044 - Ad-Dukhaan

 

  الدُّخان

 

 

044-Ad-Dukhaan

 

 

044-Ad-Dukhaan: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

حم﴿١﴾

1. Haa Miym.[1]

 

 

وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ﴿٢﴾

2. Naapa kwa Kitabu (Qur-aan) kinachobainisha.[2]

 

 

 

 

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ﴿٣﴾

3. Hakika Sisi Tumekiteremsha katika usiku uliobarikiwa.[3] Hakika Sisi daima Ni Wenye Kuonya.

 

 

 

فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ﴿٤﴾

4.  Katika (usiku) huo hupambanuliwa kila jambo la hikmah.

 

 

 

أَمْرًا مِّنْ عِندِنَا ۚ إِنَّا كُنَّا مُرْسِلِينَ﴿٥﴾

5.  Ni amri kutoka Kwetu. Hakika Sisi ndio Wenye Kutuma (Rusuli).

 

 

 

 

رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ﴿٦﴾

6. Ni Rehma kutoka kwa Rabb wako. Hakika Yeye Ndiye Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote.

 

 

 

 

 

رَبِّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا ۖ إِن كُنتُم مُّوقِنِينَ﴿٧﴾

7. Rabb wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake, mkiwa ni wenye yakini.

 

 

 

 

 

لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ ۖ رَبُّكُمْ وَرَبُّ آبَائِكُمُ الْأَوَّلِينَ﴿٨﴾

8. Hapana muabudiwa wa haki ila Yeye, Anahuisha na Anafisha. Ni Rabb wenu na Rabb wa baba zenu wa awali.

 

 

 

 

بَلْ هُمْ فِي شَكٍّ يَلْعَبُونَ﴿٩﴾

9. Bali wao wamo katika shaka wanacheza.

 

 

 

 

فَارْتَقِبْ يَوْمَ تَأْتِي السَّمَاءُ بِدُخَانٍ مُّبِينٍ﴿١٠﴾

10. Basi ngojea siku mbingu zitakapoleta moshi bayana.[4]

 

 

 

 

يَغْشَى النَّاسَ ۖ هَـٰذَا عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿١١﴾

11. Utawafunika watu. Hii ni adhabu iumizayo.

 

 

 

 

رَّبَّنَا اكْشِفْ عَنَّا الْعَذَابَ إِنَّا مُؤْمِنُونَ﴿١٢﴾

12. (Watasema): Rabb wetu! Tuondoshee adhabu! Hakika sisi ni wenye kuamini.

 

 

 

أَنَّىٰ لَهُمُ الذِّكْرَىٰ وَقَدْ جَاءَهُمْ رَسُولٌ مُّبِينٌ﴿١٣﴾

13. Vipi wao wataweza kukumbuka na hali amekwishawajia Rasuli mwenye kubainisha!  

 

 

 

 

ثُمَّ تَوَلَّوْا عَنْهُ وَقَالُوا مُعَلَّمٌ مَّجْنُونٌ﴿١٤﴾

14. Kisha wakamkengeuka na wakasema: Amefundishwa na majnuni.

 

 

 

 

إِنَّا كَاشِفُو الْعَذَابِ قَلِيلًا ۚ إِنَّكُمْ عَائِدُونَ﴿١٥﴾

15. Hakika Sisi Tutaiondosha adhabu kidogo, lakini nyinyi hakika mtarudia vile vile.

 

 

 

يَوْمَ نَبْطِشُ الْبَطْشَةَ الْكُبْرَىٰ إِنَّا مُنتَقِمُونَ﴿١٦﴾

16. Siku Tutakayoshambulia mashambulio makubwa, hakika Sisi Ni Wenye Kulipiza. 

 

 

 

 

وَلَقَدْ فَتَنَّا قَبْلَهُمْ قَوْمَ فِرْعَوْنَ وَجَاءَهُمْ رَسُولٌ كَرِيمٌ﴿١٧﴾

17. Na kwa yakini Tuliwatia mtihanini kabla yao watu wa Firawni, na aliwajia Rasuli mtukufu.

 

 

 

 

أَنْ أَدُّوا إِلَيَّ عِبَادَ اللَّـهِ ۖ إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ﴿١٨﴾

18. (Akiwaambia): Wakabidhini kwangu Waja wa Allaah, hakika mimi kwenu ni Rasuli mwaminifu.

