01 - Mambo Ya Haramu Kwa Vinyozi: Kukata Nywele Kwa Mitindo Ya Kikafiri

Mambo ya Haramu yanayofanyika katika kazi ya Unyozi:

 

1. Kukata Nywele Kwa Mitindo Ya Kikafiri

 

Mitindo kama inayojulikana kama “Marines” au “panki” au “denge” na majina mengine mfano wa hayo. Mitindo kama hiyo ya kukata nywele sehemu ya kichwa na kuacha sehemu nyingine. Ima kwa kunyoa kipara kwa maeneo ya pembeni kote na kuacha sehemu ya juu ya kichwa, au kupunguza sana sehemu za chini na kuacha nyingi sehemu ya juu.

Unyoaji huo ujulikanao Kiislamu kama Al-Qaza’ umeharamishwa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye anasema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza (unyoaji wa) Al-Qaza’. [Al-Bukhaariy na Muslim]

Mitindo hiyo ya kunyoa au kupunguza nywele na kuziacha baadhi yake kama mitindo iliyopo sasa watu hunyoa kama kunguru kichwa chote hunyolewa na kuachwa nywele nyingi sehemu moja kama vile utosini na kadhalika, ni mitindo isiyofaa, bali ni mitindo haramu. Hiyo ni katika mtindo inayopendezeshwa na washirikina kwa Waislamu haswa waliofitinishwa na mchezo mpira na muziki; huwa wanawaiga wachezaji na wanamuziki katika kila kitu likiwemo hili la mitindo ya kunyoa nywele zao, hivyo ieleweke kuwa haifai kwani unyoaji huo umekatazwa na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama tulivyoeleza hapo juu katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambayo kwa kirefu ni kama ifuatavyo:

“Kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza Al-Qaza’; akasema: nikamuuliza Naafi’ ni nini Al-Qaza’? Akasema: kunyoa baadhi ya kichwa cha mtoto na na kuacha baadhi yake (panki)” Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Mavazi na mapambo, mlango kuchukiwa kwa Al-Qaza' (kunyoa panki)’.

Ole wake yule anayependa kufufuliwa akiwa pamoja na aliyempenda katika makafiri wacheza mpira au wasanii.

Share