068 - Al-Qalam

 

   الْقَلَم

 

068-Al-Qalam

 

068-Al-Qalam: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

 

ن ۚ وَالْقَلَمِ وَمَا يَسْطُرُونَ﴿١﴾

1. Nuwn.[1] Naapa kwa kalamu [2]na yale wayaandikayo.

 

 

 

 

مَا أَنتَ بِنِعْمَةِ رَبِّكَ بِمَجْنُونٍ﴿٢﴾

2. Kwa Neema ya Rabb wako, wewe (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) si majnuni.[3]

 

 

 

 

وَإِنَّ لَكَ لَأَجْرًا غَيْرَ مَمْنُونٍ﴿٣﴾

3. Na hakika wewe bila shaka una ujira usiokatika.[4]

 

 

 

وَإِنَّكَ لَعَلَىٰ خُلُقٍ عَظِيمٍ﴿٤﴾

4. Na hakika wewe uko juu ya kiwango adhimu cha tabia njema.[5]

 

 

 

 

فَسَتُبْصِرُ وَيُبْصِرُونَ﴿٥﴾

5. Basi hivi karibuni utaona, na wao wataona.

 

 

 

 

بِأَييِّكُمُ الْمَفْتُونُ﴿٦﴾

6. Ni nani kati yenu aliyesibiwa na uwendawazimu.

 

 

 

 

إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ﴿٧﴾

7. Hakika Rabb wako Yeye Anamjua zaidi aliyepotea Njia Yake, Naye Anawajua zaidi walioongoka.

 

 

 

 

فَلَا تُطِعِ الْمُكَذِّبِينَ﴿٨﴾

8. Basi usiwatii wanaokadhibisha.

 

 

 

 

وَدُّوا لَوْ تُدْهِنُ فَيُدْهِنُونَ﴿٩﴾

9. Wanatamani lau kama ungelilegeza nao pia walegeze.

 

 

 

 

وَلَا تُطِعْ كُلَّ حَلَّافٍ مَّهِينٍ﴿١٠﴾

10. Na wala usimtii kila mwingi wa kuapa, dhalili.[6]

 

 

 

 

هَمَّازٍ مَّشَّاءٍ بِنَمِيمٍ﴿١١﴾

11. Mwingi wa kudharau na kukashifu, mpitaji huku na kule kufitinisha.[7]

 

 

 

 

مَّنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ أَثِيمٍ﴿١٢﴾

12. Mwingi wa kuzuia ya kheri, mwenye kutaadi, mwingi wa kutenda dhambi.

 

 

 

 

عُتُلٍّ بَعْدَ ذَٰلِكَ زَنِيمٍ﴿١٣﴾

13. Msusuwavu mtumiaji nguvu[8], na baada ya hivyo ni mwenye kujipachika tu kabila.

 

 

 

 

أَن كَانَ ذَا مَالٍ وَبَنِينَ﴿١٤﴾

14. Kwa kuwa ana mali na watoto?[9]

 

 

 

 

إِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِ آيَاتُنَا قَالَ أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ﴿١٥﴾

15. Anaposomewa Aayaat Zetu, anasema: Hekaya za watu wa kale.

 

 

 

 

سَنَسِمُهُ عَلَى الْخُرْطُومِ﴿١٦﴾

16. Tutamtia chapa juu ya pua yake.

 

 

 

 

إِنَّا بَلَوْنَاهُمْ كَمَا بَلَوْنَا أَصْحَابَ الْجَنَّةِ إِذْ أَقْسَمُوا لَيَصْرِمُنَّهَا مُصْبِحِينَ﴿١٧﴾

17. Hakika Sisi Tumewajaribu (Maquraysh) kama Tulivyowajaribu watu wa shamba pale walipoapa kuwa bila shaka watayavuna (mazao yake) watakapopambaukiwa asubuhi.[10]

 

 

 

وَلَا يَسْتَثْنُونَ﴿١٨﴾

18. Na wala hawakusema In-Shaa Allaah.  

 

 

 

 

