045 - Al-Jaathiyah

 

الْجاثِيَة

 

045-Al-Jaathiyah

 

 

045-Al-Jaathiyah: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

حم﴿١﴾

1. Haa Miym.[1] 

 

 

 

 

تَنزِيلُ الْكِتَابِ مِنَ اللَّـهِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ﴿٢﴾

2. Ni uteremsho wa Kitabu kutoka kwa Allaah Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

 

إِنَّ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَآيَاتٍ لِّلْمُؤْمِنِينَ﴿٣﴾

3. Hakika katika mbingu na ardhi bila shaka kuna Aayaat (Ishara, Dalili) kwa Waumini.

 

 

 

وَفِي خَلْقِكُمْ وَمَا يَبُثُّ مِن دَابَّةٍ آيَاتٌ لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ﴿٤﴾

4. Na katika kuumbwa kwenu, na Anaoyatawanya kati ya viumbe vinavyotembea ni Aayaat (Ishara, Dalili) kwa watu wenye yakini.

 

 

 

 

 

وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَمَا أَنزَلَ اللَّـهُ مِنَ السَّمَاءِ مِن رِّزْقٍ فَأَحْيَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا وَتَصْرِيفِ الرِّيَاحِ آيَاتٌ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ﴿٥﴾

5. Na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana, na Anayoteremsha Allaah kutoka mbinguni katika mvua, Akahuisha kwayo ardhi baada ya kufa kwake[2], na kugeukageuka upepo (wa rehma) ni Aayaat (Ishara, Dalili) kwa watu wanaotia akilini.

 

 

 

 

تِلْكَ آيَاتُ اللَّـهِ نَتْلُوهَا عَلَيْكَ بِالْحَقِّ ۖ فَبِأَيِّ حَدِيثٍ بَعْدَ اللَّـهِ وَآيَاتِهِ يُؤْمِنُونَ﴿٦﴾

6. Hizi ni Aayaat za Allaah Tunakusomea kwa haki. Basi kauli gani baada ya Allaah na Aayaat Zake wataziamini?

 

 

 

 

وَيْلٌ لِّكُلِّ أَفَّاكٍ أَثِيمٍ﴿٧﴾

7.  Ole kwa kila mzushi muongo, mtendaji mno dhambi.

 

 

 

 

يَسْمَعُ آيَاتِ اللَّـهِ تُتْلَىٰ عَلَيْهِ ثُمَّ يُصِرُّ مُسْتَكْبِرًا كَأَن لَّمْ يَسْمَعْهَا ۖ فَبَشِّرْهُ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ﴿٨﴾

8. Anazisikia Aayaat za Allaah akisomewa, kisha anang’ang’ana kuwa mwenye kutakabari kama kwamba hakuzisikia. Basi mbashirie adhabu iumizayo.

 

 

 

 

وَإِذَا عَلِمَ مِنْ آيَاتِنَا شَيْئًا اتَّخَذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ﴿٩﴾

9. Na anapojua chochote katika Aayaat Zetu huzichukulia mzaha. Hao watapata adhabu ya kudhalilisha.

 

 

 

 

 

مِّن وَرَائِهِمْ جَهَنَّمُ ۖ وَلَا يُغْنِي عَنْهُم مَّا كَسَبُوا شَيْئًا وَلَا مَا اتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ أَوْلِيَاءَ ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ﴿١٠﴾

10. Nyuma yao iko Jahannam, na wala hayatowafaa kitu yale waliyoyachuma na wala wale waliowafanya walinzi badala ya Allaah, na watapata adhabu kuu.

 

 

 

 

هَـٰذَا هُدًى ۖ وَالَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ لَهُمْ عَذَابٌ مِّن رِّجْزٍ أَلِيمٌ﴿١١﴾

11. Hii (Qur-aan) ni mwongozo. Na wale waliokanusha Aayaat (na Ishara, Dalili) za Rabb   wao watapata adhabu ya kufadhaika iumizayo.

