11 - Hitimisho: Maelekezo Inavyopaswa Saluni Ya Muislamu Anayechunga Mipaka Ya Shariy’ah
Mambo ya Haramu yanayofanyika katika kazi ya Unyozi:
11. Mwisho Tunahitimisha Kwa Maelekezo Ya Namna Inavyopaswa Kuwa Saluni Ya Muislamu Anayechunga Mipaka Ya shariy’ah Na Kumcha Allaah
Kinyozi wa Kiislamu mwenye kuchunga maadili ya Kiislamu na kuchunga shariy’ah ya Dini yake, anapaswa kuwa makini na kazi yake na kuchunga kutokiuka mipaka yoyote ile ya shariy’ah njema na bora ya Uislamu. Achunge mambo yafuatayo:
- Saluni yake isiwe na mambo mengi makuu wala vivutio vya haramu akidhani kuwa ndio sababu ya kupata wateja wengi.
- Anyoe kwa mujibu wa shariy’ah inavyofundisha.
- Kichwa akinyoe kwa kiwango sawa; saizi moja kichwa chote; wala kusiwe juu namba kubwa na chini namba ndogo ya chanuo za mashine. Asinyoe panki/denge.
- Asiweke madoido ya kuchonga chonga au kukichora kichwa kwa mitindo ya nywele.
- Asinyoe ndevu zake wala za wateja wake. Wala asichonge ndevu au kuzipunguza au kuzitengeneza kwa staili mbalimbali.
- Asinyoe wanawake.
- Asinyoe nyusi japo wanaume.
- Asiweke kwenye saluni yake mchanganyiko wa wafanyakazi wa kiume na kike.
- Asiweke mapicha kwenye saluni yake kwani Malaika hawaingii sehemu yenye picha kama Hadiyth inavyotueleza hapa chini
Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“…Hakika Malaika hawaingii nyumba ambayo ina picha.” [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]
- Asiweke vivutio vya haramu kama muziki na yenye utata kama televisheni. Uharamu wa muziki uko wazi kwenye Aayah na Hadiyth mbalimbali.
Anasema Allaah Aliyetukuka:
"Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Allaah pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha." [Luqmaan: 6]. Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema kuhusu Aayah hii "Naapa kwa Allaah hii inamaanisha ni kuimba" [At-Twabariy 20:12]
Na Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) pia amesema kuhusu Aayah: "Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi. Ni nyimbo na maneno ya yanayofanana (ya upuuzi)" [Isnaad Sahiyh kutoka kwa Shaykh Al-Albaaniy]
Na amesema vilevile Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam:
"Watakuweko watu katika Ummah wangu watakaojaribu kuhalilisha zinaa, uvaaji wa hariri, pombe na muziki. Baadhi ya watu watakuwa pembeni mwa mlima na mchungaji wao atawajia jioni na kuwaomba haja [fulani]. Watasema: "Rudi kesho." Allaah Atawaangamiza usiku, Atawaangushia milima kisha Atawabadilisha waliobakia wawe nyani na nguruwe na watabakia hivyo hadi siku ya Qiyaamah." [Al-Bukhaariy]
- Asiruhusu vigenge vya wapoteza wakati na wasengenyaji. Yeye mwenyewe ajichunge na kusengenya na umbea.
- Akiwa ni mwenye maarifa ya dini japo kidogo, atumie fursa hiyo kulingania wateja wake na kuwakumbusha ya dini.
- Achunge sana na kuhifadhi vipindi vya Swalaah. Asikose Swalaah kwa sababu ya mteja; bora apoteze mteja kuliko kupoteza Swalaah. Kipengele namba 5 juu.
Kinyozi wa Kiislamu anapaswa aamini kuwa kipato na rizki yake vyote hivyo vinatoka kwa Allaah Aliyetukuka, na atambue kuwa hawezi kwa ujanja wake kuongeza kipato chake, wala kwa khofu yake ya rizki kuwa atapungukiwa na kipato chake.
Atambue kuwa Allaah Anamruzuku yule anayemtegemea Yeye kikamilifu, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)
“Na anayemcha Allaah Humtengezea njia ya kutokea.
“Na Humruzuku kwa jiha asiyotazamia. Na anayemtegemea Allaah, Yeye Humtosha. Hakika Allaah Anatimiza amri Yake. Allaah Kajaalia kila kitu na kipimo chake.” [Atw-Twalaaq: 2-3].
Na anapaswa amtegemee Allaah kidhati kwani Allaah Atamruzuku yeye kama anavyomruzuku ndege. Imepokewa kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
“Ikiwa nyinyi mtamtegemea Allaah upeo wa kumtegemea basi Atawaruzuku nyinyi kama Anavyomruzuku ndege. Anatoka katika kiota chake asubuhi tumbo lake likiwa tupu na anarudi likiwa tumbo lake limejaa” [At-Tirmidhiy, Ahmad na Ibn Maajah na Isnadi yake ni Swahiyh]
Ingawa unyozi ni ajira yako, lakini vilevile usisahau kazi yako ya asili ambayo imeasisiwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuendelezwa na kila anayempenda, kazi ya kuwalingania wateja Waislamu kwa kuwaeleza hayo uliyoyapata na kuwakataza bali kuwawekea wazi kuwa wewe kinyozi lakini unapenda uwe na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Siku ya Qiyaamah hivyo, hautokuwa tayari kutekeleza alichokikataza Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata kama kitakutilia kipato kikubwa, vinginevyo elewa kuwa utakuwa unachangia katika kuipinga na kuikebehi bali kuibeza amri ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wenye kuibeza au kuipinga amri yake Qur-aan inawatahadharisha kwa kusema hivi:
“ …. Basi na watahadhari wanaokhalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu iumizayo.” [An-Nuwr: 63]
Mwisho, tunawanasihi vinyozi wa Kiislamu, wachunge mipaka ya Allaah na Mjumbe Wake katika kazi zao na wawe na msimamo thabiti katika dini yao na Allaah Awajaalie waweze kujiepusha na makatazo na haramu zote hizo ambazo zinahusiana na kazi hiyo.
Na Allaah ni Mjuzi zaidi.
Na Swalaah na Salaam ziwe juu ya Rasuli wa Allaah na jamaa zake na Swahaba zake.