01-Kitaab At-Tawhiyd: Fadhila Za Tawhiyd
Mlango Wa 1
فَضْلُ اَلتَّوْحِيدِ
Fadhila Za Tawhiyd
وَقَوْلُ اَللَّهِ تَعَالَى:
Na kauli Ya Allaah Ta’aalaa:
وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ﴿٥٦﴾
((Na Sikuumba majini na wana Aadam isipokuwa waniabudu)) [Adh-Dhaariyaat (51: 56)]
وَقَوْلُهُ تَعَالَى:
Na kauli Yake Ta’aalaa:
وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ ۖ
((Na kwa yakini Tulituma katika kila ummah Rasuli (alinganie) kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na twaghuti)) [An-Nahl (16: 36).]
وَقَوْلُهُ:
Na kauli Yake:
وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ
((Na Rabb wako Amehukumu kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na (Ameamrisha) kuwafanyia ihsaan wazazi wawili)) [Al-Israa (17: 23)]
وَقَوْلُهُ:
Na kauli Yake:
وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ
((Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote)) [An-Nisaa (4: 36)]
وَقَوْلُهُ:
Na kauli Yake:
قُلْ تَعَالَوْا أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ ۖ أَلَّا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۖ وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُم مِّنْ إِمْلَاقٍ ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُكُمْ وَإِيَّاهُمْ ۖ وَلَا تَقْرَبُوا الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ ۖ وَلَا تَقْتُلُوا النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿١٥١﴾
((Sema: “Njooni nikusomeeni yale Aliyoyaharamisha Rabb wenu kwenu. Kwamba msimshirikishe na chochote, na muwafanyie ihsaan wazazi wawili, na wala msiwaue auladi wenu kutokana na umasikini. Sisi Tunakuruzukuni pamoja nao. Na wala msikaribie machafu yaliyo dhahiri na yaliyofichika. Na wala msiue nafsi ambayo Ameiharamisha Allaah (kuiua) isipokuwa kwa haki (ya shariy’ah). Hivyo ndivyo Alivyokuusieni kwayo mpate kutia akilini”))
وَلَا تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ حَتَّىٰ يَبْلُغَ أَشُدَّهُ ۖ وَأَوْفُوا الْكَيْلَ وَالْمِيزَانَ بِالْقِسْطِ ۖ لَا نُكَلِّفُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۖ وَإِذَا قُلْتُمْ فَاعْدِلُوا وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَىٰ ۖ وَبِعَهْدِ اللَّـهِ أَوْفُوا ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿١٥٢﴾
((“Na wala msiikaribie mali ya yatima isipokuwa kwa njia ya ihsaan mpaka afikie umri wa kupevuka. Na timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu. Hatukalifishi nafsi isipokuwa kadiri ya uwezo wake. Na mnaposema basi fanyeni uadilifu japokuwa ni jamaa wa karibu. Na timizeni ahadi ya Allaah. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kukumbuka))
وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٥٣﴾
((“Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa”)) [Al-An-‘aam (6: 151-153)]
قَالَ اِبْنُ مَسْعُود (رضي الله عنه): مَنْ أَرَادَ أَنْ يَنْظُرَ إِلَى وَصِيَّةِ مُحَمَّدٍ (صَلَّى اَللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) اَلَّتِي عَلَيْهَا خَاتَمُهُ فَلْيَقْرَأْ قَوْلَهُ تَعَالَى: ((قُلْ تَعَالَوْا أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ ۖ أَلَّا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ )) إِلَى قَوْلِهِ ((وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ...)) الآيَةَ.
Amesema Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه): “Anayetaka kuangalia wasiya wa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ambao ulikuwa na muhuri wake, basi asome kauli za Allaah: ((Sema: “Njooni nikusomeeni yale Aliyoyaharamisha Rabb wenu kwenu. Kwamba msimshirikishe na chochote…)) hadi kauli Yake: ((Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. … )) mpaka mwisho wa Aayah [At-Tirmidhiy (3080) At-Twabaraaniy katika Mu’jam Al-Awsatw (1208) na amesema At-Tirmidhiy : Hii ni Hadiyth Hasan Ghariyb]
عَنْ مُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ (رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: كُنْتُ رَدِيفَ اَلنَّبِيِّ (صَلَّى اَللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) عَلَى حِمَارٍ فَقَالَ لِي: ((يَا مُعَاذُ؟ أَتَدْرِي مَا حَقُّ اَللَّهِ عَلَى الْعِبَادِ، وَمَا حَقُّ الْعِبَادِ عَلَى اَللَّهِ؟)) قُلْتُ اَللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ، قَالَ: ((حَقُّ اَللَّهِ عَلَى الْعِبَادِ أَنْ يَعْبُدُوهُ، وَلاَ يُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا، وَحَقُّ الْعِبَادِ عَلَى اَللَّهِ أَنْ لاَ يُعَذِّبَ مَنْ لاَ يُشْرِكُ بِهِ شَيْئًا)) قُلْتُ يَا رَسُولَ اَللَّهِ أَفَلاَ أُبَشِّرُ اَلنَّاسَ؟ قَالَ: ((لاَ تُبَشِّرْهُمْ فَيَتَّكِلُوا)) أَخْرَجَاهُ فِي اَلصَّحِيحَيْنِ
Imepokelewa kutoka kwa Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه) amesema: Nilikuwa nyuma ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) juu ya punda akasema: ((Ee Mu’aadh! Unajua nini haki ya Allaah juu ya waja Wake, na nini haki ya waja juu ya Allaah?)) Nikajibu: Allaah na Rasuli Wake wanajua zaidi: Akasema: ((Haki ya Allaah kwa waja wake ni kwamba wamwabudu na wasimshirikishe na chochote. Na haki ya waja kwa Allaah ni kwamba Hatomwadhibu yeyote ambaye hamshirikishi na chochote)). Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Niwabashirie watu? Akasema: ((Usiwabashirie wasije kuitegemea)) [wakaacha kufanya juhudi katika ‘ibaadah])) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Masuala Muhimu Yaliyomo:
1-Hekima ya kuumbwa majini na wana Aadam.
