Ummu Salamah (رضي الله عنها)

Ummu Salamah (رضي الله عنه)
Muhammad Faraj Saalem AS-Saiy (
رحمه الله)

 

Yaliyomo
Nasaba Yake
Anahamia Uhabeshi
Wanarudi Makka
Mkono Wa mwanawe Unavunjika
Anahamia Madiynah
Anajumuika Na Mumewe
Baadhi Ya Sifa Zake
Kufariki Kwake

 

 

Nasaba Yake

Jina lake ni Hind binti Hudhayfah bin Mughiyra Al Makhzumiy (رضي الله عنها) anayetokana na kabila la Quraysh, na baba yake alikuwa maarufu sana kwa ukarimu wake miongoni mwa waarabu, hata akapachikwa jina la ‘Zawadi ya wasafiri’, na hii ni kwa sababu wasafiri wanaofikia kwake hawakuwa na haja ya kuchukuwa mzigo wowote katika safari zao kwa sababu kwake, walikuwa wakipata mahitajio yao yote.

 

Ama mumewe wa mwanzo alikuwa 'AbduLLaah bin 'Abdil-Asad (رضي الله عنه) aliyekuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia katika dini ya Kiislaam. Alisilimu pamoja na mkewe Ummu Salamah (رضي الله عنه) wakati idadi ya Waislaam ilipokuwa chache sana isiyotimia ishirini.

 

Idadi ya Waislaam ilipoanza kuongezeka na Maquraysh walipoanza kuwatesa na kuwafanyia kila aina ya vitimbi ili wawarudishe katika dini ya kuabudu masanamu, na baada ya Rasuli (صلى الله عليه و آله و سلم) kuwataka baadhi yao wahamie Uhabeshi katika Hijrah ya mwanzo, Ummu Salamah pamoja na mumewe (رضي الله عنهما) walikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuutikia wito huo.

Anahamia Uhabeshi

 

Ummu Salamah na mumewe (رضي الله عنهما) waliihama nchi yao na kwenda kuishi ugenini wakiacha nyuma yao nyumba yao nzuri na kila walichokuwa wakimiliki kwa ajili ya kutegemea malipo kutoka kwa Allaah (سبحانه و تعالى)
Juu ya ukarimu wa An-Najashiy Mfalme wa Uhabeshi, na juu ya wema alokuwa akiwatendea wageni wake hao walioihama nchi yao na kukimbilia kwake, lakini shauku ya kurudi Makkah mahali ambapo wahyi ulikuwa ukiteremka ilikuwa ikiongezeka kila wakati unaposogea mbele, na shauku yao ya kurudi na kuishi na kuwa karibu na Rasuli wa Allaah (
صلى الله عليه و آله و سلم) aliyekuwepo huko ilikuwa kubwa zaidi.

 

 

 

Wanarudi Makkah

 

Ummu Salamah pamoja na mumewe (رضي الله عنه) walikuwa daima wakifuatilia habari za Makkah, na uvumi ukaanza kuwafikia kuwa idadi ya Waislamu imeongezeka huko Makkah na kwamba kusilimu kwa Hamzah bin 'Abdul-Muttwallib na 'Umar bin Khattwaab (رضي الله عنهما) kumewapa nguvu Waislaam na kwamba sasa Maquraysh wameacha kuwaudhi na kuwatesa.

 

Uvumi huu uliingiza shauku kubwa sana ya kutaka kurudi Makkah ndani ya nyoyo za Waislaam waliokuwepo Uhabeshi, na baadhi yao wakiwemo Ummu Salamah na mumewe 'AbduLLaah wakawa miongoni mwa watu wa mwanzo kurudi.

Lakini mara baada ya kuwasili Makkah, walivunjika moyo kuona kuwa yote waliyokuwa wakiyasikia yalikuwa ni uvumi mtupu, na kwamba  kusilimu kwa Hamzah na 'Umar bin Khattwaab (رضي الله عنهما) kuliongeza ukhabithi wa makafiri wa Makkah walioanza kuwaonyesha Waislaam kila fani ya kutesa, na Waislaam wakakabiliwa na masaibu makubwa wasiyopata kuyaona katika maisha yao, jambo lililomfanya Rasuli (صلى الله عليه و آله و سلم) awatake Waislamu kuhamia Madiynah.