 

 

 

 

وَأَن لَّا تَعْلُوا عَلَى اللَّـهِ ۖ إِنِّي آتِيكُم بِسُلْطَانٍ مُّبِينٍ﴿١٩﴾

19. Na msimfanyie jeuri Allaah, hakika mimi nakuleteeni dalili bayana.

 

 

 

 

وَإِنِّي عُذْتُ بِرَبِّي وَرَبِّكُمْ أَن تَرْجُمُونِ﴿٢٠﴾

20. Na hakika mimi nimejikinga kwa Rabb wangu na Rabb wenu msije kunirajimu.

 

 

 

 

وَإِن لَّمْ تُؤْمِنُوا لِي فَاعْتَزِلُونِ﴿٢١﴾

21. Na ikiwa hamtoniamini, basi kaeni mbali nami.  

 

 

 

 

فَدَعَا رَبَّهُ أَنَّ هَـٰؤُلَاءِ قَوْمٌ مُّجْرِمُونَ﴿٢٢﴾

22. Akamuomba Rabb wake akisema: Hawa watu ni wahalifu.

 

 

 

 

 

فَأَسْرِ بِعِبَادِي لَيْلًا إِنَّكُم مُّتَّبَعُونَ﴿٢٣﴾

23. (Allaah Akasema): Basi ondoka usiku na Waja Wangu, hakika nyinyi ni wenye kuandamwa.

 

 

 

 

وَاتْرُكِ الْبَحْرَ رَهْوًا ۖ إِنَّهُمْ جُندٌ مُّغْرَقُونَ﴿٢٤﴾

24. Na acha bahari ikiwa imetulia, hakika wao ni jeshi lenye kugharikishwa.

 

 

 

 

 

كَمْ تَرَكُوا مِن جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ﴿٢٥﴾

25. Mabustani mangapi wameacha na chemchemu. 

 

 

 

 

وَزُرُوعٍ وَمَقَامٍ كَرِيمٍ﴿٢٦﴾

26. Na mimea na makazi ya kifahari.

 

 

 

 

وَنَعْمَةٍ كَانُوا فِيهَا فَاكِهِينَ﴿٢٧﴾

27. Na neema walizokuwa wakizifurahia.

 

 

 

 

كَذَٰلِكَ ۖ وَأَوْرَثْنَاهَا قَوْمًا آخَرِينَ﴿٢٨﴾

28. Hivyo ndivyo ilivyo. Na Tukawarithisha watu wengineo.

 

 

 

 

فَمَا بَكَتْ عَلَيْهِمُ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ وَمَا كَانُوا مُنظَرِينَ﴿٢٩﴾

29. Na hazikuwalilia mbingu na ardhi[5] na hawakuwa wa kupewa muhula.

 

 

 

وَلَقَدْ نَجَّيْنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ مِنَ الْعَذَابِ الْمُهِينِ﴿٣٠﴾

30. Na kwa yakini Tuliwaokoa wana wa Israaiyl kutokana na adhabu ya kudhalilisha.

 

 

 

 

 

مِن فِرْعَوْنَ ۚ إِنَّهُ كَانَ عَالِيًا مِّنَ الْمُسْرِفِينَ﴿٣١﴾

31. Kutoka kwa Firawni. Hakika yeye alikuwa mwenye kibri miongoni mwa wenye kupindukia mipaka.

 

 

 

 

وَلَقَدِ اخْتَرْنَاهُمْ عَلَىٰ عِلْمٍ عَلَى الْعَالَمِينَ﴿٣٢﴾

32. Na kwa yakini Tuliwakhitari (wana wa Israaiyl) kwa ilimu kuliko walimwengu wowote.

 

 

 

