22-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! Kumtii Kiumbe Katika Kumuasi Allaah
إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم
Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!
22 -Kumtii Kiumbe Katika Kumuasi Allaah
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu kumtii kiumbe yeyote katika kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa dalili ya Hadiyth ifuatayo:
لاَ طَاعَةَ في مَعْصِيَةِ الله ، إِنَّمَا الطَّاعَةُ فِي المَعْرُوفِ
Hakuna kutii katika kumuasi Allaah, bali utiifu ni katika yanayokubalika ki-shariy’ah katika mema.[Al-Bukhaariy na Muslim]
Muislamu anapaswa atii amri kwa anayepasa kumuamrisha hata kama ni jambo analolichukia madamu tu haliko katika kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama alivyoamrisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عَلَى الْمَرْءِ الْمُسْلِمِ السَّمْعُ وَالطَّاعَةُ فِيمَا أَحَبَّ وَكَرِهَ إِلَّا أَنْ يُؤْمَرَ بِمَعْصِيَةٍ فَإِنْ أُمِرَ بِمَعْصِيَةٍ فَلَا سَمْعَ وَلَا طَاعَةَ
“Muislamu anapaswa kusikia na kutii kwa anayoyapenda na anayoyachukia, madhali hakuamrishwa kuasi. Na pindi akiamrishwa katika maasi, basi hakuna kusikia wala kutii.” [Al-Bukhaariy na Muslim
Mfano wa katika yasiyokubalika katika ki-shariy’ah ni kama usimulizi wa Hadiyth ifuatayo ambako kiongozi alitaka kuwaangamiza Waislamu katika moto:
عَنْ عَلِيٍّ، قَالَ: بَعَثَ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ سَرِيَّةً، وَاسْتَعْمَلَ عَلَيْهِمْ رَجُلًا مِنَ الْأَنْصَارِ وَأَمَرَهُمْ أَنْ يَسْمَعُوا لَهُ وَيُطِيعُوا، فَأَغْضَبُوهُ فِي شَيْءٍ، فَقَالَ: اجْمَعُوا لِي حَطَبًا، فَجَمَعُوا لَهُ، ثُمَّ قَالَ: أَوْقِدُوا نَارًا، فَأَوْقَدُوا، ثُمَّ قَالَ: أَلَمْ يَأْمُرْكُمْ رَسُولُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ تَسْمَعُوا لِي وَتُطِيعُوا؟ قَالُوا: بَلَى، قَالَ: فَادْخُلُوهَا، قَالَ: فَنَظَرَ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ، فَقَالُوا: إِنَّمَا فَرَرْنَا إِلَى رَسُولِ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مِنَ النَّارِ، فَكَانُوا كَذَلِكَ، وَسَكَنَ غَضَبُهُ، وَطُفِئَتِ النَّارُ، فَلَمَّا رَجَعُوا ذَكَرُوا ذَلِكَ لِلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، فَقَالَ: ((لَوْ دَخَلُوهَا مَا خَرَجُوا مِنْهَا، إِنَّمَا الطَّاعَةُ فِي الْمَعْرُوفِ))
Kutoka kwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituma jeshi chini ya uongozi wa mtu mmoja wa Answaar. Wakamkasirisha kwa sababu ya jambo fulani akawaambia: Kusanyeni kuni. Wakamkusanyia akasema: Niwashieni moto! Wakamuashia. Akasema: Kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakukuamrisheni mnitii? Wakasema: Ndio! Akasema. Basi uingieni! Wakatazamana kisha wakasema: Hakika sisi tumekimbilia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kujiepusha na moto. Wakawa hivyo hivyo. Kisha ghadhabu zake zikatulia na moto ukazimwa. Waliporudi kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakamwelezea yalivyojiri, hapo yeye akasema: “Mngeliuingia, msingetoka kamwe humo. Hakika utiifu ni katika mema.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Katika ambayo hayapasi utiifu:
1. Kutii katika mambo ya haraam. Maswahaba walimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عَنْ عَدِيّ بْنِ حَاتِمٍ: أَنَّهُ سَمِعَ اَلنَّبِيَّ (صَلَّى اَللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَقْرَأُ هَذِهِ الآيَةَ: اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚسُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٣١﴾ فَقُلْتُ لَهُ: إِنَّا لَسْنَا نَعْبُدُهُمْ. قَالَ: ((أَلَيْسَ يُحَرِّمُونَ مَا أَحَلَّ اَللَّهُ فَتُحَرِّمُونَهُ وَيُحِلُّونَ مَا حَرَّمَ اَللَّهُ فَتُحِلُّونَهُ؟)) فَقُلْتُ بَلَى. قَالَ:((فَتِلْكَ عِبَادَتُهُم))رَوَاهُ أَحْمَدُ وَاَلتِّرْمِذِيُّ وَحَسَّنَهُ
