060 - Al-Mumtahinah

 

  الْمُمْتَحِنَة

 

060-Al-Mumtahinah

 

060-Al-Mumtahinah: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا عَدُوِّي وَعَدُوَّكُمْ أَوْلِيَاءَ تُلْقُونَ إِلَيْهِم بِالْمَوَدَّةِ وَقَدْ كَفَرُوا بِمَا جَاءَكُم مِّنَ الْحَقِّ يُخْرِجُونَ الرَّسُولَ وَإِيَّاكُمْ ۙ أَن تُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ رَبِّكُمْ إِن كُنتُمْ خَرَجْتُمْ جِهَادًا فِي سَبِيلِي وَابْتِغَاءَ مَرْضَاتِي ۚ تُسِرُّونَ إِلَيْهِم بِالْمَوَدَّةِ وَأَنَا أَعْلَمُ بِمَا أَخْفَيْتُمْ وَمَا أَعْلَنتُمْ ۚ وَمَن يَفْعَلْهُ مِنكُمْ فَقَدْ ضَلَّ سَوَاءَ السَّبِيلِ﴿١﴾

1. Enyi walioamini! Msifanye adui Wangu na adui wenu kuwa marafiki walinzi mkiwapa mapenzi, na hali wamekwishakufuru yaliyokujieni ya haki, wanamfukuza Rasuli pamoja nanyi kwa sababu mmemuamini Allaah Rabb wenu. Mnapotoka kwa ajili ya Jihaad katika Njia Yangu na kutafuta Radhi Zangu mnawapa siri kwa mapenzi, na hali Mimi Najua zaidi yale mnayoyaficha na yale mnayoyadhihirisha. Na yeyote atakayefanya hivyo miongoni mwenu, basi kwa yakini amepotea njia ya sawa.[1]

 

 

 

 

إِن يَثْقَفُوكُمْ يَكُونُوا لَكُمْ أَعْدَاءً وَيَبْسُطُوا إِلَيْكُمْ أَيْدِيَهُمْ وَأَلْسِنَتَهُم بِالسُّوءِ وَوَدُّوا لَوْ تَكْفُرُونَ﴿٢﴾

2. Wakikushindeni watakuwa ni maadui kwenu, na watakunyosheeni mikono yao na ndimi zao kwa uovu, na watatamani lau mngekufuru.

 

 

 

 

لَن تَنفَعَكُمْ أَرْحَامُكُمْ وَلَا أَوْلَادُكُمْ ۚ يَوْمَ الْقِيَامَةِ يَفْصِلُ بَيْنَكُمْ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴿٣﴾

3. Hawatokufaeni jamaa zenu wa uhusiano wa damu wala watoto wenu Siku ya Qiyaamah (Allaah) Atapambanua baina yenu. Na Allaah kwa yale myatendayo Ni Mwenye Kuona.[2]

 

 

 

 

قَدْ كَانَتْ لَكُمْ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ فِي إِبْرَاهِيمَ وَالَّذِينَ مَعَهُ إِذْ قَالُوا لِقَوْمِهِمْ إِنَّا بُرَءَآؤُاْ مِنكُمْ وَمِمَّا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ كَفَرْنَا بِكُمْ وَبَدَا بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةُ وَالْبَغْضَاءُ أَبَدًا حَتَّىٰ تُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ وَحْدَهُ إِلَّا قَوْلَ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ لَأَسْتَغْفِرَنَّ لَكَ وَمَا أَمْلِكُ لَكَ مِنَ اللَّـهِ مِن شَيْءٍ ۖ رَّبَّنَا عَلَيْكَ تَوَكَّلْنَا وَإِلَيْكَ أَنَبْنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ﴿٤﴾