 

 

 

 

 

اللَّـهُ الَّذِي سَخَّرَ لَكُمُ الْبَحْرَ لِتَجْرِيَ الْفُلْكُ فِيهِ بِأَمْرِهِ وَلِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ﴿١٢﴾

12. Allaah Ambaye Amekutiishieni bahari ili zipite merikebu humo kwa Amri Yake, na ili mtafute katika Fadhila Zake, na ili mpate kumshukuru.[3]

 

 

 

 

 

وَسَخَّرَ لَكُم مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مِّنْهُ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ﴿١٣﴾

13. Na Amekutiishieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini vyote, ni ihsani itokaye Kwake. Hakika katika hayo bila shaka kuna Aayaat (Dalili, Ishara) kwa watu wanaotafakari.

 

 

 

 

قُل لِّلَّذِينَ آمَنُوا يَغْفِرُوا لِلَّذِينَ لَا يَرْجُونَ أَيَّامَ اللَّـهِ لِيَجْزِيَ قَوْمًا بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ﴿١٤﴾

14 Waambie (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) wale walioamini wawasamehe wale wasiozitaraji Siku za Allaah ili Awalipe watu kutokana na yale waliyokuwa wakiyachuma.[4]

 

 

 

 

 

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ أَسَاءَ فَعَلَيْهَا ۖ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ﴿١٥﴾

15. Yeyote atendaye jema, basi ni kwa ajili ya nafsi yake, na mwenye kufanya uovu, basi ni hasara kwake, kisha kwa Rabb wenu mtarejeshwa.

 

 

 

 

 

وَلَقَدْ آتَيْنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ الْكِتَابَ وَالْحُكْمَ وَالنُّبُوَّةَ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ﴿١٦﴾

16. Na kwa yakini Tuliwapa wana wa Israaiyl Kitabu na hikma na unabii, na Tukawaruzuku katika vizuri, na Tukawafadhilisha juu ya walimwengu.

 

 

 

 

 

وَآتَيْنَاهُم بَيِّنَاتٍ مِّنَ الْأَمْرِ ۖ فَمَا اخْتَلَفُوا إِلَّا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْعِلْمُ بَغْيًا بَيْنَهُمْ ۚ إِنَّ رَبَّكَ يَقْضِي بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ﴿١٧﴾

17. Na Tukawapa hoja bayana ya mambo (ya Dini). Basi hawakukhitilafiana isipokuwa baada ya kuwajia ilimu kwa kufanyiana uadui na husuda baina yao. Hakika Rabb wako Atahukumu baina yao Siku ya Qiyaamah katika yale waliyokuwa wakikhitilafiana.

 

 

 

 

 

ثُمَّ جَعَلْنَاكَ عَلَىٰ شَرِيعَةٍ مِّنَ الْأَمْرِ فَاتَّبِعْهَا وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَ الَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ﴿١٨﴾

18. Kisha Tukakuwekea (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Sharia ya mambo, basi ifuate, na wala usifuate hawaa za wale wasiojua.

 

 

 

 

إِنَّهُمْ لَن يُغْنُوا عَنكَ مِنَ اللَّـهِ شَيْئًا ۚ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۖ وَاللَّـهُ وَلِيُّ الْمُتَّقِينَ﴿١٩﴾

19. Hakika wao hawatokufaa chochote mbele ya Allaah. Na hakika madhalimu ni marafiki wanaoshirikiana wao kwa wao. Na Allaah Ni Rafiki Mlinzi wa wenye taqwa.

 

 

 

 

هَـٰذَا بَصَائِرُ لِلنَّاسِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ﴿٢٠﴾

20. Hii (Qur-aan) ni busara na kifumbuzi macho kwa watu, na ni mwongozo na rehma kwa watu wenye yakini.

 

 

 

 

 

أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ اجْتَرَحُوا السَّيِّئَاتِ أَن نَّجْعَلَهُمْ كَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَوَاءً مَّحْيَاهُمْ وَمَمَاتُهُمْ ۚ سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ﴿٢١﴾

21. Je, wanadhania wale waliochuma maovu kwamba Tutawafanya sawa na wale walioamini na wakatenda mema, sawasawa uhai wao na kufa kwao?[5] Uovu ulioje wa wanavyohukumu!  