Imepokewa toka kwa ‘Adiyy bin Haatim (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba amemsikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisoma Aayah: Wamewafanya Wanachuoni Marabai wao wa dini na Wamonaki wao kuwa ni miola badala ya Allaah, na (pia) Al-Masiyh mwana wa Maryam na hali hawakuamrishwa isipokuwa kumwabudu Ilaah Mmoja Pekee. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Utakasifu ni Wake kutokana na yale yote wanayomshirkisha nayo. [At-Tawbah: 31] Nikasema: Hakika sisi hatuwaabudu. Akasema: "Je, kwani hawaharamishi Aliyoyahalalisha Allaah nanyi mkayaharamisha? Na wanahalalisha Aliyoyaharamisha Allaah nanyi mnayahalalisha?" Nikasema: Ndio. Akasema: "Basi hivyo ndivyo kuwaabudu." [Ahmad na At-Tirmidhiy na ameipa daraja ya Hasan]
2. Kuwatii wazazi katika maasi na kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
Mzazi anapaswa kupewa haki yake kumfanyia ihsaan na wema. Lakini pindi anapomuamrisha mwanawe katika kumshirkisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa njia yoyote ile, au kuamrisha kufuata bid’ah (uzushi) au maasi yoyote yale mengineyo ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wameyakataza, basi haipasi kabisa kumtii mzazi, hapo inapasa mtoto akatae kuwatii, na dalili ni kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حُسْنًا ۖ وَإِن جَاهَدَاكَ لِتُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۚ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٨﴾
Na Tumemuusia insani kuwafanyia wema wazazi wake wawili. Lakini wakikushikilia kuwa Unishirikishe na ambayo huna elimu nayo, basi usiwatii; Kwangu ni marejeo yenu, Nitakujulisheni yale mliyokuwa mkiyatenda. [Al-‘Ankabuwt: 8]
Na mifano mingi tunayo katika Siyrah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Maswahaba waliokataa kuwatii wazazi wao, mmojawapo ni Sa’d bin Abiy Waqqaasw (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye mama yake alichukia mno yeye kuingia katika Dini ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Akamwambia mwanae: “Naapa ima uachane na Dini yako hii mpya au nitajifungia kula na kunywa mpaka nife.” Sa’ad akamwambia: “Ee mama yangu nina mapenzi makubwa kwako kama mama yangu uliyenizaa, lakini mapenzi yangu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Rasuli Wake ni makubwa zaidi. Wa-Allaahi lau hata roho elfu moja na moja zitaondoka (kwa kunitaka nirudi dini yangu ya zamani) kamwe sitorudia dini yangu.”
3. Kumtii mume au mke katika maasi:
Mifano ya mke kumtii mumewe katika maasi ambayo yanajulikana katika jamii, ni mume kumtaka mke achonge nyusi zake na hali laana ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) inamfikia mwenye kunyofoa au kuchonga nyusi zake.
Pia kumtii mume kutokujistiri kwa vazi la Hijaab.
Pia kumtii mume katika yaliyoharamishwa kama kumtaka jimai mchana wa Swawm ya Ramadhwaan, au kumtaka afanye naye tendo la ndoa wakati wa hedhi, au kumtaka amuingilie katika utupu wake wa nyuma... na mifano iko mingi.
Mfano mzuri tunao katika Qur-aan wa Aasiyah ambaye alikuwa mke wa Fir’awn muasi aliyejifanya kuwa mungu. Aasiyah alikataa kumtii mumewe katika maasi ya kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa sababu alimuamini Allaah. Fir’awn akamuadhibu adhabu kali na kumuua lakini yeye alibakia katika iymaan yake na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anampigia mfano wa wenye kuamini:
وَضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا لِّلَّذِينَ آمَنُوا امْرَأَتَ فِرْعَوْنَ إِذْ قَالَتْ رَبِّ ابْنِ لِي عِندَكَ بَيْتًا فِي الْجَنَّةِ وَنَجِّنِي مِن فِرْعَوْنَ وَعَمَلِهِ وَنَجِّنِي مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ﴿١١﴾
Na Allaah Amewapigia mfano wale walioamini; mke wa Fir’awn, aliposema: “Rabb wangu! Nijengee nyuma Kwako kwenye Jannah na niokoe na Fir’awn na vitendo vyake na niokoe na watu madhalimu.” [At-Tahriym: 11]
Siku ya Qiyaamah wanaofanyiana utiifu katika maasi hali itakuwa kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَوْمَ تُقَلَّبُ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ يَقُولُونَ يَا لَيْتَنَا أَطَعْنَا اللَّـهَ وَأَطَعْنَا الرَّسُولَا ﴿٦٦﴾
Siku zitakapopinduliwa nyuso zao motoni, watasema: “Laiti tungelimtii Allaah, na tungelimtii Rasuli.”
