Utengenezaji Sambusa Za Nyama Na Jinsi Ya Kuzihifadhi

Utengenezaji Sambusa Za Nyama Na Jinsi Ya Kuzihifadhi

Takriban Sambusa 350

 

Vipimo

Pastries za sambusa - *350 takriban

Nyama ya kusaga - 4 Kilo

Pilipili mbichi ilosagawa -  *3 Vijiko vya kulia

Jira (bizari pilau/cumini) - 3 vijiko vya kulia

Dania (gilgilani/coriander) -  3 vijiko vya kulia

Bizari mchanganyiko au bizari mchuzi - 1 kijiko cha kulia

Pilipili manga - 1 kijiko cha kulia

Ndimu - 7 takriban kamua

Vidonge vya supu - 5

Chumvi - *1 kijiko cha kulia

Vitunguu vilokatwakatwa (chopped) - 10 kiasi vya kiasi

Kotimiri (fresh coriander chopped) - 7 – 8  misongo

Mafuta ya kukaangia - Nusu karai

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika

  1. Osha nyama kidogo ukipenda, kisha chuja katika chujio.
  2. Weka nyama katika sufuria changanya viungo vyote vizuri kabisa.
  3. Weka katika moto, ipikie iwive huku unaikoroga isifanye madonge. Usiache mkono kwanza.
  4. Itakapokauka  kabisa, zima moto, weka vitunguu na kotmiri.  Onja ukoleze upendavyo.
  5. Epua umimine katika bakuli kubwa ipate kupoa haraka. 

       6. Tayarisha gundi kwa kuchanganya unga kiasi katika kibakuli na maji.

       7. Chukua pastry moja, kunja mkunjo wa kwanza kufanya kifuko. Jaliza kiasi vijiko viwili vya chai kisha kunja kama muelekezo wa picha. Tahadhari usibakishe uwazi pembezoni. Weka kidole gumba katika corner ya pastry pale unapokunja ili ubane pastry isibakie uwazi.

 

 

     8. Kunja mkunjo wa pili kwa kukuilekeza pastry sambamba  na ukingoni mwa pastry, huku umebana uwazi wa mfuko ili nyama isitoke. Elekeza sambamba na ukingoni wa pili. Endelea hivyo mpaka mwishowe ibakie kisehemu ndogo tu ya pastry.Tia gundi ubane vizuri sehemu zote za wazi.

 

     9. Panga katika sahani kisha zihifadhi katika mifuko ya kuhifadhi chakula katika freezer.

  

     10. Unapotaka kuzipika, ikiwa zinatoka katika freezer, zipike kwa mafuta ya dafudafu (Si yaliyochemka zitaungua sambusa kabla ya kuiva). Isipokuwa ikiwa unazipika fresh ndio mafuta yanaweza kuwa yameshika moto.

      11. Zikibadilika rangi kuwa hudhurungi (golden brown) epua uzichuje mafuta katika chujio, kisha weka katika sahani uliyoweka tissue za jikoni zizidi kuchuja mafuta.

      12. Panga katika sahani ya kupakulia zikiwa tayari.          

Vidokezo:

  1. Ukipenda fanya nusu yake. Kufanya kwa wingi kutaokoa muda wako kwa sababu sambusa zinachukua muda mwingi kuandaa. Khasa kwa Ramadhwaan, ni vyema kuandaa kabla mwezi kuingia.
  2. Pia ni wepesi kwa mwenye kufanya biashara kuzihifadhi, au wanapotokea wageni nyumbani kuwaandalia.
  3. * Pastry za sambusa zinapatikana tayari madukani, unaweza kutengeneza mwenyewe ukipenda ingawa zinahitaji muda mrefu na kazi pana. Pia kutegemea aina za pastry, nyengine zikiwa ni nyembamba mno, zinahitaji ukunje mbili mbili. Upana wa pastry pia inategemea upendavyo; zikiwa pana sambusa zitakuwa kubwa, zikiwa ndogo zitakuwa ndogondogo.
  4. *Tahadhari chumvi kwani vidonge vya supu vinakuwa na chumvi.
  5. *Kiasi cha pilipili inategemea unavopenda. Unaweza kutumia pilipili mbuzi inayotoa ladha nzuri zaidi. Unaweza kukoleza kwa sosi ya pilipili mwishoni pia kutegemea vile unavyopenda.
  6. *Kotimiri ukishaziosha, zichuje maji kwa muda ili ukijachanganya zisifanye maji katika nyama. Na kila kotmiri zikiwa nyingi ndipo zinafanya sambusa kuwa tamu.

Bis-swihhah wal-hanaa (kula kwa siha na kufurahika)

 

 

 

 

 

 

 

Share