4. Kwa yakini mna kigezo kizuri kwa Ibraahiym na wale walio pamoja naye, walipowaambia watu wao: Hakika sisi tumejitenga nanyi na yale mnayoyaabudu badala ya Allaah, tunakukanusheni, na umedhihirika baina yetu na baina yenu uadui na bughudha ya kudumu milele mpaka mumuamini Allaah Pekee. Isipokuwa kauli ya Ibraahiym kwa baba yake: Nitakuombea kwa hakika maghfirah[3], na wala sikumilikii chochote kile mbele ya Allaah. Rabb wetu! Tumetawakali Kwako, na Kwako Tunarudia kutubia, na Kwako ni mahali pa kuishia.[4]

 

 

 

 

رَبَّنَا لَا تَجْعَلْنَا فِتْنَةً لِّلَّذِينَ كَفَرُوا وَاغْفِرْ لَنَا رَبَّنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴿٥﴾

5. Rabb wetu! Usitujaalie kuwa mtihani kwa wale waliokufuru, na Tughufurie Rabb wetu. Hakika Wewe Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

 

لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِيهِمْ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ ۚ وَمَن يَتَوَلَّ فَإِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ﴿٦﴾

6. Kwa yakini imekuwa kwenu kigezo kizuri katika mwenendo wao kwa mwenye kumtaraji Allaah na Siku ya Mwisho. Na yeyote atakayekengeuka, basi hakika Allaah Ndiye Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote.

 

 

 

 

عَسَى اللَّـهُ أَن يَجْعَلَ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَ الَّذِينَ عَادَيْتُم مِّنْهُم مَّوَدَّةً ۚ وَاللَّـهُ قَدِيرٌ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٧﴾

7. Asaa Allaah Akajaalia mapenzi baina yenu na baina ya wale mlio na uadui nao. Na Allaah Ni Muweza wa yote, na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

 

لَّا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ أَن تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ﴿٨﴾

8. Allaah Hakukatazeni kuwafanyia wema na uadilifu wale wasiokupigeni vita katika Dini, na wala hawakukutoeni kutoka majumbani mwenu. Hakika Allaah Anapenda wafanyao uadilifu.[5]

 

 

 

 

إِنَّمَا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ قَاتَلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَأَخْرَجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ وَظَاهَرُوا عَلَىٰ إِخْرَاجِكُمْ أَن تَوَلَّوْهُمْ ۚ وَمَن يَتَوَلَّهُمْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴿٩﴾

9. Hakika Allaah Anakukatazeni tu kuhusu wale waliokupigeni vita katika Dini, na wakakutoeni kutoka majumbani mwenu, na wakasaidiana juu ya kukutoeni ndio msifanye urafiki nao. Na yeyote atakayewafanya marafiki, basi hao ndio madhalimu.

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا جَاءَكُمُ الْمُؤْمِنَاتُ مُهَاجِرَاتٍ فَامْتَحِنُوهُنَّ ۖ اللَّـهُ أَعْلَمُ بِإِيمَانِهِنَّ ۖ فَإِنْ عَلِمْتُمُوهُنَّ مُؤْمِنَاتٍ فَلَا تَرْجِعُوهُنَّ إِلَى الْكُفَّارِ ۖ لَا هُنَّ حِلٌّ لَّهُمْ وَلَا هُمْ يَحِلُّونَ لَهُنَّ ۖ وَآتُوهُم مَّا أَنفَقُوا ۚ وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ أَن تَنكِحُوهُنَّ إِذَا آتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ ۚ وَلَا تُمْسِكُوا بِعِصَمِ الْكَوَافِرِ وَاسْأَلُوا مَا أَنفَقْتُمْ وَلْيَسْأَلُوا مَا أَنفَقُوا ۚ ذَٰلِكُمْ حُكْمُ اللَّـهِ ۖ يَحْكُمُ بَيْنَكُمْ ۚ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ﴿١٠﴾

