Nusaybah Bin Ka'ab: Ummu 'Ammaarah: (رضي الله عنها)
Nusaybah Bint Kaa'b Al-Maaziniyyah Al-Answaariyyah
Ummu 'Ammaarah (رضي الله عنها)
Na Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy
Jina lake ni Nusaybah bint Kaa'b Al-Maaziniyyah Al-Answaariyyah, maarufu pia kwa jina la Nusaybah Al-Answaariyyah au Ummu 'Ammaarah (Radhwiya Allaahu 'anhaa). Bibi huyu alikuwa mwanamke wa ajabu sana, na mapenzi yake katika dini ya Allaah pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi sallam) yanastaajibisha zaidi. Alikuwa shujaa, mstahamilivu katika shida, akisimama imara katika vita msitari wa mbele katika kupigana jihadi dhidi ya maadui wa Allaah, aliyebahatika kupata radhi za Allaah na kubashiriwa Pepo pamoja na kuwa karibu na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya Qiyaamah.
Alikuwemo katika ujumbe uliotoka Madiynah na kwenda Makka kwa siri kwa ajili ya kukutana na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mahala panapoitwa Al-'Aqabah, na kufungamana naye katika fungamano lililokuja kujulikana kwa jina la ‘Fungamano la 'Aqabah la pili’.
Ujumbe huo ulikuwa wa wanaume wapatao sabini na tatu na wanawake wawili akiwemo Bibi Nusaybah (Ummu 'Ammaarah) (Radhwiya Allaahu 'anhaa), na alikuja kutoa ahadi ya kumlinda Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa hali na mali iwapo atahamia kwao.
Bi Nusaybah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) ni mfano mwema wa kuigwa na wanawake wa Kiislamu, na dalili iliyowazi kuwa Uislamu haumdhalilishi mwanamke na kwamba mwanamke analo jukumu kubwa katika Uislamu, na kwamba mwanamke anapokuwa na azma basi anaweza kuwashinda hata mashujaa wakubwa wa kiume.
Nusaybah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) aliyekuwa na watoto wawili wote wa kiume na majina yao ni Habiyb na 'AbduLLaah bin Zayyid Al-Maziniy.
Alisilimu mara baada ya kusikia juu ya habari za dini hii mpya, akashiriki katika vita vingi vikiwemo vita vya Uhud, Hudaybiyah, Khaybar, vita vya Al-Yamaamah na Hunayn, na alihudhuria pia siku ya Fungamano la Ridhwan, akafungamana na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi sallam) siku hiyo chini ya mti pamoja na Maswahabah wenzake (Radhwiya Allaahu 'anhaa), na kwa ajili hiyo akaingia katika wale ambao Allaah (Subhanahu wa Ta'aalaa) Ameridhika nao, wale Aliowateremshia aya ya 18 ya Suwratul Fat-h Akitujulisha radhi Zake juu yao.
Allaah Anasema;
لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَنزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ وَأَثَابَهُمْ فَتْحًا قَرِيبًا﴿١٨﴾
Kwa yakini Allaah Amewawia radhi Waumini walipofungamana nawe ahadi ya utiifu (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) chini ya mti, (Allaah) Alijua yale yaliyomo nyoyoni mwao; basi Akawateremshia utulivu, na Akawalipa ushindi wa karibu. [Al-Fat-h: 18]
Bibi Nusaybah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) aliolewa mwanzo na mtu mmoja aitwae Wahab Al-Aslamiy aliyezaa naye mtoto wa kiume waliyempa jina la Habiyb, na alipofariki Wahab, Bibi Nusaybah akaolewa na Zayyid bin Aasim Al-Maaziny (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliyezaa naye mtoto waliyempa jina la 'AbduLLaah, na 'AbduLLaah huyu ndiye aliyemuuwa Musaylimah Al-Khadhaab katika vita vya Al-Yamaamah – Musailimah ni yule muongo aliyejipachipa Utume.
Misimamo Yake Mbali Mbali Vitani
Vita Vya Uhud
Anasema Al-Waqidiy (Radhwiya Allaahu 'anhu)
“Nilimuona Ummu 'Ammaarah.(Nusaybah) siku ya vita vya Uhud, yeye, mumewe, pamoja na watoto wao Habiyb na 'AbduLLaah, lakini Ummu 'Ammaarah alikuwa akipigana vita kwa ushujaa mkubwa sana na akapata majeraha kumi na mbili.”
Inajulikana kuwa katika vita vya Uhud Waislamu walianza kwa kupata ushindi mkubwa sana na kuweza kuyarudisha nyuma majeshi ya makafiri yaliyokuja kuuvamia mji wa Madiynah. Vita vikaendelea katika hali hiyo mpaka pale Waislamu walipoanza kukusanya ngawira huku majeshi ya makafiri yakirudi nyuma.
