067 - Al-Mulk

  الْمُلْك

 

067-Al-Mulk

 

 

067-Al-Mulk: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

 

تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿١﴾

 

1. Amebarikika Ambaye Mkononi Mwake umo Ufalme, Naye juu ya kila kitu Ni Muweza.[1]

 

 

 

 

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ﴿٢﴾

2. Ambaye Ameumba mauti na uhai ili Akujaribuni ni nani kati yenu mwenye amali nzuri zaidi. Naye Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa Kughufuria.

 

 

 

 

الَّذِي خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ طِبَاقًا ۖ مَّا تَرَىٰ فِي خَلْقِ الرَّحْمَـٰنِ مِن تَفَاوُتٍ ۖ فَارْجِعِ الْبَصَرَ هَلْ تَرَىٰ مِن فُطُورٍ﴿٣﴾

3. Ambaye Ameumba mbingu saba matabaka. Hutaona katika Uumbaji wa Ar-Rahmaan tofauti yoyote. Basi rejesha jicho. Je, unaona mpasuko wowote ule?

 

 

 

 

ثُمَّ ارْجِعِ الْبَصَرَ كَرَّتَيْنِ يَنقَلِبْ إِلَيْكَ الْبَصَرُ خَاسِئًا وَهُوَ حَسِيرٌ﴿٤﴾

4. Kisha rejesha jicho tena na tena, litakupindukia jicho likiwa limehizika, nalo limenyong’onyea.

 

 

 

 

وَلَقَدْ زَيَّنَّا السَّمَاءَ الدُّنْيَا بِمَصَابِيحَ وَجَعَلْنَاهَا رُجُومًا لِّلشَّيَاطِينِ ۖ وَأَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابَ السَّعِيرِ﴿٥﴾

5. Na kwa yakini Tumeipamba mbingu ya dunia kwa mataa, na Tukazifanya kuwa ni makombora ya kuwavurumishia mashaytwaan,[2] na Tumewaandalia adhabu ya moto uliowashwa vikali mno. 

 

 

 

 

وَلِلَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ عَذَابُ جَهَنَّمَ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ﴿٦﴾

6. Na wale waliomkufuru Rabb wao wana adhabu ya Jahannam. Ni ubaya ulioje mahali pa kuishia! 

 

 

 

 

إِذَا أُلْقُوا فِيهَا سَمِعُوا لَهَا شَهِيقًا وَهِيَ تَفُورُ﴿٧﴾

7. Watakapotupwa humo, watasikia sauti yake mbaya ya kuchukiza mno, nao huku unafoka.

 

 

 

 

تَكَادُ تَمَيَّزُ مِنَ الْغَيْظِ ۖ كُلَّمَا أُلْقِيَ فِيهَا فَوْجٌ سَأَلَهُمْ خَزَنَتُهَا أَلَمْ يَأْتِكُمْ نَذِيرٌ﴿٨﴾

8. Unakaribia kupasuka kwa ghadhabu. Kila wanapotupwa humo kundi, walinzi wake watawauliza: Je, hajakufikieni mwonyaji yeyote? 

 

 

 

 

قَالُوا بَلَىٰ قَدْ جَاءَنَا نَذِيرٌ فَكَذَّبْنَا وَقُلْنَا مَا نَزَّلَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا فِي ضَلَالٍ كَبِيرٍ﴿٩﴾

9. Watasema: Sivyo hivyo! Bali kwa yakini alitujia mwonyaji, lakini tulikadhibisha, na tukasema: Allaah Hakuteremsha kitu chochote, nyinyi si chochote isipokuwa mumo katika upotofu mkubwa.[3]

 

 

 

 

وَقَالُوا لَوْ كُنَّا نَسْمَعُ أَوْ نَعْقِلُ مَا كُنَّا فِي أَصْحَابِ السَّعِيرِ﴿١٠﴾

10. Na watasema: Lau tungelikuwa tunasikiliza au tunatia akilini, tusingelikuwa katika watu wa motoni. 

 

 

 

 

فَاعْتَرَفُوا بِذَنبِهِمْ فَسُحْقًا لِّأَصْحَابِ السَّعِيرِ﴿١١﴾

11. Basi watakiri madhambi yao, na (wataambiwa): Tokomeeni mbali watu wa motoni. 

 

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُم بِالْغَيْبِ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ﴿١٢﴾

12. Hakika wale wanaomkhofu Rabb wao wakiwa pweke mbali na macho ya watu, watapata maghfirah na ujira mkubwa.[4]

 

