010-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake: أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-AAKHIRU
أسماء الله الحسنى وصفاته
Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake:
الآخِرُ
010 - AL-AAKHIRU
AL-AAKHIRU: Wa Mwisho, hapana kitu baada Yake.
Kama ilivyotangulia katika Jina la Allaah, Al-Awwalu, kwamba Majina manne ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) yametajwa katika Aayah:
هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٣﴾
Yeye Ndiye wa Awali hakuna kitu kabla Yake, na wa Mwisho hakuna kitu baada Yake, na Aliye juu kabisa hakuna kitu juu Yake, na Aliye karibu kabisa, hakuna kitu kilicho karibu kuliko Yeye, Naye kwa kila kitu ni Mjuzi. [Al-Hadiyd: 3]
Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
… وَأَنْتَ الآخِرُ فَليْسَ بَعْدَكَ شيء،
… Nawe ni wa Mwisho, basi hakuna kitu baada Yako, [Muslim
Majina mawili ya Al-Awwalu na Al-Aakhiru kuenea kwake (’Azza wa Jalla) katika zama zote, na kwa viumbe vyote katika kila hali. [Madaarij As-Saalikiyn (1/31]
Allaah Mtukuka Ndiye wa Mwisho baada ya kila kitu, Asiyekuwa na ukomo, katika uwepo, sifa; sifa za kutukuka. Yeye Ndiye Mwenye kubaki baada ya kufa kila kitu na kuondoka, vyenye kuzungumza na vilivyokuwa kimya,
كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ ۚ
Kila kitu ni chenye kuhiliki isipokuwa Wajihi Wake. [Al-Qaswasw: 88]
Hakuna atakayebakia ardhini wala mbinguni kwa kuwa vyote vina mwanzo na mwisho isipokuwa Yeye (‘Azza wa Jalla):
رَفِيعُ الدَّرَجَاتِ ذُو الْعَرْشِ يُلْقِي الرُّوحَ مِنْ أَمْرِهِ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ لِيُنذِرَ يَوْمَ التَّلَاقِ ﴿١٥﴾
(Allaah) Mwenye uluwa juu ya vyeo na daraja. Mwenye ‘Arsh, Anapelekea Ar-Ruwh (Wahy) kwa amri Yake kwa Amtakaye miongoni mwa waja Wake, ili aonye Siku ya kukutana.
يَوْمَ هُم بَارِزُونَ ۖ لَا يَخْفَىٰ عَلَى اللَّـهِ مِنْهُمْ شَيْءٌ ۚ لِّمَنِ الْمُلْكُ الْيَوْمَ ۖ لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ ﴿١٦﴾
Siku watakayotokeza wao, hakitofichika kitu chochote chao kwa Allaah. “Ufalme ni wa nani leo?” (Allaah Mwenyewe Atajijibu): “Ni wa Allaah Pekee Mmoja, Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Asiyepingika.” [Ghaafir: 15-16]
Na katika Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) iliyopokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
يَطوي اللهُ عزَّ وجلَّ السَّماواتِ يومَ القيامةِ. ثمَّ يأخذُهنَّ بيدِه اليُمنَى. ثمَّ يقولُ: أنا الملِكُ. أين الجبَّارون؟ أين المُتكبِّرون؟ ثمَّ يَطوي الأرضين بشمالِه. ثمَّ يقولُ: أنا الملِكُ. أين الجبَّارون؟ أين المُتكبِّرون؟
Allaah ‘(Azza wa Jalla) Atakunja mbingu zote Siku ya Qiyaamah kisha Atazikamata Mkononi Mwake wa kuume Atasema: Mimi Ndiye Mfalme. Wako wapi waliojifanya majabari? Wako wapi waliotakabari? Kisha Atakunja ardhi mbili kwa Mkono Wake wa kushoto Atasema: Mimi Ndiye Mfalme, wako wapi waliojifanya majabari. Wako wapi waliotakabari?)) [Muslim 2788]
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Ambaye mambo ya waja Wake wote huishia Kwake, katika mambo yote ya kidunia na ya kidini. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba du’aa wakati wa kutaka kulala:
اللّهُـمَّ أَسْـلَمْتُ نَفْـسي إِلَـيْكَ، وَفَوَّضْـتُ أَمْـري إِلَـيْكَ، وَوَجَّـهْتُ وَجْـهي إِلَـيْكَ، وَأَلْـجَـاْتُ ظَهـري إِلَـيْكَ، رَغْبَـةً وَرَهْـبَةً إِلَـيْكَ، لا مَلْجَـأَ وَلا مَنْـجـا مِنْـكَ إِلاّ إِلَـيْكَ...
Allaahumma aslamtu nafsiy Ilayka, wa fawwadhwtu amriy Ilayka, wa wajjahtu waj-hiya Ilayka, wa alja-tu dhwahriy Ilayka, raghbatan warahbatan Ilayka. Laa malja-a walaa manjaa Minka illaa Ilayka...
Ee Allaah nimeisalimisha nafsi yangu Kwako, na nimekuachia mambo yangu Wewe na nimeuelekeza uso wangu Kwako na nimeutegemeza mgongo wangu Kwako, kwa matajarajio na kwa kukuogopa, hapana sehemu ya kukimbilia wala ya kujiokoa ila Kwako... [Al-Bukhaariy pamoja na Al-Fat-h (11/113) Muslim (4/2081)]
Jina hili Adhimu linathibitisha kuwa hatima ya wana Aadam wote ni kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ambaye Hana Mwisho.
Anasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۖ ثُمَّ إِلَيْنَا تُرْجَعُونَ ﴿٥٧﴾
Kila nafsi itaonja mauti, kisha Kwetu mtarejeshwa. [Al-‘Ankabuwt: 57]
قُلْ يَتَوَفَّاكُم مَّلَكُ الْمَوْتِ الَّذِي وُكِّلَ بِكُمْ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ ﴿١١﴾
Sema: “Atakufisheni Malaika wa mauti ambaye amewakilishwa kwenu, kisha kwa Rabb wenu mtarejeshwa.” [As-Sajdah: 11]
Na Jina hili linamtambulisha bin Aadam kwamba yeye hana budi kuwa na mwisho, kinyume na Allaah Ambaye ni Wa Mwisho hakuna kitu baada Yake, na kwamba mwisho wa mwana Aadam ni kurudia kwa Muumba wake (‘Azza wa Jalla) na kusimamishwa mbele Yake kuhesabiwa matendo yake:
إِنَّهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ بِالْقِسْطِ ۚ
Hakika Yeye Anaanzisha uumbaji, kisha Anaurejesha ili Awalipe kwa uadilifu wale walioamini na wakatenda mema. [Yuwnus: 4]
Na Anasema pia:
أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لَا تُرْجَعُونَ ﴿١١٥﴾
“Je, mlidhania kwamba Sisi Tulikuumbeni bila kusudio mcheze tu na kwamba nyinyi Kwetu hamtorejeshwa?” [Al-Muuminuwn: 115]