Wapigaji mishale ambao Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwataka wabaki juu ya jabali la Uhud na wasiteremke hata kama Waislamu watashinda au watashindwa, wakenda kinyume na amri hiyo, kwani mara baada ya kuwaona wenzao wanakusanya ngawira, na wao wakashuka chini na kuungana nao katika kuifanya kazi hiyo.
Walipokuwa katika hali hiyo, Khaalid bin Waliyd aliyekuwa kiongozi wa majeshi ya makafiri wakati huo, akaitumia fursa hiyo kwa kuwaamrisha wapiga mishale katika jeshi lake wende nyuma ya jabali la Uhud, walipande kupitia huko na kuwauwa watu wachache waliobaki juu, kisha waanze kuwamiminia Waislamu mishale kutoka jabalini wakati yeye akiongoza jeshi la wapanda farasi na wendao kwa miguu akiwazunguka. Waislamu waliokuwa wakimbia huku na kule bila mpango baada ya kuona wenzao wakiuliwa kwa mishale.
Kwa njia hii makafiri wakaweza kuwauwa Waislamu wengi sana na kufanikiwa kuyabadilisha matokeo ya vita hivyo kwa maslahi yao.
Wakati huo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa amesimama upande mmoja wa uwanja wa vita akiwa pamoja na Waislamu wenzake tisa tu, huku akilitazama jeshi lake linavyorudishwa nyuma na watu wake wanavyokimbia huku na kule, hakuwa na hiari nyingine isipokuwa moja katika mbili zifuatazo.
Ama aondoke kimya kimya yeye pamoja na wenzake tisa alokuwa nao na kukimbilia mahali penye usalama, au ahatarishe maisha yake kwa kunyanyua sauti na kuwaita watu wake warudi katika uwanja wa vita.
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaamua kuhatarisha maisha yake kwa kuwaita Waislamu, akapaza sauti yake juu huku akipiga ukelele;
“Rudini enyi Waislamu!, mimi hapa Rasuli wa Allaah.”
Kwa kufanya hivyo makafiri wakapajuwa mahali alipo, na kuanza kuelekea huko wote kwa nguvu moja wakijaribu kumfikia wao kwanza kabla ya Waislamu.
Hapo ndipo patashika ilipoanza, na Maswahabah tisa alokuwa nao wakaanza kupigana kufa na kupona kwa ajili ya kumuokoa Rasuli wao (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekwishawabashiria kuwa pamoja naye Peponi.
Anasema Al-Mubarak Furry katika kitabu cha ‘Ar-Rahiyq Al-Makhtum’ kuwa;
“Saba kati ya Maswahabah hao (Radhwiyah Allaahu 'anhum) wakauliwa, wakabaki wawili tu nao ni Twalha bin 'UbayuduLLaah na Sa'ad bin Abi-Waqqaas (Radhwiya Allaahu anhum)".
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akajeruhiwa begani, shavuni na kichwani pia, na Twlha (Radhwiya Allaahu 'anhu) akakatwa sehemu ya mkono wake, na hapo ndipo alipotokea kafiri aitwae 'AbduLLaah bin Qam-ah aliyetaka kumuuwa Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na hapo ndipo alipoingia Bi Nusaybah (Radhwiyah Allaahu 'anhaa) na kupigana kwa ujasiri mkubwa kwa ajili ya kumuokoa.
Hebu tumsikilize Bi Nusaybah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) mwenyewe akituhadithia jinsi alivyopigana kwa ushujaa na ustahamilivu mkubwa ili Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asidhurike.
Anasema Ummu 'Amaarah - Nusaybah binti Kaa'b (Radhwiya Allaahu 'anhaa);
“Nilitoka wakati wa asubuhi siku hiyo nikiwa nimebeba birika la maji na kuelekea moja kwa moja penye uwanja wa vita nikajionee mwenyewe yanayotendeka huko. Nikamuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa kati ya Swahabah zake na wakati huo Waislamu walikuwa wakiwashambulia makafiri na kuwashinda. Ghafla mambo yakabadilika na Waislam wakaanza kushindwa, na kurudi nyuma.
Nilipomuona Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amezungukwa na maadui, nikautoa upanga wangu na kusimama mbele yake na kuanza kupigana huku na kule.
Akatangulia kafiri mmoja anayeitwa Abu Qam-ah huku akisema kwa sauti kubwa;
“Nionesheni alipo Muhammad!, hatosalimika leo ikiwa mimi nitakuwa salama”, Anasema Nusaybah (Radhwiya Allaahu 'anhaa);
“Alipomfikia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wakati huo alikuwa kisha anguka chini akiwa amejeruhiwa, mimi nikamkabili kafiri huyo upanga mkononi nikiwa nimesimama baina yake na baina ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), huku akinichoma kwa upanga wake mara nyingi, na mimi nikampiga kwa upanga wangu mara nyingi pia, lakini adui wa Allaah yule alikuwa amevaa nguo mbili za chuma”.