 

 

 

وَأَسِرُّوا قَوْلَكُمْ أَوِ اجْهَرُوا بِهِ ۖ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ﴿١٣﴾

13. Na fanyeni siri kauli zenu, au zidhihirisheni, hakika Yeye Ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.[5]

 

 

 

 

أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ﴿١٤﴾

14. Kwani Hajui Yule Aliyeumba! Na hali Yeye Ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri!

 

 

 

 

هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ ذَلُولًا فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِن رِّزْقِهِ ۖ وَإِلَيْهِ النُّشُورُ﴿١٥﴾

15. Yeye Ndiye Aliyeidhalilisha ardhi kwa ajili yenu, basi nendeni katika pande zake na kuleni katika Riziki Yake, na Kwake ndio kufufuliwa.

 

 

 

 

أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ فَإِذَا هِيَ تَمُورُ﴿١٦﴾

16. Je, mnadhani mko katika amani na (Allaah) Aliyeko mbinguni[6] kwamba Hatokudidimizeni ardhini, tahamaki hiyo inatikisika?

 

 

 

 

أَمْ أَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يُرْسِلَ عَلَيْكُمْ حَاصِبًا ۖ فَسَتَعْلَمُونَ كَيْفَ نَذِيرِ﴿١٧﴾

17. Au mnadhani mko katika amani na (Allaah) Aliyeko mbinguni kwamba Hatokutumieni tufani ya mawe? Basi mtajua vipi Maonyo Yangu!

 

 

 

 

 

وَلَقَدْ كَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَكَيْفَ كَانَ نَكِيرِ﴿١٨﴾

18. Na kwa yakini walikadhibisha wale walio kabla yao, basi ilikuwaje Kukana Kwangu (kwa adhabu ya maangamizi)?![7]  

 

 

 

 

أَوَلَمْ يَرَوْا إِلَى الطَّيْرِ فَوْقَهُمْ صَافَّاتٍ وَيَقْبِضْنَ ۚ مَا يُمْسِكُهُنَّ إِلَّا الرَّحْمَـٰنُ ۚ إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ بَصِيرٌ﴿١٩﴾

19. Je, hawawaoni ndege juu yao, wakiwa wanakunjua na kukunja (mbawa)! Hakuna anayewashikilia isipokuwa Ar-Rahmaan. Hakika Yeye Ni Mwenye Kuona kila kitu.

 

 

 

 

أَمَّنْ هَـٰذَا الَّذِي هُوَ جُندٌ لَّكُمْ يَنصُرُكُم مِّن دُونِ الرَّحْمَـٰنِ ۚ إِنِ الْكَافِرُونَ إِلَّا فِي غُرُورٍ﴿٢٠﴾

20. Au ni lipi hilo jeshi lenu linaloweza kukunusuruni badala ya Ar-Rahmaan? Makafiri hawamo isipokuwa katika ghururi.

 

 

 

 

أَمَّنْ هَـٰذَا الَّذِي يَرْزُقُكُمْ إِنْ أَمْسَكَ رِزْقَهُ ۚ بَل لَّجُّوا فِي عُتُوٍّ وَنُفُورٍ﴿٢١﴾

21. Au ni nani huyu ambaye atakuruzukuni ikiwa (Allaah) Atazuia Riziki Yake? Bali wanang’ang’ania kwenye ufidhuli na kukimbilia mbali kwa chuki.

 

 

 

 

أَفَمَن يَمْشِي مُكِبًّا عَلَىٰ وَجْهِهِ أَهْدَىٰ أَمَّن يَمْشِي سَوِيًّا عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ﴿٢٢﴾

22. Je, yule anayekwenda akiwa gubigubi juu ya uso wake ameongoka zaidi, au yule anayekwenda sawasawa kuelekea njia iliyonyooka? 

 

 

 

 

قُلْ هُوَ الَّذِي أَنشَأَكُمْ وَجَعَلَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ ۖ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ﴿٢٣﴾

23. Sema: Yeye Ndiye Aliyekuanzisheni, na Akakujaalieni kusikia na kuona na nyoyo za kutafakari. Ni kidogo sana mnayoshukuru.