 

 

 

 

 

وَخَلَقَ اللَّـهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ وَلِتُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ﴿٢٢﴾

22. Na Allaah Ameumba mbingu na ardhi kwa haki, na ili ilipwe kila nafsi kwa yale iliyoyachuma, nao hawatodhulumiwa.

 

 

 

 

 

أَفَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَـٰهَهُ هَوَاهُ وَأَضَلَّهُ اللَّـهُ عَلَىٰ عِلْمٍ وَخَتَمَ عَلَىٰ سَمْعِهِ وَقَلْبِهِ وَجَعَلَ عَلَىٰ بَصَرِهِ غِشَاوَةً فَمَن يَهْدِيهِ مِن بَعْدِ اللَّـهِ ۚ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ﴿٢٣﴾

23. Je, umemuona yule aliyejichukulia hawaa zake kuwa ndio mwabudiwa wake[6], na Allaah Akampotoa baada ya kufikiwa na ilimu na hoja, na Akapiga mhuri juu ya masikio yake na moyo wake, na Akaweka kifuniko juu ya macho yake? Basi nani atamuongoa baada ya Allaah? Je, basi hamkumbuki?

 

 

 

 

 

وَقَالُوا مَا هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا يُهْلِكُنَا إِلَّا الدَّهْرُ ۚ وَمَا لَهُم بِذَٰلِكَ مِنْ عِلْمٍ ۖ إِنْ هُمْ إِلَّا يَظُنُّونَ﴿٢٤﴾

24. Na wakasema: Huu si chochote isipokuwa ni uhai wetu wa dunia, tunakufa na tunahuika, na hakuna cha kutuangamiza isipokuwa zama tu. Na wala hawana kwayo ujuzi wowote, ila wao wanadhania tu.[7]

 

 

 

 

 

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ مَّا كَانَ حُجَّتَهُمْ إِلَّا أَن قَالُوا ائْتُوا بِآبَائِنَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴿٢٥﴾

25. Na wanaposomewa Aayaat Zetu bayana haikuwa hoja yao isipokuwa kusema: Tuleteeni mababa zetu mkiwa nyinyi ni wakweli.

 

 

 

 

 

قُلِ اللَّـهُ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يَجْمَعُكُمْ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ لَا رَيْبَ فِيهِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ﴿٢٦﴾

26. Sema: Allaah Anakuhuisheni, kisha Atakufisheni, kisha Atakukusanyeni Siku ya Qiyaamah isiyo na shaka ndani yake, lakini watu wengi hawajui.

 

 

 

 

 

وَلِلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ يَوْمَئِذٍ يَخْسَرُ الْمُبْطِلُونَ﴿٢٧﴾

27. Na ni wa Allaah Pekee ufalme wa mbingu na ardhi. Na Siku itakayosimama Saa, watakhasirika Siku hiyo wabatilifu.

 

 

 

 

 

وَتَرَىٰ كُلَّ أُمَّةٍ جَاثِيَةً ۚ كُلُّ أُمَّةٍ تُدْعَىٰ إِلَىٰ كِتَابِهَا الْيَوْمَ تُجْزَوْنَ مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ﴿٢٨﴾

28. Na utaona kila ummah umepiga magoti kwa unyenyekevu na khofu [8]. Kila ummah utaitwa kwenye kitabu chake (cha matendo): Leo mtalipwa yale mliyokuwa mkiyatenda.

 

 

 

 

هَـٰذَا كِتَابُنَا يَنطِقُ عَلَيْكُم بِالْحَقِّ ۚ إِنَّا كُنَّا نَسْتَنسِخُ مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ﴿٢٩﴾

29. Hiki ni kitabu Chetu, kinatamka (kushuhudia) juu yenu kwa haki. Hakika Sisi Tulikuwa Tunaamuru yaandikwe yale mliyokuwa mkiyatenda.

