00-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! Utangulizi

 

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

 

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!

 

 00-Utangulizi

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ الله الرَّحْمنِ الرَّحِيم

 

الْحمْدُ لِلَّه وَالصَّلاةُ وَالسِّلامُ عَلى خَاتم الأنْبِيَاء وَالْمُرْسَلِين، الْمَبْعُوثُ رَحْمَةً لِلْعَالَمِين، مُحَمَّد وَعَلى آلِه وَأصْحابِه أجْمَعِين وَمَنْ تَبِعَهُمْ بِإِحْسَانٍ إِلَى يَوْمِ الدِّينِ.

Himdi Anastahiki Allaah, Swalaah na salaam zimfikie Nabiy na Rasuli wa mwisho, aliyetumwa awe rahmah kwa walimwengu, Muhammad, pamoja na ahli zake na Maswahaba zake wote, na wanaowafuata kwa ihsaan mpaka Siku ya Malipo.

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾

hakika shirki ni dhulma kubwa mno [Luqmaan: 13]

 

 

Kinyume ya shirki ni Tawhiyd ambayo ni kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Rubuwbiyyah (Uola) Uluwhiyyah (‘ibaadah) Yake na katika Asmaa na Swifaat (Majina na Sifa nzuri) Zake.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ﴿٦٥﴾

Kwa yakini umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka zitaporomoka ‘amali zako na bila shaka utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”

 

بَلِ اللَّـهَ فَاعْبُدْ وَكُن مِّنَ الشَّاكِرِينَ﴿٦٦﴾

Bali Allaah Pekee mwabudu, na uwe miongoni mwa wenye kushukuru. [Az-Zumar: 65-66]

 

 

Waislamu wengi wako katika hali ya kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa); wengine wakiwa wanatambua hatari zake, na wengine wakiwa hawatambui kuwa wanamshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), kwa sababu baadhi ya ‘amali zinazotendwa zinaonekana kuwa kama ni nzuri na hali zimeingia shirki ndani yake.

 

Imaam Muhammad bin ‘Abdil-Al-Wahhaab amesema katika Al-Qawaaid Al-Arba’: “Kwamba washirikina wa zama zetu ni waovu zaidi (shirki zao ni kubwa zaidi) kuliko washirikina wa awali, kwa sababu, wa awali walimshirikisha Allaah katika raha, lakini wakizitakasa ‘Ibaadah zao wakati wa shida. Ama washirikina wa sasa, shirki zao ni wakati wote, wakiwa katika raha au katika shida … na dalili ni kauli Yake Ta’aalaa:

 

فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ ﴿٦٥﴾

Wanapopanda merikebu humwomba Allaah wakiwa wenye kumtakasia Yeye Dini, lakini Anapowaokoa katika nchi kavu, tahamaki hao wanamshirikisha. [Al-‘Ankabuwt: 65]

 

Kwa hiyo, kuna umuhimu mkubwa wa Waislamu kujifunza somo hili ili kujitahadharisha na hatari zake ili waweze kufunga milango na njia zote kubwa na ndogo za shirki. Makala hizi In Shaa Allaah zitaweza kutambulisha na kubainisha matendo mengi yanayomshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na namna ya kuyaepuka, ili Muislamu abakie katika amri ya Muumba wake Ambaye Ameamrisha kuabudiwa Yeye Pekee bila ya kumshirikisha. Kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni katika dhambi kubwa mno kama alivyobainisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ اِبْنِ مَسْعُودٍ ‏ رضى الله عنه ‏ قَالَ سَأَلْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم: أَيُّ اَلذَّنْبِ أَعْظَمُ؟ قَالَ: ((أَنْ تَجْعَلَ لِلَّهِ نِدًّا, وَهُوَ خَلَقَكَ))‏  

Imepokelewa kutoka kwa ibn Mas-‘uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Je, dhambi ipi kubwa mno?” Akasema: ((Kumfanyia Allaah mlinganishi (wa kumshirikisha) na hali Yeye Amekuumba)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Nukta chache zifuatazo ni mukhtasari wa hatari za kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

1. Shirki inaharibu ‘amali za mtu. Dhambi hii kubwa walitahadharishwa Rasuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa ukali mno pale Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaposema:

 

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٨٨﴾

Na kama wangemshirikisha bila shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakitenda. [Al-An’aam: 88]

 

 

2. Shirki ni dhambi pekee ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Haisamehe isipokuwa tu mtu akirudi kutubia Kwake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا﴿١١٦﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali. [An-Nisaa: 116]

 

 

3. Shirki inamtoa mtu nje ya Uislamu!

 

Imeelezwa shirki kuwa ni miongoni mwa matendo yanayomtoa mtu nje ya Uislamu, kama ilivyo katika Nawaaqidhw Al-Islaam cha Imaam Muhammad ibn Al-Wahhaab (Rahimahu-Allaah).

 

Na miongoni mwa mengi wanayotenda baadhi ya Waislamu ni kumwendea kahini anayetabiri mambo ya ghayb; elimu ambayo hakuna aijuae isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hatari ya tendo hili ni kama alivyotahadharisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):   

 

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) عَنِ النَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((مَنْ أَتَى كَاهِنًا، فَصَدَّقَهُ بِمَا يَقُولُ فَقَدْ كَفَرَ بِمَا أُنْزِلَ عَلَى مُحَمَّدٍ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ)) رَوَاهُ أَبُو دَاوُدَ

Imepokewa toka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayemkaribia kahini na kuamini anayoyasema basi amekanusha aliyoteremshiwa Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم))  [Abu Daawuwd]

 

 

4-Mwenye kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni mwenye hatima mbaya mno ya makazi ya Moto. Ametahadharisha hilo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ﴿٧٢﴾

Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni motoni. Na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru.” [Al-Maaidah: 72]

 

Tunataraji tawfiyq ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) makala hizi ziwazidishie elimu yenye manufaa Waislamu kuhusiana na somo hili na Atuepushe sote kumshirikisha Yeye Subhaanahu wa Ta’aalaa. 

 

 

 

Share