 

 

 

 

قُلْ هُوَ الَّذِي ذَرَأَكُمْ فِي الْأَرْضِ وَإِلَيْهِ تُحْشَرُونَ﴿٢٤﴾

24. Sema: Yeye Ndiye Aliyekutawanyeni kwenye ardhi, na Kwake mtakusanywa.

 

 

 

 

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴿٢٥﴾

25. Na wanasema: Ni lini hiyo ahadi (ya kufufuliwa), mkiwa ni wasemao kweli?[8]

 

 

 

 

قُلْ إِنَّمَا الْعِلْمُ عِندَ اللَّـهِ وَإِنَّمَا أَنَا نَذِيرٌ مُّبِينٌ﴿٢٦﴾

26. Sema: Hakika ujuzi wake uko kwa Allaah tu. Na hakika mimi ni mwonyaji mwenye kuwabainishia.

 

 

 

 

فَلَمَّا رَأَوْهُ زُلْفَةً سِيئَتْ وُجُوهُ الَّذِينَ كَفَرُوا وَقِيلَ هَـٰذَا الَّذِي كُنتُم بِهِ تَدَّعُونَ﴿٢٧﴾

27. Basi watakapoiona (adhabu ya Qiyaamah) inakaribia, zitadhikika nyuso za wale waliokufuru, na itasemwa: Hii ndio ambayo mlikuwa mkiiomba.

 

 

 

 

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَهْلَكَنِيَ اللَّـهُ وَمَن مَّعِيَ أَوْ رَحِمَنَا فَمَن يُجِيرُ الْكَافِرِينَ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ﴿٢٨﴾

28. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Je, mnaonaje ikiwa Allaah Ataniangamiza na walio pamoja nami, au Akiturehemu, basi ni nani atakayewakinga makafiri na adhabu iumizayo?

 

 

 

 

قُلْ هُوَ الرَّحْمَـٰنُ آمَنَّا بِهِ وَعَلَيْهِ تَوَكَّلْنَا ۖ فَسَتَعْلَمُونَ مَنْ هُوَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ﴿٢٩﴾

29. Sema: Yeye Ndiye Ar-Rahmaan tumemwamini, na Kwake tunatawakali. Basi karibuni hivi mtakuja kujua ni nani ambaye yumo katika upotofu wa bayana.

 

 

 

 

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَصْبَحَ مَاؤُكُمْ غَوْرًا فَمَن يَأْتِيكُم بِمَاءٍ مَّعِينٍ﴿٣٠﴾

30. Sema: Mnaonaje yakijakuwa maji yenu yamedidimia, basi ni nani atakayeweza kukuleteeni maji (ya chemchemu) yatiririkayo?

 

 

 

 

[1] Fadhila Za Suwrah Al-Mulk:

 

Rejea Utangulizi wa Suwrah kwenye faida na fadhila zake.

 

[2] Nyota Zimeumbwa Kwa Mambo Matatu:

 

Rejea Al-An’aam (6:97) kwenye Hadiyth iliyotaja mambo matatu ya kuumbiwa nyota. Na rejea pia An-Nahl (16:16) na Asw-Swaaffaat (37:10).

 

[3] Allaah (عزّ وجلّ) Hakuwaangamiza Makafiri Ila Baada Ya Kuwatumia Mwonyaji:

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) katika Kauli Zake nyenginezo kuwa, Hakuwaangamiza watu ila baada ya kuwatumia waonyaji, na kwamba kuangamizwa kwao kumesababishwa na dhulma zao za kukadhibisha Risala Yake kupitia Rusuli Wake:  

 

إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ بِالْحَقِّ بَشِيرًا وَنَذِيرًا ۚ وَإِن مِّنْ أُمَّةٍ إِلَّا خَلَا فِيهَا نَذِيرٌ ﴿٢٤﴾

“Hakika Sisi Tumekupeleka kwa haki ili ubashiri na uonye. Na hakuna ummah wowote isipokuwa amepita humo mwonyaji.” [Faatwir (35:24)]

 

Rejea pia Al-Israa (17:15), Yuwnus (10:47), An-Nahl (16:36), (16:63), Al-Muuminuwn (23:44), Al-Qaswasw (28:59), Al-An’aam (6:42), (6:131), Sabaa (34:34), Az-Zukhruf (43:23), Huwd (11:117), Al-Kahf (18:59), Al-Hajj (22:45), (22:48), Ash-Shu’araa (26:208), Al-Qaswasw (28:58),  Atw-Twalaaq (65:8).

 

Basi makafiri wanapoona adhabu ya moto wa Jahanna na kuingizwa humo, huulizwa na Malaika walinzi wa moto kama hawakuletewa waonyaji, na hapo hukiri kuwa walitumiwa waonyaji. Kisha hubaki kujuta kama ilivyotajwa katika Aayah za Suwrah hii Al-Mulk (67:6-11). Rejea pia Faatwir (35:37), Az-Zumar (39:71), Al-An’aam (6:130).

