24-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! Vipi Kujiepusha Na Shirki
إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم
Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!
24-Vipi Kujiepusha Na Shirki
Ndugu Muislamu! Hakika shirki ni dhulma kubwa mno! Kwa kumfanyia shirki Rabb wako Aliyekuumba, Ambaye unaishi katika ardhi Yake, Ambaye Anakuruzuku na Akakujaalia neema nyingi mno zisizohesabika, Ambaye Anakurehemu na Akakujaalia fadhila na neema za kila aina.
Miongoni mwa neema Zake Allaah ('Azza wa Jalla) ni kukujaalia uhai mpaka hii leo uweze kutambua yanayomshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ili urudie kutubia Kwake kabla ya kufariki kwako. Basi hii ni fursa adhimu kwa kila aliyekuwa akimshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) atekeleze yafuatayo ambayo yatasaidia kumuepusha na shirki In Shaa Allaah:
1. Tawbah ya kweli:
Rudi kwa Rabb wako kwa kutubia tawbah ya nasuha (kwelikweli) kama Anavyoamrisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يُكَفِّرَ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيُدْخِلَكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ يَوْمَ لَا يُخْزِي اللَّـهُ النَّبِيَّ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ ۖ نُورُهُمْ يَسْعَىٰ بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَبِأَيْمَانِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا أَتْمِمْ لَنَا نُورَنَا وَاغْفِرْ لَنَا ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٨﴾
Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya nasuha (kwelikweli); asaa Rabb wenu Akakufutieni maovu yenu, na Akakuingizeni Jannaat zipitazo chini yake mito. Siku ambayo Allaah Hatomfedhehesha Nabiy (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na wale walioamini pamoja naye. Nuru yao itatembea mbele yao na kuliani mwao, watasema: “Rabb wetu! Tutimizie Nuru yetu, na Tughufurie, hakika Wewe juu ya kila kitu ni Muweza. [At-Tahriym: 8]
Twabah ya nasuha ina masharti yafuatayo:
a. Kuomba maghfirah
b. Kuacha hayo maasi
c. Kujuta
d. Kuweka niyyah (azma) kuwa hatorudia tena
e. Kama kaidhulumu haki ya mtu basi ni kuirudisha hiyo haki.
Na kutubia shirki ni kujisalimisha katika Uislamu pekee kama alivyosema Imaam As-Sa’dy (Rahimahu Allaah) kuhusu Aayah:
قُل لِّلَّذِينَ كَفَرُوا إِن يَنتَهُوا يُغْفَرْ لَهُم مَّا قَدْ سَلَفَ وَإِن يَعُودُوا فَقَدْ مَضَتْ سُنَّتُ الْأَوَّلِينَ﴿٣٨﴾
Waambie waliokufuru kwamba wakikoma wataghufuriwa yaliyopita, lakini wakirudia, basi imekwishapita desturi ya watu wa awali. [Al-Anfaal: 38]
Akasema: “Wakikoma; inamaanisha kufru zao, nako ni kujisilimisha kwa Allaah Pekee bila ya kumshirikisha.”
Adhkaar mbalimbali zimethibiti katika Sunnah jinsi ya kuomba maghfirah, na Sayyidul-Istighfaar (du’aa kuu kabisa ya kuomba maghfirah) ni:
اللّهـمَّ أَنْتَ رَبِّـي لا إلهَ إلاّ أَنْتَ، خَلَقْتَنـي وَأَنا عَبْـدُك، وَأَنا عَلـى عَهْـدِكَ وَوَعْـدِكَ ما اسْتَـطَعْـت، أَعـوذُبِكَ مِنْ شَـرِّ ما صَنَـعْت، أَبـوءُ لَـكَ بِنِعْـمَتِـكَ عَلَـيَّ وَأَبـوءُ بِذَنْـبي فَاغْفـِرْ لي فَإِنَّـهُ لا يَغْـفِرُ الذُّنـوبَ إِلاّ أَنْتَ .
Allaahumma Anta Rabbiy laa ilaaha illaa Anta Khalaqtaniy wa ana ‘abduka wa anaa ‘alaa ‘ah-dika wawa’-dika mastatwa’-tu, a’uwdhu bika min sharri maa swana’-tu, abuw-u Laka bini’-matika ‘alayya wa abuw-u bidhanbiy, faghfirliy fainnahu laa yaghfirudh- dhunuwba illaa Anta.
