02 - Mambo Ya Haramu Kwa Vinyozi: Kunyoa Ndevu
Mambo ya Haramu yanayofanyika katika kazi ya Unyozi:
2. Kunyoa Ndevu
Unyoaji ndevu kwa vinyozi wengi ni jambo la kawaida sana –ila wale wachache sana waliorehemewa na Allaah- hadi inaonekana ajabu mtu anapowafikishia na kuwajulisha kuwa kazi hiyo ni haramu na inapingana na mafundisho ya dini.
Vinyozi kunyoa wateja wao ndevu au kuzichonga kama ramani fulani au kuzinyoa zote na kubakisha mduara kidevuni ujulikanao kama alama ya "o" kwa kuiga makafiri na wasio na maadili, ni jambo limezoeleka na hata kuwepo picha za mitindo hiyo kwa vinyozi ni kitu kilichoenea sana. Yote hayo ni haramu na yanapingana na mafunzo ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mwenendo wa Rusuli (‘Alayhimus-Salaam) waliotangulia na pia mwenendo wa Maswahaba na wema waliotangulia.
Ndevu ni pambo la mwanamme ambalo limeamrishwa kuliweka na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth nyingi.
Na Wanachuoni wakiwemo ma-Imaam wakubwa wanne wote wamekubaliana kuwa ni haramu kunyoa ndevu.
Baadhi za Hadiyth zenye kuthibitisha uwajibu wa kufuga ndevu kwa wanaume ni hizi zifuatazo:
a- Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru kuziachilia. Amri hii ni ya lazima, kwani hakuna kiashirio chochote kinachoigeuza na kuipeleka katika usunnah. Na kati ya amri hizo ni neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
“Kuweni kinyume na washirikina; fugeni ndevu kwa wingi na punguzeni masharubu.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na neno lake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
“Kateni masharubu na ziachilieni ndevu; nendeni kinyume na wanaoabudu moto.” [Muslim]
b- Ni kwamba kuzinyoa ni sawa na kujifananisha na makafiri kama inavyoonekana katika Hadiyth mbili zilizotangulia.
c- Ni kwamba kuzinyoa ni sawa na kuubadilisha Uumbaji wa Allaah na kumtii Shaytwaan asemaye:
“...na hakika nitawaamrisha, basi watabadili Aliyoyaumba Allaah” [An-Nisaa: 119]
d- Ni kwamba kuzinyoa ni sawa na kujifananisha na wanawake. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake. [Al-Bukhaariy na At-Tirmidhiy]
Na kwa ajili hiyo, Shaykh Al-Islaam amesema:
“Na inaharamishwa kunyoa ndevu zake.” [“Al-Ikhtiyaaraat Al-Fiqhiyyah” cha ‘Alaaud-Diyn Al-Ba’aly, uk.10, na “Al-Furuw’” cha Ibn Muflih (1/291).]
Ibn Hazm na wengineo, wamenukuu Ijmaa’ ya Wanachuoni juu ya uharamu wa kunyoa ndevu.
Amesema Ibn ‘Abdil-Barri (Allaah Amrehemu) katika kitabu chake At-Tamhiyd:“Na ni haramu kunyoa ndevu, na hawanyoi isipokuwa Makhanithi katika wanaume.”
Khanithi ni nani?
Ni yule mwenye tabia za kike, anapenda mambo ya kike kike.
Amesema Al-Imaam Ash-Shanqiytwiy (Allaah Amrehemu) katika Tafsiyr yake Adhw-waau Al-Bayaan:
"Vitofautisho vilivyo wazi mno baina ya mwanamme na mwanamke ni ndevu.”
Wanachuoni wengine wanasema:
"Kunyoa ndevu (jambo hilo) huzingatiwa kuwa ni kujifananisha na wanawake.”
Uharamu wa unyoaji ndevu uko wazi na hauna shaka kwa mwenye kutafuta haki na mwenye kutaka kuifuata Dini yake na mafunzo sahihi yaliyothibiti kutoka kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ama kwa yule mwenye matamanio yake na mpenda dunia, huyo hana la kufanywa ikiwa hataki kukubali haki.
Kadhaalika Wanachuoni wengi wameonelea hata kupunguza ndevu pia ni jambo lisilokubalika, isipokuwa baadhi yao wanaonelea ni makruuh na wengine wanaonelea kuzipunguza kunaruhusiwa pindi zinapozidi mshiko wa kiganja cha mkono. ‘Alaa kulli haal, kwa kifupi kuzipunguza vilevile ni jambo lenye utata na linapaswa kuepukwa.
Mwanachuoni Shaykh ‘Abdul-Muhsin Al-‘Abbaad (Hafidhwahu Allaah) anasema:
“Na mwanaume akinyoa ndevu zake anafanana na mwanamke. Mwanamke ndiye asiyekuwa na ndevu. Mwanaume akinyoa ndevu zake anakuwa kama mwanamke.”
Na akanukuu Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:
“Allaah Kamlaani mwanamme mwenye kujifananisha na wanawake. Na mwanamke mwenye kujifananisha na wanaume.”[Al-Bukhaariy]
Mwisho wa kumnukuu.
Na kujifananisha mwanamme na wanawake, ni pamoja na kunyoa ndevu alizoamrishwa na shariy’ah azifuge, kuvaa hereni, kuvaa mikufu, kutoboa masikio, kusuka nywele na kuvaa mabangili na mfano wa hayo yafanywayo na wanawake.
Na katika mitihani mingine iliyopo vilevile katika saluni zingine za Waislamu, ni kusuka wanaume nywele.
Kunyoa ndevu haifai kabisa, mwanamme Muislamu anatakiwa awe anafuga ndevu na kupunguza masharubu na si kinyume chake; hivyo basi kwa kuwa wewe ni kinyozi bila shaka yoyote wako wanaokuja kutaka uwanyoe ndevu na haya yamekatazwa na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alichoamrisha ni kufuga na kuzikuza ndevu na si kuzinyoa kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliposema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Wakhalifuni washirikina (muwe tofauti na wanavyofanya) wacheni ndevu zenu na punguzeni masharubu yenu – na katika riwaya nyingine: kupunguza masharubu ni katika fitwrah (maumbile ya asli – Uislamu -)” [Al-Bukhaariy]
Na Ahaadiyth za kuamrishwa kufuga ndevu ni nyingi mno.