فَطَافَ عَلَيْهَا طَائِفٌ مِّن رَّبِّكَ وَهُمْ نَائِمُونَ﴿١٩﴾

19. Basi (shamba lao) likazungukwa na chenye kuzunguka (moto) kutoka kwa Rabb wako na hali wao wamelala.

 

 

 

 

فَأَصْبَحَتْ كَالصَّرِيمِ﴿٢٠﴾

20. Likawa kama lilovunwa likabakishwa majivu meusi.

 

 

 

 

فَتَنَادَوْا مُصْبِحِينَ﴿٢١﴾

21. Wakaitana, walipopambaukiwa asubuhi.

 

 

 

 

أَنِ اغْدُوا عَلَىٰ حَرْثِكُمْ إِن كُنتُمْ صَارِمِينَ﴿٢٢﴾

22. Kwamba nendeni asubuhi mapema shambani mwenu, mkiwa mnataka kuvuna.

 

 

 

 

فَانطَلَقُوا وَهُمْ يَتَخَافَتُونَ﴿٢٣﴾

23. Wakatoka na huku wanakwenda kimya kimya wakinong’onezana.

 

 

 

 

أَن لَّا يَدْخُلَنَّهَا الْيَوْمَ عَلَيْكُم مِّسْكِينٌ﴿٢٤﴾

24. Kwamba: Asikuingilieni humo kwa hali yoyote leo masikini.

 

 

 

 

وَغَدَوْا عَلَىٰ حَرْدٍ قَادِرِينَ﴿٢٥﴾

25. Wakatoka asubuhi mapema kwa kusudio la nguvu, wakidhani wana uwezo (wa kuwazuia maskini).

 

 

 

 

فَلَمَّا رَأَوْهَا قَالُوا إِنَّا لَضَالُّونَ﴿٢٦﴾

26. Basi walipoliona wakasema: Hakika sisi bila shaka Tumepotea.

 

 

 

 

بَلْ نَحْنُ مَحْرُومُونَ﴿٢٧﴾

27. (Walivyotanabahi!): Bali sisi tumenyimwa!

 

 

 

 

قَالَ أَوْسَطُهُمْ أَلَمْ أَقُل لَّكُمْ لَوْلَا تُسَبِّحُونَ﴿٢٨﴾

28. Mbora wao akasema: Je, sikukuambieni kuwa angalau hata museme Subhaana Allaah (au In-Shaa Allaah)!

 

 

 

 

قَالُوا سُبْحَانَ رَبِّنَا إِنَّا كُنَّا ظَالِمِينَ﴿٢٩﴾

29. Wakasema: Subhaana Rabbinnaa! Ametakasika Mola wetu! Hakika sisi tulikuwa madhalimu.

 

 

 

 

فَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَلَاوَمُونَ﴿٣٠﴾

30. Wakakabiliana wenyewe kwa wenyewe wakilaumiana.

 

 

 

 

قَالُوا يَا وَيْلَنَا إِنَّا كُنَّا طَاغِينَ﴿٣١﴾

31. Wakasema: Ole wetu! Hakika sisi tumekuwa warukao mipaka.

 

 

 

 

عَسَىٰ رَبُّنَا أَن يُبْدِلَنَا خَيْرًا مِّنْهَا إِنَّا إِلَىٰ رَبِّنَا رَاغِبُونَ﴿٣٢﴾

32. Asaa Rabb wetu Akatubadilishia lililo bora kuliko hilo. Hakika sisi tuna raghba kuelekea kwa Rabb wetu.

 

 

 

 

كَذَٰلِكَ الْعَذَابُ ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَكْبَرُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ﴿٣٣﴾

33. Hivyo ndivyo adhabu. Na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni kubwa zaidi lau wangelikuwa wanajua.

 

 

 

 

إِنَّ لِلْمُتَّقِينَ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتِ النَّعِيمِ﴿٣٤﴾

34. Hakika wenye taqwa watapata kwa Rabb wao Jannaat za neema.

 

 

 

 