 

[4] Fadhila Za Kumkhofu Allaah (عزّ وجلّ), Muumini Anapokuwa Peke Yake:

 

Muumini kumkhofu Allaah (عزّ وجلّ) kwa siri, au anapokuwa pekee, ni katika alama za ikhlaasw. Na kumkhofu Allaah (عزّ وجلّ) kwa ghaibu (kwa siri) kuna fadhila adhimu ikiwemo kuingizwa Jannah (Peponi). Rejea Qaaf (50:31-35).

 

Na fadhila nyengine ya Muumini kumkhofu Allaah (عزّ وجلّ) anapokuwa pekee, ni kujaaliwa kuweko katika Kivuli cha Allaah (عزّ وجلّ) Siku ya Qiyaamah, Siku ambayo hakutakuwa na kivuli isipokuwa Kivuli cha Allaah kama ilivyotajwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ ((سَبْعَةٌ يُظِلُّهُمْ اللَّهُ فِي ظِلِّهِ يَوْمَ لا ظِلَّ إِلا ظِلُّهُ: الإِمَامُ الْعَادِلُ، وَشَابٌّ نَشَأ فِي عِبَادَةِ رَبِّهِ، وَرَجُلٌ قَلْبُهُ مُعَلَّقٌ فِي الْمَسَاجِدِ، وَرَجُلَانِ تَحَابَّا فِي اللَّهِ اجْتَمَعَا عَلَيْهِ وَتَفَرَّقَا عَلَيْهِ، وَرَجُلٌ طَلَبَتْهُ امْرَأَةٌ ذَاتُ مَنْصِبٍ وَجَمَالٍ فَقَالَ إِنِّي أَخَافُ اللَّهَ، وَرَجُلٌ تَصَدَّقَ بِصَدَقَةٍ فَأَخْفَاهَا حَتَّى لا تَعْلَمَ شِمَالُهُ مَا تُنْفِقُ يَمِينُهُ، وَرَجُلٌ ذَكَرَ اللَّهَ خَالِيًا فَفَاضَتْ عَيْنَاهُ)) متفق عليه

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Watu saba Allaah Atawafunika katika kivuli Chake, Siku ambayo hakutokuwa na kivuli ila kivuli Chake: (i) Imaam (kiongozi) muadilifu. (ii) Kijana ambaye amekulia katika ibaada ya Rabb wake. (iii) Mtu ambaye moyo wake umeambatana na Misikiti (iv) Watu wawili wanaopendana kwa ajili ya Allaah; wanakutana kwa ajili Yake na wanafarikiana kwa ajili Yake. (v) Mwanamme aliyetakwa na mwanamke mwenye hadhi na mrembo wa kuvutia akasema: Mimi namkhofu Allaah! (vi) Mtu aliyetoa swadaqa yake akaificha hadi kwamba mkono wake wa kushoto usijue nini ulichotoa mkono wake wa kulia. (vii) Mtu aliyemdhukuru Allaah kwa siri macho yake yakatokwa machozi.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Bonyeza pia viungo vifuatavyo kupata faida nyenginezo:

 

006-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Taqwa – Kumkhofu Allaah

 

054-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Fadhila ya Kulia Kutokana na Kumuogopa Allaah na Shauku Kwake

 

Watu Saba Watakaofunikwa Katika Kivuli Cha Allaah Siku Ya Qiyaamah

 

[5] Allaah (عزّ وجلّ) Ni Mjuzi Wa Yaliyo Vifuani:

 

 

Rejea Ghaafir (40:19) ambako kuna maelezo na rejea mbalimbali zenye kuthibitisha kwamba hakuna chochote kile kinachofichika kwa Allaah (عزّ وجلّ).

 

[6] Allaah (سبحانه وتعالى) Yuko Juu Kwa Dhati Yake Inayolingana Na Uadhama Na Ujalali Wake.

 

Aayah hii tukufu na inayofuatia (67:17) ni uthibitisho mmojawapo kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Yuko juu ya mbingu saba juu ya ‘Arsh Yake, kwa Dhati Yake inayolingana na Uadhama na Ujalali Wake.  Rejea Al-A’raaf (7:54) na Twaahaa (20:5) kwenye maelezo bayana yanayohusiana. Hii ni ‘Aqiydah ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah. Na katika Qur-aan dalili za kuweko Kwake Allaah (سبحانه وتعالى) juu, zimo katika Aayah kadhaa, miongoni mwazo ni: Aal-‘Imraan (3:55), Al-Ma’aarij (70:4), As-Sajdah (32:5), An-Nahl (16:50), Faatwir (35:10).

