12 - Nasaha Kwa Vinyozi - Makala Kamili

Nasaha Kwa Vinyozi

 

www.alhidaaya.com

 

 

Kazi ya unyozi ni kazi ambayo asli yake ni halali, lakini ni kazi ambayo imeingizwa uharamu mwingi sana na waifanyao kazi hiyo. Aidha kwa kuiga wasio Waislamu katika utekelezaji wa kazi hiyo, au kwa ujinga na kukosekana ufuatwaji wa mafunzo sahihi ya kishariy’ah katika kuitekeleza kazi hiyo.

 

Aghlabu mtu anapokwenda kwa vinyozi wengi hukutana na mambo yafuatayo ya haramu:

  1. Kunyolewa watu nywele kwa mitindo mbalimbali ya kuiga makafiri na watu wasio na maadili, unyoaji ambao unapingana na shariy’ah na mafunzo aliyofundisha mbora wa viumbe, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
  2. Unyoaji wa ndevu.
  3. Unyoaji wa nyusi.
  4. Vikao vya usengenyaji na umbea. Kuweka miziki na televisheni.
  5. Aghlabu vinyozi wengi hukosa Swalaah au kwa uchache kukosa Swalaah kwa wakati.
  6. Mengine katika hizo kazi za unyoaji hupelekea vinyozi wengi kufanya matendo kinyume na urijali.
  7. Kubandikwa mapicha mbalimbali ndani ya saluni zao.
  8. Baadhi ya vinyozi kuweka wanawake wa kuwaosha wanaume nywele zao na hata wengine kuchuliwa (massage) na wanawake.
  9. Baadhi ya saluni vinyozi huwanyoa nywele wanawake.
  10.  Baadhi ya watu wanaojinasibisha na uongozi wa dini wanachangia sana kudumisha mitihani hiyo kwa kuwakumbatia vinyozi wafanyao maasi na hata kuwashirikisha kwenye uongozi wa mambo ya dini.

 

​ 11. ​Mwisho tutahitimisha kwa maelekezo ya namna inavyopaswa kuwa saluni ya Muislamu anayechunga mipaka ya shariy’ah na kumcha Allaah.

 

 

Kinyozi wa Kiislamu anapaswa ajiepushe na yote hayo yaliyoelezwa katika vipengele hapo juu ili kuilinda Dini yake na heshima yake na vilevile kazi yake iwe ni halali na iwe yenye kipato cha halali na vilevile iwe ni kazi yenye kumridhisha Allaah (‘Azza wa Jalla).

 

Inasikitisha sana kupita kiasi, kuona vinyozi wengi wa Kiislamu hawana tofauti yoyote na vinyozi makafiri kwa namna wanavyofanya kazi zao na hata mionekano ya sehemu zao za kazi.

 

Unapokwenda au kupita maeneo ya kazi ya vinyozi wengi wa Kiislamu, huwezi kuona tofauti yoyote ile na maeneo ya kazi ya makafiri. Kuanzia unyoaji, utendaji mzima wa kazi hiyo, usengenyaji, umbea, upotezaji wakati, mapicha ya wasanii na waigizaji wa kikafiri, na mfumo mzima wa mazingira yaliyomo humo ndani.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema katika Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

“Anayejifananisha na watu, basi ni miongoni mwao.” [Hadiyth hii iliyokusanywa na Abuu Daawuwd japo ina kauli tofauti, lakini ni Hadiyth Hasan kwa mujibu wa Imaam Ibn Hajr na vilevile Shaykh Al-Albaaniy, na ni Jayyid kwa mujibu wa Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah]

 

Maana ya “anayejifananisha na watu, basi atakuwa ni miongoni mwao” ni kuwa, atakuwa miongoni mwao kwa madhambi. Atashirikiana na hao anaojifananisha nao kwa madhambi.

 

Shaykh Al-Islaam ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) anasema:

“Hii Hadiyth inaonesha kwa dhahiri kuwa ni haramu kuwaiga watu (makafiri) na japokuwa udhahiri wake unaonesha kuwa anayewaiga, basi naye ni kafiri kama ambavyo Aayah inavyodhihirisha hilo:

“…Na yeyote atakayewafanya marafiki wao wandani; basi hakika yeye ni miongoni mwao...” [Al-Maaidah: 51]

[Mwisho wa kumnukuu Shaykh Al-Islaam katika kitabu chake Iqtidhwaau Swiraatw Al-Mustaqiym, uk, 83]

 

Aayah hiyo kwa ukamilifu inaeleza hivi:

“Enyi mlioamini! Msifanye Mayahudi na Manaswara marafiki wandani na ushirikiano. Wao kwa wao ni marafiki wandani. Na yeyote atakayewafanya marafiki wao wandani; basi hakika yeye ni miongoni mwao. Hakika Allaah Haongoi watu madhalimu.” [Al-Maaidah: 51]

 

Kadhaalika, makafiri hawatoridhika nawe hata uwaige utakavyowaiga. Anasema Allaah Aliyetukuka: 

"Na hawatoridhika nawe Mayahudi wala Manaswara mpaka ufuate mila zao. Sema: “Hakika mwongozo wa Allaah ndio mwongozo (pekee).” Na ukifuata hawaa zao baada ya yale ambayo yaliyokujia katika elimu, basi hutopata kutoka kwa Allaah mlinzi yeyote wala mwenye kunusuru." [Al-Baqarah: 120]

 

 

 

Mambo ya Haramu yanayofanyika katika kazi ya Unyozi:

 

  1. Kukata Nywele Kwa Mitindo Ya Kikafiri

 

Mitindo kama inayojulikana kama “Marines” au “panki” au “denge” na majina mengine mfano wa hayo. Mitindo kama hiyo ya kukata nywele sehemu ya kichwa na kuacha sehemu nyingine. Ima kwa kunyoa kipara kwa maeneo ya pembeni kote na kuacha sehemu ya juu ya kichwa, au kupunguza sana sehemu za chini na kuacha nyingi sehemu ya juu.

