23-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! Sihri (Uchawi) Na Michezo Ya Mazingaombwe
إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم
Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!
23- Sihri (Uchawi) Na Michezo Ya Mazingaombwe
Neno “As-Sihr” (uchawi) maana yake ni kitendo cha kujikurubisha na shaytwaan na kwa msaada wake (shaytwaan) na uchawi ni kulibadilisha jambo mbali na uhakika wake, nako ni kuwadhihirishia watu jambo lisilo la kweli wakaliona kuwa ni la kweli.” [Lisaan Al-‘Arab]
Na Sihri ni tendo la kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kuwa linahusiana na shaytwaan 'aaswi mwenye kumkufuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kauli Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَاتَّبَعُوا مَا تَتْلُو الشَّيَاطِينُ عَلَىٰ مُلْكِ سُلَيْمَانَ ۖ وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ وَلَـٰكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ وَمَا أُنزِلَ عَلَى الْمَلَكَيْنِ بِبَابِلَ هَارُوتَ وَمَارُوتَ ۚ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلَا تَكْفُرْ ۖفَيَتَعَلَّمُونَ مِنْهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِ بَيْنَ الْمَرْءِ وَزَوْجِهِ ۚ وَمَا هُم بِضَارِّينَ بِهِ مِنْ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ ۚ وَلَقَدْ عَلِمُوا لَمَنِ اشْتَرَاهُ مَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ ۚ وَلَبِئْسَ مَا شَرَوْا بِهِ أَنفُسَهُمْ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿١٠٢﴾
Na wakafuata yale waliyoyasoma mashaytwaan juu ya ufalme wa Sulaymaan; na Sulaymaan hakukufuru lakini mashaytwaan ndio waliokufuru; wanafundisha watu sihiri na yaliyoteremshwa kwa Malaika wawili katika (mji wa) Baabil; Haaruwt na Maaruwt. Nao wawili hawamfundishi yeyote mpaka waseme: “Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru.” Kisha wakajifunza kutoka kwa hao wawili yenye kupelekea kufarikisha kwayo baina ya mtu na mkewe. Na wao hawawezi kamwe kumdhuru yeyote kwayo isipokuwa kwa idhini ya Allaah; na wanajifunza yanayowadhuru na wala hayawanufaishi; na kwa yakini walijua kwamba atakayechuma haya hatopata katika Aakhirah fungu lolote, na ni ubaya ulioje walichojiuzia nafsi zao, lau wangelikuwa wanajua. [Al-Baqarah: 102]
Pia, sihri ni miongoni mwa Al-Kabaair (madhambi makubwa) na ni miongoni mwa ambayo yanamuangamiza mtu kwa dalili ya Hadiyth:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((اجْتَنِبُوا السَّبْعَ الْمُوبِقَاتِ)) قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَمَا هُنَّ؟ قَالَ: ((الشِّرْكُ بِاللَّهِ وَالسِّحْرُ وَقَتْلُ النَّفْسِ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلاَّ بِالْحَقِّ وَأَكْلُ الرِّبَا وَأَكْلُ مَالِ الْيَتِيمِ وَالتَّوَلِّي يَوْمَ الزَّحْفِ وَقَذْفُ الْمُحْصَنَاتِ الْمُؤْمِنَاتِ الْغَافلاَتِ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Jiepusheni na mambo saba yanayoangamiza!)) Wakauliza: Ni yepi hayo yaa Rasuwla Allaah? Akawaambia: ((Ni kumshirikisha Allaah, sihri [uchawi], kuua nafsi Aliyoiharamisha Allaah isipokuwa kwa haki, kula ribaa, kula mali ya yatima, kukimbia wakati wa kupambana na adui na kuwatuhumu uzinifu wanawake Waumini waliohifadhika walioghafilika)). [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na sihri ilikuwa ni miongoni mwa shirki za kaumu ya Fir’awn na ndio sababu mojawapo ya kutumwa Nabiy Muwsaa ('Alayhis-Salaam) kuwataka waache. Alipowaonesha miujiza ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wachawi wa Fir’awn hapo hapo walisujudu kwa kuwa walitambua kuwa sihri ni batili na ni shirki, wakakubali haki na wakajiepusha nayo kama ilivyokuja katika Qur-aan:
قَالَ لَهُم مُّوسَىٰ أَلْقُوا مَا أَنتُم مُّلْقُونَ ﴿٤٣﴾
Muwsaa akawambia: “Tupeni vile mnavyotupa.”