 

وَآتَيْنَاهُم مِّنَ الْآيَاتِ مَا فِيهِ بَلَاءٌ مُّبِينٌ﴿٣٣﴾

33. Na Tukawapa katika Aayaat (Miujiza) yenye majaribio bayana ndani yake.[6]

 

 

 

 

إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ لَيَقُولُونَ﴿٣٤﴾

34. Hakika hawa (Maquraysh) bila shaka wanasema.

 

 

 

 

إِنْ هِيَ إِلَّا مَوْتَتُنَا الْأُولَىٰ وَمَا نَحْنُ بِمُنشَرِينَ﴿٣٥﴾

35. Haya si chochote isipokuwa ni mauti yetu ya awali, nasi hatutofufuliwa.

 

 

 

 

فَأْتُوا بِآبَائِنَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴿٣٦﴾

36. Basi tuleteeni mababu zetu mkiwa ni wakweli.

 

 

 

 

أَهُمْ خَيْرٌ أَمْ قَوْمُ تُبَّعٍ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۚ أَهْلَكْنَاهُمْ ۖ إِنَّهُمْ كَانُوا مُجْرِمِينَ﴿٣٧﴾

37. Je, kwani wao ni bora zaidi au kaumu ya Tubba’[7] na wale waliokuwa kabla yao!  Tuliwaangamiza. Hakika wao walikuwa wahalifu.

 

 

 

 

 

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا لَاعِبِينَ﴿٣٨﴾

38. Na Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake kwa mchezo na upuuzi.

 

 

 

 

مَا خَلَقْنَاهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ﴿٣٩﴾

39. Hatukuumba viwili hivyo isipokuwa kwa haki, lakini wengi wao hawajui.

 

 

 

 

إِنَّ يَوْمَ الْفَصْلِ مِيقَاتُهُمْ أَجْمَعِينَ﴿٤٠﴾

40. Hakika Siku ya hukumu ni wakati wao maalumu uliopangwa kwa wote.

 

 

 

 

 

 

يَوْمَ لَا يُغْنِي مَوْلًى عَن مَّوْلًى شَيْئًا وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ﴿٤١﴾

41. Siku ambayo jamaa wa karibu hatomfaa jamaa yake wa karibu chochote, na wala wao hawatonusuriwa.

 

 

 

 

 

إِلَّا مَن رَّحِمَ اللَّـهُ ۚ إِنَّهُ هُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ﴿٤٢﴾

42. Isipokuwa yule Atakayerehemewa na Allaah.  Hakika Yeye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

 

إِنَّ شَجَرَتَ الزَّقُّومِ﴿٤٣﴾

43. Hakika mti wa az-zaqquwm.[8]

 

 

 

 

طَعَامُ الْأَثِيمِ﴿٤٤﴾

44. Ni chakula cha mtendaji mno dhambi.

 

 

 

 

كَالْمُهْلِ يَغْلِي فِي الْبُطُونِ﴿٤٥﴾

45. Kama masazo ya zebaki nyeusi iliyoyeyushwa, inatokota matumboni.

 

 

 

 

كَغَلْيِ الْحَمِيمِ﴿٤٦﴾

46. Kama kutokota kwa maji yachemkayo.

 

 

 

 

 

خُذُوهُ فَاعْتِلُوهُ إِلَىٰ سَوَاءِ الْجَحِيمِ﴿٤٧﴾

47. (Itaamrishwa): Mchukueni na msokomezeni katikati ya moto uwakao vikali mno.