 

 

 

 

 

فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَيُدْخِلُهُمْ رَبُّهُمْ فِي رَحْمَتِهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْمُبِينُ﴿٣٠﴾

30. Basi wale walioamini na wakatenda mema, Rabb wao Atawaingiza katika Rehma Yake. Huko ndiko kufuzu kulio wazi.

 

 

 

 

 

وَأَمَّا الَّذِينَ كَفَرُوا أَفَلَمْ تَكُنْ آيَاتِي تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَاسْتَكْبَرْتُمْ وَكُنتُمْ قَوْمًا مُّجْرِمِينَ﴿٣١﴾

31. Ama wale waliokufuru (wataambiwa): Je, kwani hazikuwa Aayaat Zangu zikisomwa kwenu, mkatakabari na mkawa watu wahalifu?

 

 

 

 

 

وَإِذَا قِيلَ إِنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَالسَّاعَةُ لَا رَيْبَ فِيهَا قُلْتُم مَّا نَدْرِي مَا السَّاعَةُ إِن نَّظُنُّ إِلَّا ظَنًّا وَمَا نَحْنُ بِمُسْتَيْقِنِينَ﴿٣٢﴾

32. Na inaposemwa: Hakika Ahadi ya Allaah ni haki, na Saa haina shaka ndani yake mlisema: Hatujui Saa ni nini! Hatudhanii isipokuwa ni dhana tupu, nasi sio wenye kuyakinika kikweli.

 

 

 

 

 

وَبَدَا لَهُمْ سَيِّئَاتُ مَا عَمِلُوا وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ﴿٣٣﴾

33. Na yatawafichukia maovu waliyoyatenda, na yatawazunguka yale waliyokuwa wakiyafanyia istihzai.

 

 

 

 

 

وَقِيلَ الْيَوْمَ نَنسَاكُمْ كَمَا نَسِيتُمْ لِقَاءَ يَوْمِكُمْ هَـٰذَا وَمَأْوَاكُمُ النَّارُ وَمَا لَكُم مِّن نَّاصِرِينَ﴿٣٤﴾

34. Na itasemwa: Leo Tunakusahauni kama mlivyosahau kukutana na Siku yenu hii, na makazi yenu ni motoni, na wala hamna yeyote mwenye kunusuru.

 

 

 

 

ذَٰلِكُم بِأَنَّكُمُ اتَّخَذْتُمْ آيَاتِ اللَّـهِ هُزُوًا وَغَرَّتْكُمُ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا ۚ فَالْيَوْمَ لَا يُخْرَجُونَ مِنْهَا وَلَا هُمْ يُسْتَعْتَبُونَ﴿٣٥﴾

35. Hivyo ni kwa sababu nyinyi mlizichukulia mzaha Aayaat za Allaah, na ukakudanganyeni uhai wa dunia. Basi leo hawatotolewa humo, na wala hawataachiliwa nafasi ya kujitetea (kwa Allaah).

 

 

 

 

 

فَلِلَّـهِ الْحَمْدُ رَبِّ السَّمَاوَاتِ وَرَبِّ الْأَرْضِ رَبِّ الْعَالَمِينَ﴿٣٦﴾

36. Basi AlhamduliLLaah (Himidi Anastahiki Allaah) Rabb wa mbingu na Rabb wa ardhi, Rabb wa walimwengu.

 

 

 

 

وَلَهُ الْكِبْرِيَاءُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴿٣٧﴾

37. Na Ukubwa, Uadhama, Ujalali ni Wake Pekee mbinguni na ardhini. Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.[9]

 

 

 

 

[1] الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):

 

Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).

 

[2] Mfano Wa Ardhi Iliyokufa (Kame), Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akaihuisha Kwa Mvua, Ni Mfano Wa Kuwahuisha Watu Kutoka Makaburini Mwao Siku Ya Qiyaamah:

 

Rejea Ar-Ruwm (30:50) kwenye maelezo bayana na rejea mbalimbali.