2-Al-‘Ibaadah inamaanisha (hususani) Tawhiyd kwani ndio mada kuu ya hoja (hapo juu) na kinyume chake ni shirki ambayo humbaidisha mtu na Allaah (سبحانه وتعالى) na ndio jambo walotatizana Rusuli na washirikina.
3-Asiyetekeleza masharti ya Tawhiyd, atakuwa hajamwabudu Allaah (سبحانه وتعالى) ipasavyo kwa sababu katika Tawhiyd tu ndio huthibitika maana ya kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ ﴿٣﴾
((“Na wala nyinyi si wenye kuabudu Yule Ninayemwabudu)) [Al-Kaafiruwn (109: 3)]
4-Hekima ya kutumwa Rusuli.
5-Ujumbe huo (wa Tawhiyd) umefikishwa kwa kila ummah.
6-Dini ya Rusuli ni moja (haitofautiani).
7-Suala lenye umuhimu mkubwa hapa ni kwamba, kumwabudu Allaah hakutambuliki pasina kukanusha twaghuti. Hapo ndipo kwenye maana ya kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):
فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ
((Basi atakayemkanusha twaghuti na akamwamini Allaah kwa hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika)) [Al-Baqarah (2: 256)]
8-Neno ‘twaghuti’ humaanisha kwa ujumla kila kitu kinachoabudiwa asiyekuwa Allaah (سبحانه وتعالى), (na kinachovuka mipaka katika ‘ibaadah).
9-Salaf walitambua umuhimu mkubwa wa Aayah tatu katika Suwrat Al-An’aam kwamba ni Muhkamaat. Aayah hizi zimejumuisha mambo kumi na la awali ni kukatazwa shirki.
10-Aayah za Muhkamaat katika Suwrat Al-Israa ambazo ni kuanzia Aayah 22 hadi 39, zina mambo kumi na nane, na Allaah (سبحانه وتعالى) Anaanza kwa kauli Yake:
لَّا تَجْعَلْ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتَقْعُدَ مَذْمُومًا مَّخْذُولًا ﴿٢٢﴾
((Usifanye pamoja na Allaah muabudiwa mwengine, ukaja kushutumiwa na mwenye kutelekezwa mbali (motoni)) [Al-Israa (17: 22)]
Na Anayahitimisha kwa kusema:
وَلَا تَجْعَلْ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتُلْقَىٰ فِي جَهَنَّمَ مَلُومًا مَّدْحُورًا ﴿٣٩﴾
((Na wala usifanye pamoja na Allaah muabudiwa mwengine ukaja kutupwa katika Jahannam hali ya kuwa mwenye kulaumiwa na kuwa mardudi (na rahmah ya Allaah)) [Al-Israa (17: 39)]
Na Allaah Ametubainishia umuhimu wake kwa kauli Yake:
ذَٰلِكَ مِمَّا أَوْحَىٰ إِلَيْكَ رَبُّكَ مِنَ الْحِكْمَةِ ۗ
((Hayo ni miongoni mwa hikmah ambayo Amekufunulia Wahy Rabb wako)) [Al-Israa (17: 39)]
11-Aayah ya Suwrah An-Nisaa ambayo imeitwa Aayah za haki kumi. Allaah (سبحانه وتعالى) Amezianza kwa kusema:
وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ
((Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote)) [An-Nisaa (4: 36)]
12-Tanbihi ya wasiya wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) wakati wa kufariki kwake.
13-Kuzijua haki za Allaah (سبحانه وتعالى) juu yetu.
14-Kuzijua haki za waja juu Yake pindi wakitekeleza haki Zake.
15-Maswahaba wengi hawakuwa wakijua jambo hili.
16-Ruhusa ya kuficha elimu inapokuwa na manufaa. Kama hapo ilikuwa ni kwa ajili wajitahidi zaidi kumwabudu Allaah (سبحانه وتعالى).
17-Inapendekezeka kumbashiria Muislamu khabari njema ya kumfurahisha.
18-Khofu (ya watu) kutegemea wingi wa rahmah ya Allaah (سبحانه وتعالى).
19-Kauli ya mtu anayeulizwa pindi asipojua jibu, “Allaah na Rasuli Wake Wanajua zaidi.”
20-Ruhusa ya kutoa baadhi ya elimu kwa baadhi ya watu bila wengine.
21-Unyenyekevu wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kupanda mnyama pamoja na Swahaabah.
22-Kujuzu watu wawili kupanda mnyama mmoja.
23-Fadhila za Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه).
24-Umuhimu mkubwa wa jambo hili (la Tawhiyd).