Imaam Ibn Baaz: Hukmu Ya Mke Kubakia Kuishi Na Mume Asiyeswali
Hukmu Ya Mke Kubakia Kuishi Na Mume Asiyeswali
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
SWALI:
Ni ipi hukmu ya kishariy’ah - kwa mtazamo wenu - kwa mwanamke ambaye anaswali na mumewe haswali, naye (mwanamke huyo) ameshikamana na Swalaah, pamoja na kutambua kuwa, amefanya juhudi kubwa kumkinaisha (mumewe) aswali, lakini haswali hata rakaa moja, naye (mwanamke huyo) anaendelea kusubiri kwa matumaini, je, mnamwelekezaje?
JIBU:
Ambaye haswali anazingatiwa ni Kafiri. Tunamuomba Allaah afya (hifadhi, stara). Hii ndio kauli iliyo sahihi zaidi katika kauli za Wanachuoni katika hii maudhui. Nayo ni kwa (dalili ya) kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Baina ya mtu na baina ya ushirikina na ukafiri ni kuacha Swalaah.” [Muslim]
Na anasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Agano (Kinachotutofautisha) baina yetu (Waumini) na baina yao (Washirikina, Makafiri na Wanafiki) ni Swalaah, anayeiacha (Swalaah) amekufuru.” [At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na An-Nasaaiy]
Swalah ni nguzo ya Uislamu, na yule ambaye haswali hana khayr na wala hazingatiwi kuwa ni Muislamu.
Ni juu yake (mwanamke) kutengana naye na wala asimwachie nafsi yake, ni juu yake aachane naye na kumnyima nafsi yake (mwili wake), na aende kwa familia yake apate kujisalimisha naye na kuachana na matendo yake maovu.
Hili ndilo la sawa.
[Al-Mawqi' Ar-Rasmiy li-Samaahat Ash-Shaykh Al-Imaam Ibn Baaz]