Unyoaji huo ujulikanao Kiislamu kama Al-Qaza’ umeharamishwa na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye anasema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza (unyoaji wa) Al-Qaza’. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Mitindo hiyo ya kunyoa au kupunguza nywele na kuziacha baadhi yake kama mitindo iliyopo sasa watu hunyoa kama kunguru kichwa chote hunyolewa na kuachwa nywele nyingi sehemu moja kama vile utosini na kadhalika, ni mitindo isiyofaa, bali ni mitindo haramu. Hiyo ni katika mtindo inayopendezeshwa na washirikina kwa Waislamu haswa waliofitinishwa na mchezo mpira na muziki; huwa wanawaiga wachezaji na wanamuziki katika kila kitu likiwemo hili la mitindo ya kunyoa nywele zao, hiyvo ieleweke kuwa haifai kwani unyoaji huo umekatazwa na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama tulivyoeleza hapo juu katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambayo kwa kirefu ni kama ifuatavyo:

“Kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza Al-Qaza’; akasema: nikamuuliza Naafi’ ni nini Al-Qaza’? Akasema: kunyoa baadhi ya kichwa cha mtoto na na kuacha baadhi yake (panki)” Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Mavazi na mapambo, mlango kuchukiwa kwa Al-Qaza' (kunyoa panki)’.

 

Ole wake yule anayependa kufufuliwa akiwa pamoja na aliyempenda katika makafiri wacheza mpira au wasanii.

 

 

2. Kunyoa Ndevu

 

Unyoaji ndevu kwa vinyozi wengi ni jambo la kawaida sana –ila wale wachache sana waliorehemewa na Allaah- hadi inaonekana ajabu mtu anapowafikishia na kuwajulisha kuwa kazi hiyo ni haramu na inapingana na mafundisho ya dini.

 

Vinyozi kunyoa wateja wao ndevu au kuzichonga kama ramani fulani au kuzinyoa zote na kubakisha mduara kidevuni ujulikanao kama alama ya "o" kwa kuiga makafiri na wasio na maadili, ni jambo limezoeleka na hata kuwepo picha za mitindo hiyo kwa vinyozi ni kitu kilichoenea sana. Yote hayo ni haramu na yanapingana na mafunzo ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mwenendo wa Rusuli (‘Alayhimus-Salaam) waliotangulia na pia mwenendo wa Maswahaba na wema waliotangulia.

 

Ndevu ni pambo la mwanamme ambalo limeamrishwa kuliweka na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth nyingi.

Na Wanachuoni wakiwemo ma-Imaam wakubwa wanne wote wamekubaliana kuwa ni haramu kunyoa ndevu.

Baadhi za Hadiyth zenye kuthibitisha uwajibu wa kufuga ndevu kwa wanaume ni hizi zifuatazo:

 

a- Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru kuziachilia. Amri hii ni ya lazima, kwani hakuna kiashirio chochote kinachoigeuza na kuipeleka katika usunnah. Na kati ya amri hizo ni neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

“Kuweni kinyume na washirikina; fugeni ndevu kwa wingi na punguzeni masharubu.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na neno lake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

“Kateni masharubu na ziachilieni ndevu; nendeni kinyume na wanaoabudu moto.” [Muslim]

 

b- Ni kwamba kuzinyoa ni sawa na kujifananisha na makafiri kama inavyoonekana katika Hadiyth mbili zilizotangulia.

 

c- Ni kwamba kuzinyoa ni sawa na kuubadilisha Uumbaji wa Allaah na kumtii Shaytwaan asemaye:

“...na hakika nitawaamrisha, basi watabadili Aliyoyaumba Allaah” [An-Nisaa: 119]

 

d- Ni kwamba kuzinyoa ni sawa na kujifananisha na wanawake. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake. [Al-Bukhaariy na At-Tirmidhiy]

 

Na kwa ajili hiyo, Shaykh Al-Islaam amesema:

“Na inaharamishwa kunyoa ndevu zake.” [“Al-Ikhtiyaaraat Al-Fiqhiyyah” cha ‘Alaaud-Diyn Al-Ba’aly, uk.10, na “Al-Furuw’” cha Ibn Muflih (1/291).]

Ibn Hazm na wengineo, wamenukuu Ijmaa’ ya Wanachuoni juu ya uharamu wa kunyoa ndevu.

 

Amesema Ibn ‘Abdil-Barri (Allaah Amrehemu) katika kitabu chake At-Tamhiyd:

“Na ni haramu kunyoa ndevu, na hawanyoi isipokuwa Makhanithi katika wanaume.”

 

Khanithi ni nani?

Ni yule mwenye tabia za kike, anapenda mambo ya kike kike.

 

Amesema Al-Imaam Ash-Shanqiytwiy (Allaah Amrehemu) katika Tafsiyr yake Adhw-waau Al-Bayaan:

"Vitofautisho vilivyo wazi mno baina ya mwanamme na mwanamke ni ndevu.”

 

Wanachuoni wengine wanasema:

"Kunyoa ndevu (jambo hilo) huzingatiwa kuwa ni kujifananisha na wanawake.”

 

Uharamu wa unyoaji ndevu uko wazi na hauna shaka kwa mwenye kutafuta haki na mwenye kutaka kuifuata Dini yake na mafunzo sahihi yaliyothibiti kutoka kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ama kwa yule mwenye matamanio yake na mpenda dunia, huyo hana la kufanywa ikiwa hataki kukubali haki.

 

Kadhaalika Wanachuoni wengi wameonelea hata kupunguza ndevu pia ni jambo lisilokubalika, isipokuwa baadhi yao wanaonelea ni makruuh na wengine wanaonelea kuzipunguza kunaruhusiwa pindi zinapozidi mshiko wa kiganja cha mkono. ‘Alaa kulli haal, kwa kifupi kuzipunguza vilevile ni jambo lenye utata na linapaswa kuepukwa.