 

Mkono Wa Mwanawe Unavunjika

 

 

Ummu Salamah na mumewe wakawa miongoni mwa watu wa mwanzo kuitikia wito huo wa Rasuli (صلى الله عليه و آله و سلم) isipokuwa mara hii mambo hayakuwa mepesi kwao.

Hebu tumsikilize Ummu Salamah (رضي الله عنها) akituhadithia yaliyomkuta katika hijrah yake hii.

Anasema Ummu Salamah (رضي الله عنها):

“Mume wangu Abuu Salamah alipotia azma ya kuhajir kwenda Madiynah akanitayarishia ngamia, kisha akatusaidia mimi na mwanangu Salamah kumpanda ngamia huyo na kuianza safari yetu hiyo ndefu huku tukienda taratibu, sisi tukiwa juu ya ngamia na yeye akiwa ameshika hatamu zake huku akituongoza na hakuwa akitazama huku wala kule.

Lakini kabla ya kuuacha mji wa Makkah, jambo la kusikitisha sana likatokea, pale watu wa kabila langu la Bani Makhzum walipotuona na kutujia na kuuzuwia msafara wetu tusiondoke. Wakamwambia mume wangu Abuu Salamah:

“Ikiwa wewe unataka kuondoka, basi unaweza kufanya hivyo, lakini binti yetu huyu utamwacha hapa hapa kwetu.”

Kisha wakanichukuwa kwa nguvu mimi pamoja na mwanangu Salamah, na walipokuwa katika hali ile, watu wa kabila la mume wangu Banu Abdul-Asad wakatuona na kutujia na kusema kwa ghadhabu:

“WaLLahi hatutokuacheni mumchukue mtoto huyu, kwani mtoto huyu ni wetu na sisi ndio tunayemstahikia zaidi.”

Kisha wakaanza kumgombania mwanangu huyo mbele yangu. Watu wa kabila langu wakawa wanamvuta mkono wake mmoja, na watu wa kabila la mume wangu nao wanamvuta mkono mwingine, kila mmoja akimvuta upande wake kwa nguvu mpaka mkono wake ulipochomoka, ndipo watu wa kabila la mume wangu wakafanikiwa kumchukua.

 

Kuanzia hapo nikaanza kuishi maisha ya upweke yaliyojaa majonzi, mbali na mume wangu aliyehajir peke yake kwenda Madiynah, na mbali na mwanangu aliyechukuliwa na watu wa mume wangu akiwa na mkono ulionyofoka.

Ama mimi, nikachukuliwa na watu wa kabila langu Bani Makhzum walionirudisha kwetu baada ya kunitenga na wapenzi wangu wawili hao.

Nikawa kila siku kuanzia wakati wa asubuhi mpaka unapoingia wakati wa magharibi hutoka na kukaa mahali pale yaliponitokea masaibu hayo ya kutenganishwa na mume wangu na kuchukuliwa kwa mwanangu, nikiwa sina kazi nyingine isipokuwa kulia tu mpaka usiku unapoingia.

 

Anahamia Madiynah

 

Nikawa katika hali hiyo karibu mwaka mzima, nikikaa na kujikumbusha ule wakati matukio yale yalipokuwa yakitokea kisha ninalia mpaka unapoingia wakati wa usiku na kurudi nyumbani, mpaka siku ile alipopita mmoja katika jamaa zangu aliyenionea huruma baada ya kuniona katika hali ile, akawaambia watu wa kabila langu:
“Kwa nini hamumuachi masikini huyu ende kuungana na mumewe? Kwa nini mnaendelea kumtenganisha na mumewe?”

Akawa anaendela kuwasemesha mpaka huruma ikaingia nyoyoni mwao, wakaniambia:

“Ukitaka unaweza kwenda kwa mumeo.”.