أَفَنَجْعَلُ الْمُسْلِمِينَ كَالْمُجْرِمِينَ﴿٣٥﴾

35. Je, Tuwafanye Waislamu (watiifu) sawa kama wahalifu?

 

 

 

 

مَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ﴿٣٦﴾

36. Mna nini! Vipi mnahukumu?

 

 

 

 

أَمْ لَكُمْ كِتَابٌ فِيهِ تَدْرُسُونَ﴿٣٧﴾

37.  Au mna Kitabu mnachodurusu humo?

 

 

 

 

إِنَّ لَكُمْ فِيهِ لَمَا تَخَيَّرُونَ﴿٣٨﴾

38.  Ambapo humo mnapata mnachopendelea?

 

 

 

 

أَمْ لَكُمْ أَيْمَانٌ عَلَيْنَا بَالِغَةٌ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ ۙ إِنَّ لَكُمْ لَمَا تَحْكُمُونَ﴿٣٩﴾

39. Au mnazo ahadi za viapo juu Yetu zinazofikia mpaka Siku ya Qiyaamah, kwamba mtapata mnayojihukumia?

 

 

 

 

سَلْهُمْ أَيُّهُم بِذَٰلِكَ زَعِيمٌ﴿٤٠﴾

40. Waulize (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Ni nani kati yao mdhamini wa hayo?

 

 

 

 

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ فَلْيَأْتُوا بِشُرَكَائِهِمْ إِن كَانُوا صَادِقِينَ﴿٤١﴾

41. Au wana washirika? Basi wawalete washirika wao wakiwa wakweli.

 

 

 

 

يَوْمَ يُكْشَفُ عَن سَاقٍ وَيُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ فَلَا يَسْتَطِيعُونَ﴿٤٢﴾

42. Siku utakapofunuliwa Muundi na wataitwa kusujudu lakini hawatoweza.[11]

 

 

 

 

 

خَاشِعَةً أَبْصَارُهُمْ تَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ ۖ وَقَدْ كَانُوا يُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ وَهُمْ سَالِمُونَ﴿٤٣﴾

43. Macho yao yatainama chini, udhalilifu utawafunika. Na hali walikuwa wakiitwa wasujudu (kuswali duniani) walipokuwa wazima wa afya.

 

 

 

 

فَذَرْنِي وَمَن يُكَذِّبُ بِهَـٰذَا الْحَدِيثِ ۖ سَنَسْتَدْرِجُهُم مِّنْ حَيْثُ لَا يَعْلَمُونَ﴿٤٤﴾

44. Basi Niache (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na anayekadhibisha Qur-aan hii. Tutawavuta pole pole adhabuni kwa namna wasiyoijua.

 

 

 

 

وَأُمْلِي لَهُمْ ۚ إِنَّ كَيْدِي مَتِينٌ﴿٤٥﴾

45. Nami Ninawapa muhula. Hakika mpango Wangu ni thabiti.

 

 

 

 

أَمْ تَسْأَلُهُمْ أَجْرًا فَهُم مِّن مَّغْرَمٍ مُّثْقَلُونَ﴿٤٦﴾

46. Au unawaomba ujira (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi wao zimewawia uzito gharama zake?

 

 

 

 

أَمْ عِندَهُمُ الْغَيْبُ فَهُمْ يَكْتُبُونَ﴿٤٧﴾

47. Au wanayo (ilimu) ya ghaibu, basi wao wanaandika?

 

 

 

 

فَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ وَلَا تَكُن كَصَاحِبِ الْحُوتِ إِذْ نَادَىٰ وَهُوَ مَكْظُومٌ﴿٤٨﴾

48. Basi subiri (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa hukumu ya Rabb wako, na wala usiwe kama swahibu wa samaki (Nabiy Yuwnus) pale aliponadi (kutuomba) naye akiwa amebanwa na dhiki.[12]

 

 

 

 

لَّوْلَا أَن تَدَارَكَهُ نِعْمَةٌ مِّن رَّبِّهِ لَنُبِذَ بِالْعَرَاءِ وَهُوَ مَذْمُومٌ﴿٤٩﴾

