فَوَيْلٌ يَوْمَئِذٍ لِّلْمُكَذِّبِينَ ﴿١١﴾
Basi ole Siku hiyo kwa wakadhibishao.
الَّذِينَ هُمْ فِي خَوْضٍ يَلْعَبُونَ ﴿١٢﴾
Ambao wamo katika kushughulika na upuuzi wakicheza. [At-Twuwr: 11-12]
Amesema Imaam Ibn Kathiyr: "Ni wale ambao duniani wanacheza katika mambo ya batili." Na kusengenya ni maovu, dhambi na batili inayompasa Muislamu ajiepushe nayo.