 

[3] Miongoni Mwa Neema Za Allaah (سبحانه وتعالى) Kwa Viumbe Vyake:

 

Aayah hii (12) na inayofuatia (13) zinataja baadhi ya Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) kwa viumbe ardhini. Rejea Suwrah Ibraahiym (14:34) kwenye maelezo bayana na uchambuzi wa Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) na rejea mbalimbali na kwamba Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) haiwezekani kamwe kuziorodhesha hesabuni!

 

[4] Maana Ya Siku Za Allaah: 

 

Rejea Ibraahiym (14:5).

 

Allaah (عزّ وجلّ) Anawaamrisha waja Wake Waumini kuwa na khulqa (tabia) njema na wawe na subira juu ya maudhi ya washirikina wasiotaraji siku za Allaah, yaani: hawataraji thawabu zake na wala hawaogopi adhabu Zake kwa watakaomuasi. Kwani Allaah (سبحانه وتعالى) Atawalipa kila watu yale waliyokuwa wakiyachuma. Basi nyinyi enyi Waumini, Atawalipa thawabu tele kwa imaan zenu na kusamehe kwenu na subra zenu. [Tafsiyr As-Sa’diy]   

 

[5] Haiwezekani Makafiri Kulingana Sawa Na Waumini Katika Imaan Zao, Uhai Wao Duniani Na Aakhirah:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anakanusha madai ya makafiri kuwa wao wanalingana na Waumini. Anabainisha hapa kuwa makafiri hawawezi kulingana sawa na Waumini kwa sababu ya ‘Aqiydah yao ya kuamini Risala ya Allaah (سبحانه وتعالى) kupitia Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), imaan yao, taqwa zao, kumkhofu Allaah (سبحانه وتعالى), kutekeleza Amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake. Kwa msingi huu, Waumini wanaishi duniani kwa lengo la kumridhisha Rabb wao, na kutaraji Rehma Yake Allaah (سبحانه وتعالى) Awaingize Jannah (Peponi). Ama makafiri, wao ni tofauti na Waumini katika hayo yote, na wao wanaishi duniani bila ya lengo la kumridhisha Rabb wao, hivyo basi hatima yao ni motoni. Rejea Kauli Zake nyenginezo za Allaah (سبحانه وتعالى) kama ifuatavyo: Al-Hashr (59:20), Al-Qalam (68:35-36), Swaad (38:28), As-Sajdah (32:18-20).

 

[6] Hawaa (Matamanio) Ya Mtu Kuwa Ndio Mwabudiwa:

 

Rejea Al-Furqaan (25:43) kwenye maelezo bayana.

 

[7] Washirikina Na Makafiri Hawaamini Kufufuliwa: 

 

Rejea Al-Israa (17:49) kwenye maelezo bayana. Na rejea pia Suwrah hii Al-Jaathiyah (45:32).

 

Na Aayah namba (26) ya Suwrah hii Al-Jaathiyah, inathibitisha wazi Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) wa Kuwafufua viumbe Siku ya Qiyaamah.

 

[8] Al-Jaathiya (Jina La Suwrah): Kupiga Magoti Kwa Unyenyekevu Na Kukhofu Na Kungojea Kuhesabiwa

 

Kila Ummah utahudhurishwa pamoja na Shahidi wake. Rejea Al-Baqarah (2:143), An-Nisaa (4:41), An-Nahl (16:89), Al-Israa (17:71), Al-Hajj (22:78), Az-Zumar (39:69).

 

[9] Utukufu, Uadhwamah, Ujalali Wa Allaah (عزّ وجلّ):

 

 عن أَبي هريرة رضي الله عنه ، قَالَ : قَالَ رسول الله صلى الله عليه وسلم : ((  قَالَ الله (عزّ وجلّ) : العِزُّ إزَاري ، والكبرياءُ رِدائي ، فَمَنْ يُنَازِعُنِي في وَاحِدٍ منهما فَقَد عَذَّبْتُهُ )) رواه مسلم .

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: "Amesema Allaah (عزّ وجلّ): Utukufu ni kikoi Changu, na kiburi ni shuka Yangu, na atakayeshindana Nami katika moja wapo ya viwili hivi Nitamuadhibu." [Muslim]

 

 

Share