49. Lau isingelimfikia neema kutoka kwa Rabb wake, bila shaka angelitupwa ufukoni mtupu akiwa mwenye kulaumiwa.

 

 

 

 

فَاجْتَبَاهُ رَبُّهُ فَجَعَلَهُ مِنَ الصَّالِحِينَ﴿٥٠﴾

50.  Na Rabb wake Akamteua na Akamjaalia miongoni mwa Swalihina.

 

 

 

 

وَإِن يَكَادُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَيُزْلِقُونَكَ بِأَبْصَارِهِمْ لَمَّا سَمِعُوا الذِّكْرَ وَيَقُولُونَ إِنَّهُ لَمَجْنُونٌ﴿٥١﴾

51. Na wale waliokufuru hukaribia bila shaka kukutelezesha kwa macho yao (ya uhasidi)[13] wanaposikia Ukumbusho, na wanasema: Hakika yeye bila shaka ni majnuni.[14]

 

 

 

 

وَمَا هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِّلْعَالَمِينَ﴿٥٢﴾

52. Na haikuwa (hii Qur-aan) isipokuwa ni ukumbusho kwa walimwengu.

 

 

 

 

[1] الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):

 

Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).

 

[2] Kalamu Ni Kitu Cha Kwanza Kuumbwa:

 

Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:

 إِنَّ أَوَّلَ مَا خَلَقَ اَللَّهُ تَعَالَى الْقَلَمَ فَقَالَ لَهُ:  اُكْتُبْ! فَجَرَى فِي تِلْكَ اَلسَّاعَةِ بِمَا هُوَ كَائِنٌ إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ  

“Kitu cha mwanzo Allaah kukiumba ni kalamu. Akaiambia: Andika! Na katika saa hiyo, (yakaandikwa) yote yatakayotokea mpaka Siku ya Qiyaamah.” [Ahmad, At-Tirmidhiy]

 

[3] Allaah (سبحانه وتعالى) Anamliwaza Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) Kuhusu Kusingiziwa Sifa Ovu Na Washirikina Wa Makkah:

 

Kuanzia Aayah hii namba (2) na kuendelea hadi namba (15), Allaah (سبحانه وتعالى) Anamliwaza Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kuthibitisha fadhila na khulqa zake adhimu, na pia kwa kumuamuru asiwatii makafiri wa Makkah ambao wao ndio wenye sifa mbalimbali ovu, na ambao walimtaka Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) anyamaze asibalighishe Risala Yake, na asikataze kuabudiwa masanamu yao. Basi wakampachika Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) sifa ovu kadhaa. Rejea Al-Furqaan (25:4) kwenye uchambuzi wa hayo na rejea mbalimbali.

 

[4] Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Ana Ujira Usiokatika:

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kupata faida:

 

33-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Ana Ujira Usiokatika Anasifika Na Maarufu Mno

 

[5] Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kupata faida tele:

 

Sifa-Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

[6] Makatazo Ya Kuapa Ovyo Ovyo:

 

Rejea Al-Baqarah (2:225), Al-Maaidah (5:89).

 

[8] Msusuwavu Mtumiaji Nguvu (Na Mwenye Kutakabari Mjeuri) Wameahidiwa Moto:

 

حَدَّثَنَا مُحَمَّدُ بْنُ كَثِيرٍ، أَخْبَرَنَا سُفْيَانُ، حَدَّثَنَا مَعْبَدُ بْنُ خَالِدٍ الْقَيْسِيُّ، عَنْ حَارِثَةَ بْنِ وَهْبٍ الْخُزَاعِيِّ، عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ ‏ "‏ أَلاَ أُخْبِرُكُمْ بِأَهْلِ الْجَنَّةِ، كُلُّ ضَعِيفٍ مُتَضَاعِفٍ، لَوْ أَقْسَمَ عَلَى اللَّهِ لأَبَرَّهُ، أَلاَ أُخْبِرُكُمْ بِأَهْلِ النَّارِ كُلُّ عُتُلٍّ جَوَّاظٍ مُسْتَكْبِرٍ ‏"‏‏.‏

