17-Wewe Pekee Tunakuabudu: Tawassul Zinazokubalika: Kutawassal Kwa Suwratul-Faatihah
إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ
Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada
Tawassul Zinazokubalika
17-Kutawassal Kwa Suwratul-Faatihah
Hii ni Suwrah tukufu kabisa katika Qur-aan, ina fadhila nyingi. Inaitwa Ummul-Kitaab (Mama wa Kitabu). Pia inaitwa Al-Faatihah (Ufunguo) kwa kuwa ni Suwrah ya mwanzo katika Muswhaf, na ni Suwrah inayopasa kusomwa katika kila rakaa ya Swalaah na bila kwayo, Swalaah haitimii. Inajulikana pia kwa majina yafuatayo: AlhamduliLLaah, Ummul-Qur-aan (Mama wa Qur-aan), Ash-Shifaa (Ponyo), Asw-Swalaah, Ar-Ruqya (tiba), Sab’ul-Mathaaniy (Aayah saba zinazokaririwa).
Na Allaah Ameigawa Suwrah hii sehemu mbili kama ilivyokuja maelezo yake katika Hadiyth Al-Qudsiy:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَنْ صَلَّى صَلاَةً لَمْ يَقْرَأْ فِيهَا بِأُمِّ الْقُرْآنِ فَهِيَ خِدَاجٌ)) ثَلاَثًا ((غَيْرُ تَمَامٍ)) فَقِيلَ لإِبِي هُرَيْرَةَ: إِنَّا نَكُونُ وَرَاءَ الإِمَامِ؟ فَقَالَ: اقْرَأْ بِهَا فِي نَفْسِكَ فَإِنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ يَقُولُ: ((قَالَ اللَّهُ تَعَالَى قَسَمْتُ الصَّلاَةَ بَيْنِي وَبَيْنَ عَبْدِي نِصْفَيْنِ, وَلِعَبْدِي مَا سَأَلَ. فَإِذَا قَالَ الْعَبْدُ (الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ) قَالَ اللَّهُ تَعَالَى: حَمِدَنِي عَبْدِي, وَإِذَا قَالَ (الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ), قَالَ اللَّهُ تَعَالَى: أَثْنَى عَلَيَّ عَبْدِي, وَإِذَا قَالَ (مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ) قَالَ: مَجَّدَنِي عَبْدِي, وَقَالَ مَرَّةً فَوَّضَ إِلَيَّ عَبْدِي, فَإِذَا قَالَ (إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ) قَالَ: هَذَا بَيْنِي وَبَيْنَ عَبْدِي وَلِعَبْدِي مَا سَأَلَ))
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeswali Swalaah bila ya kusoma humo Mama wa Qur-aan, basi haijatimia)) (alikariri mara tatu “haijatimia”). Mtu mmoja akamwambia Abuu Hurayrah: Je, hata tukiwa nyuma ya Imaam? Akasema: Isome katika nafsi yako kwani nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Allaah Ta’aalaa Amesema: Nimeigawa Swalaah baina Yangu na mja Wangu nusu mbili, mja Wangu atapata yale aliyoyaomba. Mja anaposema “Al-HamduliLaah Rabb wa walimwengu.” Allaah Ta’aalaa Husema: Mja Wangu amenihimidi. Na anaposema “Ar-Rahmaan, Mwenye kurehemu. ”Allaah Ta’aalaa Husema: Mja wangu amenisifu na kunitukuza kwa wingi. Na anaposema “Mfalme wa Siku ya Malipo.” Allaah Ta’aalaa Husema: Mja wangu ameniadhimisha. Na mara moja alisema: Mja wangu ameniaminisha. Na anaposema “Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.” Husema: Hii ni baina Yangu na mja Wangu, na mja Wangu atapata kile alichokiomba. Na anaposema “Tuongoze njia iliyonyooka, njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea.” Husema: Hii ni ya mja Wangu na mja Wangu atapata kile alichokiomba)) [Muslim, Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy , Ibn Maajah, Maalik]
Ibn Al-Qayyim amesema: “(Suwrah hii) imejumuisha baina Tawassul kwa Allaah (Ta’aalaa) kwa himdi na thanaa (kumsifu na kumtukuza kwa wingi) na kumuadhimisha, na kutawassal Kwake kwa kumfanyia Yeye ‘ibaadah na Tawhiyd (kumpwekesha Kwake). Kisha likaja ombi muhimu kabisa la kuombwa na la tamanio la kufaulu kabisa nalo ni hidaaya baada ya wasiylah mbili. Basi mwombaji kwayo ana uhakika wa wa kuitikiwa” [Madaarij As-Saalikiyn (1/24)]