Mwanawe 'AbduLLaah bin Zayyid (Radhwiya Allaahu 'anhu) alisema;
“Baada ya vita vya Uhud kumalizika niliona majeraha mengi juu ya mwili wa mama yangu Nusaybah, na majeraha mengine yalikuwa makubwa hata ukiingiza kiganja cha mkono ndani yake kitazama”.
Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akizungumza juu ya ushujaa wa bibi huyo siku ya Uhud alisema;
“Daraja ya Nusaybah bint Kaa'b leo, ni kubwa kuliko fulani na Fulani”.
Na alikuwa akisema kumwambia Nusaybah (Radhwiya Allaahu 'anhaa);
“Nani atakayeweza kustahamili ulivyostahamilia wewe ewe Ummu 'Ammaarah?”
Na Ummu 'Ammarah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) akawa anamjibu;
“Mimi niko tayari kustahamili chochote ewe Rasuli wa Allaah, isipokuwa nataka tu uniombee niwe pamoja nawe siku ya Qiyaamah.”
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia;
“(Bali utakuwa pamoja nami), tena si peke yako, wewe na wanao na 'aila yako yote. Ee Mola wangu! Mjaalie yeye na 'aila yake yote wawe pamoja nami Peponi”.
Siku moja wakati wa ukhalifah wake 'Umar bin Khattwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliletewa kitambaa kizuri sana, na watu alokuwa nao wakawa wanasema;
“Kitambaa hiki thamani yake ni kadha wa kadha, yareti kama ungelimpelekea Swafiya bint Abu 'Ubaydah mke wa mwanao AbduLLaah bin 'Umar bin Khattwaab.”
'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) akasema;
“Bali nitampelekea anayekistahikia zaidi kuliko yeye, (nitampelekea) Ummu 'Ammaarah Nusaybah bint Kaa'b, kwani nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhu wa aalihi wa sallam) siku ya Uhud akisema juu yake:
“Nilikuwa ninapogeuka kushoto au kulia namuona yeye akipigana kwa ajili yangu.”
'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) akampelekea Nusaybah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kitambaa hicho.
Vita Vya Al-Yamaamah
Hivi ni vita vilivyopiganwa baina ya majeshi ya Kiislamu na majeshi ya Musaylimah Al-Kadhaab, aliyejipachika utume wa uongo.
Imepokelewa kuwa Habiyb mwana wa Nusaybah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) siku moja alitekwa na Musaylimah Al-Kadhaab, akawa anamtesa huku akimuuliza;
“Unashuhudia kuwa Muhammad ni Rasuli wa Allaah?"
Habiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu) akawa anajibu;
“Ndiyo nashuhudia hivyo”.
Musaylimah akamuuliza;
“Na unashuhudia kuwa mimi pia ni Rasuli wa Allaah?”
Habib akajibu;
“Mimi kiziwi sisikii”
Akamuuliza tena;
“Unashuhudia kuwa Muhammad ni Rasuli wa Allaah?”
Habiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu) akajibu tena;
“Ndiyo nashuhudia hivyo”.
Musaylimah akamuuliza tena;
“Na unashuhudia kuwa mimi pia ni Mtume wa Allaah?”
Habiyb akajibu tena;
“Mimi kiziwi sisikii”.
Akawa anaendelea kumuuliza hivyo, na kila anapoulizwa iwapo anashuhudia kuwa Muhammad ni Rasuli wa Allaah, alikuwa akijibu;
“Ndiyo nashuhudia hivyo”.
Na anapoulizwa iwapo anashuhudia kuwa Musaylimah pia ni Rasuli wa Allaah, alikuwa akijibu;
“Mimi kiziwi sisikii”.
Mwisho Musaylimah akasema;
“Niitieni mshika panga wangu na mpiga mjeledi”
Wakaanza kumtesa Habiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu) huku wakimpiga mijeledi na kumkata vipande vipande huku wakimuuliza masuali yale yale na yeye alikuwa akiwapa majibu yale yale, mpaka akafa shahid (Radhwiya Allaahu 'anhu).
Ummu 'Ammaarah (Nusaybah) (Radhwiya Allaahu 'anhaa) aliposikia juu ya kuuliwa kwa mwanawe akasema;
“Mwanangu keshanitangulia Peponi”.
Vita vya Al-Yamaamah baina ya majeshi ya Kiislamu na majeshi ya Musaylimah Al-Kadhaab vilipiganwa wakati wa ukhalifah wa Abu Bakr As-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu).