 

Amesimulia Haarithah Bin Wahb Al-Khuzaa‘iyy (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Je, niwajulishe nyinyi watu wa Jannah? Kila mnyonge na mwenye kunyongeshwa, lau atakula yamini kwa Allaah basi atakubaliwa. Je, niwapashe khabari ya watu wa motoni? Kila msusuwavu mtumiaji nguvu, mwenye kutakabari mjeuri.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

[9] Matajiri Wa Makkah Waliomkadhibisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Na Risala:

 

Aayah hizi zimeteremshwa kuhusu baadhi ya washirikina kama Waliyd bin Mughiyrah na wengineo [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[10] Kisa Cha Watu Wa Shamba Waliozuia Maskini Wasiingie Shambani Kupata Swadaqa Ya Mazao:

 

Kuanzia Aayah hii namba (17) hadi namba (33), kinazungumzwa kisa cha watu wa shamba kama alivyoelezea Imaam Ibn Kathiyr katika Tafsiyr yake:

 

Baadhi ya Salaf wametaja kuwa hawa walikuwa ni watu kutoka Yemen. Said Bin Jubayr amesema: Walikuwa ni watu kutoka kijiji kilichoitwa Dhwarwaan ambacho kilikuwa ni maili sita kutoka (mji wa) Sanaa (uliko Yemen).  Imesemwa pia kuwa: Walikuwa ni watu kutoka Habasha (Ethiopea) ambao baba yao aliwaachia shamba na walikuwa ni Ahlul-Kitaab. Baba yao alikuwa akilishughulikia shamba kwa njia nzuri. Alichokivuna, alikuwa akirudishia katika shamba kukidhi mahitaji yake, na hubakisha kinginecho kama ni chakua kwa ahli zake cha kuwatosheleza mwaka, na akitolea swadaqa chochote kilichozidi (katika mazao).  Alipofariki, watoto wake wakarithi shamba hilo huku wakasema: Hakika baba yetu alikuwa mjinga kugawa mazao ya shamba kwa mafaqiri. Lakini sisi tukiwazua shambani tutapata zaidi. Basi walipoazimia kufanya hivyo, wakaadhibiwa kinyume na niyya yao, basi Allaah Akaondoshea walichokuwa nacho mikononi mwao, mtaji, faida na swadaqa, hivyo kukawa hakuna chochote kilishosalia kwao. Ndipo Allaah (سبحانه وتعالى) Akasema katika Aayah ya mwisho kumalizikia kisa hiki:

 

كَذَٰلِكَ الْعَذَابُ ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَكْبَرُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ﴿٣٣﴾

“Hivyo ndivyo adhabu. Na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni kubwa zaidi lau wangelikuwa wanajua.”

 

Yaani: Hiyo ni adhabu kwa yeyote anayepinga Amri za Allaah, na anayefanya ubakhili katika neema alizojaaliwa na Allaah, akanyima haki za masikini na mafaqiri na kubadilisha neema za Allaah kwa kufru. Basi,

 

وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَكْبَرُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ﴿٣٣﴾

“Na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni kubwa zaidi lau wangelikuwa wanajua.”

 

Yaani: Hii ni adhabu ya duniani kama mlivyosikia. Na adhabu ya Aakhirah ni ya mashaka zaidi. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Kisa hiki kinawafunza na kuwashajiisha Waumini waliojaaliwa neema yoyote ile, iwe neema ya mali, ya watoto, ya siha na afya, ya kila kiungo cha mwili wa mwanaadam, ya nguvu, ya akili na ya busara na kadhaalika, kwamba watumie neema hizo katika ya kumridhisha Allaah (عزّ وجلّ), na si kiyume chake. Na katika neema ya mali, ni kuitolea haki yake ya Zakaah na swadaqa katika wanachokivuna au wanachokichuma.