 

Na katika Sunnah, kuna dalili tele ya kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Yuko juu. Miongoni mwazo ni:

 

(i)

 

حَدَّثَنَا قُتَيْبَةُ، حَدَّثَنَا عَبْدُ الْوَاحِدِ، عَنْ عُمَارَةَ بْنِ الْقَعْقَاعِ بْنِ شُبْرُمَةَ، حَدَّثَنَا عَبْدُ الرَّحْمَنِ بْنِ أَبِي نُعْمٍ، قَالَ سَمِعْتُ أَبَا سَعِيدٍ الْخُدْرِيَّ، يَقُولُ بَعَثَ عَلِيُّ بْنُ أَبِي طَالِبٍ ـ رضى الله عنه ـ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم مِنَ الْيَمَنِ بِذُهَيْبَةٍ فِي أَدِيمٍ مَقْرُوظٍ لَمْ تُحَصَّلْ مِنْ تُرَابِهَا، قَالَ فَقَسَمَهَا بَيْنَ أَرْبَعَةِ نَفَرٍ بَيْنَ عُيَيْنَةَ بْنِ بَدْرٍ، وَأَقْرَعَ بْنِ حَابِسٍ وَزَيْدِ الْخَيْلِ، وَالرَّابِعُ إِمَّا عَلْقَمَةُ وَإِمَّا عَامِرُ بْنُ الطُّفَيْلِ، فَقَالَ رَجُلٌ مِنْ أَصْحَابِهِ كُنَّا نَحْنُ أَحَقَّ بِهَذَا مِنْ هَؤُلاَءِ‏.‏ قَالَ فَبَلَغَ ذَلِكَ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ ‏"‏ أَلاَ تَأْمَنُونِي وَأَنَا أَمِينُ مَنْ فِي السَّمَاءِ، يَأْتِينِي خَبَرُ السَّمَاءِ صَبَاحًا وَمَسَاءً ‏"‏‏

Amesimulia Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy  (رضي الله عنه) katika Hadiyth ndefu: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Je, hamuniamini ilhali mimi nimeaminiwa na Aliye  mbinguni; zinanijia khabari za mbinguni asubuhi na jioni?.”

 

 

(ii) Safari ya Israa na Mi’raaj.

 

Rejea Al-Israa (17:1), An-Najm (53:1-18). Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipandishwa na Malaika Mtukufu Jibriyl hadi kuvuka mbingu ya saba ambako Allaah (سبحانه وتعالى) Alimfaridhisha Swalaah tano huko. Na Hadiyth ifuatayo inaelezea tukio hilo kwa mukhtasari:

 

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesimulia safari yake muhimu kutoka Makkah hadi Quds na kutoka hapo hadi juu mbinguni kama ifuatavyo: Jibriyl alinichukua hadi mbingu ya chini kabisa na kuwaomba walinzi wake kufungua mlango. Akaulizwa: Huyu ni nani? Alijibu: Jibriyl. Wakauliza: Upo na nani? Akajibu: (Nipo na) Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم). Wakauliza. Je amepata mwaliko? Jibriyl Akajibu: Naam. Kisha akakaribishwa kwa tamko la: “Anakaribishwa sana.” Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akaendelea na safari, ulipofunguliwa mlango, nikaingia na hapo nikakutana na Aadam. Jibriyl akaniambia: Huyu ni baba yako, msalimie. Aadam akanisalimia, kwa kusema: “Karibu, mwana Mchaji  Allaah na Rasuli Mchaji Allaah.” Kisha Jibriyl akapanda hadi mbingu ya pili na kuwaomba walinzi wake kufungua mlango. Masuala yaliyoulizwa kwenye mbingu ya chini yalirudiwa kabla ya mlango kufunguliwa. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alieleza alichokiona katika kila mbingu, hadi mwisho akachukuliwa hadi mbingu ya saba ambapo Swalaah za fardhi zilikabidhiwa kwake. [Imaam Al-Bukhaariy, Imaam Muslim na wengineo]

 

(iii) Kila Siku Inapobakia Thuluthi Ya Mwisho Ya Usiku, Allaah (سبحانه وتعالى) Anateremka Hadi Mbingu Ya Dunia Kuwakidhia Haja Waja Wake:   