10. Enyi walioamini! Wanapokujieni Waumini wa kike waliohajiri basi wajaribuni. Allaah Ni Mjuzi zaidi wa iymaan zao. Kisha mkiwatambua kuwa ni Waumini basi msiwarejeshe kwa makafiri. Wao si wake halaal kwao, na wala wao waume hawahalaliki kwao. Na wapeni (makafiri mahari) waliyotoa. Na wala si dhambi kufunga nao nikaah mkiwapa mahari yao. Na wala msiwaweke wanawake makafiri katika fungamano la ndoa. Na takeni mlichotoa (katika mahari), nao watake walichotoa. Hiyo ndio Hukumu ya Allaah, Anahukumu baina yenu. Na Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote.[6]

 

 

 

 

وَإِن فَاتَكُمْ شَيْءٌ مِّنْ أَزْوَاجِكُمْ إِلَى الْكُفَّارِ فَعَاقَبْتُمْ فَآتُوا الَّذِينَ ذَهَبَتْ أَزْوَاجُهُم مِّثْلَ مَا أَنفَقُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي أَنتُم بِهِ مُؤْمِنُونَ﴿١١﴾

11. Na kama akikutorokeni yeyote kati ya wake zenu kurejea kwa makafiri kisha ikatokea kuwa mmelipiza mkashinda na kupata ngawira, basi wapeni wale walioondokewa na wake zao mfano wa walichotoa (mahari), na mcheni Allaah Ambaye nyinyi mnamuamini.

 

 

 

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا جَاءَكَ الْمُؤْمِنَاتُ يُبَايِعْنَكَ عَلَىٰ أَن لَّا يُشْرِكْنَ بِاللَّـهِ شَيْئًا وَلَا يَسْرِقْنَ وَلَا يَزْنِينَ وَلَا يَقْتُلْنَ أَوْلَادَهُنَّ وَلَا يَأْتِينَ بِبُهْتَانٍ يَفْتَرِينَهُ بَيْنَ أَيْدِيهِنَّ وَأَرْجُلِهِنَّ وَلَا يَعْصِينَكَ فِي مَعْرُوفٍ ۙ فَبَايِعْهُنَّ وَاسْتَغْفِرْ لَهُنَّ اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿١٢﴾

12. Ee Nabiy! Wakikujia Waumini wa kike kuahidiana nawe ahadi ya utiifu kwamba hawatomshirikisha Allaah na chochote, wala hawatoiba, wala hawatozini, wala hawataua watoto wao, wala hawatoleta usingiziaji wa kashfa walioizua baina ya mikono yao na miguu yao[7], na wala hawatakuasi katika mema, basi pokea ahadi yao ya utiifu, na waombee maghfirah kwa Allaah. Hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَوَلَّوْا قَوْمًا غَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ قَدْ يَئِسُوا مِنَ الْآخِرَةِ كَمَا يَئِسَ الْكُفَّارُ مِنْ أَصْحَابِ الْقُبُورِ﴿١٣﴾

13. Enyi walioamini! Msiwafanye marafiki watu ambao Allaah Amewaghadhibikia, wamekwishakata tamaa na (kheri za) Aakhirah kama walivyokwishakata tamaa makafiri na watu wa makaburini.[8] 

 

[2] Ndugu Wa Uhusiano Wa Damu Hautamfaa Ndugu Siku Ya Qiyaamah:

 

Undugu wa uhusiano wa damu hauwezi kumfaa nduguye mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

Rejea Hadiyth inayohusiana na kuteremshwa kwa Aayah ya Suwrah Ash-Shu’araa:

 

وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ ﴿٢١٤﴾

Na onya (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) jamaa zako wa karibu. [Ash-Shu’araa (26:214)]

 

ambayo inathibitisha kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwaonya ahli zake waokoe nafsi zao, kwa sababu yeye hatoweza kuwafaa kitu mbele ya Allaah Siku ya Qiyaamah.    