 

Kisa kinginecho cha utoaji wa swadaqa ya mavuno ya shamba ni kama kilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:

 

 عن أَبي هريرة رضي الله عنه ، عن النبيِّ صلى الله عليه وسلم ، قَالَ : (( بَيْنَمَا رَجُلٌ يَمْشِي بِفَلاَةٍ مِنَ الأَرْضِ ، فَسَمِعَ صَوْتاً في سَحَابَةٍ ، اسقِ حَدِيقَةَ فُلانٍ ، فَتَنَحَّى ذَلِكَ السَّحَابُ فَأفْرَغَ مَاءهُ في حَرَّةٍ ، فإِذَا شَرْجَةٌ مِنْ تِلْكَ الشِّرَاجِ قَدِ اسْتَوْعَبَت ذَلِكَ الماءَ كُلَّهُ ، فَتَتَبَّعَ المَاءَ ، فإذَا رَجُلٌ قَائمٌ في حَدِيقَتِهِ يُحَوِّلُ الماءَ بِمسحَاتِهِ، فَقَالَ لَهُ : يَا عَبْدَ اللهِ، ما اسمُكَ ؟ قال : فُلانٌ للاسم الذي سَمِعَ في السَّحابةِ ، فقال له : يا عبدَ الله ، لِمَ تَسْألُنِي عَنِ اسْمِي ؟ فَقَالَ : إنِّي سَمِعْتُ صَوتْاً في السَّحابِ الَّذِي هَذَا مَاؤُهُ ، يقولُ : اسْقِ حَدِيقَةَ فُلاَنٍ لاسمِكَ ، فَمَا تَصْنَعُ فِيهَا ، فَقَالَ : أمَا إذ قلتَ هَذَا ، فَإنِّي أنْظُرُ إِلَى مَا يَخْرُجُ مِنْهَا ، فَأتَصَدَّقُ بِثُلُثِهِ، وَآكُلُ أنَا وَعِيَالِي ثُلُثاً، وَأردُّ فِيهَا ثُلُثَهُ )) رواه مسلم .

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: "Mtu alipokuwa anatembea jangwani, alisikia sauti katika wingu (ikisema): Nyweshea shamba la   fulani! Wingu hilo likakaribia na kumimina maji yake kwenye ardhi ya mawe. Maji hayo yakaenea katika kijito na kumiminika katika hodhi kubwa. Akafuata maji akamuona mtu amesimama ndani ya shamba lile anagawa maji kwa jembe lake. Akamwambia: Ee mja wa Allaah, jina lako nani? Akasema: Fulani. Akataja jina ambalo amelisikia katika wingu. Akamwambia: Ee mja wa Allaah! Kwa nini unaniuliza jina langu? Akasema: Nimesikia sauti katika wingu ambalo haya ndio maji yake ikisema: Nyweshea shamba la fulani kwa jina lako. Je, unafanya nini katika hili? Akasema: Kwa sababu umeniuliza hili, basi (nakujuilsha kwamba), mimi naangalia kinachotoka humo, na kutoa swadaqa thuluthi, na thuluthi nakula pamoja na ahli wangu, na narudisha humo (shambani) thuluthi yake.” [Muslim]

 

Hakika katika visa viwili hivyo kuna mafunzo yafuatayo:

 

(i) Neema zote anazojaaliwa mtu, zinatoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى), na mtu hana uwezo wa kuzipata bila ya Tawfiyq ya Allaah (عزّ وجلّ). Kauli Yake Allaah (عزّ وجلّ):

 

وَمَا بِكُم مِّن نِّعْمَةٍ فَمِنَ اللَّـهِ

Na Neema yoyote mliyo nayo, basi ni kutoka kwa Allaah. [An-Nahl (16:53)]

 

ii-Kutoa swadaqa katika neema alizojaaliwa mtu na Allaah (عزّ وجلّ), ni katika shukurani, na kinyume chake ni kuikufuru neema hiyo. Na kila mtu anapotoa katika neema Aliyomjaalia Allaah, basi Allaah (عزّ وجلّ) Humzidishia kama Anavyosema:

