009-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-AWWALU

 

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

الأوَّلُ

009 - AL-AWWALU

 

 

 

AL-AWWALU:  Wa Awali bila ya mwanzo.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٣﴾

Yeye Ndiye wa Awali hakuna kitu kabla Yake, na wa Mwisho hakuna kitu baada Yake, na Aliye juu kabisa hakuna kitu juu Yake, na Aliye karibu kabisa, hakuna kitu kilicho karibu kuliko Yeye, Naye kwa kila kitu ni Mjuzi.  [Al-Hadiyd: 3]

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufasiria maana ya Majina ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) manne hayo yaliyotajwa pamoja, alikuwa akiomba katika du’aa:  

 اللهُمَّ أَنْتَ الأَوَّلُ فَليْسَ قَبْلكَ شيء، وَأَنْتَ الآخِرُ فَليْسَ بَعْدَكَ شيء، وَأَنْتَ الظَّاهِرُ فَليْسَ فَوْقَكَ شيء، وَأَنْتَ البَاطِنُ فَليْسَ دُونَكَ شيء، اقْضِ عَنَّا الدَّيْنَ وَاغْنِنَا مِنَ الفَقْرِ

Ee Allaah, Wewe wa Awali hivyo basi hakuna kitu kabla Yako, Nawe ni wa Mwisho, basi hakuna kitu baada Yako, Nawe Uko juu kabisa hakuna kitu juu yako, Nawe uko karibu kabisa, hakuna kitu kilicho karibu kuliko Wewe, Nikidhie deni langu na nitosheleze kutokana na ufakiri. [Muslim]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye wa Awali wala hakukuwepo na kitu kabla Yake hata kabla ya kuumba chochote kile:  

 عن عِمْرَانَ رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قَال: ((كَانَ اللهُ وَلمْ يَكُنْ شَيْءٌ غيرهُ، وَكَانَ عَرْشُهُ عَلى المَاءِ، ثُمَّ خَلقَ السَّمَاوَاتِ وَالأرْض، وَكَتَبَ فِي الذِّكْرِ كُل شَيْءٍ))  

Imepokelewa kutoka kwa ‘Imraan bin Huswayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Alikuwa Allaah na hakukuwa na kitu kabla Yake, na ‘Arsh Yake ilikuwa katika maji, kisha Akaumba mbingu na ardhi, na Akaandika kila kitu katika Adh-Dhikri (Ubao Uliohifadhiwa) [Al-Bukhaariy fiy Kitaabi Bad-i Al-Khalqi]

 

Naye (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Aliyetangulia kila kitu kwa muda usiokuwa na mwisho wake katika kuwepo Kwake, na katika Sifa Zake. Amekamilika dhati Yake, shani Yake iko juu ya kila kitu, kila kitu kina mwanzo wake na mwisho wake isipokuwa Yeye (‘Azza wa Jalla). Kila kitu kinarejea Kwake kwa kupewa na kupatikana na kuendelea, wakati wote. Hakuna Alichokiumba ila tu kitarudi Kwake ndio maana pale mtu anapopatwa na msiba khasa wa kufariki mtu hutamka kalimah ya Istirjaa’

إِنَّا لِلّهِ وَإِنَّـا إِلَيْهِ رَاجِعونَ

Sisi ni wa Allaah, na Kwake tunarejea [Muslim na imetajwa katika Qur-aan]  

 

Miongoni mwa faida za maarifa ya Jina hili tukufu ni kuwa, ili mwana Aadam atambue kwamba kwa vile asili yake kuumbwa ni udongo, na kwamba yeye ana mwanzo na ana uhai kwa muda na kisha ana mwisho wake wa kurudia kwa Rabb wa walimwengu. Anasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

كَيْفَ تَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَكُنتُمْ أَمْوَاتًا فَأَحْيَاكُمْ ۖ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٢٨﴾

Vipi mnamkufuru Allaah na hali mlikuwa wafu Akakuhuisheni, kisha Atakufisheni, kisha Atakuhuisheni, kisha Kwake mtarejeshwa?  [Al-Baqarah: 28]

 

Na pia:

هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٥٦﴾

Yeye Ndiye Anayehuisha na Anayefisha, na Kwake (Allaah) mtarejeshwa. [Yuwnus: 56]

 

Na kutambua pia uumbaji wa yote yaliyoko duniani yana mwanzo wake. Anasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

إِنَّهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ

Hakika Yeye Anaanzisha uumbaji, kisha Anaurejesha. [Yuwnus: 4]

 

Na Anasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ ۚ وَعْدًا عَلَيْنَا ۚ إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ ﴿١٠٤﴾

Kama Tulivyoanza umbo la awali Tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu Yetu. Hakika Sisi ni Wenye kufanya. [Al-Anbiyaa: 103]

 

Pia mwana Aadam anapata kuona na kukumbuka fadhila za Rabb Wake, na kutangulia Kwake katika kila neema, iwe ni ya ki-Dini au ya kidunia, na sababu na msababishi ni Yeye. Anasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

أَمَّن يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ وَمَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ ۚ قُلْ هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٦٤﴾

Au nani Anayeanzisha uumbaji, kisha Anaurejesha; na nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? [An-Naml: 64]

 

Na pia:

اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَكُمْ ثُمَّ رَزَقَكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ ۖ هَلْ مِن شُرَكَائِكُم مَّن يَفْعَلُ مِن ذَٰلِكُم مِّن شَيْءٍ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٤٠﴾

Allaah, Ambaye Amekuumbeni, kisha Akakuruzukuni, kisha Anakufisheni, kisha Atakuhuisheni.  [Ar-Ruwm: 40]

 

 

 

 

Share