Lakini vipi nitakwenda kwa mume wangu wakati mwanangu kipande cha ini langu yuko Makkah kwa jamaa zake mume wangu watu wa kabila la Banu Abdil-Asad?

Nitaishi namna gani mimi nikiwa huko Madiynah wakati mwanangu yupo Makka nami sijuwi lolote juu yake?

Watu wa kabila langu wakaiona ile huzuni iliyojaa usoni mwangu na kuhisi yale yaliyokuwa yakipita moyoni mwangu, wakaamua kuwasemesha watu wa kabila la Bani Abdul-Asad wanirudishie mwanangu, ambao walikubali.

 

 

Sikuweza kustahamili kwa furaha iliyonijaa moyoni mwangu baada ya kurudishiwa mwanangu Salamah na kujuwa kuwa sasa ninaweza kusafiri hadi Madiynah kwa mume wangu bila kipingamizi chochote, na kwa ajili hiyo nikaamua hapo hapo kuifunga safari bila kungoja wala kutafuta mtu wa kufuatana naye nikiogopa watu wangu au watu wa kabila la mume wangu wasije wakabadilisha fikra zao na kuamua kunizuwia tena mimi au kumzuwia mwanangu nisisafiri naye.

 

 

Kwa ajili hiyo nikamtayarisha ngamia wangu na kumbebesha vifaa vyangu vya lazima kwa ajili ya safari ndefu hiyo na kuianza safari ya kwenda kwa mume wangu nikiwa peke yangu bila ya mtu wa kufuatana naye.

Nilipowasili mji wa Tan-iym, mji uliopo nje kidogo na Makkah kwa kiasi cha maili tatu, nikakutana na 'Uthmaan bin Twalhah aliyekuwa bado hakusilimu wakati huo, akaniuliza:
“Unaelekea wapi ewe binti wa ‘Zawadi ya wasafiri’?”
Nikamwambia:
“Nakwenda Madina kwa mume wangu.”
Akaniambia:
“Unaye wa kufuatana naye?”
Nikamjibu:
“Hapana WaLLaahi sina isipokuwa Allaah na mwanangu huyu.”
Akaniambia;:
“WaLlaahi sitokuacha usafiri peke yako abadan, mpaka nikufikishe Madiynah.”
Akashika hatamu za ngamia wangu na kuianza safari ya kuelekea Madiynah.

 

WaLLaahi sikupata kusafiri na mtu miongoni mwa waarabu aliye mkarimu na mwenye heshima kuliko yeye. Alikuwa pale ninapotaka kuteremka juu ya ngamia, anamkalisha kisha anasogea mbele kidogo ili niweze kuteremka juu yake bila yeye kuniona, na baada ya kuteremka alikuwa akija na kumfunga ngamia na mti, kisha anajisogeza penye mti mwingine ulio mbali na mimi na kulala chini yake akiwa mbali na mimi.

Wakati wa kuanza safari unapowadia, alikuwa akija kumfungua ngamia, kisha ananitayarishia kwa ajili ya kumpanda, kisha anatangulia mbele kidogo ili asinione huku nikimpanda, na baada ya kumpanda ngamia na kukaa sawa juu yake, huja na kumshika hatamu zake na kumuongoza.

Akawa anaendelea kufanya hivyo kila siku mpaka tulipowasili  mji wa Qubaa (uliopo mbali kidogo na Madiynah kwa kiasi cha maili mbili), akaniambia:

“Mumeo yupo katika kijiji hiki cha Amru bin-'Auf, mwendee kwa baraka za Allaah.”
Kisha akaniacha na kuianza safari ya kurudi Makkah.”

 

 

Anajumuika Na Mumewe

 

Furaha ilioje waliyokuwa nayo siku hiyo pamoja huku machozi ya furaha yakiwatoka pale Ummu Salamah alipojumuika tena na mumewe pamoja na mtoto wao baada ya kufarikiana muda mrefu, na Abuu Salamah (رضي الله عنه) naye alifurahi kupita kiasi.

