07-Madhara Ya Ghiybah: Vipi Kujiokoa Na Kuokoa Jamii Kutokana na Ghiybah

Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) Na An-Namiymah (Kufitinisha)

 

07-Vipi Kujiokoa Na Kuokoa Jamii Kutokana na Ghiybah

 

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَإِذَا رَأَيْتَ الَّذِينَ يَخُوضُونَ فِي آيَاتِنَا فَأَعْرِضْ عَنْهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ ۚ وَإِمَّا يُنسِيَنَّكَ الشَّيْطَانُ فَلَا تَقْعُدْ بَعْدَ الذِّكْرَىٰ مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٦٨﴾

Na unapowaona wale wanaoshughulika kupiga porojo katika Aayaat Zetu; basi jitenge nao mpaka watumbukie kwenye mazungumzo mengineyo. Na kama shaytwaan akikusahaulisha, basi baada ya kukumbuka, usikae pamoja na watu madhalimu. [Al-An'aam: 68]

 

 

Hiyo ni moja ya njia ya kujiokoa na maovu haya ya Ghiybah, nayo ni kujiepusha na wanaopendelea kuzungumza yasiyo na maana na yanayomkosesha mtu radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Njia nyingine nyingi ni kama yafuatayo:

 

 

Njia Za Kujiokoa Na Kuwaokoa Wenzako Na Ghiybah:

 

1.  Kuwa na taqwa na umkhofu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na kusoma Aayah na Hadiyth zenye maonyo na adhabu za Ghiybah.

 

2. Kufikiria khasara utakayopata kuporomoka ‘amali zako njema zote na badala yake kujazwa madhambi   kama inavyosema Hadiyth ifuatayo:

 

 

‏ ‏عن ‏ ‏أبي هريرة رضي الله عنه  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهم عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((أَتَدْرُونَ مَا الْمُفْلِسُ)) قَالُوا: الْمُفْلِسُ فِينَا مَنْ لا دِرْهَمَ لَهُ وَلا مَتَاعَ، فَقَالَ: ((إِنَّ الْمُفْلِسَ مِنْ أُمَّتِي يَأْتِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ بِصَلاةٍ وَصِيَامٍ وَزَكَاةٍ وَيَأْتِي قَدْ شَتَمَ هَذَا وَقَذَفَ هَذَا وَأَكَلَ مَالَ هَذَا وَسَفَكَ دَمَ هَذَا وَضَرَبَ هَذَا فَيُعْطَى هَذَا مِنْ حَسَنَاتِهِ وَهَذَا مِنْ حَسَنَاتِهِ فَإِنْ فَنِيَتْ حَسَنَاتُهُ قَبْلَ أَنْ يُقْضَى مَا عَلَيْهِ أُخِذَ مِنْ خَطَايَاهُمْ فَطُرِحَتْ عَلَيْهِ ثُمَّ طُرِحَ فِي النَّارِ)) مسلم، الترمذي

Imetoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mnamjua nani aliyefilisika?)) Wakasema (Maswahaba): Aliyefilisika ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na dirham au mali. Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Aliyefilisika katika Ummah wangu ni yule atakayekuja siku ya Qiyaamah na Swalaah zake, Swawm zake na Zakaah zake, lakini atakuja akiwa amemtukana huyu, amemtuhumu huyu, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya huyu na amempiga huyu, yatachukuliwa mema yake na kulipwa wale aliowadhulumu. Yatakapomalizika mema yake kabla ya kufidia madhambi aliyowakosea wenzake, zitachukuliwa dhambi za wale aliowakosea kisha atajaziwa yeye na mwishowe atakuwa ni wa kutupwa motoni)) [Muslim, At-Tirmidhiy]

 

 

3.  Fikiria aibu zako au aibu za ndugu, jamaa zako na uwaze kama utapenda aibu hizo zidhihirike kwa wengine.

 

 

4.  Mshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kukuepusha na aibu kama za wenzako na muombe Asikupe mtihani wa aibu kama hizo au nyinginezo.

 

 

5.  Jiepushe na watu waovu na vikao viovu na andamana na watu wema ambao watakuwa na mazungumzo ya kukupa faida badala ya kukuangamiza.

 

 

6. Atakapokutafuta mwenzio kutaka kusengenya, muelezee wazi kuwa hutaki tena kusikia umbeya kwani unamkhofu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na umnasihi naye pia aache maouvu hayo kwa kumkumbusha adhabu zake.

 

 

7. Jipe adhabu mwenyewe kila unapomsengenya mtu kama walivyokuwa wakifanya Salafus-Swaalih (wema waliotangulia);

 

-Funga Swawm ya siku moja kila unapomsengenya mtu, hatimaye utashindwa kukaa na njaa kila siku.

 

-Toa kiasi fulani cha pesa kila unapomsengenya mtu, utakapojiona unafilikisha utaacha kusengenya. 

 

 

8. Hifadhi ulimi wako usizungumze ila mema tu, jifunze pole pole hata kwa kujikumbusha, mfano uweke kitu mdomoni kama kijiwe au chembe ngumu isiyotafunika ili ibakie kukukumbusha kuzuia ulimi kusema yasiyo na maana.

 

9. Jiepushe na moto pindi utakapolinda heshima ya mwenzio, kumbuka Hadiyth ifuatayo:

 

عن أبي الدرداء رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((مَنْ رَدَّ عَنْ عِرْضِ أَخِيهِ رَدَّ اللهُ عَنْ وَجْهِهِ النَّارَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ)) رواه الترمذي وحسنه

 

Abuu Ad-Dardaa (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayetetea heshima ya nduguye (Muislamu), Allaah Atamuepusha uso wake na moto)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth hii ni Hasan]

 

 

10.           Utakaposikia uzushi, kashfa au mtu atakapomsengenya mwenziwe mbele yako sema kama Anavyotufunza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Aayah zifuatazo kuhusu kisa cha 'ifk' (uzushi wa kusingiziwa Mama wa Waumimi 'Aaishah Radhwiya Allaahu 'anhaa):

 

 

Kwanza: Jifikirie nafsi yako kama wewe pia unaweza kufanya maovu hayo yanayozungumzwa? Kwa hiyo uweke dhana nzuri pia kwa Waumini wenzako.

 

 

لَّوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْرًا وَقَالُوا هَـٰذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ ﴿١٢﴾

Kwa nini mlipoisikia (kashfa ya kusingiziwa), Waumini wanaume na Waumini wanawake wasiwadhanie wenzao kheri, na wakasema: “Hii ni kashfa ya kusingizwa iliyo dhahiri?” [An-Nuwr: 12]

 

 

Pili:  Kanusha kabisa uliyoyasikia na chukulia hayo kuwa ni uzushi na Msabbih Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   

وَلَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَـٰذَا سُبْحَانَكَ هَـٰذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ ﴿١٦﴾

Na kwa nini mlipoisikia (kashfa ya kusingiziwa) msiseme: “Haitupasi sisi tuzungumze haya; Subhaanak! (Utakasifu ni Wako) huu ni usingiziaji wa dhulma mkubwa mno!” [An-Nuwr: 16]

 

 

 

Share