فَأَلْقَوْا حِبَالَهُمْ وَعِصِيَّهُمْ وَقَالُوا بِعِزَّةِ فِرْعَوْنَ إِنَّا لَنَحْنُ الْغَالِبُونَ ﴿٤٤﴾
Wakatupa kamba zao na fimbo zao; na wakasema: “Kwa utukufu wa Fir’awn! Hakika sisi ni wenye kushinda.”
فَأَلْقَىٰ مُوسَىٰ عَصَاهُ فَإِذَا هِيَ تَلْقَفُ مَا يَأْفِكُونَ ﴿٤٥﴾
Basi Muwsaa akatupa fimbo yake, tahamaki inameza vyote walivyovizua.
فَأُلْقِيَ السَّحَرَةُ سَاجِدِينَ ﴿٤٦﴾
Basi wale wachawi wakaanguka wakisujudu.
قَالُوا آمَنَّا بِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٤٧﴾
Wakasema: “Tumemwamini Rabb wa walimwengu.
رَبِّ مُوسَىٰ وَهَارُونَ ﴿٤٨﴾
“Rabb wa Muwsaa na Haaruwn.” [Ash-Shu’araa: 43-48]
Na pia katika Suwrah nyengine baada ya wachawi kusujudu wakasilimu wakasema:
إِنَّا آمَنَّا بِرَبِّنَا لِيَغْفِرَ لَنَا خَطَايَانَا وَمَا أَكْرَهْتَنَا عَلَيْهِ مِنَ السِّحْرِ ۗ وَاللَّـهُ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ﴿٧٣﴾
“Hakika sisi tumemwamini Rabb wetu ili Atughufurie madhambi yetu, na yale uliyotushurutisha katika ya sihiri. Na Allaah ni Mbora Zaidi na Mwenye kudumu zaidi.” [Twaahaa: 73]
Fir’awn akatakabari na kukanusha haki akasema:
قَالَ آمَنتُمْ لَهُ قَبْلَ أَنْ آذَنَ لَكُمْ ۖ إِنَّهُ لَكَبِيرُكُمُ الَّذِي عَلَّمَكُمُ السِّحْرَ فَلَسَوْفَ تَعْلَمُونَ ۚ لَأُقَطِّعَنَّ أَيْدِيَكُمْ وَأَرْجُلَكُم مِّنْ خِلَافٍ وَلَأُصَلِّبَنَّكُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٤٩﴾
(Fira’wn) Akasema: “Je, mmemwamini kabla sijakupeni idhini? Hakika bila shaka kubwa lenu ndiye amekufunzeni sihiri. Basi mtakuja kujua. Nitakukatenikateni mikono yenu na miguu yenu kinyume (kulia kwa kushoto), kisha nitakusulubuni nyote.” [Ash-Shu’araa: 49]
Lakini wachawi baada ya kuamini wakasema:
قَالُوا لَا ضَيْرَ ۖ إِنَّا إِلَىٰ رَبِّنَا مُنقَلِبُونَ ﴿٥٠﴾
Wakasema: “Hakuna dhara yoyote! Hakika sisi tunarudi kwa Rabb wetu.
إِنَّا نَطْمَعُ أَن يَغْفِرَ لَنَا رَبُّنَا خَطَايَانَا أَن كُنَّا أَوَّلَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٥١﴾
“Hakika sisi tunatumai kwamba Rabb wetu Atatughufuria madhambi yetu kwa vile tumekuwa wa kwanza wenye kuamini.” [Ash-Shu’araa: 49-51]
Kuna aina mbili za uchawi: Kufanya sihri kwa ajili ya kumuathiri mtu na kufanya micheo ya sihri (mazingaombwe).
1- Kufanya sihri kwa ajili ya kumuathiri mtu:
Wachawi hutumia mashaytwaan kushirikiana nao. Hufanya sihiri kwa malengo mbali mbali; kumroga mtu apatwe na masaibu, maafa, au amuue, au afarikiane mke na mume kama ilivyotajwa juu katika Suwratul-Baqarah, au aelekeze mapenzi ya mtu kwa mtu fulani na mengi mengineyo. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameonya:
عن ابي هريرة رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم: مَنْ عَقَدَ عُقْدَةً ثُمَّ نَفَثَ فِيهَا, فَقَدْ سَحَرَ, وَمَن ْسَحَرَ فَقَدْ أَشْرَكَ, وَمَنْ تَعَلَّقَ شَيْئًا وُكِلَ إِلَيْهِ))
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayefunga fundo kisha akalipuliza amefanya uchawi. Na atakayefanya uchawi amefanya shirki, na atakayetundika kitu [talasimu, au kuvaa hirizi, zindiko] basi amejiweka katika ulinzi wa hicho kitu alichokivaa)) [na itamdhalilisha])) [An-Nasaaiy]
Na pia:
مَنْ أَتَى كَاهِنًا أَوْ سَاحِرًا فَصَدَّقَهُ بِمَا يَقُولُ فَقَدْ كَفَر بِمَا أُنْزِلَ عَلى مُحَمَّدٍ صلى الله عليه وسلّم
Atakayemwendea kahini au mchawi akasadiki yale anayoyasema basi amekufuru ambayo Ameteremshiwa nayo Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) [Tafsiyr Ibn Kathiyr; Hadiyth ina isnaad ya upokezi Swahiyh na kuna Hadiyth zinazokubaliana na hii].