 

Mwanachuoni Shaykh ‘Abdul-Muhsin Al-‘Abbaad (Hafidhwahu Allaah) anasema:

“Na mwanaume akinyoa ndevu zake anafanana na mwanamke. Mwanamke ndiye asiyekuwa na ndevu. Mwanaume akinyoa ndevu zake anakuwa kama mwanamke.”

Na akanukuu Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

“Allaah Kamlaani mwanamme mwenye kujifananisha na wanawake. Na mwanamke mwenye kujifananisha na wanaume.”[Al-Bukhaariy]

Mwisho wa kumnukuu.

 

Na kujifananisha mwanamme na wanawake, ni pamoja na kunyoa ndevu alizoamrishwa na shariy’ah azifuge, kuvaa hereni, kuvaa mikufu, kutoboa masikio, kusuka nywele na kuvaa mabangili na mfano wa hayo yafanywayo na wanawake.

Na katika mitihani mingine iliyopo vilevile katika saluni zingine za Waislamu, ni kusuka wanaume nywele.

 

Kunyoa ndevu haifai kabisa, mwanamme Muislamu anatakiwa awe anafuga ndevu na kupunguza masharubu na si kinyume chake; hivyo basi kwa kuwa wewe ni kinyozi bila shaka yoyote wako wanaokuja kutaka uwanyoe ndevu na haya yamekatazwa na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alichoamrisha ni kufuga na kuzikuza ndevu na si kuzinyoa kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) aliposema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Wakhalifuni washirikina (muwe tofauti na wanavyofanya) wacheni ndevu zenu na punguzeni masharubu yenu – na katika riwaya nyingine: kupunguza masharubu ni katika fitwrah (maumbile ya asli – Uislamu -)” [Al-Bukhaariy]

 

Na Ahaadiyth za kuamrishwa kufuga ndevu ni nyingi mno.

 

 

3. Kunyoa Nyusi

 

Vilevile baadhi ya vinyozi hukata vijana wa kiume nyusi. Vijana wanaoiga wanamuziki na wachezaji mpira. Kijana akiona mcheza mpira maarufu kaweka mistari kwenye nyusi zake naye aenda kumuiga.

 

Vinyozi wanapoendewa na vijana kama hao, wao “pesa mbele dini baadae” wanatekeleza wateja wao wanavyotaka. Mteja akikaa tu kwenye kiti, akiamrisha afanyiwe mtindo wowote, basi naye kinyozi asiyejitambua ambaye ima hajui chochote kuhusu mafunzo ya dini yake na hataki kujishughulisha kujua, au anajua lakini pesa imegeuka kuwa ndio dini yake, basi hutekeleza yale mteja anayoyataka tena wakati mwengine kwa fakhari aonekane mnyoaji mahiri na hakuna mtindo unaomshinda!

 

Kutoka kwa 'Abdullah bin Mas'uwd (Radhwiya Allahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Amewalaani watu wenye kuwachanja wenzao (tattoo) na wenye kuchanjwa, na wenye kuwanyoa wenzao nyusi na wenye kunyolewa na wenye kuchonga meno yao (kama kufanya mwanya) kwa ajili ya kujipamba kubadilisha maumbile ya Allaah) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kitendo cha unyoaji nyusi japo kwa mazoea kinafanywa na wanawake, na laana hizo zinawaendea wanaofanya na kuwafanyia wenzao hivyo, lakini kwa mwanamme laana inakuwa ni kali zaidi kwani kunapatikana maharamisho mawili ndani yake; ya kunyoa nyusi na ya kujifanananisha na wanawake.

 

Eee mja ikiwa unamuogopa Mola wako na Siku ya Mwisho na adhabu ya Moto, jiepushe na matamanio hayo machafu ya kipumbavu ambayo hayakunufaishi chochote wala kukuongezea zaidi ya kumuasi Mola wako na kujipalilia adhabu Yake isiyostahamilika.

 

 

4. Vikao Vya Kusengenya Na Umbea

 

Mara nyingi katika saluni za kunyolea, kunakuwa na mazungumzo ya kusengenya na umbea umbea mwingi. Hususan saluni hizi ambazo tunazizungumzia hapa zenye sifa zisizo za Kiislamu.

 

Si rahisi kukuta vinyozi wengi kufanya kazi zao huku wanamtaja Allaah na kumsabbih au kumhimidi au kufanya istighfaar au kwa uchache kufanya kazi kimya kimya. Utakuta ni wazungumzaji na wenye soga nyingi za kipuuzi wakidhani ndio kumfurahisha mteja au kumchangamsha. Na ikiwa mteja si mtu wa upuuzi na hapendi usengenyaji au umbea au hawajamzoea, basi wao kwa wao huendeleza mazungumzo ya kipuuzi au ya kidunia. Ni nadra sana kukuta kuna mazungumzo ya dini ya kufaidishana. Hata yakiwepo mazungumzo ya dini, basi ni yale hasi na si chanya. Ima watakosoa mambo ya dini ambayo wao hawako tayari kuyatekeleza kama haya tunayoyataja humu ndani yasiyofaa wao kuyafanya, au utawakuta wanasengenya watu wanaojishughulisha na Dini na Da’wah.

 

Katika mifano hai ambayo iko tele, lakini tukigusa mifano miwili mitatu, kuna baadhi ya saluni ndio vituo vikubwa vya watu wapinzani wa dini, na wale wasioswali, wale mabingwa wa kusengenya na umbea na mipasho, na hata wale maadui wakubwa wa dini kama wale watukanao Maswahaba.