 

 

 

 

ثُمَّ صُبُّوا فَوْقَ رَأْسِهِ مِنْ عَذَابِ الْحَمِيمِ﴿٤٨﴾

48. Kisha mwagieni juu ya kichwa chake adhabu ya maji yachemkayo.

 

 

 

 

ذُقْ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْكَرِيمُ﴿٤٩﴾

49. Onja! Si ndiye weye mwenye nguvu mheshimiwa![9] 

 

 

إِنَّ هَـٰذَا مَا كُنتُم بِهِ تَمْتَرُونَ﴿٥٠﴾

50. Hakika haya ndiyo ambayo mlikuwa mkiyatilia shaka.

 

 

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي مَقَامٍ أَمِينٍ﴿٥١﴾

51. Hakika wenye taqwa watakuwa katika mahali pa amani.

 

 

 

 

فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ﴿٥٢﴾

52. Katika Jannaat (Pepo) na chemchemu.[10]

 

 

 

 

يَلْبَسُونَ مِن سُندُسٍ وَإِسْتَبْرَقٍ مُّتَقَابِلِينَ﴿٥٣﴾

53. Watavaa hariri laini na hariri nzito nyororo wakiwa wamekabiliana. 

 

 

 

 

كَذَٰلِكَ وَزَوَّجْنَاهُم بِحُورٍ عِينٍ﴿٥٤﴾

54. Hivyo ndivyo!  Na Tutawaozesha hurulaini: wanawake weupe wazuri wa Jannah wenye macho makubwa ya kupendeza.

 

 

 

 

يَدْعُونَ فِيهَا بِكُلِّ فَاكِهَةٍ آمِنِينَ﴿٥٥﴾

55. Wataagiza humo kila aina ya matunda wakiwa katika amani.

 

 

 

 

 

لَا يَذُوقُونَ فِيهَا الْمَوْتَ إِلَّا الْمَوْتَةَ الْأُولَىٰ ۖ وَوَقَاهُمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ﴿٥٦﴾

56. Hawatoonja humo mauti isipokuwa mauti yale ya awali, na (Allaah) Atawakinga na adhabu ya moto uwakao vikali mno.

 

 

 

 

 

فَضْلًا مِّن رَّبِّكَ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿٥٧﴾

57. Ni fadhila kutoka kwa Rabb wako. Huko ndiko kufuzu adhimu.

 

 

 

 

 

فَإِنَّمَا يَسَّرْنَاهُ بِلِسَانِكَ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ﴿٥٨﴾

58. Basi hakika Tumeiwepesisha (Qur-aan) kwa ulimi wako ili wapate kukumbuka.[11]

 

 

فَارْتَقِبْ إِنَّهُم مُّرْتَقِبُونَ﴿٥٩﴾

59. Basi ngojea (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), hakika wao pia ni wenye kungojea.   

 

 

 

[1] الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):

 

Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).

 

[2] Qur-aan Na Kuteremshwa Kwake Laylatul-Qadr:

 

Tafsiyr Aayah (2) hadi (4):

 

Ameapa Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Qur-aan iliyowazi kimatamshi na kimaana. Sisi Tumeiteremsha katika Usiku wa Cheo uliobarikiwa wenye kheri nyingi, nao unapatikana katika mwezi wa Ramadhwaan. Sisi ni Wenye kuonya watu kwa kile kinachowanufaisha na kuwadhuru, nako ni kule kupeleka Rusuli na kuteremsha Vitabu, ili hoja ya Allaah iwasimamie Waja Wake. Katika usiku huo, linaamuliwa na kupambanuliwa kutoka kwenye Lawh Al-Mahfuwdhw (Ubao Uliohifadhiwa) na kuletewa waandishi kati ya Malaika, kila jambo lililokadiriwa la muda wa kuishi na riziki katika mwaka huo, na mambo mengine yatakayokuwa na kukadiriwa na Allaah (سبحانه وتعالى) mpaka mwisho wa mwaka, hayabadilishwi wala hayageuzwi. Mambo haya yaliyopangwa kimadhubuti ni amri inayotoka Kwetu, kwani yote yanayokuwa na Anayokadiria Allaah (سبحانه وتعالى) na Wahy Anaouleta, vyote hivyo vinatokana na Amri Yake na Idhini Yake na Ujuzi Wake. [Tafsiyr Al-Muyassar] 

 

[3] Usiku Uliobarikiwa (Laylatul-Qadr):

 

Rejea Suwrah Al-Qadr (97) kwenye viungo vyenye faida kuhusu Usiku huu mtukufu na fadhila zake.

