Mume Mwenye Tabia Chafu Ya Liwati Anafaa Kuwa Imaam? Je, Inafaa Kumuozesha Mke?
SWALI:
Mwanamme anaemuendea kinyume cha maumbile mkewe (sehemu ya haja kubwa), anafaa mume huyu awe imamu? Nimeangalia baadhi ya majibu yaliyotolewa kuhusu mume mwenye sifa hii chafu, lkn sijaona kuhusu uimamu?
Jee jamii imuangalie vipi mwanamme huyu? Jee inafaa kumuozesha mtoto wa mtu mwanamme mwenye tabia hii ya Kaumu Lut?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwenda kinyume na maumbile/liwaat ni katika madhambi makubwa na ni katika uchafu wenye kupelekea kuharibika kwa maumbile, fitwrah, dini na dunia, bali ni uchafu unaofisidi na kuhariku uhai wote ndio Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akawaadhibu watu waliozuwa uchafu huo adhabu kali sana kama inavyothibitisha Qur-aan kwa kusema:
“Na tulimtuma Luutw', alipowaambia watu wake: Je, mnafanya uchafu ambao hajakutangulieni yeyote kwa uchafu huo katika viumbe vyote! Hivyo nyinyi mnawaingilia wanaume kwa matamanio mkawawacha wanawake? Kumbe nyinyi ni watu wafujaji! Na haikuwa jawabu ya kaumu yake isipokuwa kuambizana: Wafukuzeni katika mji wenu, maana hao ni watu wanaojitakasa. Basi tukamwokoa yeye na watu wake, isipokuwa mkewe, alikuwa miongoni mwa waliobakia nyuma. Na tukawamiminia mvua. Basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa wakosefu.” Al-A’raaf: 80-84 na pia tazama Suurat Huud: 77-83.
Basi ni vyema jamii ielimishwe na ielezwe bila ya kuogopa kuwa yaliyowafika wenye tabia chafu ya kwenda kinyume na maumbile, tabia ambayo hata wanyama hawanayo, ni katika mabalaa yanayoweza yakatufika kama hakutokuwa na wenye kusema kuwa haya ni machafu na ni haraam na hatarajiwi yeyote katika wenye kuaminiu Allaah na Siku ya Mwisho na akawa anatarajia malipo kwa Allaah kuthubutu kuruhusu amali kama hii, wachilia mbali kuthubutu kuruhusu nchi yake iwe ndio pahala pa kuhalalisha amali aliyoiharamisha Allaah na kuwaadhibu wahusika kwa adhabu kali kabisa. Na wanaofanya hayo ni miongopni mwa wale waliofadhilisha uhai huu kwa kuuza dini yao kwa kitu kidogo katika dunia kwa kuwakubalia wafadhili wao wahalalishe Alichokiharamisha Allaah na Akatoa adhabu ya kuigeuza nchi juu chini, na kuteremshiwa mvua ya changarawe za udongo mgumu uliokamatana wa Motoni na yaliyowafika wenda kinyume na maumbile/ liwaat hayako mbali na wenye kuihalalisha wachilia mbali wenye kutenda amali hiyo kama hawakutubia, na Allaah Ameijaalia kuwa miongoni mwa Aayah za Qur-aan inayotakiwa kusomwa (sio kusomewa maiti) ili iwe ni funzo na mawaidha kwa jamii na kwa wahusika kama wako katika jamii.
Suala lina utata isipokuwa tu kama muulizaji ni mke wa huyo mume basi hapana kitu kwani huwa anatafuta hukumu ya kisheria; ama ikiwa muulizaji anauliza tu kwa kumdhania mtu fulani Mwanamme anaemuendea kinyume cha maumbile mkewe, bila ya kuwa na ushahidi unaokubalika katika Uislamu; basi ieleweke kuwa yeyote katika wenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho iwe muulizaji wetu na wengine, akitujia na kutupa habari kama hii au yoyote yenye kuhitaji ushahidi na uthibitisho kwa kuwa ina hatari ndani yake madhara ni makubwa kuliko tunavyofikiria kwa jamii kama ulivyogusia ‘anafaa mume huyu awe imamu’ na kwa anaedhaniwa ‘jamii imuangalie vipi mwanamme huyu? hapa kama muulizaji ni mke wa huyo mume basi ni sawa, vyenginevyo patahitajika kufanyika uchunguzi ili kuweza kufikia kuelewa ukweli wake, kwa kuchelea tusije tukawaletea watu madhara, kwa kutojua hali yao tukabakia kujuta.