وَقَالُوا رَبَّنَا إِنَّا أَطَعْنَا سَادَتَنَا وَكُبَرَاءَنَا فَأَضَلُّونَا السَّبِيلَا ﴿٦٧﴾
Na watasema: “Rabb wetu! Hakika sisi tumewatii mabwana zetu, na wakuu wetu, basi wametupoteza njia.”
رَبَّنَا آتِهِمْ ضِعْفَيْنِ مِنَ الْعَذَابِ وَالْعَنْهُمْ لَعْنًا كَبِيرًا ﴿٦٨﴾
“Rabb wetu! Wape adhabu maradufu, na walaani laana kubwa.” [Al-Ahzaab: 66-68]
4. Kumtii rafiki kuacha Swalaah na maasi mengineyo:
Kumtii rafiki anayemuamrisha mwenzie aache Swalaah ili wakimbilie katika michezo fulani, mechi za mpira n.k. Au kumtii rafiki katika kusililiza muziki na ngoma, kwenda sehemu zinazotendeka maasi n.k.
Siku ya Qiyaamah rafiki huyo atamkanusha mwenziwe kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَيَوْمَ يَعَضُّ الظَّالِمُ عَلَىٰ يَدَيْهِ يَقُولُ يَا لَيْتَنِي اتَّخَذْتُ مَعَ الرَّسُولِ سَبِيلًا ﴿٢٧﴾
Na siku dhalimu atakapotafuna mikono yake akisema: “Laiti ningeshika njia pamoja na Rasuli.
يَا وَيْلَتَىٰ لَيْتَنِي لَمْ أَتَّخِذْ فُلَانًا خَلِيلًا ﴿٢٨﴾
“Ee ole wangu! Laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki mwandani.”
لَّقَدْ أَضَلَّنِي عَنِ الذِّكْرِ بَعْدَ إِذْ جَاءَنِي ۗ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِلْإِنسَانِ خَذُولًا ﴿٢٩﴾
“Kwa yakini amenipoteza mbali na Ukumbusho baada ya kunijia.” Na shaytwaan kwa insani daima ni mwenye kutelekeza. [Al-Furqaan: 27- 29]
Ndugu Muislamu, inapokuwa ni amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ya kujiepusha na maasi basi usimtii yeyote isipokuwa Yeye (‘Azza wa Jalla) na hapo ndipo itakapohakiki iymaan ya mtu kwa dalili ifuatayo ya Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((ثَلاَثٌ مَنْ كُنَّ فِيهِ وَجَدَ حَلاَوَةَ الإِيمَانِ: أَنْ يَكُونَ اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَحَبَّ إِلَيْهِ مِمَّا سِوَاهُمَا, وَأَنْ يُحِبَّ الْمَرْءَ لاَ يُحِبُّهُ إِلاَّ لِلَّهِ, وَأَنْ يَكْرَهَ أَنْ يَعُودَ فِي الْكُفْرِ كَمَا يَكْرَهُ أَنْ يُقْذَفَ فِي النَّارِ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mambo matatu atakayekuwa nayo, atapata utamu wa ‘iymaan: Allaah na Rasuli Wake wawe vipenzi zaidi kwake kuliko wengineo, ampende mtu na wala asimpende isipokuwa kwa ajili ya Allaah, na achukie kurudi katika ukafiri baada ya Allaah kumuokoa kutoka huko kama anavyochukia kuingizwa motoni." [Al-Bukhaariy na Muslim]
Hitimisho ni kwamba mtu anapochochewa kutenda maasi basi inamtosheleza kujibu kwa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ifuatayo:
إِنِّي أَخَافُ إِنْ عَصَيْتُ رَبِّي عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿١٣﴾
“Hakika nikimuasi Rabb wangu, nina khofu adhabu ya Siku adhimu.” [Az-Zumar: 13]