Mwenye Kuzini Kwa Siri Nini Hukmu Yake?

  

SWALI:

Assalam aleykum, nawashukuru kwa kutuelimisha Allah (S.W.T) atawalipa Inshaalah je nini hukmu ya mtu aneyezini lakini ikawa anafanya siri.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake, Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka siku ya Mwisho

Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah سبحانه وتعالى Atutakabalie hizo du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelemishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn

Hukumu ya zinaa ikiwa ni kwa siri au ni dhahiri adhabu yake ni mijeledi 100 ikiwa mwanamke au mwanamume hajaolewa na ikiwa ameoa au ameolewa basi adhabu yake ni kupigwa mawe mpaka kufa. Mara nyingi sisi kama wanadamu na hasa kama waislamu tunakosa hisia kwa kuona kuwa tukifanya dhambi kwa siri basi huwa hakuna dhambi wala adhabu.

Sisi kwa siri hiyo tunaweza kukwepa adhabu ya hapa duniani lakini tujue ya kwamba adhabu ya Akhera inaumiza zaidi. Allah Anasema:

 ((كَذَلِكَ الْعَذَابُ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَكْبَرُ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ))  

((Namna hivi inakuwa adhabu (Ya Mola duniani) Na adhabu Akhera ni kubwa zaidi, laiti wangalijua!)) [Al-Qalam:33] 

 

Haya yetu ya kufanya madhambi kwa siri ni kukosa kwetu Ihsaan, kwani Mtume wa Allah amesema: “Ni kumuabudu Allah kama kwamba unamuona, kwani ikiwa humuoni basi Yeye Anakuona” (Muslim, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Abu Daawuud kutoka kwa ‘Umar ibn al-Khatwtwaab).

Na Mtume ametuusia kuwa tumche Allah popote pale tulipo na tukifanya baya basi tufuatishe kwa zuri, litafuta hilo baya

عن أبي ذَرٍّ جُنْدُب بِن جُنَادَة، وأبي عبد الرحمن مُعَاذ بِن جَبَلٍ رضي الله عنهما، عن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((اتَّقِ اللهَ حَيْثُما كنْتَ، وأَتْبِعِ السَّيئةَ الحسنةَ تَمْحُها، وخالقِ الناسَ بخُلُقٍ حسنٍ)). رَوَاهُ التِّرْمِذِيُّ   وَقَالَ: حَدِيثٌ حَسَنٌ، وَفِي بَعْضِ النُّسَخِ: حَسَنٌ صَحِيحٌ.

Kutoka kwa Abu Dharr Jundub Ibn Junaada na Abu 'Abdur- Rahmaan Mu'aAdh Ibn Jabal رضي الله عنهما  ambao wamemsikia Mtume صلى الله عليه وسلم akisema: ((Mche Allaah popote pale ulipo na fuatisha kitendo kibaya   kwa kitendo kizuri  kitafuta (kitendo kibaya) na ishi na watu kwa uzuri)) [Imesimuliwa na At-Tirmidhi na kasema kuwa ni hadithi Hasan na katika maandiko mengine imesemwa kuwa ni Hasan Sahihi]

Hii ni nasaha mzuri hivyo tunawausia ndugu na dada zetu sote kwa pamoja tumche Allah kwani mafanikio yetu hapa duniani na kesho Akhera ni kuwa katika msimamo huo.

Ikiwa tumefanya jambo baya, la makosa hiyo ni katika udhaifu wetu, binadamu. Hivyo, tuombe toba na tufanye mambo mema. Na tunamuomba Allah Atuepushe kufanya madhambi kwa siri au dhahiri.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share