00-Kitaab At-Tawhiyd: Historia Fupi Ya Imaam Muhammad Bin ‘Abdil-Wahhaab

00-Historia Fupi Ya Imaam Muhammad Bin ‘Abdil-Wahhaab[1]

 

 

 Asili yake

 

Jina lake ni Abul-Husayn Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab bin Sulaymaan bin ‘Aliy Musharrif Al-Wuhaybiy. Kabila lake ni Bani Tamiym. Amezaliwa mwaka 1115 H (1704 M) katika mji ya ‘Uyaynah kijiji cha Yamaamah ndani ya Najd, kaskazini Magharibi ya mji wa Riyadhw, Saudi Arabia. Ametoka katika familia ya Wanachuoni kwani baba yake ‘Abdul-Wahhaab alikuwa ni Mwanachuoni maarufu wa Najd na Qaadhwiy wa mji huo.

 

 

Elimu Yake

 

Alijifunza kusoma Qur-aan alipokuwa na umri mdogo na akaihifadhi akiwa chini ya umri wa miaka kumi. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Alimjaalia kuwa na uhodari na akili nzuri, wepesi wa kufahamu na kumaizi jambo au somo. Alipendezewa mno kusoma kazi za Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah na mwanafunzi wake Ibn Al-Qayyim (رحمهما الله).

Alifanya bidii kwenye masomo yake na kuendelea kujifunza chini ya usimamizi wa baba yake. Akajifunza elimu ya Dini chini ya Wanachuoni walioko mjini mwake wakiwemo baba yake na ‘ammi yake. Alisafiri kutoka kwenda Madiynah kusoma chini ya Wanachuoni wakubwa wa huko akiwemo; Shaykh ‘Abdullaah bin Ibraahiym bin Ash-Shamariyy, na Mwanachuoni maarufu wa India Shaykh Muhammad Hayaat Al-Sindi. Alikwenda Makkah pia na alitekeleza Hajj. Hatimaye akaelekea Baswrah (Kaskazini Iraq) kutafuta elimu zaidi akasoma chini ya Wanachuoni wa huko akawa maarufu kwa mijadala baina yake na Wanachuoni.

 

Harakaat Na Mitihani

 

Watu wa Najd walikuwa katika shirki na bid’ah (uzushi). Walikuwa wakiabudu waabudiwa wengi na kuabudu makaburi, miti, mawe, mapango, majini na mashaytwaan, waja wema waliojulikana kama ni mawalii. Uchawi na unajimu (utabiri wa nyota) ulisambaa pia. Hakuna aliyekataza ‘iIbaadah potofu hizo kwani watu walikuwa katika kuchuma manufaa na starehe za dunia zaidi na wakakhofia kuyapoteza hayo. Hivyo Shaykh akaona umuhimu mkubwa uliohitajika kuwarudisha watu katika manhaj ya Qur-aan na Sunnah. Akaanza kuwalingania watu katika Tawhiyd - kumpwekesha Allaah (سبحانه وتعالى) bila ya kumshirikisha na lolote katika ‘ibaadah. Akaazimia kujitumikisha peke yake kwa uvumilivu katika konde. Akajua hakuna lolote kitachofaulu kufanyika ila jihaad katika njia ya Allaah.

 

Shaykh alikumbana na mitihani, misukosuko, na vitisho, lakini alikuwa ameshategemea hali hiyo kumfikia na alikuwa tayari kukabaliana nayo kwani alitambua kuwa hilo ni jambo lisiloepukika kwa kila mlinganiaji kwani ndio hali waliyokutana nayo Manabii wote, na Salafus-Swaalih (waja wema waliotangulia).

 

Miongoni mwa mitihani aliyokumbana nayo ni kutokana na Wanachuoni dhaifu wasiokuwa na hoja ambao walimpinga na kumfanya akabiliane na misukosuko, vitisho na kukasirikiwa. Pia alikabiliana na misukosuko na mateso chini ya mikono ya madhalimu wa Huraymilaa. Na alipowashawishi watawala wahukumu madhalimu kwa Shariy’ah ya Kiislamu, ilisababisha baadhi ya watu kuyaweka maisha yake khatarini lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Alimnusuru.

Aliamua kurudi kwao ‘Uyaynah, ambako kipindi hicho kulikuwa chini ya utawala wa mtoto wa Mfalme ‘Uthmaan bin Muhammad bin Mu’ammar, ambaye alimpokea Shaykh kwa ukarimu na kumuahidi kumuunga mkono na kumsaidia kuwaita watu katika Uislamu.