“Enyi mlioamini! Akikujieni mpotovu na khabari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kuto jua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyo yatenda.” Al-Hujuuraat : 6.
Hali ya pili ni kuwa muulizaji kama sio mke wa huyo mume, huenda akawa katika waliotakiwa kujitenga mbali na wingi wa kudhania dhana mbovu kwa watu, kwani katika baadhi ya dhana ni dhambi zinazostahiki adhabu (kama hii ya kwenda kinyume na maumbile ikiwa hakuna ushahidi) na kama jambo hilo lipo basi kwanini usimuaidhi kama wewe ni mke, au ilikuwa vyema upeleke lalamiko lako kwa wazazi au wahusika ili awaidhiwe na afaidike huenda akatubia na kuacha, kwani (kama muulizaji sio mke) kupekuwa na kuchunguza au kuwa na tabia ya kutafuta aibu na kuwatupia Waislamu si jambo linalotakiwa awe nalo Muislamu, kwani unaemsingizia ni ndugu yako Muislamu unaetakiwa umsitiri kwa kumuwaidhi na kumuelimisha; na kama unayosayema hanayo basi kufanya hivyo huwa ni ‘buhtaan’ (kosa kubwa zaidi ya kusengenya) kumzulia na kumsingizia mtu jambo ambalo hana.
Asli katika Uimamu (kuswalisha watu) ni kuwa aswalishe aliye bora katika kusoma Qur-aan: mwenye kusoma Qur-aan vizuri kama inavyotakiwa,
“…itapofikia wakati wa Swalah basi na aadhini mmoja wenu na aswalishe mkubwa wenu -na katika riwaya ya Abu Daawuud- Awaswalishe qawm (watu) aliye mbora wao katika kusoma Qur-aan….” Imepokelewa na Al-Bukhaariy na Abu Daawuud.
Jee jamii imuangalie vipi mwanamme huyu? Kwa kuwa hatuna uwezo wa kupitisha hukumu kwa hali tulizonazo hivi sasa na nchi tunazoishi ambazo hazifuati sheria za Kiislam, lakini hukumu yake Kiislam ni kuuliwa na kulaaniwa kwa yule mfanyaji na mfanywaji
Inafaa kumuozesha mtoto wa mtu mwanamme mwenye tabia ya kwenda kinyume na maumbile/ liwaat? Sehemu hii ya suala pia ina utata kwani kikawaida aliyefitinishwa na fitna kama hii huwa hana haja yoyote ile na wanawake isipokuwa kuwa shoga katika shoga zake na hili pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelikataza kumruhusu hanithi kuwa na ushoga na mkeo au mwanamke mwenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho, kwani kwa amali hii huweza kufikia akawa hana uwezo wa kumtekelezea mke haki yake ya kindoa (kumuingilia) kwani umuhimu wa mtu kuwa mwanamume na kuoa (sio mali) ni kuwa na uume na kama uume hauko au haufanyi kazi ni mzigo usio faida katika mwili basi ndio janga kubwa.
Tujaalie au tukadirie kuwa mtu mwenye tabia chafu na mbovu
Mke huwa ni mhanga ‘dhwahiyyah’ hivyo huwa hana raha wala utulivu na kubwa kuliko hayo huwa hana mapenzi ‘mawaddah’ wala rahmah ambazo ni katika desturi na kawaida za maisha ya mke na mume, hivyo basi uhai wa mke (kama hakulalamika na watu kulishughulikia lalamiko lake) humalizikia kuwa ni adhabu aliyotundikwa nayo; kwani anayumbayumba baina ya huku na huko, huku hayuko na huko hayuko; hayuko katika walioolewa, maana kubwa katika kuolewa ni kupatikana tendo la ndoa na yeye hajapata kulionja toka aolewe wala hakuna njia ya kulipata kwani halipo kwa aliyetarajiwa awe nalo (wala hayuko katika wajane) anatambuliwa na jamii kama ni mke wa Fulani (wala hayuko katika walioachwa) hii ni sababu tosha kwa mwanamke kudai talaka; hivyo kumuoza mtoto mtu mwenye tabia ya kwenda kinyume na maumbile/ liwaat ni kama kumchinja mtoto wako kwa kisu kisicho na makali na kumzika hali ya kuwa hai, kwani huenda akaingia katika zinaa kwa kutamani kupata wanachopata wanawake wenzake kwa waume zao au huenda akatumbukizwa katika jangwa lisilokadirika kwa huyo anayeitwa mume kumtafutia beberu la kumtimizia mkewe mahitaji yake. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atuepushe na uchafu huu na Awaepushe dada zetu na waume wenye sifa
Na Allaah Anajua zaidi