Ee Allaah, Wewe ni Rabb wangu, hapana mwabudiwa wa haki ila Wewe, umeniumba mimi na mimi ni mja Wako, nami niko juu ya ahadi Yako, na agano Lako, kiasi cha uwezo wangu, najikinga Kwako kutokana na shari ya nilichokifanya, nakiri Kwako kwa kunineemesha, na nakiri kwa madhambi yangu, basi nakuomba unighufurie kwani hakuna wa kughufuria madhambi ila Wewe. [Al-Bukhaariy (7/150) [2306] kutoka kwa Shaddaad bin Aws Radhwiya Allaahu ’anhu]
Na Nabiy (Swalla Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akistaghfiru mara 70 kila siku na katika riwaayah nyingine mara 100 kwa siku:
الْأَغَرِّ الْمُزَنِيِّ رضي الله عنه أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: (إِنِّي لَأَسْتَغْفِرُ اللَّهَ فِي الْيَوْمِ مِائَةَ مَرَّةٍ) رواه مسلم (2702
Al-Agharr Al-Muzaniyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amepokea kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba: ((Hakika mimi nastaghfiru kwa Allaah mara mia katika siku moja)). [Muslim (2702)]
Na vilevile:
وقَالَ أَبُو هُرَيْرَةَ رضي الله عنه : سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ : ( وَاللَّهِ إِنِّي لاَسْتَغْفِرُ اللَّهَ وَأَتُوبُ إِلَيْهِ فِي الْيَوْمِ أَكْثَرَ مِنْ سَبْعِينَ مَرَّةً ) رواه البخاري (6307).
Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ’anhu) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Wa-Allaahi mimi nastaghfiru kwa Allaah na natubia Kwake zaidi ya mara sabini katika siku moja)). [Al-Bukhaariy (6307)]
Hivyo ni kusema: ”Astaghfiru Allaah wa atuwubu Ilayhi.”
Juu ya hayo, faida kadhaa za kuomba maghfirah zinamrudia bin-Aadam anayemuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) maghfirah.
2. Kuomba Isti’aanah (msaada) kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
Zidisha kuswali Swalaah za Sunnah na kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) humo Akuepushe na shirki. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ ﴿٤٥﴾
Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalaah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu. [Al-Baqarah: 45]
Pia, du’aa muhimu kabisa ya kujiepusha na shirki kama ilivyothibti katika Sunnah:
اللّهُـمَّ إِنّـي أَعـوذُبِكَ أَنْ أُشْـرِكَ بِكَ وَأَنا أَعْـلَمْ، وَأَسْتَـغْفِرُكَ لِما لا أَعْـلَم
Allaahumma inniy a’uwdhu Bika an ushrika Bika wa anaa a’-alamu wa astaghfiruka limaa laa a’-lam
Ee Allaah hakika mimi Najikinga Kwako kutokana na kukushirikisha hali ya kuwa najua na ninakuomba maghfirah kwa nisiyoyajua. [Ahmad (4/403) na wengineo; Taz. Swahiyh Al-Jaami’(3/233) [3731] na Swahiyh At-Targhiyb wat-Tarhiyb ya Al-Albaaniy (1/122) [36]
3. Kumdhukuru Allaah Kwa Wingi:
Mdhukuru mno Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) khaswa kwa kusoma Qur-aan kwa kuwa ni poza ya nyoyo kwa kila aina ya maradhi; kufru, shirki na kadhaalika. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ﴿٥٧﴾
Enyi watu! Kwa yakini yamekujieni mawaidha kutoka kwa Rabb wenu, na shifaa ya yale yaliyomo vifuani, na mwongozo na rahmah kwa Waumini. [Yuwnus: 57]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
اتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ ۗ وَلَذِكْرُ اللَّـهِ أَكْبَرُ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَصْنَعُونَ ﴿٤٥﴾
Soma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) uliyoletewa Wahy katika Kitabu na simamisha Swalaah, hakika Swalaah inazuia machafu na munkari. Na bila shaka kumdhukuru Allaah ni kubwa zaidi. Na Allaah Anajua yale mnayoyatenda. [Al-‘Ankabuwt: 45]
4. Kutafuta Na Kuongeza ‘Ilmu:
Mojawapo ya kinga ya shirki ni kuongeza ‘ilmu sahihi ya Dini hii tukufu ili kutambua yanayothibitisha Tawhiyd (Kumwpekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na yaliyo kinyume chake (yanayomshirikisha). Bila ya kuwa na ‘ilmu hutoweza kutambua. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ ۗ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٩﴾