Aghlabu ya njia wanazotumia wachawi na jinsi ya kumtambua mchawi:
- Huwakamata wale wenye ugonjwa wa ngozi (zeruzeru) na kuwaua na kutumia viungo vyao katika uchawi wao. Hii ni dhulma kubwa mno wanayowafanyia bin Aadamu wenzao! Allaah Awahifadhi bin Aadam hao waliosibiwa na maradhi hayo, jambo ambalo limekuwa ni mtihani kwao kudhulumiwa na wachawi!
- Hutamka kauli au maneno ya kufru.
- Huandika maneno katika vijikaratasi na kumtaka mtu avivae kama hirizi, au avifukize apate moshi wake, au kutundika vitu mahali fulani kama vile katika miti, au kumtaka mtu atupe vitu baharini, au avifukie ardhini.
- Humtaka mtu alete wanyama wenye sifa fulani, au wanyama wenye rangi fulani awachinje bila ya kutaja Jina la Allaah!
- Husoma Qur-aan kinyumenyume, au kuikhini Qur-aan kwa kuiweka sehemu zisizopasa.
- Huandika maneno ya Qur-aan na mengine ya kufru na kumtaka achemshe vikaratasi hivyo na kunywa maji yake, au hutia zaafarani au rangi kisha humfanyia kombe anywe kwa muda fulani.
- Humuuliza mtu jina la mama yake.
- Humtaka mtu nguo zake za ndani kwa ajili ya kupata jasho lake.
- Humtaka mtu ajitenge na watu abakie katika chumba cha kiza na aepukane na jua kwa muda wa masiku.
- Humtaka mtu asioge kwa masiku na aghalabu hutumia idadi ya arobaini (40).
- Humpa mtu kinywaji kisha humtapisha kwa njia mbali mbali na kumzuga macho aone kuwa ametokwa na vidudu tumboni!
- Humzuga macho na mwili kwa njia zake na kumchoma visu mwilini bila ya mtu kuhisi maumivu.
- Humpa mtu miiko asile vyakula fulani.
- Aghlabu hutumia vitambaa vyekundu katika kazi zao za uchawi.
- Na mengine mengineyo.
Rejea Makala: Jini, Shaytwaan Na Mchawi
2- Kufanya Au Kuhudhuruia Michezo Ya Sihri (Mazingaombwe)
Ama pia njia nyengine ya sihri ni watu kufanya michezo yake (mazingaombwe) na watu kugharamika kununua tiketi za kuingia michezoni kutazama uchawi. Hapo hufanya mazingaombwe ya kuwafanya watu watekwe akili zao na waone miujiza isiyokuwa ya kweli kama vile wachawi wa Fir’awn kabla ya kuamini kwao walipowahudhurisha halaiki ya watu uwandani wakayazuga macho yao:
قَالُوا يَا مُوسَىٰ إِمَّا أَن تُلْقِيَ وَإِمَّا أَن نَّكُونَ نَحْنُ الْمُلْقِينَ﴿١١٥﴾
(Wachawi) Wakasema: “Ee Muwsaa, ima utupe wewe au tuwe sisi wa (kwanza) kutupa.”
قَالَ أَلْقُوا ۖ فَلَمَّا أَلْقَوْا سَحَرُوا أَعْيُنَ النَّاسِ وَاسْتَرْهَبُوهُمْ وَجَاءُوا بِسِحْرٍ عَظِيمٍ﴿١١٦﴾
(Muwsaa) Akasema: “Tupeni!” Basi walipotupa, waliyasihiri macho ya watu na wakawatia woga, na wakaja na sihiri kuu. [Al-A’raaf: 115-116]
Ee ndugu Muislamu! Jiepushe na sihri na wachawi ubakie salama katika maasi, kufru na shirki kubwa kama hii!
Kwa aliyetendewa Sihri (uchawi) basi atafute Tiba ya Sunnah, maelezo yanapatikana katika kiungo kifuatacho:
10-Ruqya: Kutafuta Shifaa: Poza Ya Maradhi, Sihri (Uchawi) Katika Baadhi Ya Vyakula