 

Katika saluni za moja ya miji ya Ulaya, kuna adui mmoja wa dini ambaye saluni hiyo ni kituo chake kikubwa cha kupotezea wakati na kupotosha itikadi za Waislamu. Waislamu hao wenye saluni ni watu wanaojinasibisha na Usunni lakini wasiotaka kujishughulisha na elimu na wajuaji wasiotaka kufunzwa. Adui huyo maarufu kazi yake ni kwenda kuwatia hao wenye saluni na wateja wao, mashaka katika dini yao kama kuwatia kasoro Maswahaba na kuwatukana, pia kuhalalisha haramu kama ribaa za benki akiwakinaisha hao wasiojitambua huku akiwachezea kwa kuzipindua Aayah na kuzibadilisha maana, vilevile kuhalalisha ndoa ya muda, kuhalalisha unyoaji ndevu kwani yeye mwenyewe kajipamba kwa sifa ya uke, kuhalalisha mavazi yaliyokatazwa uvaaji wake kama vile mwanamme kuburuza nguo n.k, kwani yeye mwenyewe nguo zake zinafagia barabara na hana alama ya kutambulisha Uislamu wake si kwa dhahiri wala kimatendo! Na zaidi adui huyo huwatukana Wanachuoni wa haki na hata Walinganiaji wa dini na kuwabeza kwa sababu hawakubaliani na itikadi yake ya kikafiri.

 

Na maskini hao wajuaji wenye masaluni hayo wasiojua chochote zaidi ya kusengenya, huwa wakimsikiliza adui huyo muovu na kuvutika naye kwa sababu huwa anawapeleka kule kule matamanio yao yanapotaka!

 

Jambo la kushangaza, adui huyo wa dini mwenye chuki na Maswahaba kama ilivyo dini yao ambayo inajinasibisha na Uislamu ilhali Uislamu uko mbali nao, anashinda masaa mengi kwenye saluni hiyo kupoteza watu na akionekana kuzungumzia mambo ya dini lakini haonekani kuswali na nyakati zote za Swalaah zinamkuta akipiga domo hapo kuwapoteza wajinga wajuaji wasiotaka kujishughulisha na elimu. Lakini  hao wenye saluni, hawana hata ile akili ndogo ya kujiuliza mbona huyu kiumbe anajifanya kuzungumzia mambo ya dini na kuyachambua lakini hata haendi kuswali???

 

Huo ni mfano mmoja wa mabalaa yanayopatikana kwenye saluni za Waislamu wasiojitambua na wasiotaka kufuata mafunzo ya dini yao, achilia mbali mazungumzo ya kutiana mashaka mashaka katika masaail mbalimbali ya dini wakibeza Sunnah za Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kufanyia maamrisho ya dini istihzai. Wakibeza mavazi, madhahiri (mionekano) ya watu wanaofuata Sunnah, na hata wakibeza mafunzo mbalimbali ya dini...

 
Allaah Anasema kuwaelekezea watu sampuli hiyo:
 

“Na ukiwauliza, bila shaka watasema: “Hakika tulikuwa tunaporoja na tunacheza.” Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayaat Zake na Rasuli Wake?

“Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu. Tukilisamehe kundi miongoni mwenu, Tutaliadhibu kundi (jingine), kwa kuwa wao walikuwa wahalifu.” [At-Tawbah: 65-66]

 

Vilevile kunajadiliwa maisha ya watu, hali ya kuwa wao wenyewe wana mabalaa makubwa yasiyoelezeka. Lakini mara nyingi mtu hajioni aibu zake.

 

 

5. Aghlabu Vinyozi Wengi Hukosa Swalaah Au Kwa Uchache Kukosa Swalaah Kwa Wakati

 

Kama tulivyogusia katika kipengele kilichotangulia, vinyozi wengi hawaswali na wale wanaoswali hawaswali kwa kipindi. Wengi wanapitwa na Swalaah kwa khofu ya kumuacha mteja wake anamsubiri au khofu ya wateja kumkimbia!

 

Maskini hawatambui kuwa rizki yao ishakadiriwa na Allaah, na hata wafanye ujanja wote na hila zote na mbinu zote hawatoweza kuongeza kile walichokadiriwa.

 

Khofu hiyo ya rizki na pia zaidi ni tamaa ya kupata zaidi na kutajirika na kuwa na maisha mazuri na kushindana na walio juu yao kidunia, huwapelekea hata vinyozi wengine katika baadhi ya miji wakionekana kwenda kufanya vibarua vingine vya ziada vya kuzidisha kipato japo utaona kazi yake inamuingizia kipato cha kutosha – japo kwa haramu nyingi kama tulivyoona juu -.

 

Tamaa na kukosa kuridhika, kunachangia sana katika kukiukwa maamrisho ya Allaah na Mtume Wake na ni sababu ya maasi kuzidi.

 

Saluni zingine ziko karibu na Misikiti lakini hata hawajui nyakati za Jamaa’ah hususan kuna maeneo Adhana haisikiki nje. Kuna mteja mmoja alikwenda kukatwa nywele na ilipofika karibu na Swalaah ya Maghrib akauliza Maghrib bado dakika ngapi, basi hakuna katika waliokuwemo humo ndani aliyemjibu. Akaaga na kuwahimiza kwenda kuswali, wakamwambia tunakuja “ya kumtoa njiani”!

Hiyo ndio misiba katika misiba mingi iliyomo kwenye maeneo hayo.

 

Wale wanaojitahidi kuswali, basi hupishana hapo hapo saluni, mmoja ataingia pembeni kuswali "Swalaah ya kuwahi mteja asiondoke", na kisha mwenzake kukipungua wateja naye ndio atakwenda kuswali hata kama muda wa Swalaah umekwisha au zimepandiana Swalaah mbili au tatu kwa wakati mmoja!