 

Tokea siku ile siku zikapita kwa haraka sana. Vita vya Badar vikapiganwa na Abuu Salamah (رضي الله عنه) alishiriki katika vita hivyo na kurudi Madiynah pamoja na jeshi la Waislaam wakiwa wamepata ushindi mkubwa mbele ya makafiri.

Kisha vikaja vita vya Uhud, vita ambavyo ndani yake Abuu Salamah alipigana kwa ujasiri mkubwa, lakini akajeruhiwa vibaya sana na kupata majeraha makubwa yaliyomsababisha kuumwa kwa muda mrefu.

Asubuhi moja Rasuli (صلى الله عليه و آله و سلم) alikwenda kumtembelea Abuu Salamah (رضي الله عنه) aliyekuwa amelala juu ya tandiko lake na hali yake ilikuwa mbaya sana, na alipokuwa mlangoni akitoka nje baada ya kumaliza ziara yake, Abuu Salamah akafariki dunia, na Rasuli (صلى الله عليه و آله و سلم) akaitwa na kurudi ndani, na kuyafumba macho ya sahibu yake kwa mikono yake miwili, kisha akaunyanyua uso wake mbinguni na kuomba dua ifuatayo:
“Mola wangu Mghufirie Abuu Salamah madhambi yake, na Mnyanyue daraja yake na Umjaalie awe pamoja na walio karibu Nawe, Umjaalie apate mtu mwema wa kuwalea watoto wake, na Utughufirie sisi na yeye pia ewe Mola wa ulimwengu, Umjaalie nafasi kubwa katika kaburi lake na Umuingizie nuru ndani yake.”

 

Ama Ummu Salamah (رضي الله عنها), baada ya kufariki mumewe yeye alikuwa akiomba du'aah maarufu inayosema:

“Mola wangu kwako nategemea malipo ya msiba wangu huu.”

Lakini hakuwa akipenda kuikamilisha du'aah hii aliyofundishwa na mumewe siku ile alipoingia nyumbani na kumwambia:
“Ewe Ummu Salamah, nilimsikia Rasuli (
صلى الله عليه و آله و سلم) akisema:
“Mtu anapopatwa na msiba kisha akasema: 

ما من مسلم تصيبه مصيبة فيقول ما أمره الله  إنا لله وإنا إليه راجعون   اللهم أجرني في مصيبتي وأخلف لي خيراً منها إلا أخلف الله له خيراً منها

 

Muislaamu yeyote akipatwa na msiba basi aseme, "Sisi ni wa Allaah nasi Kwake tutarejea, Ee Allaah  nilipe kwa msiba wangu na unipe badili yake bora kuliko huo”.

Mtu haombi du'aah hii isipokuwa Allaah Atampa.”

Hakuwa akipenda kuikamilisha kwa sababu alikuwa akijiuliza;

“Kipi kinachoweza kuwa bora kuliko mume wangu Abuu Salamah?”
Lakini alipokumbuka maneno ya mumewe akawa anaiomba du'aah hiyo kwa ukamilifu.

 

Watu wote wa Madiynah walimhurumia sana Ummu Salamah, hasa kwa vile pale Madiynah hapakuwa na mtu wake yeyote isipokuwa wanawe waliokuwa wengi na wadogo wakati ule, na pia alikuwa akilea mayatima watoto wa ndugu yake aliyefariki.

 

Kwa ajili hiyo watu wengi wakataka kumuoa, lakini Ummu Salamah aliwakataa wote wakiwemo Abuu Bakr As-Swidiyq na 'Umar bin Khattwaab (رضي الله عنهما), mpaka pale alipokuja kuposwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه و آله و سلم), na Ummu Salamah ( رضي الله عنها) akamjibu kwa kumwambia;

“Ewe Rasuli wa Allaah, mimi nina ila tatu. Kwanza mimi ni mtu mwenye wivu sana, naogopa nisije nikakughadhibisha kisha Allaah kwa ajili hiyo Akaja kuniadhibisha. Pili mimi ni mwanamke niliyekwisha zeeka, na tatu mimi nina watoto wengi.”