 

وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ﴿٧﴾

Na pindi Alipotangaza Rabb wenu: Ikiwa mtashukuru, bila shaka Nitakuzidishieni (Neema Zangu), na mkikufuru, basi hakika Adhabu Yangu ni kali. [Ibraahiym (14:7)]

 

Basi Tanabahi kisa cha mtu ambaye alikuwa akitoa swadaqa thuluthi ya mazao ya shambani mwake, kisha Allaah Akamnyeshewa mvua katika shamba lake bila ya yeye kuhangaika kutafuta maji au kuyagharimia!

 

 

iii-Kuikufuru neema ya Allaah kwa kutokuitendea haki inasababisha maangamizi toka kwa Allaah:

 

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ بَدَّلُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ كُفْرًا وَأَحَلُّوا قَوْمَهُمْ دَارَ الْبَوَارِ﴿٢٨﴾

Je, huoni wale waliobadilisha Neema ya Allaah kwa kufru, na wakawafikisha watu wao nyumba ya mateketezo? [Ibraahiym (14:28)]

 

vi-Kuwagaia vyakula mafuqara, masikini na wahitaji ni katika himizo la Allaah (سبحانه وتعالى) na jambo hili lina fadhila na malipo adhimu kutoka kwa Allaah (عزّ وجلّ) kama Anavyosema katika Kauli Zake:

 

وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا﴿٨﴾ إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّـهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا﴿٩﴾

Na wanalisha chakula, juu ya kuwa wao wanakipenda, masikini na mayatima na mateka. Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya Wajihi wa Allaah, hatukusudii kutoka kwenu jazaa wala shukurani. [Al-Insaan (76:8-9)]

 

Na Anaonya wasiofanya hima kulisha mafuqara, masikini na wahitaji hao:

 

وَلَا تَحَاضُّونَ عَلَىٰ طَعَامِ الْمِسْكِينِ ﴿١٨﴾

Na wala hamhamasishani katika kulisha maskini. [Al-Fajr (89:18)]

 

Rejea pia Al-Haaqqah (69:34), Al-Maa’uwn (107:3).

 

 

iv-Tahadharisho la mtu kuulizwa Siku ya Qiyaamah, ameitumiaje neema aliyojaaliwa,      Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ ﴿٨﴾

Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema. [At-Takaathur (102:8)]

 

 

v-Allaah (سبحانه وتعالى) Huibadilisha neema pindi mtu anapokosa kuitendea haki:

 

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ لَمْ يَكُ مُغَيِّرًا نِّعْمَةً أَنْعَمَهَا عَلَىٰ قَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ  

Hayo ni kwa kuwa Allaah Hakuwa Mwenye Kubadilisha neema yoyote Aliyoineemesha kwa watu mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao. [Al-Anfaal (8:53)]

 

[11] Siku Utakapofunuliwa Muundi:

 

Itakapofika Siku ya Qiyaamah, yakatokea ya kuwatia watu viwewe na mitetemeko ya ardhi, na hali za vitisho visivyokuwa vya ndoto au dhana za uongo, kisha Akaja Muumba (Allaah) Ahukumu baina ya waja Wake na kuwalipa matendo yao, Atafunua Muundi (Mguu) Wake Mtukufu usiofanana na chochote kile! Na viumbe wakaona Ujalali wa Allaah na Uadhwama Wake usioweza kuelezeka, basi hapo wataitwa kumsujudia Allaah. Waumini waliokuwa wakimsujudia Allaah kwa khiari na kupendelea kwao watasujudu. Ama wahalifu na wanafiki, hao watataka kusujudu lakini hawataweza kamwe! Na migongo yao itakuwa ni kama pembe za ng'ombe. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Na katika Hadiyth:

 