Tunawazindua umuhimu wa Swalaah na madhara ya mwenye kutokuswali au kuzipuuza Swalaah kwa kuswali atakavyo au kuswali na kuacha.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa wale wanaopoteza Swalah zao:

"Lakini wakaja baada yao walio wabaya, wakaacha Swalah, na wakafuata matamanio. Basi watakuja kuta malipo ya ubaya." [Maryam: 59]

 

Kutoka kwa Jaabir bin 'Abdillaah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika Baina ya mtu na shirki, na kufru, ni kuacha Swalaah." [Muslim]

 

Kutoka kwa Buraydah bin Al-Haswiyb (Radhiya Allaahu 'anhu ambaye amesema: "Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Ahadi (mafungamano) baina yetu na baina yao (wasio Waislam) ni Swalaah, atakayeiacha atakuwa amekufuru." [Ahmad, Abu Daawuwd, An-Nasaaiy na Ibn Maajah]

 

Anasema Ibn Hazm;

“Imepokelewa kutoka kwa 'Umar bin Khatwtwaab na 'Abdur-Rahmaan bin 'Awf na Mu'aadh bin Jabal na Abu Hurayrah na Maswahaba wengi (Radhwiya Allaahu 'anhum) kuwa: “Atakayeacha kuswali (Swalaah moja tu ya) fardhi kusudi (bila ya udhuru wowote) mpaka wakati wake (Swalaah hiyo) ukatoka, anakuwa kafiri.”

 

Imaam Ash-Shawkaaniy amesema: 

“Kwa hakika asiyeswali ni Kafiri, kwa sababu Hadiyth zote zilizopokelewa katika maudhui haya zinamwita hivyo (kuwa ni kafiri), na mpaka uliowekwa baina ya mtu anayestahiki kuitwa kafiri na yule asiyestahiki kuitwa kafiri ni Swalaah.”

 

Vile vile asiyeswali atafufuliwa na watu waovu kabisa siku ya Qiyaamah kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika riwaya ifuatayo:

Kutoka kwa 'Abdullaah bin 'Amru bin Al-'Aasw: "Atakayeihifadhi atakuwa na mwanga na uongofu, na kufuzu siku ya Qiyaamah, na asiyeihifadhi hatokuwa na mwanga wala uongofu wala kufuzu, na siku ya Qiyaamah atakuwa pamoja na Qaaruwn, Fir'awn, Haamaan na Ubayy bin Khalaf." [Musnad Ahmad ikiwa na isnaad Swahiyh]

 

Katika kuifasiri Hadiyth hii, anasema mwanachuoni maarufu Ibn Qayyim Al-Jawziyyah:

“Mwenye kuacha Swalah huwa ameshughulika na mojawapo kati ya yafuatayo; ama atakuwa imemshughulisha mali yake au ufalme wake au cheo chake au biashara zake. Yule aliyeshughulika na mali yake, atafufuliwa pamoja na Qaaruwn, na aliyeshughulika na ufalme wake, huyo atakuwa pamoja na Fir'awn, na aliyeshughulika na cheo chake atakuwa pamoja na Haamaan na yule aliyeshughulika na biashara zake (akaacha kuswali), huyo atakuwa pamoja na Ubayy bin Khalaf.”

 

 

6. Mengine Katika Hizo Kazi Za Unyoaji Hupelekea Vinyozi Wengi Kufanya Matendo Kinyume Na Urijali

 

Katika misiba iliyopo kwa vinyozi hao wenye kutumbukia kwenye haramu hizo, katika hiyo kazi ya kunyoa ndevu za wanaume, kunafikia hadi wakageuka kama wanawake. Maeneo mengi, vinyozi baada ya kumaliza kumnyoa mwanaume ndevu, humpaka aidha majimaji ya marashi yenye kuwasha yajulikanayo kama “after shave” au humpaka poda! Na katika upakaji huo anampapasa kidevu na mashavu na kumsugua kama anamfanyia “massage”!

Hali hiyo inakwenda kinyume na urijali, mwanamme hapaswi kuwa hivyo kabisa!! Si kazi ya kiume hiyo, na isitoshe tayari mwanzo kushapatikana uharamu wa kunyoa ndevu! Allaahul-Musta’aan.

 

 

7. Kubandikwa Mapicha Mbalimbali Ndani Ya Saluni Zao Na Kuwakimbiza Malaika Katika Maeneo Yao

 

Inafahamika kuwa Malaika hawaingii sehemu yenye picha, na isitoshe picha zenyewe nyingi wanazobandika ni za watu zenye kuonesha mitindo ya nywele ya kikafiri na za ukosefu wa adabu na maadili. Na picha zingine ni za wanamuziki wakosa maadili na watu wajinga waliokosa mielekeo katika hii dunia.

 

Imepokewa kwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kuwa niliupamba mto wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na picha (michoro) za wanyama ambacho kilionekana kama mto mdogo. Alikuja akasimama kati ya watu akiwa na taharuki iliyoonekana usoni mwake. Nikasema, “Ee Rasuli wa Allaah! Kuna nini?” Akasema: “Huu mto ni wa nini?” Nilisema: “Nimeutayarisha kwa ajili yako ili upate kuuegemea.” Alisema: “Kwani wewe hujui kuwa Malaika hawaingii katika nyumba ambazo kuna picha ndani yake; na yeyote mwenye kutengeneza picha ataadhibiwa Siku ya Qiyaamah na ataambiwa kukipatia uhai (kwa alichokiumba).” [Al-Bukhaariy]

 

Mambo ya picha za viumbe ni ya kuepukwa kwa makemeo makali yatokayo kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyosimulia Ibn Mas‘uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Hakika aliye na adhabu kali zaidi ya wote Siku ya Qiyaamah ni watengeneza picha.” [Al-Bukhaariy, Muslim na An-Nasaaiy]

 

