Suwrah Zinazojulikana Kama: As-Sab’u Atw-Twiwaal, Al-Mathaaniy, Al-Mufasw-swal, Al-Mi-iyn

 

Ni Zipi Suwrah Zinazojulikana Kama:

 

As-Sab’u Atw-Twiwaal, Al-Mathaaniy, Al-Mufasw-swal Na Al-Mi-iyn

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

عَنْ واثلةَ بنِ الأسقعِ قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: أعطيتُ مكانَ التوراةِ السبعَ الطِّوالَ، ومَكَانَ الزَّبُورِ الْمَئِينَ، ومَكَانَ الْإِنْجِيلِ الْمَثَانِيَ ، وَفُضِّلْتُ بِالْمُفَصَّلِ. رواه  أحمد والطبراني والبيهقي والألباني في صحيح الجامع الصغير والسلسلة الأحاديث الصحيحة.  

Kutoka kwa Waathilah bin Al-Asqa'i, kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Nimepewa nafasi ya Tawraat 'As-Sab'u Atw-Twiwaal'. Na nimepewa nafasi ya Zabuwr 'Al-Ma-iyn (Al-Mi-iyn)’.  Na nimepewa nafasi ya Injiyl 'Al-Mathaaniy'. Na nimefadhilishwa kwa ‘Al-Mufasw-swal’. [Ahmad, Atw-Twabaraaniy, na Al-Bayhaqiy na Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami' Asw-Swaghiyr na As-Silsilat Al-Ahaadiyth Asw-Swahiyhah]

 

 

Ufafanuzi:

 

As-Sab'u Atw-Twiwaal:

Ni Suwrah saba ndefu, nazo ni Suwrah Al-Baqarah, Aal-‘Imraan, An-Nisaa, Al-Maaidah, Al-An’aam, Al-A’raaf, na At-Tawbah. Wako ambao wanaoona Suwrah Al-Anfaal na At-Tawbah ndio za saba kwa sababu zilikuwa zikihesabika kuwa ni Suwrah moja

Kadhaalika, kuna wanaoona Suwrah ya saba ni Suwrah Yuwnus.

Lakini iliyo maarufu na iliyo karibu kwenye usahihi Suwrah ya saba ni Suwrah At-Tawbah kwa kuwa Aayah zake ni nyingi zaidi kuliko Suwrah Yuwnus.

 

 

Al-Ma-iyn (Al-Mi-iyn):

Ni Suwrah ambazo Aayah zake, zinakaribia mia au kuzidi.

Kadhaalika, katika hili wako wanaosema hizo Suwrah ‘Al-Mi-iyn’ ni Suwrah saba; ya mwanzo wake ni Suwrah Al-Israa, na ya mwisho ni Suwrah Al-Mu-uminuwn. Na wako wanaoona ‘Al-Mi-iyn’ ni zile Suwrah ambazo Aayah zake zinafika mia au kuzidi na zinafuatia zile Suwrah saba ndefu (As-Sab’u Atw-Twiwaal).

 

 

Al-Mathaaniy:

Ni Suwrah zinazofuatia baada ya ‘Al-Ma-iyn (Al-Mi-iyn)’, na pia ina maana ya Qur-aan yote, na vilevile Suwrah Al-Faatihah ikaitwa ‘Sab’an minal Mathaaniy’ kwa sababu ya kurudiwa katika kila Rakaa. Kadhaalika, imeitwa Al-Mathaaniy, kwa sababu ndani ya Qur-aan kunarudiwa Khabari mbalimbali na Visa mbalimbali, Adhabu mbalimbali na Hukmu mbalimbali.

Neno ‘Al-Mathaaniy’ lipo katika Suwrah Al-Hijr:

 

وَلَقَدْ آتَيْنَاكَ سَبْعًا مِّنَ الْمَثَانِي وَالْقُرْآنَ الْعَظِيمَ﴿٨٧﴾

Na kwa yakini Tumekupa (Aayaat) Saba zinazokaririwa (kusomwa) na Qur-aan adhimu.

 

Na Az-Zumar:

 

اللَّـهُ نَزَّلَ أَحْسَنَ الْحَدِيثِ كِتَابًا مُّتَشَابِهًا مَّثَانِيَ

Allaah Ameteremsha kauli nzuri kabisa, Kitabu; zinazoshabihiana ibara zake, zenye kukaririwa kila mara  [Az-Zumar: 23]

 

Wamesema Quraa-a kuwa ‘Al-Mathaaniy’ ni Suwrah ambazo Aayah zake ni chini ya Aayah mia, kwa sababu zinarudia rudia kuliko zinavyorudia zile za ‘Atw-Twiwaal’ na ‘Al-Mi-iyn’.

 

 

Al-Mufasw-swal:

Ni Suwrah Qaaf hadi Suwrah An-Naas.

Na vilevile wako waliosema kuwa ‘Al-Mufasw-swal’ ni zile Suwrah kuanzia Suwrah Al-Hujuraat.

Na inasemwa, zimeitwa ‘Al-Mufasw-swal’ kwa sababu ya wingi wa kutenganishwa Suwrah zake kwa BismiLLaah. Na imesemwa kwa sababu ya uchache wa kuwepo Aayah zilizo ‘Mansuwkh’ (zilizofutwa), na huitwa ‘Al-Muhkam’ (zilizo wazi, au ambazo hazijafutwa) kama ilivyo kwenye ‘Al-Bukhaariy kutoka kwa Sa’iyd bin Jubayr, amesema: “Hakika kile mnachokiita ‘Al-Mufasw-swal’, ni ‘Al-Muhkam’”.

 

Al-Mufasw-swal’ imegawika katika mafungu matatu, nayo ni:

Twiwaal (zilizo ndefu)

Awsaatw (zilizo kati kwa kati)

Qiswaar (zilizo fupi)

 

 

Twiwaal (zilizo ndefu):

Ni kutoka Suwrah Qaaf (au Al-Hujuraat kutokana na ikhtilaaf iliyopo ya kuwa ipi ni ya mwanzo) hadi Suwrah Al-Buruwj na wengine wamesema hadi Suwrah An-Naba-i.

 

 

Awsaatw (za kati kwa kati):

Ni kutoka Suwrah Al-Buruwj (au Atw-Twaariq) hadi Suwrah Al-Bayyinah, na wengine wanaona ni kutoka Suwrah An-Naba-i hadi Suwrah Adhw-Dhwuhaa.

 

 

Qiswaar (zilizo fupi):

Ni kutoka Suwrah Al-Bayyinah (au Az-Zilzalah) hadi Suwrah An-Naas (mwisho wa Qur-aan), na wengine wanaona ni kutoka Suwrah Adhw-Dhwuhaa hadi mwisho wa Qur-aan.

 

Na vilevile kuna zile Suwrah zenye kujulikana kama ‘Al-Hawaamiym’, nazo ni zile zenye kuanzwa na ‘Haa Miym حم﴿

 

 

 

Share