Dada Anatumia Uzuri Wake Kulaghai Wanaume Apate Pesa Kuzini, Anadai Mumewe Anamtesa – Anatia Aibu Familia

 

SWALI:

 

Assalamu aleikum

Nina swali langu siku zote nyumbani kila umuulizae kishashindwa nimeamua nkuulizeni nyie. Nina dada angu kaolewa hivi sasa ni mume wa tatu na kwa wote kapata watoto wanne lakini hajuulishi, ivi saivi karudi zake nyumbani sasa lakini ana mtindo wa kupenda wanaume wadogo na kuwala pesa na kuzini nao kwa kuutumia uzuri wake na kutojuulisha kama amezaa wala ameolewa, na kujitangazia kua mumewe hataki kutoa talaka ndo mana amejifunga na raha zaidi, tushakwisha mpa maneno ya dini mengi lakini anasema hanae mtu wa kumsaidia kipesa, na hua anapakazia familia yake kwa ubaya kama anateswa na maneno mengine zaidi ili watu wamuonee huruma na kumpa hizo pesa. Na hatujui nyumbani kama anarudi tahara au mchafu kimwili na analala na mwanawe wa miaka 3.. swali hili lishamshinda mpaka mama etu nyumbani naomba mutusaidie.

Natarajia jibu zuri inshallah

Ahsanteni

Wabillah tawfiq


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu dada yenu kutumia uzuri wake kwa ajili ya kuzini.

 

Ukweli wa mambo ni kuwa ‘amali mbovu zinamfanya mtendaji wake aingie katika madhara hapa duniani na pia Kesho Akhera. Zinaa ni katika dhambi kubwa ambalo tumeagiziwa na Allaah Aliyetukuka kuwa tusiikaribie kwa hali yoyote ile.

 

Bado nyie kama ndugu zake mnatakiwa muzungumze naye kwa njia ya upole, uzuri na maneno matamu kwa kumuonyesha makosa anayofanya. Jukumu hilo linawaangukia nyie, kwani Allaah Aliyetukuka Ametuambia tuokoe nafsi zetu na za familia zetu na moto wa Jahanamu (at-Tahriym [66]: 6). Mtahadharisheni kuwa uzinzi kwa siku hizi unaweza kumletea ugonjwa ambao hauna tiba kabisa kwa hivyo atahadhari sana kuhusu suala hilo.

 

Kulingana na swali lenu ni kuwa dada yenu bado ni mke wa mtu bila kutazama makosa yaliyotendeka. Ilikuwa ni busara zaidi kwenu kutomruhusu kurudi nyumbani kwenu akiwa yeye ni mke wa mtu. Inatakiwa muwasiliane na shemeji yenu kwa haraka mtake kujua ni kwa nini dada yenu ametoroka kutoka kwake. Ikiwa nyinyi mumemuachilia pia nanyi mtaingia katika madhambi kwa madhambi anayofanya dada yenu. Mkisha wasiliana na shemeji yenu inatakiwa muitishe kikao cha kusuluhisha baina ya mume (shemeji yenu) na dada yenu. Wala katika upatanishi musiwe ni wenye kumtetea dada yenu bali kuweni waadilifu na kumpatia makosa dada yenu ikiwa atakuwa amekosa. Na bila shaka mume wake atakapokuja katika kikao aje pamoja na wawakilishi wake, ikiwa ni baba na mamake au jamaa zake wengine. Na ikiwa kweli mnataka suluhu juu ya hilo, Allaah Aliyetukuka Atasahilisha suluhu na upatanishi baina yao. Ikiwa hakukupatikana suluhu baina ya wanandoa na dada yenu akashikilia kuwa anataka talaka akiwa yeye ni mkosa basi itabidi arudishe mahari kwa mumewe ili apate talaka hiyo kwa Qaadhi.

 

Ikiwa dada yenu amepata talaka kutoka kwa mume wake kwa radhi za mume mwenyewe itabidi mke mumrudishe kwa mumewe mpaka eda imalizike. Ikiwa amejivua katika ndoa kwa kumlipa mumewe mahari itabidi akae kwake (yaani nyumbani kwenu) lakini mumuekee masharti ya kuwa atajiwekea katika maadili ya Kiislamu yote yanayotakiwa. Ikiwa mumempatia nasaha na maneno ya Dini lakini amejikita katika maasiya ya zinaa basi itabidi mumpatie onyo kuwa akiendelea na madhambi yake hayo itabidi atoke akatafute nyumba nyingine sio pale kwenu.

 

Kususia watu wa maasi kunakubalika katika shari’ah yetu ya Kiislamu. Na hiyo twaipata katika Hadiyth ya 21 katika Riyaadhw asw-Swaaliyn cha Imaam an-Nawawiy ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaagizia Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhum) kuwasusia wale Maswahaba wengine watatu waliokosa kwenda katika Vita vya Jihaad bila ya udhuru wowote.

 

Kwa hivyo, hiyo ndio njia ya mwisho ambao mnaweza kuitumia katika kumkwaza dada yenu asiyaendee madhambi yaliyo makubwa na aache yaliyo madogo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share