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ، مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم

AmesimuliaAbuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Allaah (تبارك وتعالى) Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba duaa Nimuitike? Nani Ananiomba jambo Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

(iv) Mtumwa Alitambua Kuwa Allaah (عزّ وجلّ) Yuko Juu:

 

Amesimulia Mu’awiyah As-Sahmiy (رضي الله عنه): Nilikuwa na kondoo ambao niliwaweka baina ya Uhud na Juwaniyyah, wakiwa na mtumwa wa kike ili kuwaangalia. Siku moja, nilienda nje kuwaangalia kondoo wangu na kugundua kwamba mbwa mwitu amemnyakua mmoja wao. Kwa vile mimi ni binaadam tu, (nilighadhibika) na kumpiga msichana kofi. Baadaye, nilienda kwa Rasuli wa Allah (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumsimulia tukio hilo, naye akanichukulia kuwa nimetenda kitendo kikubwa (kibaya). Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Je nimuachie huru (kama ni njia ya kujiokoa na dhambi yangu).  Akasema “Muite.” Nilipomuita, alimuuliza: “Allaah Yuko wapi?” Alisema: Juu ya mbingu.  Kisha akamuuliza: “Ni nani mimi?” Akasema: Rasuli wa Allaah.  Baada ya hapo, Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniamuru akiniambia: “Muache huru, Yeye ni Muumini.” [Imaam Muslim, Abuu Daawuwd, na wengineo]

 

(v) Roho Za Wanaadam Zinapotolewa Hupandishwa Juu Kwa Allaah (عزّ وجلّ):

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Kawaida ya Malaika wa kutoa roho huwa wanamfikia mtu anayefariki. Iwapo ni mchaji Allaah (mwenye taqwa), wataiambia roho yake, Ee roho njema! Toka nje ya mwili mzuri, na furahia kwa kupata rehma na ulinzi kutoka kwa Rabb Ambaye Ameridhika nawe. Malaika wataendelea kuisisitiza kwa maneno haya hadi roho inapotoka nje ya mwili. Kisha itachukuliwa juu hadi mbinguni ambapo ruhusa ya kufungua milango ya mbingu itaombwa. Walinzi watauliza: Ni nani huyu? Malaika watajibu. Fulani mwana wa fulani. Walinzi watasema: Unakaribishwa sana ee roho njema.  Roho hiyo itasifiwa kwa maneno hayo hadi mwishoni itakapochukuliwa juu ya mbingu ambako ni kwa Allaah.” [Imaam Ahmad, Al-Haakim na wengineo]

 

(vi) Rehma ya Allaah (سبحانه وتعالى) Kutoka mbinguni:

 

‘Abdullaah bin ‘Amr (رضي الله عنه)  amesimulia kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ambaye amesema: “Kuwa na huruma kwa waliopo ardhini, ili Yule Aliyeko juu ya mbingu Apate kuwa na rehma kwako.” [Imaam Al-Bukhaariy, Imaam Muslim na wengineo]

Basi hizo ni baadhi tu ya dalili katika Sunnah kwani ziko zaidi ya hizo.

 

Rejea pia Al-Mujaadalah (58:7) kwenye faida tele nyenginezo:

 

[7] Kukana:

 

Maana ya Kukana hapa kwa Allaah ni namna ambavyo Allaah (عزّ وجلّ) Aliwajibisha makafiri hao kwa jibisho kali la kuwateremshia adhabu kali za kuwaangamiza kama zilivyotajwa katika Qur-aan Tukufu kama kugharikishwa, kutumiwa upepo mkali wa dhoruba, kupinduliwa miji juu chini, kudidimizwa na kadhalika. Na hiyo ni baada ya kuwatumia Rusuli wakiwa na hoja bayana, miujiza ya kuthibitisha Utume wao mbali na neema nyingi Alizowaneemesha. Hayo yote waliyakanusha na kuyakataa kwa inadi na kiburi tu, na wakasahau pia Neema nyingi za Allaah kwao. Na hapo ndipo lilipokuja Jibisho Kali la Allaah dhidi yao.

 

Rejea pia: Al-Hajj (22:44), Sabaa (34:45), Faatwir (35:26).

 

[8] Ada Ya Makafiri Kuuliza Lini Adhabu Itawafikia Au Lini Qiyaamah Kitatokea:

 

Rejea Yuwnus (10:48).

 

 

 

Share