 

[4] Sababun-Nuzuwl (Sababu Ya Kuteremshwa) Aayah Au Suwrah:

 

Kuanzia Aayah hii ya (10) hadi (15), kuna sababu ya kuteremshwa.

 

Bonyeza kiungo kifuatacho:

 

044-Asbaabun-Nuzuwl: Ad-Dukhaan Aayah 10-15: ‏فَارْتَقِبْ يَوْمَ تَأْتِي السَّمَاءُ بِدُخَانٍ مُبِينٍ

 

[5] Mbingu Na Ardhi Huwalilia Waumini:

 

Tafsiyr za ‘Ulamaa:

 

Yaani: Baada ya Allaah (سبحانه وتعالى) Kuwaangamiza, mbingu na ardhi hazikuwalilia wala kuhuzunika kwa sababu ya kuangamia kwao, bali kila kimoja kilifurahi na kupeana bishara, mpaka mbingu na ardhi, kwa sababu hawakuacha athari isipokuwa itayozifanya nyuso zao kuwa nyeusi, na kuwajibisha wao kupata laana na kukasirikiwa na Allaah Rabb wa viumbe wote. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Amesema Ibn Jariyr: Kutoka kwa Sa’iyd Bin Jubayr amesema: Mtu mmoja alimjia Ibn ‘Abbaas akasema: Ee Baba yake ‘Abbaas, hivi waonaje Kauli ya Allaah:

 

فَمَا بَكَتْ عَلَيْهِمُ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ وَمَا كَانُوا مُنظَرِينَ﴿٢٩﴾

Na hazikuwalilia mbingu na ardhi, na hawakuwa wa kupewa muhula.

 

Je mbingu na ardhi zinaweza kumlilia mtu yeyote yule? Akasema: Naam, kwani hakuna kiumbe yeyote yule isipokuwa ana mlango wake mbinguni. Rizki yake inateremka hapo na matendo yake pia yanapanda kupitia hapo. Anapofariki Muumini na ukafungwa mlango wake mbinguni ambao amali zake zilikuwa zinapanda kupitia hapo, basi mbingu humlilia, na sehemu anayoswalia hapa ardhini na kumdhukuru Allaah ikimkosa, basi ardhi nayo inamlilia kwa kumkosa aliyekuwa akiswalia pale. Na kwa hakika watu wa Firawni hawakuwa na athari njema katika ardhi, wala haikuwahi kupanda kheri yeyote mbinguni kutoka kwao. Ndio maana mbingu na ardhi hazikuwalilia. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Fatwa ya Imaam Ibn Baaz (رحمه الله):

Swali aliloulizwa kuhusu maana ya Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

فَمَا بَكَتْ عَلَيْهِمُ السَّمَاءُ وَالْأَرْضُ وَمَا كَانُوا مُنظَرِينَ﴿٢٩﴾

Na hazikuwalilia mbingu na ardhi, na hawakuwa wa kupewa muhula.

 

Akajibu: “‘Ulamaa wametaja katika hili kwamba, wao hawakuwa na matendo mema, na mbingu na ardhi huwa zinalia zikikosa matendo mema kutoka kwa watu wa kheri.

Ama kwa hawa, hakuna kheri kwao na wala hakuna matendo mema yanayopanda mbinguni, kwa sababu hiyo, haziwalilii mbingu wala ardhi kwa kutokuwa na matendo mema. Na hivyo basi hawakuachiwa muda bali waliangamizwa muda uleule. Tunamuomba Allaah Al-‘Aafiyah.” Al-Mawqi' Ar-Rasmiy li-Samaahat Ash-Shaykh Al-Imaam Ibn Baaz]

 

[6] Miujiza Bayana Ya Majaribio:

 

Tafsiyr za ‘Ulamaa:

وَآتَيْنَاهُم  

Na Tukawapa.

 

Yaani: Bani Israaiyl. Na

 

    مِّنَ الْآيَاتِ مَا فِيهِ بَلَاءٌ مُّبِينٌ﴿٣٣﴾

Katika Aayaat (Miujiza) yenye majaribio bayana ndani yake.

