Kumpatia Jirani Kazi Isiyo Ya Halali
SWALI:
Jirani yangu hana kazi kwa bahati msamaria mmoja akaniambia kuwa kuna nafasi ya kazi hotelini wasiwasi wangu ni kwamba hotelini kuna sehemu nyingi tu lakini yeye akanambia atamuweka popote atapojaaliwa hofu ni kwamba kama atafanya mambo ambayo si mazuri madhambi nitapata mimi nilomtafutia au yeye mwenywe
Muislamu mwenzenu
WABILLAHI TAUFIQ
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaama.
Jirani anafaa atendewe wema kwani Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wametuusia kuhusu hilo.
Kazi nayo ni ‘Ibadah katika Uislamu na hivyo Muislamu yafaa ajitahidi kutafuta kazi ya halali ili apate pato la halali na kuweza kujikimu kimaisha yeye pamoja na familia yake.
Muislamu hajaruhusiwa kufanya kazi yoyote apendayo, amewekewa masharti ya kazi atakayo kuifanya. Hakika ni katika jambo la thawabu kwa Muislamu kuweza kumpatia jirani yake na haswa akiwa ni Muislamu kazi ambayo ni ya halali. Haifai kwa Muislamu kumtafutia kazi ya haramu jirani yake. Ikiwa katika hoteli yenyewe kunauzwa vitu vya haramu kama vileo vya aina yoyote, au vyakula vya haramu kama nguruwe, na kadhalika itakuwa haifai kwako kufanya hilo. Ikiwa umempatia kazi ya haramu kwa kutojua utakuwa huna dhambi lakini kwa kujuta kwa hilo inatakiwa ulete istighfari nyingi pamoja na kufanya mema na huku unamuomba Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akusamehe madhambi yako. Hivyo, ikiwa kazi uliyompatia ni ya halali utapata thawabu na ikiwa ni ya haramu ujue utapata madhambi kabisa.
Inafaa baada ya kumpatia kazi umpatie nasaha kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Dini ni kupeana nasaha (kwa ikhlasi)” {Muslim, an-Nasaa’iy na Abu Daawuud}.
Dunia ina fitna katika mapambo yake na mambo ya maasiya. Baada ya kumpatia nasaha kuhusu hayo lau atafanya dhambi inatakuwa ni yake mwenyewe nawe hutambebea mzigo wake. Hata hivyo, inatakiwa kuwa ikiwa atafanya makosa basi umpatie nasaha kuhusu maisha na kufanya hivyo kutakuwa ni thawabu kwako. Lako wewe si lazima aongoke kwani mwenye kuongoa ni Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na wajibu wako ni kufikisha tu ujumbe. Lau katika kufikisha risala mtu mwenyewe atakuwa ni mwenye kusikiliza na kufuata basi utakuwa na ujira mkubwa zaidi.
Na Allaah Anajua zaidi