Sa‘iyd bin Abil-Hasan amesema nilipokuwa na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alikuja mtu akasema, “Ee Ibn ‘Abbaas! Riziki yangu inatokana na kazi yangu ya kutengeneza picha hizi.” Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alisema: “Nitakuambia yale tu niliyoyasikia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Nilimsikia akisema, ‘Yeyote mwenye kutengeneza picha ataadhibiwa na Allaah mpaka aitie uhai na hatoweza kufanya hivyo.” Aliposikia hayo yule mtu alivuta pumzi na uso wake ukaiva. Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alimuambia: “Sikitiko lilioje! Ikiwa huna budi mpaka ufanye picha basi nakunasihi uchore picha za miti na kitu chengine chochote ambacho hakina uhai.” [Al-Bukhaariy]

 

Hizo ni dalili chache katika nyingi zenye kuonesha ubaya wa picha, na inampasa yeyote yule mwenye kuiweka dini yake mbele kuliko matamanio ya nafsi yake na tamaa za chumo na kipato cha haraka, ajiepushe na mambo hayo ili kuilinda dini yake na kuhifadhi heshima yake.

 

 

8. Baadhi Ya Vinyozi Kuweka Wanawake Wa Kuwaosha Wanaume Nywele Zao Na Hata Wengine Kuchuliwa (Massage) Na Wanawake

 

Ingawa nasaha hizi zilikusudiwa vinyozi wa nchi za Ulaya na mazingira mfano wake, lakini si vibaya kuchanganya na mazingira ya vinyozi walioko Afrika ambao ndio wengi hufanya jambo hili. Ifahamike kuwa hili ni jambo lisilofaa na kukubalika kishariy’ah, achilia mbali kidini, bali japo kimaadili na hayaa za kiuana Aadam ni jambo lililo kinyume na murua.

Ikiwa tu Rasuli katoa makemeo makali mno kwa mwanamme na mwanamke kupeana mikono au kugusana, ijekuwa kuoshwa mwanamme na mwanamke asiye mahram wake!

Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam):

“Mmoja wenu kudungwa kichwa kwa sindano ya chuma ni bora kwake kuliko kumgusa mwanamke asiyeruhusiwa kwake.” [At-Twabaraaniy katika Al-Mu’jam Al-Kabiyr na imepewa daraja ya Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’]

 

Ee mja wa Allaah, jiweke mbali na makaripio hayo makali na epuka ukharibifu huo wa shariy’ah na maadili kwa tamaa za kuvuta wateja dhaifu walitawaliwa na matamanio ya nafsi. Usiwe wewe ndio kichocheo cha maasi na uchafu.

 

 

9. Baadhi Ya Saluni Vinyozi Huwanyoa Nywele Wanawake

 

Mwanamke kunyoa nywele zake kipara au kunyolewa ni jambo lililokatazwa na shariy’ah. Kadhaalika mwanamke kukata nywele zake kimitindo kama makafiri.

 

Kutoka kwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anaeleza kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza wanawake kunyoa nywele zao. [At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy]

 

Kadhaalika, Al-Khallaal (Rahimahu Allaah) anasimulia kutoka kwa Qataadah (Rahimahu Allaah) naye kutoka kwa ‘Ikrimah (Rahimahu Allaah) ambaye amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza wanawake kunyoa nywele zao.”

 

Vilevile Hadiyth iliyohadithiwa na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kunyoa nywele si jukumu lililowekewa wanawake; kukata kidogo ndivyo inavyotakiwa.” [Abuu Daawuwd].

Na Hadiyth nyingine kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) ni kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Wanawake (mahujaji) hawafai kunyoa (vichwa vyao); wanaweza tu kupunguza nywele zao.” [Abuu Daawuwd].

Ibn al-Mundhir amesema: “Yapo maafikiano miongoni mwa Wanachuoni kuhusu hili, kwa kuwa kunyoa nywele za kichwa cha mwanamke ni aina ya adhabu.”

 

Kwa hali ya dharura kama maradhi ya kichwa au wadudu wa kichwani, hapo ndipo tu mwanamke anaporuhusiwa kunyoa kipara.

 

Ee kinyozi wa Kiislamu, mche Mola wako na jiepushe kunyoa wanawake nywele. Kumbuka kuwa, katika kumnyoa mwanamke nywele, mbali na makatazo yaliyo hapo juu, vilevile kunahusisha kutazama maeneo ya wazi ya mwanamke yasiyoruhusiwa kishariy’ah na kadhaalika kumgusa mwanamke na kumshika. Yote hayo ni haramu ya wazi.

 
 

10. Baadhi Ya Watu Wanaojinasibisha Na Uongozi Wa Dini Wanachangia Sana Kudumisha Mitihani Hiyo Kwa Kuwakumbatia Vinyozi Wafanyao Maasi Na Hata Kuwashirikisha Kwenye Uongozi Wa Mambo Ya Dini

 

Matatizo haya ya hizi kazi na uharamu wake, unatiliwa nguvu na baadhi ya watu wanaojipa majukumu ya dini au kujinasibisha na uongozi wa dini kwa kuwakumbatia hao vinyozi na kushirikiana nao katika mambo mbalimbali ya baatwil na kutowapa nasaha wala kuwasaidia katika kuwaongoza na kuwaonya na haramu wanazozifanya.

 

Viongozi kama hao wa taasisi na jumuiya za dini kama ilivyo baadhi ya maeneo katika nchi za Ulaya, wanaweka maslahi mbele kuliko shariy’ah ya dini. Dini kwao itatumika tu pale katika kuvuta yale maslahi yao au kuzuia maslahi yao yasiharibike.

 

Mitihani na khasara inapatikana zaidi kwa kuwa hao wanaojinasibisha na dini na uongozi wake, ni watu dhaifu kielimu na kimaadili, ndio maana ni vigumu wao kuwa mfano katika yale ya kuamrisha mema na kukataza maovu.

 

Inasikitisha utawakuta hao viongozi ndio wenye kuwatumia hao vinyozi na watu wanaokiuka maadili na shariy’ah za dini, kuwatumia kwa maslahi yao, au kuwasaidia katika maovu. Kumetokea qadhiyyah nyingi katika jamii kama hao viongozi kuwatumia vinyozi na watu mfano wao, katika kutoa ushahidi wa uongo au kujipa mahusiano baatwil ili kutwaa wasiyostahiki au kuchukua majukumu ambayo hawakuwa na haki nayo.

 

Hili –la viongozi wa dini kuwakumbatia watu waovu na wasio na maadili- limechangia sana kuharibu jamii na kuleta ufisadi mwingi.

Baya zaidi, ni hao viongozi wakishirikiana na vinyozi waovu wasio na maadili na watu wengine waovu katika jamii kupambana na watu wanaosimamia dini na kuamrisha mema na kukataza maovu. Matokeo ni kukithiri jamii ya watu wenye uadui na mafunzo sahihi ya Uislamu.

Lakini, tunatarajia nini ikiwa viongozi sampuli hiyo wao wenyewe hawajawa tayari kufuata dini ingawa wanapenda uongozi na kuung’ang’ania kwa ajili ya maslahi yao ya kidunia, ilhali nao wenyewe wanafanya kazi za haramu na hawafanyii kazi nasaha wanazopewa?

 
Viongozi hao ukiwatazama walivyo kuanzia madhahiri yao kidini ni mtihani na maadili na mwenendo wa kimaisha vilevile msiba. Kwa wenye kupenda dini na ufahamu dini wameshajaribu sana kuwapa nasaha lakini hawako tayari kwani hima yao kubwa si dini bali ni dunia. Lakini khasara kubwa ni kwa wale watu wengi wa kawaida wasiojua dini yao, wao ni wenye kuhadaiwa na kuzolewa na watu sampuli hiyo na mwisho kupotezwa!
 
Na wanawatumia watu wasiojua dini wenye matatizo mengi ya kimaadili na kuwapa nafasi za uongozi na majukumu kwenye jumuiya zao za dini ili wafunikiane yale maovu yao. Ndio si ajabu kuwaona kila mara hao viongozi kuwatembelea hao vinyozi kwenye masaluni yao na kucheka nao na kusengenya na kupiga porojo. Hakuna kunasihiana, wala kuamrishana mema, wala kukatazana maovu!
 

Allaah Anatuamrisha tuwe ni wenye kuamrishana mema na kukatazana maovu, Aliposema:

“Na uweko (watokeze) kutoka kwenu Ummah unaolingania kheri na unaoamrisha ma’aruwf (mema) na unaokataza munkari. Na hao ndio waliofaulu.” [Aal-‘Imraan: 104]

 

Vilevile Allaah Anatuhadharisha na kutoamrisha mema, Anapotupa mfano wa Banuu Israaiyl:

“Wamelaaniwa wale waliokufuru miongoni mwa wana wa Israaiyl kwa lisani  ya Daawuwd na ‘Iysaa mwana wa Maryam. Hivyo ni kwa sababu ya kuasi kwao na walikuwa wakitaadi.

“Walikuwa hawakatazani munkari waliyofanya. Uovu ulioje waliyokuwa wakiyafanya.” [Al-Maaidah: 78-79]

 

Kadhaalika Allaah Anatoa makemeo ya kusaidiana katika maovu, madhambi, uadui, Anaposema:

“Na saidianeni katika wema na uchaji Allaah. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui.” [Al-Maaidah : 02]

 

Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

“Atakayeona munkari [uovu] basi aubadilishe kwa mkono wake, na asipoweza basi kwa ulimi wake, na asipoweza basi kwa moyo wake [achukizwe] na huo ni udhaifu wa Iymaan.” [Muslim]

 

Muumin ni yule anayekataza maovu na asipoweza achukie kwa moyo wake au sivyo atakuwa katika khatari ya kupotoka, kupata adhabu na kutokukubaliwa du’aa yake. Anasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake, hakika mtaamrishana ma’aruwf [wema] na mtakatazana munkari [maovu], au Allaah Atakuleteeni adhabu, kisha mtamuomba wala Hatokuitikieni.” [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan]

 

Tunatahadharisha na viongozi wa dini sampuli hiyo ambayo wanapigania matumbo yao na umaarufu na madaraka katika jamii, hawasaidii jamii isipokuwa maslahi yao, na wakisaidia ni katika maovu na kueneza uozo katika jamii. Inafika hadi wale watu wa Sunnah “Ghurabaa” wanaotengeneza yale yaliyofisidiwa na watu, jamii inawaona hao ndio maadui na wale wanaoozesha jamii ndio wazuri!! Ni yale aliyotukhabarisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  kuwa mwisho wa zama mambo yatageuka ndio sio na sio ndio, pale aliposema:

“Zitakuja kwa watu zama za udanganyifu, atasadikishwa yule muongo na atakadhibishwa yule mkweli, ataaminiwa yule khaini na atakhiniwa yule mwaminifu, na atazungumza yule “Ruwaybidhwah.” Itasemwa: ‘Ni nani “Ruwaybidhwah”? Atajibu: ‘Ni yule mjinga asiye na kima anayezungumzia mambo ya watu’.” [Ibn Maajah, na Al-Albaaniy kasema Swahiyh katika Swahiyh Ibn Maajah]

 

Watu wanapaswa wakae mbali sana na wajiepushe na viongozi kama hao waovu wanaojinasibisha na dini ilhali dini iko mbali nao kwa maadili yao mabovu, maadui wa Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wenye ulafi wa madaraka, tamaa za dunia na ukosefu wa maadili na wenye kula chumo la haramu.

 

 

11. Mwisho Tunahitimisha Kwa Maelekezo Ya Namna Inavyopaswa Kuwa Saluni Ya Muislamu Anayechunga Mipaka Ya shariy’ah Na Kumcha Allaah

 

Kinyozi wa Kiislamu mwenye kuchunga maadili ya Kiislamu na kuchunga shariy’ah ya Dini yake, anapaswa kuwa makini na kazi yake na kuchunga kutokiuka mipaka yoyote ile ya shariy’ah njema na bora ya Uislamu. Achunge mambo yafuatayo:

  • Saluni yake isiwe na mambo mengi makuu wala vivutio vya haramu akidhani kuwa ndio sababu ya kupata wateja wengi.
  • Anyoe kwa mujibu wa shariy’ah inavyofundisha.
  • Kichwa akinyoe kwa kiwango sawa; saizi moja kichwa chote; wala kusiwe juu namba kubwa na chini namba ndogo ya chanua za mashine. Asinyoe panki/denge.
  • Asiweke madoido ya kuchonga chonga au kukichora kichwa kwa mitindo ya nywele.
  • Asinyoe ndevu zake wala za wateja wake. Wala asichonge ndevu au kuzipunguza au kuzitengeneza kwa staili mbalimbali.
  • Asinyoe wanawake.
  • Asinyoe nyusi japo wanaume.
  • Asiweke kwenye saluni yake mchanganyiko wa wafanyakazi wa kiume na kike.
  • Asiweke mapicha kwenye saluni yake kwani Malaika hawaingii sehemu yenye picha kama Hadiyth inavyotueleza hapa chini
Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“…Hakika Malaika hawaingii nyumba ambayo ina picha.” [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

  • Asiweke vivutio vya haramu kama muziki na yenye utata kama televisheni. Uharamu wa muziki uko wazi kwenye Aayah na Hadiyth mbalimbali.

Anasema Allaah Aliyetukuka:

"Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Allaah pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha." [Luqmaan: 6Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema kuhusu Aayah hii "Naapa kwa Allaah hii inamaanisha ni kuimba" [At-Twabariy 20:12]

 

Na Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) pia amesema kuhusu Aayah: "Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi. Ni nyimbo na maneno ya yanayofanana (ya upuuzi)" [Isnaad Sahiyh kutoka kwa Shaykh Al-Albaaniy]

 

Na amesema vilevile Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam:

"Watakuweko watu katika Ummah wangu watakaojaribu kuhalilisha zinaa, uvaaji wa hariri, pombe na muziki. Baadhi ya watu watakuwa pembeni mwa mlima na mchungaji wao atawajia jioni na kuwaomba haja [fulani]. Watasema: "Rudi kesho." Allaah Atawaangamiza usiku, Atawaangushia milima kisha Atawabadilisha waliobakia wawe nyani na nguruwe na watabakia hivyo hadi siku ya Qiyaamah." [Al-Bukhaariy]

  • Asiruhusu vigenge vya wapoteza wakati na wasengenyaji. Yeye mwenyewe ajichunge na kusengenya na umbea.
  • Akiwa ni mwenye maarifa ya dini japo kidogo, atumie fursa hiyo kulingania wateja wake na kuwakumbusha ya dini.
  • Achunge sana na kuhifadhi vipindi vya Swalaah. Asikose Swalaah kwa sababu ya mteja; bora apoteze mteja kuliko kupoteza Swalaah. Kipengele namba 5 juu.

 

Kinyozi wa Kiislamu anapaswa aamini kuwa kipato na rizki yake vyote hivyo vinatoka kwa Allaah Aliyetukuka, na atambue kuwa hawezi kwa ujanja wake kuongeza kipato chake, wala kwa khofu yake ya rizki kuwa atapungukiwa na kipato chake.

 

Atambue kuwa Allaah Anamruzuku yule anayemtegemea Yeye kikamilifu, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

“Na anayemcha Allaah Humtengezea njia ya kutokea.

“Na Humruzuku kwa jiha asiyotazamia. Na anayemtegemea Allaah, Yeye Humtosha. Hakika Allaah Anatimiza amri Yake. Allaah Kajaalia kila kitu na kipimo chake.” [Atw-Twalaaq: 2-3].

 

Na anapaswa amtegemee Allaah kidhati kwani Allaah Atamruzuku yeye kama anavyomruzuku ndege. Imepokewa kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

Ikiwa nyinyi mtamtegemea Allaah upeo wa kumtegemea basi Atawaruzuku nyinyi kama Anavyomruzuku ndege. Anatoka katika kiota chake asubuhi tumbo lake likiwa tupu na anarudi likiwa tumbo lake limejaa” [At-Tirmidhiy, Ahmad na Ibn Maajah na Isnadi yake ni Swahiyh]  

 

Ingawa unyozi ni ajira yako, lakini vilevile usisahau kazi yako ya asili ambayo imeasisiwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuendelezwa na kila anayempenda, kazi ya kuwalingania wateja Waislamu kwa kuwaeleza hayo uliyoyapata na kuwakataza bali kuwawekea wazi kuwa wewe kinyozi lakini unapenda uwe na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Siku ya Qiyaamah hivyo, hautokuwa tayari kutekeleza alichokikataza Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata kama kitakutilia kipato kikubwa, vinginevyo elewa kuwa utakuwa unachangia katika kuipinga na kuikebehi bali kuibeza amri ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wenye kuibeza au kuipinga amri yake Qur-aan inawatahadharisha kwa kusema hivi:

“ …. Basi na watahadhari wanaokhalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu iumizayo.” [An-Nuwr: 63]

 

Mwisho, tunawanasihi vinyozi wa Kiislamu, wachunge mipaka ya Allaah na Mjumbe Wake katika kazi zao na wawe na msimamo thabiti katika dini yao na Allaah Awajaalie waweze kujiepusha na makatazo na haramu zote hizo ambazo zinahusiana na kazi hiyo.

 

Na Allaah ni Mjuzi zaidi.

Na Swalaah na Salaam ziwe juu ya Mjumbe wa Allaah na jamaa zake na Swahaba zake.

 

 

Share