Amesema pia: “Juu ya ufupi wake lakini inabeba aina zote tatu za Tawhiyd; Tawhiyd Ar-Rubuwbiyyah (Kumpwekesha Allaah katika Uola), Tawhiyd Al-Uluwhiyyah (kumpwekesha Allaah katika ‘ibaadah), na Tawhiyd Al-Asmaa Wasw-Swifaat (Kumpwekesha Allaah katika Majina Na Sifa Zake).” [Madaarij As-Saalikiyn (1/24-27)]
Dalili ya Suwratul-Faatihah kuwa ni shifaa, ni kisa katika Hadiyth ifuatayo; kwa hiyo anaweza mtu kutawassal nayo ili aponyeshwe ugonjwa wake:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: كُنَّا فِي مَسِيرٍ لَنَا فَنَزَلْنَا فَجَاءَتْ جَارِيَةٌ فَقَالَتْ: "إِنَّ سَيِّدَ الْحَيِّ سَلِيمٌ وَإِنَّ نَفَرَنَا غَيْبٌ فَهَلْ مِنْكُمْ رَاقٍ؟" فَقَامَ مَعَهَا رَجُلٌ مَا كُنَّا نَأْبُنُهُ بِرُقْيَةٍ, فَرَقَاهُ فَبَرَأَ فَأَمَرَ لَهُ بِثَلاَثِينَ شَاةً وَسَقَانَا لَبَنًا فَلَمَّا رَجَعَ قُلْنَا لَهُ: "أَكُنْتَ تُحْسِنُ رُقْيَةً أَوْ كُنْتَ تَرْقِي؟" قَالَ: "لاَ مَا رَقَيْتُ إلاَّ بِأُمِّ الْكِتَابِ." قُلْنَا: "لاَ تُحْدِثُوا شَيْئًا حَتَّى نَأْتِيَ أَوْ نَسْأَلَ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ)." فَلَمَّا قَدِمْنَا الْمَدِينَةَ ذَكَرْنَاهُ لِلنَّبِيِّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فَقَالَ: ((وَمَا كَانَ يُدْرِيهِ أَنَّهَا رُقْيَةٌ؟ اقْسِمُوا وَاضْرِبُوا لِي بِسَهْمٍ))
Amesimulia Abuu Sa'iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه): Tulikuwa katika safari tukateremka mahali, akaja kijakazi akasema: Bwana wetu ametafunwa na nge na wanaume wetu hawapo, je, yupo kati yenu tabibu? Akasimama pamoja naye mtu mmoja ambaye hatukudhania kuwa anajua ruqyah (utabibu). Akamtibu kwa ruqyah akapona. Akampa kondoo thelathini na akatupa maziwa tunywe (kama ni malipo). Aliporudi tukamwambia: Je, ulikuwa kweli unajua kutibu kwa ruqyah, au ulikuwa unabahatisha tu? Akasema: Hapana, bali nimemsomea Ummul-Kitaab (Suwrah Al-Faatihah). Tukasema: Tusiseme kitu hadi tumfikie au tumuulize Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Tulipofika Madiynah, tulimwelezea Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Alijuaje kuwa (Al-Faatihah) ni ruqyah? Gawaneni na mnitolee sehemu (ya kondoo.” [Al-Bukhaariy]
Ibn Al-Qayyim amesema: “(Suwrah Al-Faatihah) ni ufunguo wa Kitabu na Mama wa Kitabu na Aayah saba zinazokaririwa, na shifaa kamili na dawa ya kunufaisha, na ruqya kamili, na ufungo wa utajiri na kufaulu, na hifadhi ya nguvu, na kinga ya dhiki na ghamu na khofu na huzuni kwa mwenye kuijua thamani yake na akaipa haki yake na akautumia vizuri uteremsho wake (Al-Faatihah) kwa ugonjwa wake na akajua njia ya kuiombea shifaa na kupata dawa kwayo na ni siri ambayo imekusudiwa kwa ajili yake….” [Zaad Al-Ma’aad (4/318)]
Amesema pia: “Nilikuwa na maumivu mabaya mno kiasi ilikaribia kunifanya nishindwe kutembea, na hivyo ilikuwa wakati wa twawaaf na kwengineko. Basi nikakimbilia kusoma Suwratul-Faatihah na kupangusa kwayo mahali pa maumivu. Ikawa kama kijiwe kinaanguka. Nikajaribu hiyvo mara kadhaa na nikawa nachukua gilasi ya maji ya zamzam nayasomea Al-Faatihah mara kwa mara kisha nakunywa. Nikapata nafuu na nguvu ambayo sijapatapo kuipata mfano wake katika dawa.” [Madaarij As-Saalikiyn (1/58)]