 

Yaani: Miujiza ya wazi, ihsaani nyingi za wazi kutoka Kwetu juu yao, na hoja juu yao kuhusiana na usahihi wa aliyowaletea Nabiy wao Muwsaa (عليه السّلام). [Tafsiyr As-Sa’diy]

Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

وَآتَيْنَاهُم مِّنَ الْآيَاتِ

Na Tukawapa katika Aayaat (Miujiza).

 

Hoja za wazi na mambo yanayokwenda kinyume na mazoea.

  مَا فِيهِ بَلَاءٌ مُّبِينٌ﴿٣٣﴾

Yenye majaribio bayana ndani yake.

 

Ni mtihani wa wazi kwa aliyeongoka kwao. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

[7] Tubba’

 

Ni Mfalme katika wafalme wa Yemen na alikuwa mshirikina kisha akasilimu.

 

Amesimulia Sahl bin Sa’d (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Msimtukane Tubba’ah kwani amesilimu.” [Ahmad katika Musnad yake, na ameisahihisha Al-Albaaniy katika As-Silsilah Asw- Swahiyhah (2423)]

 

[8] Mti wa Zaqquwm:

 

Mti mchungu mno motoni wa karaha ambao utakuwa chakula cha wakaazi wake humo. Rejea Al-Israa (17:60), Asw-Swaaffaat (37-63-68).

 

Adhabu Na Chakula Cha Watu Wa Motoni: Rejea An-Nabaa (78:21) kwenye fafanuzi na rejea nyenginezo.

 

[9] Kafiri Aliyejifanya Mheshimiwa Mwenye Nguvu Anafanyiwa Kejeli Motoni:

 

Tafsiyr za ‘Ulamaa:

 

Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

ذُقْ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْكَرِيمُ﴿٤٩﴾

“Onja! Si ndiye weye mwenye nguvu mheshimiwa!”

 

Na ataambiwa yule ataeadhibiwa: Onja adhabu hii iumizayo, na malipo mabaya, kwa madai yako kwamba wewe ni mtukufu, unaweza kujizuia na adhabu ya Allaah, na wewe ni muheshimiwa mbele ya Allaah, kwamba Hatokulipa adhabu. Sasa leo hii ndio imebainika kwako kwamba wewe ni dhalili usiye na chembe ya thamani. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

ذُقْ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْكَرِيمُ﴿٤٩﴾

“Onja! Si ndiye weye mwenye nguvu mheshimiwa!”

 

 

Mwambieni maneno hayo, kwa sura ya kumlaumu na kumcheza shere. Na Adhw-Dhwahaak amesema kutoka kwa Ibn ‘Abbaas: Sio mtukufu wala sio mheshimiwa. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

[10] Neema Za Watu Wa Jannah:

 

Rejea pia Faatwir (35:35) kwenye maelezo bayana na rejea mbalimbali.

 

[11] Qur-aan Imefanywa Nyepesi Kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  Na Waumini:

 

Tafsiyr za ‘Ulamaa:

 

Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

فَإِنَّمَا يَسَّرْنَاهُ بِلِسَانِكَ

Basi hakika Tumeiwepesisha (Qur-aan) kwa ulimi wako.

 

Hakika Tumeifanya Qur-aan kuwa nyepesi, ambayo Tumeiteremsha ikiwa nyepesi, iko wazi, kwa lugha yako ambayo ndio (lugha) fasaha zaidi ya zote, ni nzuri na iko juu zaidi.

 

لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ﴿٥٨﴾

Ili wapate kukumbuka.

 

Watafahamu na kuelewa, kisha baada ya uwazi na ubainifu huu, wapo wengine walikufuru kupinga na wengine kukaidi. Ndio Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema kumliwaza Rasuli Wake na kumuahidi msaada na nusra, na kuwaahidi adhabu kali na kuangamia kwa watakao mkadhibisha Allaah. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Rejea pia Al-Qamar (54:17).

 

Share