08-Madhara Ya Ghiybah: Kafara (Fidia) Ya Ghiybah

 

Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) Na An-Namiymah (Kufitinisha)

 

08- Kafara (Fidia) Ya Ghiybah

 

 

 

Ghiybah ni madhambi ambayo yanayomharibia mtu ‘amali zake njema na badala yake ni kujazwa dhambi za yule anayemsengenya na hatimaye kumuangamiza motoni. Hivyo inampasa Muislamu mwenye tabia hii ovu ambayo ni hatari kwake, afanye haraka kafara ya maovu hayo kama ifuatavyo:

 

 

1-Tawbah (Kutubia)

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا

  Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya nasuha (kwelikweli) [At-Tahriym: 8]

 

 

Tawbatun-Naswuwhaa (Tawbah ya kweli) ni ile mtu anayokamilisha shuruti zake nazo ni:

 

 

  • Kuacha kitendo kiovu hicho.
  • Kujuta
  • Kuazimia kutokurudia tena maovu
  • Ikiwa inahusu haki ya binaadamu basi lazima kwanza kurudisha haki hiyo.

 

2-Vipi ujihalalishe na Ghiybah

 

Kama ilivyo sharti ya nne kuwa kwa vile Ghiybah inahusu haki ya binaadamu basi lazima kwanza urudishe haki ya uliyemsengenya hapa duniani kabla ya kuhesabiwa Aakhirah, kwani Hadiyth ifuatayo inatuelezea,

 

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم  قال: ((من كانت عنده مظلمة لأخيه من عرضه أو من شيء، فليتحلله منها اليوم قبل أن لا يكون دينار ولا درهم، إن كان له عمل صالح أخذ منه بقدر مظلمته، وإن لم يكن له حسنات أخذ من سيئات صاحبه فحمل عليه  [رواه البخاري

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesimulia kwamba: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kitu cha dhulma cha nduguye kutokana na kumvunjia heshima au kitu chochote, basi amuombe amhalalishie leo kabla haijafika siku ambayo hakutakuwa na dinari wala dirhamu; akiwa ana amali njema itachukuliwa kwa kadiri ya alichodhulumu, na akiwa hana amali njema, zitachukuliwa dhambi za aliyemdhulumu na abebeshwe)) [Al-Bukhaariy]

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قَالَ:  ((مَنْ كَانَتْ عِنْدَهُ مَظْلَمَةٌ مِنْ أَخِيهِ مِنْ عِرْضِهِ أَوْ  مِنْ شَيْءٍ  فَلْيَتَحَلَّلْهُ مِنْهُ الْيَوْمَ قَبْلَ أَنْ لاَ يَكُونُ دِينَارٌ وَلاَ دِرْهَمٌ ، وَإِنْ كَانَ لَهُ عَمَلٌ صَالِحٌ أُخِذَ مِنْهُ بِقَدْرِ مَظْلَمَتِهِ. وَإِنْ لَمْ يَكُنْ لَهُ أُخِذَ مِنْ سَيِّئَاتِ صَاحِبِهِ فَحُمِل عَلَيْهِ))  رواه البخاري

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Aliyekuwa na kitu cha dhulma cha nduguye kutokana na kumvunjia heshima au kitu chochote, basi amuombe amhalalishie leo kabla haijafika siku ambayo hakutakuwa na dinari wala dirham. Ikiwa ana ‘amali njema, basi zitachukuliwa kwa kadiri ya alichodhulumiwa. Na ikiwa hana, basi zitachukuliwa dhambi za aliyemdhulumu abebeshwe)). [Al-Bukhaariy]

 

 

3-Mwenye kusengenywa asiwe na huzuni kwa kufanyiwa maovu haya kwani ni yeye mwenye kufaidika kwa kuchuma mema ambayo hakutia juhudi zake zozote za kuzifanyia kazi.  

 

 

Inasemekana kuwa Hasan Al-Baswry alimpelekea zawadi mtu aliyemsengenya na kumshukuru kwa kumchumia amali ambazo hakuzifanyia kazi kabisa.

 

 

4-Tutazame kauli zifuatazo za Salaf kuhusu kujihalalisha na Ghiybah:

 

 

- Sufyaan bin 'Uyaynah amesema: "Ghiybah ni dhambi kubwa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuliko zinaa au kunywa pombe kwani hizo ni dhambi baina ya mja na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), utakapotubu Atakughufuria, lakini Ghiybah ni baina ya mja na nduguye hadi amsamehe."

 

Kama tunavyojua kuwa ni vigumu sana mtu kuwa na moyo wa kumsamehe mwenzake anapomsengenya, ndio maana labda Salaf huyu akaona kuwa kusengenya ni madhambi makubwa zaidi kuliko madhambi mengine makubwa.

 

 

- Ibn Taymiyah, Ibnul Qayyim na wengineo, wameona kuwa sharti ya kujihalalisha na Ghiybah inaanguka pindi ukihisi kuwa utaharibu uhusiano wa uliyemsengenya na kuzidisha chuki na uadui baina yenu.

 

 

5-Sio wepesi kwa mtu mwenye kusengenya kumfuata mwenziwe na kumuomba msamaha kwa khofu ya kuwa ataharibu uhusiano. Hali kadhalika sio wepesi kwa mwenye kusengenywa kusamehe, kwani ni jambo linalomuumiza mtu moyoni khaswa ikiwa aliyekusengenya ni rafiki yako mpenzi au mtu wa karibu yako. Pindi hali ikiwa ni hivyo ya kusababisha chuki, uadui na kutoweka mapenzi na masikilizano, ni bora kutokumuomba msamaha bali fanya yafuatayo:

 

 

  • Muombee maghfirah kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amghufurie madhambi yake.
  • Muombee du'aa za kumtakia kheri nyingi duniani na Aakhirah.
  • Mfanyie wema kwa wingi.  

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atuepushe na maovu haya tusifike hadi hali zetu zikawa za kujuta na khasara ya kupoteza ‘amali zetu tunazojitahidi kuzifanya duniani kumbe hatuzimiliki Aakhirah.

 

 

 

Share