Siku ya vita hivyo Nusaybah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) alimwendea Khalifa wa Waislamu na kumtaka ruhusa na yeye ashiriki.
Abu Bakar (Radhwiya Allaahu 'anhu) akamwambia;
“Tunaulewa vizuri ushujaa wako na ustahamilivu wako ewe Ummu 'Ammaarah, ingia vitani ukitaka kwa baraka za Allaah”.
Kisha Abu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) akamuusia Khaalid bin Waliyd (Radhwiya Allaahu 'anhu) juu ya Nusaybah, na Khaalid ndiye aliyekuwa jemadari wa majeshi ya Waislamu katika vita hivyo ambavyo Nusaybah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) alipigana kwa ushujaa mkubwa sana, akapata majeraha mengi na mkono wake ulikatwa.
Anasema Ummu Sa'ad (Radhwiya Allaahu 'anhaa):
“Nilimuona Nusaybah bint Kaa'b mkono wake ukiwa umekatika, nikamuuliza:
“Lini umekatika mkono wako?”
Akanambia;
“Siku ya (vita vya) Al-Yamaamah nilikuwa pamoja na watu wa Madiynah, tulipofika katika bustani ya Musaylimah, vita vikali vikapiganwa kwa muda hivi kwa ajili ya kupateka mahali hapo, na Abu Dujanah aliuliwa mahali hapo, kisha nikaingia mimi ndani ya qasri nikimtafuta adui wa Allaah Musaylimah Al-Kadhaab, akanitokea mmoja katika watu wake, nikapambana naye, akanipiga na kunikata mkono wangu, basi waLLaahi sijauendea kuuokota, nilisonga mbele kumtafuta mpaka nikamuona khabithi yule (Musaylimah) akiwa amekufa, na mwanangu ('AbduLLaah bin Zayyid) akiwa karibu yake huku akiufuta upanga wake juu ya mwili wa Musaylimah.
Nikamuuliza;
“Wewe ndiye uliyemuuwa?”
Akanijibu:
“Ndiyo ewe mama yangu”.
Nikasujudu kumshukuru Allaah”.
Hebu tumsikilize Wahshiy, (huyu ni yule aliyemuua Hamza (Radhwiya Allaahu 'anhu) ammy yake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika vita vya Uhud, kisha akasilimu):
Anasema Wahashiy:
“Waislamu walipotoka kwenda kupigana na majeshi ya Musaylimah Al-Kadhaab na mimi nikatoka nao na kuuchukuwa mkuki wangu ule ule niliomuulia Hamza. Vita vilipoanza na baada ya kuingia bustanini kwake nikamuona Musaylimah, nikaulenga mkuki wangu kuulekeza kwake, nikamuona mmoja katika watu wa Madiynah akiwa amesimama upande mwingine naye pia akijiatayarisha kumuuwa. Kila mmoja wetu anamlenga yeye, nikaunyanyua mkuki wangu juu nikaulenga vizuri mpaka nilipoona kuwa sasa umemuelekea, nikautikisa kisha nikamvurumishia nao, ukamzama mwilini mwake, na wakati huo huo nikamuona yule mtu wa Madiynah ('AbduLLaah bin Zayyid) akimchoma kwa upanga wake, na Allaah peke yake ndiye anayejuwa yupi kati yetu aliyemuua.
Ikiwa mimi ndiye niliyemuuwa basi kabla ya kusilimu kwangu nilimuuwa mtu bora kupita wote baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na baada ya kusilimu kwangu nimemuuwa mtu muovu kupita wote”.
Ummu 'Ammaarah (Radhwiya Allaahu 'nhaa) alikuwa Swahabiyyah anayesifika kwa ushujaa, mwenye kupigiwa mifano katika ustahamilivu na katika malezi bora, uchaji Allaah na katika kutoipa umuhimu dunia mbele ya kupigana na maadui wa Allaah.
Mwanawe Habiyb aliuliwa na Musaylimah Al-Khadhdhaab kwa kukatwa vipande vipande, na mwanawe wa pili akalipa kisasi kwa kumuua Musaylimah akishirikiana na Wahshiy.
Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimpenda sana, na imepokelewa kuwa mara nyingi alikuwa akimuita mwanawe AbduLLaah na kumwambia;
“Njoo tumuombee Du'aa mama yako”
Akawa anakaa naye na kumuombea Du'aa yeye na wanawe na 'ailah yake yote wawe pamoja naye Peponi, jambo ambalo halipati isipokuwa mchaji Allaah kikweli.
Kufariki Kwake
Nusaybah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) alifariki dunia wakati wa ukhalifah wa 'Umar bin Khattwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu).