001-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: ALLAAH
أسماء الله الحسنى وصفاته
Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake
الله
001-ALLAAH
ALLAAH: Mwenye Uluwhiyyah (Anayestahiki kuabudiwa Pekee bila kumshirikisha) na Al-‘Ubuwdiyyah (Unyenyekevu, mapenzi, khofu ya adhabu za Allaah na kutaraji rahma za Allaah, utiifu na udhalili kwa Allaah Aliyetukuka, na kutovuka mipaka Yake, na kutekeleza maamrisho Yake na kujizuia na makatazo Yake, kwa kujikurubisha kwa Allaah na kutaka thawabu Zake na kujihadhari na ghadhabu na ikabu Zake).
Mwenye kustahiki kupwekeshwa katika kuabudiwa kwa Alivyojisifu kwa Sifa za Uwluwhiyyah nazo ni Sifa za ukamilifu.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Mwenye Kustahiki kurejewa kwa mapenzi, kwa unyeyenyekevu, kwa khofu, matumaini, matarajio, kuadhimishwa na kutiiwa. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۖ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا ۚ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ ﴿٢٥٥﴾
Allaah, hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye, Aliyehai daima, Msimamia kila kitu. Haumchukui usingizi wala kulala. Ni Vyake pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi. Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake. Anajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawawezi kuzunguka chochote katika elimu Yake isipokuwa kwa Alitakalo. Imeenea Kursiyy Yake mbingu na ardhi. Wala hakumchoshi kuvihifadhi viwili hivyo. Naye ni Mwenye Uluwa, Ametukuka, Adhimu; Mkuu kabisa. [Al-Baqarah 2: 255]
Maana ya Allaah kilugha: Allaah; Asili yake ni Al-Ilaah, na Al-Ilaah katika lugha ya Kiarabu ina maana nne:
Kwanza: Al-Ma’buwd: Mwenye kuabudiwa. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
وَهُوَ الَّذِي فِي السَّمَاءِ إِلَـٰهٌ وَفِي الْأَرْضِ إِلَـٰهٌ ۚ
Na Yeye Ndiye Muabudiwa wa haki mbinguni na ardhini [Az-Zukhruf 43: 84]
Pili: Mwenye kukimbiliwa katika hali ya khofu:
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
وَاتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ آلِهَةً لَّعَلَّهُمْ يُنصَرُونَ ﴿٧٤﴾
Na wamejichukulia badala ya Allaah miungu (ya uongo) ili (wakitumaini) watawanusuru! [Yaasiyn 36: 74]
Yaani; Wanategemea wawanusuru dhidi ya maadui wao, Waarabu wakawa wanaelekea miungu yao kuomba nusra.
Tatu: Al-Mahbuwb Al-Mu’adhwam – Mpendwa Mtukuzwa.
Waarabu wakawa wanapenda masanamu yao waliyokuwa wakiyaabudu na wakayatukuza Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
وَمِنَ النَّاسِ مَن يَتَّخِذُ مِن دُونِ اللَّـهِ أَندَادًا يُحِبُّونَهُمْ كَحُبِّ اللَّـهِ ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَشَدُّ حُبًّا لِّلَّـهِ ۗ
Na miongoni mwa watu wako wenye kuchukua asiyekuwa Allaah na kuwafanya kuwa ni wanaolingana (na Allaah) wanawapenda kama kumpenda Allaah. Na wale walioamini wana mapenzi zaidi kwa Allaah. [Al-Baqarah 2: 165]
Nne: Ambaye kwayo akili zinakanganyika
Yaani: zinakanganya nyoyo zinapotafakari utukufu Wake (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kisha zikashindwa kufikia ufahamu wa dhati ya Ujalali Wake na Utukufu Wake (‘Azza wa Jalla).
Jina hili ni Jina tukufu kabisa kuliko yote miongoni mwa Asmaul-Husnaa, na ni lilotukuka zaidi na lililojumuisha maana za Majina Yake yote. Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa) Amejipwekesha Kwalo kutokana na walimwengu wote. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akazitia khofu nyoyo za majahili na ndimi zao zikatamka bila kipingamizi wala taradadi. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ اللَّـهُ ۚ
Na ukiwauliza: “Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi?” bila shaka watasema: “Allaah.” [Luqmaan 31: 21]
Jina hili ni Ambalo linalokusanya Majina Mazuri yote na Sifa tukufu za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Mja anapoomba husema “Allaahumma” hivyo atakuwa ameomba kwa kila Majina Mazuri na Sifa Zake tukufu [Madaarij As-Saalikiyn (1/32)] Ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anaongezea Jina hili Tukufu katika Al-Asmaaul-Husnaa yote mfano kauli Yake:
وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا
Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo [Al-A’raaf 7: 180]
Na ndio maana pia baadhi ya ‘Ulamaa wakaona kuwa Jina hili la Allaah Ndilo Jina tukufu kabisa ambalo likiombwa kwalo du’aa hutakabaliwa.
Na husemwa Ar-Rahmaan na Ar-Rahiym, Al-Qudduws, As-Salaam, Al-‘Aziyz, Al-Hakiym kuwa ni miongoni mwa Asmaaul-Husnaa wala haisemwi “Allaah” ni miongoni mwa Majina ya Ar-Rahmaan wala miongoni mwa Majina ya Al-‘Aziyz n.k, na ndipo Anaposema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ ۖ هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ ﴿٢٢﴾
Yeye ni Allaah, Ambaye hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye. Mjuzi wa ghayb na ya dhahiri, Yeye Ndiye Mwingi wa rahmah, Mwenye kurehemu.
هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٢٣﴾
Yeye Ndiye Allaah Ambaye hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye. Mfalme, Mtakatifu Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye kusalimisha, Amesalimika na kasoro zote, Mwenye kusadikisha ahadi, Mwenye kuaminisha, Mwenye kutawalia, kuchunga na kuhifadhi, Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Jabari, Asiyeshindwa kufanya Atakalo, Mwenye kutakabari dhidi ya dhulma nk, Yuko juu ya viumbe, Utakasifu ni wa Allaah! kutokana na ambayo wanamshirikisha.
هُوَ اللَّـهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ ۖ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ۚ يُسَبِّحُ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢٤﴾
Yeye Ndiye Allaah, Muumbaji, Mwanzishi viumbe bila kasoro, Muundaji sura na umbile, Ana Majina Mazuri kabisa, kinamsabbih Pekee kila kilichokuweko katika mbingu na ardhi, Naye Ndiye Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [Al-Hashr 59: 22-24]
Jina hili ndio asili ya Majina ya Majina ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na yanayofuatia mengine yote yamejumuika ndani Yake.
Jina la Allaah linamhusu Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Anasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا فَاعْبُدْهُ وَاصْطَبِرْ لِعِبَادَتِهِ ۚ هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا ﴿٦٥﴾
Rabb wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake; basi mwabudu Yeye tu na dumisha subira katika ‘ibaadah Yake. Je, unamjua mwenye Jina kama Lake (Allaah)? [Maryam 19: 65]