Sema: “Je, wanalingana sawa wale wanaouja na wale wasiojua?” Hakika wanakumbuka wenye akili tu. [Az-Zumar: 9]
Na pia:
فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مُتَقَلَّبَكُمْ وَمَثْوَاكُمْ﴿١٩﴾
Basi jua kwamba laa ilaaha illa-Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah na omba maghfirah kwa dhambi zako na kwa ajili ya Waumini wa kiume na Waumini wa kike. Na Allaah Anajua harakati zenu huku na kule na pahala penu pa kupumzikia. [Muhammad: 19]
5. Kuwa Na Taqwa:
Kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kila wakati, kila mahali. Jibriyl ('Alayhis-Salaam) alipomwendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza maswali mojawapo lilikuwa kuhusu ihsaan akajibu:
أنْ تَعْبُدَ الله كَأَنَّكَ تَرَاهُ فإنْ لَمْ تَكُنْ تَرَاهُ فإنَّهُ يَرَاك
((Umwabudu Allaah kama kwamba unamuona, na ikiwa humuoni, basi Yeye hakika Anakuona)) [Muslim]
6. Kuwaza Adhabu Za Allaah Duniani Na Aakhirah:
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
حُنَفَاءَ لِلَّـهِ غَيْرَ مُشْرِكِينَ بِهِ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَكَأَنَّمَا خَرَّ مِنَ السَّمَاءِ فَتَخْطَفُهُ الطَّيْرُ أَوْ تَهْوِي بِهِ الرِّيحُ فِي مَكَانٍ سَحِيقٍ ﴿٣١﴾
Muelemee haki kwa kumwabudu Allaah Pekee bila ya kumshirikisha. Na yeyote anayemshirikisha Allaah basi kama kwamba ameporomoka kutoka mbinguni, wakamnyakua ndege au upepo ukamtupa mahali mbali mno. [Al-Hajj: 31]
Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
لَّا تَجْعَلْ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتَقْعُدَ مَذْمُومًا مَّخْذُولًا ﴿٢٢﴾
Usifanye pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine, ukaja kushutumiwa na mwenye kutelekezwa mbali (motoni). [Al-Israa: 22]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلَا تَجْعَلْ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتُلْقَىٰ فِي جَهَنَّمَ مَلُومًا مَّدْحُورًا ﴿٣٩﴾
Na wala usifanye pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine ukaja kutupwa katika Jahannam hali ya kuwa mwenye kulaumiwa na kufukuziliwa mbali. [Al-Israa: 39]
Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuhusu sifa za ‘Ibaadur-Rahmaan (Waja wa Mwingi wa Rahmah):
وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا ﴿٦٨﴾
Na wale ambao hawaombi pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine na wala hawaui nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha isipokuwa kwa haki, na wala hawazini. Na atakayefanya hivyo atakutana na adhabu.
يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا ﴿٦٩﴾
Ataongezewa adhabu maradufu Siku ya Qiyaamah, na mwenye kudumu humo akiwa amedhalilika.
إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾
Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda ‘amali njema; basi hao Allaah Atawabadilishia maovu yao kuwa mema. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.
وَمَن تَابَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَإِنَّهُ يَتُوبُ إِلَى اللَّـهِ مَتَابًا ﴿٧١﴾
Na atakayetubu na akatenda mema, basi hakika yeye anatubia kwa Allaah tawbah ya kweli. [Al-Furqaan: 68-71]
Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَالْمُشْرِكِينَ فِي نَارِ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَاۚ أُولَـٰئِكَ هُمْ شَرُّ الْبَرِيَّةِ ﴿٦﴾
Hakika wale waliokufuru miongoni mwa watu wa kitabu na washirikina watakuwa katika moto wa Jahannam, ni wenye kudumu humo; hao ndio waovu kabisa wa viumbe. [Al-Bayyinah: 6]
Na dalili nyingi nyenginezo zimetajwa katika Qur-aan na Sunnah kuhusu adhabu za mwenye kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) zikiwemo ambazo zimetajwa katika milango iliyotangulia ya somo hili la ‘Hakika Shirki ni Dhulma Kubwa Mno’, basi rudia ee ndugu Muislamu upate kujikumbusha na kuwaidhika zaidi.
Wa biLLaahi At-Tawfiyq.