Imaam Ibn Baaz: Hukmu Ya Kuswali Kwenye Miswala Au Mazulia Yenye Mapambo
Hukmu Ya Kuswali Kwenye Miswala Au Mazulia Yenye Mapambo
Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah)
SWALI:
Nini hukmu ya Swalaah kwenye miswala au mazulia yenye kuswaliwa ambayo yamechorwa picha za Misikiti, kwani nimesikia kwamba haifai kuswalia?
JIBU:
Swalaah kwenye mazulia hayo ni sahihi japokuwa yana picha za Misikiti au picha nyinginezo, Swalaah ni sahihi. Lakini inampasa mwenye kuswali achunge sehemu yake ya kuswalia (mazulia au miswala) iwe mbali na nakshi zisizokuwa zenye picha, ikiwa ni Misikitini au kwengineko, ili isimshughulishe na Swalaah yake. Zulia (au Mswala) uwe mtupu usiwe na lolote (lenye michoro au mapicha au marembo). Hivi ndivyo inavyopaswa na ndio salama kwa Muumini. Na ndio maana Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposwali na joho lenye alama za marembo, alipomaliza kuswali na kutoa salaam, alimuagiza (mama 'Aaishah) ipelekwe kwa Abuu Jahm. Akamwambia kuwa: “Imenishughulisha na Swalaah yangu.” Basi lililokusudiwa ni kwamba Muumini ajitahidi achunge katika Swalaah zake na nguo zake na mazulia (au Miswala) ziwe hazina vyenye kumshughulisha. Ziwe mbali na nakshi (marembo) yenye kumshughulisha.
[Fatwa Ibn Baaz, http://www.binbaz.org.sa/noor/5503]