 

Na pia Hadiyth ifuatayo imethibitisha kuwa hata wazazi makafiri hawawezi kunufaishana na wana wao walioamini mbele ya Allaah Siku ya Qiyaamah kwa kuwa makafiri watakuwa motoni:

 

حَدَّثَنَا أَبُو بَكْرِ بْنُ أَبِي شَيْبَةَ، حَدَّثَنَا عَفَّانُ، حَدَّثَنَا حَمَّادُ بْنُ سَلَمَةَ، عَنْ ثَابِتٍ، عَنْ أَنَسٍ، أَنَّ رَجُلاً، قَالَ يَا رَسُولَ اللَّهِ أَيْنَ أَبِي قَالَ ‏"‏ فِي النَّارِ ‏"‏ ‏.‏ فَلَمَّا قَفَّى دَعَاهُ فَقَالَ ‏"‏ إِنَّ أَبِي وَأَبَاكَ فِي النَّارِ ‏"‏ ‏.‏

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Mtu mmoja alimuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): Je baba yangu yuko wapi? Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akajibu: “Yuko motoni.” (Yule mtu) alipogeuka, Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwita na kumwambia: “Hakika baba yangu na baba yako wako motoni.” [Muslim]

 

Rejea Al-Hujuraat (49:13), Al-Mujaadalah (58:22) kwenye faida kadhaa na rejea zake.

 

[7] Usingiziaji Wa Kashfa Baina Ya Mikono Na Miguu Yao:

 

‘Ulamaa wengi wamekubaliana kwamba ni mke kumpachikia au kumnasibishia mumewe mtoto wa zinaa toka kwa mwanaume mwingine.

 

[8] Maana Ya Kama Walivyokwishakata Tamaa Makafiri Na Watu Wa Makaburini:

 

Kauli za Mufassiruna kuhusu ya Allaah (سبحانه وتعالى):

كَمَا يَئِسَ الْكُفَّارُ مِنْ أَصْحَابِ الْقُبُورِ﴿١٣﴾

“Kama walivyokwishakata tamaa makafiri na watu wa makaburini.”

 

Imaam As-Sa’diy:

 

i- Watakapofika Aakhirah wakatambua uhakika wa jambo hilo na wakajua kwa yakini kwamba wamenyimwa kheri za Aakhirah hivyo hawana sehemu yake.

 

ii-Wameikanusha Aakhirah na kuikataa, basi kwa hali yao hiyo, haishangazi kuwaona wakikimbilia kwenye mambo yenye kumghadhibisha Allaah na kulazimisha Adhabu Yake na wakikata tamaa ya Aakhirah, kama walivyokata tamaa makafiri wanaokadhibisha kufufuliwa hapa duniani ya kurejea watu wa makaburini kwa Allaah (سبحانه وتعالى).  [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Imaam Ibn Kathiyr:

 

i-Makafiri walio hai wamekata tamaa ya kukutana na jamaa zao waliozikwa makaburini kwa sababu hawaamini ufufuo au kufufuliwa. Kwa hiyo kutokana na itikadi zao, hawana tena matumaini kwamba watakutana nao tena.

 

Na Hasan Al-Baswriy amesema: Makafiri walio hai wamekata tamaa na wafu.

 

Qataadah na Adhw-Dhwahaak wamesema: (Wamekata tamaa) wawarudie kwao watu wa waliofariki wakawa makaburini.

 

ii- Kama vile makafiri waliozikwa makaburini wamekata matumaini ya kupata aina yoyote ya kheri (yaani, baada ya kuiona adhabu na kujua kwamba Qiyaamah ni kweli).

 

Al-A’mash amesimulia kutoka kwa Abuu Adhw-Dwuhaa kutoka kwa Masruwq kwamba Ibn Mas’wud amesema:  “Vile kafiri huyu alivyokata tamaa baada ya kufariki na akaona malipo yake (ya kufru, na maovu yake).” Amesema Mujaahid, ‘Ikrimah, Muqaatil, Ibn Zayd, Al-Kalbiy na Manswur. Ibn Jariyr ameiwafiki kauli hii.

 

 

 

 

Share