 

Akaendelea kufundisha na kutoa da’wah hatimaye akashawishika kidhati na kwa vitendo kuondoa dini ya waabudiwa wengi pale alipoona baadhi ya watu ni wagumu kurudi katika Uislamu. Aliweza kumshawishi gavana wa mji huo kulivunja zege lililojengewa juu ya kaburi la Zayd bin Al-Khattwaab ambaye alikuwa ni kaka wa ‘Umar bin Al-Khattwaab (رضي الله عنهما). Akavunjavunja mangome mengineyo, mapango, miti n.k. Akaamrisha Shariy’ah ya Kiislamu itekelezwe.

Shaykh aliendelea na harakati zake za kauli na ‘amali ambazo zilimfanya azidi kuwa maarufu. Hatimaye akawa Jaji (Qaadhwiy) wa mji wa ‘Uyaynah. Lakini hakuweza kuendelea hapo kwani Mfalme alishawishiwa na viongozi wa miji ya jirani amuue Shaykh kwa vile hawakupendezewa na da’wah yake. Ikabidi afukuzwe katika mji huo.

 

Akakaribishwa mji wa Ad-Dir’iyyah ambao ulikuwa ni jirani yake. Huko akakaribishwa ingawa kwanza alitiliwa shaka. Alifikia kwa mja mwema aliyempokea ila alimkhofia kutokukubaliwa na mtoto wa Mfalme Muhammad bin Sa’uwd.  Khabari zikamfikia kwanza mke wa Ibn Sa’uwd ambaye alikuwa mkarimu na mwenye taqwa. Akamfahamisha mumewe kwa kumwambia, “Hii ni tawfiyq kubwa umeletewa kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى); huyo ni mtu ambaye anawaita watu katika Uislamu, anawaita katika Qur-aan na Sunnah za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Tawfiyq iliyoje? Mkimbilie haraka na umuunge mkono wala usimpinge au kumkataza kwa hayo.” Muhammad bin Sa’uwd akakubali ushauri wa mkewe na akaenda kwa Shaykh na akafanya mkataba naye kwamba asiondoke nchini hapo. Ndipo Shaykh akaweka makazi yake hapo na kuendelea na da’wah. Akaendelea na harakati za da’wah hapo Dar’iyyah. Akaheshimika na kupendwa mno na akaungwa mkono na watu. Da’wah yake iliwaathiri na kuwapendeza mno watu. Ikaenea katika nchi za Kiislamu na nyinginezo. Wakimiminika watu kufika hapo Dar’iyyah kujifunza kwake

 

Kama ijulikanavyo, kila jema halikosi mitihani. Wakatokeza wapinzani na waliokuwa na chuki naye. Kulikuweko waliompinga da’wah yake ya kuondosha shirki na bid’ah na kuwaita watu katika Tawhiyd. Kuna wengine waliompinga kabisa kwa sababu ya kukhofu kufukuzwa katika nafasi au vyeo vyao vya kazi. Kwa hiyo wengine walimpinga kwa ajili ya Dini, na wengine walimpinga kisiasa. Wapinzani wake walimzushia ya kumzushia walifika hadi kudai kwamba Shaykh alikuwa ni mfuasi wa Khawaarij. Na mara nyingine wakimlaumu bure bila ya dalili na nje ya upeo wa elimu zao. Hivyo yakaweko malumbano na majibishano yaliyoendelea katika mijadala kadhaa. Shaykh aliwaandikia kuwajibu madai yao, na wao walimrudishia majibu na yeye akawa akiwathibitishia ufahamu wao mbaya wa shariy’ah na Dini kwa ujumla kwa dalili. Ndipo wingi wa maswali na majibu yakawajumuisha watu na wakazidi kuongezeka. Baadhi ya mijadala hiyo iliandikwa na kuchapishwa katika vitabu.

 

Athari Ya D’awah Yake

 

Da’wah yake ya takriban miaka 50 imedhihirika na kuleta athari kubwa kwanza kwa Waislamu wa zama hizo. Watu waliacha kuabudu makaburi, miti, mawe, majini, utabiri wa nyota na kila aina ya shirki. Imewatoa pia watu katika ujinga wa kufuata mila za mababu bila ya dalili.  Maamrisho ya mema na makatazo ya maovu yakalinganiwa katika Misikiti. Na hapo msimamo wa Qur-aan na Sunnah ukahuishwa na shirki na bid’ah zikatoweka. Amani na utulivu ukawafunika watu kila mahali. Hadi zama hizi da’wah yake imekuwa na umuhimu mkubwa katika jamii ya Kiislamu. Vijana khasa kutoka nchi za Magharibi na zaidi wale wanaosilimu wamekuwa na hamasa na shauku kubwa ya kujifunza Dini iliyo sahihi na si ile iliyochanganywa na shirki na bid’ah. Kwa hiyo, mafundisho ya msimamo wake wa Ahlus-Sunnah wal-Jama’ah umekuwa ni jambo lililopewa kipaumbele katika lengo la kutafuta elimu kwa Waislamu wanaotafuta na kupenda haki.