Rasuli (صلى الله عليه و آله وسلم) akamwambia:

“Amma kuhusu wivu wako, namuomba Allaah Akuondolee. Ama kuhusu uzee, hata mimi pia nishazeeka kama wewe. Ama kuhusu kuwa na watoto, basi wanao ni wanangu.”

Ummu Salamah (رضي الله عنها) akakubali kuolewa na  Rasuli (صلى الله عليه و آله و سلم) na kwa ajili hiyo du'aah yake ikawa imekubaliwa kwa kulipwa na Allaah kilicho bora kuliko msiba wa kufiwa na mumewe.

 

 

Baadhi Ya Sifa Zake

 

Ummu Salamah (رضي الله عنها) alikuwa mwanamke mzuri wa umbo, mtulivu wa tabia, mwenye akili yenye uwezo wa kupima mambo, na mwingi wa hekima ambaye Rasuli (صلى الله عليه و آله و سلم) alikuwa mara nyingi akichukuwa ushauri wake katika baadhi ya mambo.

Katika mwaka wa sita baada ya Hijrah, Rasuli (صلى الله عليه و آله و سلم) aliondoka Madiynah kuelekea Makkah akiwa amefuatana na baadhi ya Maswahaba (رضي الله عنهم) kwa niyyah ya kufanya Umrah, lakini Maquraysh walimkatalia  kuingia Makkah, na kwa ajili hiyo vita vikali vikataka kuzuka baina yao.

Baada ya mashauriano na majadiliano yaliyochukuwa muda mrefu, Rasuli (صلى الله عليه و آله و سلم) akakubali kufanya sulhu kwa kuandikiana mkataba na Makafiri hao, mkataba uliokuja kujulikana kwa jina la ‘Sulhu Al-Hudaybia.’.

Jambo hilo halikuwafurahisha Waislaam waliokuwa na hamu kubwa sana ya kupambana na Makafiri hao, na pia kwa sababu mkataba huo ulikuwa na baadhi ya shuruti ambazo kwa dhahiri yake hazikuonekana kuwa ni nzuri, ingawaje undani wake kulikuwa na manufaa kwa Waislaam katika siku za mbele.

Baada ya kumaliza kuandikiana mkataba huo na kupigwa mihuri, Rasuli (صلى الله عليه و آله و سلم) akawataka Waislaam wainuke, wachinje wanyama wao na wanyoe nywele zao, lakini hapana hata mmoja kati yao aliyeinuka.

Rasuli (صلى الله عليه و آله و سلم) akarudia kuwaambia mara tatu:
“Inukeni muchinje wanyama wenu na munyowe nywele zenu,” lakini hapana aliyeinuka kutii amri hiyo wakitarajia kuwa amri ya kupigana jihadi huenda ikateremshwa.

Jambo hilo halikumfurahisha Rasuli (صلى الله عليه و آله و سلم) aliyekwenda moja kwa moja mpaka penye hema la mkewe akaingia ndani na kumhadithia Ummu Salamah (رضي الله عنه) juu ya jambo hilo.

Ummu Salamah (رضي الله عنه) akamwambia:
“Ewe Rasuli wa Allaah, watokee na usimsemeshe yeyote kati yao mpaka utakapomaliza kuchinja na kumwita kinyozi wako akunyoe.”
Rasuli (
صلى الله عليه و آله و سلم) akafanya kama alivyoshauriwa na Mkewe, akatoka na hakumsemesha mtu yeyote mpaka alipomaliza kuchinja na kunyoa, ndipo Maswahaba (رضي الله عنهم) walipoinuka na wao pia wakachinja na kuanza kunyoana nywele zao.

 

 

Kufariki Kwake

 

Ummu Salamah (رضي الله عنه) alifariki dunia katika mwaka wa hamsini na tisa baada ya Hijrah na katika maziko yake aliswaliwa na Abuu Hurayrah (رضي الله عنه).
Anasema Ibni Abiy Khaythamah kuwa Ummu Salamah (
رضي الله عنها) alifariki dunia wakati wa utawala wa Yaziyd bin Muawiyyah (رضي الله عنه).

 

 

 

Share