حَدَّثَنَا آدَمُ، حَدَّثَنَا اللَّيْثُ، عَنْ خَالِدِ بْنِ يَزِيدَ، عَنْ سَعِيدِ بْنِ أَبِي هِلاَلٍ، عَنْ زَيْدِ بْنِ أَسْلَمَ، عَنْ عَطَاءِ بْنِ يَسَارٍ، عَنْ أَبِي سَعِيدٍ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ سَمِعْتُ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم يَقُولُ ‏ "‏ يَكْشِفُ رَبُّنَا عَنْ سَاقِهِ فَيَسْجُدُ لَهُ كُلُّ مُؤْمِنٍ وَمُؤْمِنَةٍ، وَيَبْقَى مَنْ كَانَ يَسْجُدُ فِي الدُّنْيَا رِئَاءً وَسُمْعَةً، فَيَذْهَبُ لِيَسْجُدَ فَيَعُودُ ظَهْرُهُ طَبَقًا وَاحِدًا ‏"‏‏.‏

 

Amesimulia Abu Sa’iyd (رضي الله عنه):  Nimemsikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: Rabb wetu Atafunua Muundi Wake, watamsujudia Waumini wote Wanaume na Waumini Wanawake. Kisha watabakia waliokuwa wakisujudu duniani kwa riyaa; kujionyesha kwa ajili ya kutaka kusifiwa na umaarufu. Watu hao watajaribu kusujudu (Siku hiyo ya Qiyaamah), lakini mgongo wa kila mmoja wao utakuwa mgumu kana kwamba ni uti wa mgongo wenye mfupa mmoja (bila ya mgawanyiko wa diski).” [Al-Bukhaariy Kitabu Cha Tafsiyr (65)]

 

[12] Nabiy Yuwnus (عليه السّلام) Alipokuwa Tumboni Mwa Samaki Na Duaa Aliyoiomba:

 

Rejea Al-Anbiyaa (21:87) kwenye duaa ya Nabiy Yuwnus (عليه السّلام) ambayo ni mojawapo wa sababu za kutakabaliwa haja, na pia ni duaa ya kuomba mtu anapopata jana au balaa.

 

Rejea pia Asw-Swaffaat (37:143-144) kwenye maelezo mengineyo kuhusu hali ya Nabiy Yuwnus (عليه السّلام) alipokuwa tumboni mwa Samaki.

 

[13] Jicho Baya La Uhasidi:

 

Washirikina walikuwa wakimtazama Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa jicho baya kutokana na uhasidi wao, wivu, chuki zao. Na hiki ni kwango cha mwisho cha madhara waliyoweza kumfanyia kwani Allaah Amemhifadhi na Amemkinga na kumnusuru [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  amethibitisha kwamba jicho baya linawea kumpata mtu kwa kauli yake:

إِذَا رَأَى أَحَدُكُمْ مِنْ أَخِيهِ أَوْ مِنْ نَفْسِهِ أَوْ مِنْ مَالِهِ مَا يُعْجِبُهُ فَلْيُبَرِّكْهُ فَإِنَّ الْعَيْنَ حَقٌّ

“Mmoja wenu akiona kwa ndugu yake au kwake, au mali yake kinachomfurahisha akiombee baraka kwani kijicho ni haki.” [Hadiyth ya ‘Aamir bin Rabiy’ah na Sahl bin Hunayf (رضي الله عنهما) - Ahmad (4/447), Ibn Maajah [3509], Maalik [1697, 1698] na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (1/212)]

 

Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuacha kutufunza kujikinga na jicho baya. Bonyeza viungo vifuatavyo kupata adhkaar na duaa za kujikinga na jicho baya na faida nyenginezo.

 

125-Hiswnul-Muslim: Du’aa Anayeogopa Kupatwa Na Kijicho

 

048-Hiswnul-Muslim: Du’aa Ya Kuwakinga Watoto

 

Du’aa Za Ruqyah (Kinga) Faida Na Sharh Zake

 

05-Ruqyah Dhidi Ya Uhasidi Na Jicho Baya

 

[14] Washirikina Wa Makkah Kumpachika Sifa Ovu Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

Rejea Al-Furqaan (25:4) kwenye uchambuzi na rejea mbalimbali. 

 

 

 

Share