Kazi Zake

 

Ameandika vitabu vingi vya mafunzo mbali mbali lakini alitilia mkazo zaidi katika somo la Tawhiyd na ‘Aqiydah. Na alitumia hikmah ya kuandika vitabu vidogo vidogo vilivyokusanya nukta mbalimbali muhimu kabisa kuhusiana na misingi ya Dini. Vilikuwa ni mukhtasari wa maudhui aliyotaka kuidhihirisha. Na vitabu hivyo vimekuja kufafanuliwa kwa kushereheshwa na ‘Ulamaa kadhaa na vimekuwa vina umuhimu mno katika vyuo vya Kiislamu vinavyofuata mwenendo wa Ahlus-Sunnah wal-Jama’ah.

 

Vifuatavyo ni baadhi ya vitabu vyake maarufu.

Vinne vya mwanzo ni mashuhuri zaidi. Na vinginevyo vimekusanywa na kujumuishwa katika ‘Maj’muw’at Mu-allafaatil-Imaam Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab’.

1.      Kitaabut-Tawhiyd - kitabu hiki kimekuwa mashuhuri mno na kimeenea sana na somo lake limekuwa ni lenye kutoa mafunzo muhimu kuhusu kumpwekesha Allaah na kuepukana na shirki.

2.      Al-Uswuul Ath-Thalaathah – kitabu kitoacho mafunzo kuhusu asili au misingi ya Uislamu.

3.      Al-Qawaaid Al-Arba’- kinatoa mafunzo ya kanuni za ufahamu wa shirki kwa ujumla.

4.      Kashf Ash-Shubuhaat - kinakanusha hoja zinazojulikana na watetezi wa shirki na bid’ah.

5.      Mukhtaswar Al-Inswaaf was-Sharh Al-Kabiyr.

6.      Mukhtaswar Zaad Al-Ma’aad.

7.      Mukhtaswar As-Siyrah.

8.      Mukhtaswar al-Fat-h.

9.       Masaail Al-Jaahiliyyah.

10.  Adaab Al-Mashiy ilaa As-Swalaah.

11.  Nawaaqidhw Al-Islaam.

 

Wanafunzi Wake

 

Alikuwa na wanafunzi wengi mno. Miongoni mwao ni watoto na wajukuu wake ambao waliendeleza kazi yake ya da’wah na Jihaad katika njia ya Allaah, walifungua vyuo karibu na kwao wakifunza watu masomo ya Dini. Kati ya watoto wake ni Al-Husayn, ‘Aliy, ‘Abdullaah na Ibraahiym. Na kati ya wajukuu wake ni ‘Aliy bin Al-Husayn, na pia ‘Abdur-Rahmaan bin Al-Hasan aliyeandika kitabu cha ‘Fat-h Al-Majiyd Sharh Kitaab At-Tawhiyd’. Wanafunzi wake wengineo ni ‘Abdul-‘Aziyz bin Muhammad bin Sa’uwd, Hamad bin Naaswir bin Mu’ammar na ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Husayn.

 

Familia Yake

Alikuwa na watoto sita; Al-Husayn, ‘Abdullaah, Al-Hasan, ‘Aliy, Ibraahiym, ‘Abdul-‘Aziyz.

Shaykh anatokana na kizazi kinachojulikana kwa ‘Aal-Shaykh’ ambacho kimetoa Wanachuoni kadhaa akiwemo Shaykh Muhammad bin Ibraahiym Aal-Shaykh aliyekuwa Mufti mkuu wa awali Saudi Arabia na Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz Aal-Shaykh  ambaye ni Mufti mkuu wa sasa.

 

Kifo Chake

 

Alifariki mwaka 1206 H (1792 M) akiwa na umri wa miaka 91. Rahmah za Allaah ziwe juu yake na Allaah Amruzuku Jannah ya Firdaws. Aamiyn.

 

 

 

 

[1]Marejeo: Imaam Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab Da’watuhuu wa Siyraatuhu - Shaykh Ibn Baaz.

 

Share