10-Kitaab At-Tawhiyd: Kuchinja Kwa Ajili Ya Asiyekuwa Allaah

 

Mlango Wa 10

ماَ جاءَ فِي الذَّبْحِ لِغِيْرِ اللَّه

Kuchinja Kwa Ajili Ya Asiyekuwa Allaah

 


 

وقوله تعالى:

Na kauli Yake Ta’aalaa:

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٢﴾

((Sema: “Hakika Swalaah yangu, na kuchinja kafara na ‘ibaadah zangu na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu.”))

 

لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ ﴿١٦٣﴾

((Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza)) [Al-An’aam (6: 162-163)]

 

وَقَوْلِهِ:

Na kauli Yake:

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾

((Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja kwa ajili Yake)) [Al-Kawthar (108: 2)]

 

عَنْ عَلِيِّ بن أبي طالب (رضي الله عنه) قَالَ: حَدَّثَنِي رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) بأرْبَعِ كَلِمَاتٍ: ((لَعَنَ اللَّهُ مَنْ ذَبَحَ لِغَيْرِ اللَّهِ، وَلَعَنَ اللَّهُ مَنْ لَعَنَ وَالِدَيْهِ، وَلَعَنَ اللَّهُ مَنْ آوَى مُحْدِثًا، وَلَعَنَ اللَّهُ مَنح مَنَارَ الأَرْضِ))

Imepokelewa kutoka kwa ‘Aliy bin Abiy Twaalib(رضي الله عنه)  kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alinihadithia maneno manne:  ((Allaah Amemlaani anayechinja si kwa ajili ya Allaah, na Allaah Amemlaani anayewalaani wazazi wake, na Allaah Amelaani anayemkaribisha na kumhami mkhalifu, na Allaah Amelaani anayemlaani mzazi wake, na Allaah Amelaani anayebadilisha mipaka ya ardhi  [anayomiliki] )) [Muslim]

 

وَعنْ طاَرِق بْنِ شهاب (رضي الله عنه) أنَّ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَال: ((دَخَلَ الْجَنَّةَ رَجُلٌ فِي ذُبَابِ، وَدَخَلَ النَّارَ رَجُلٌ فِي ذُبَابِ)): قَالُوا: وَكَيْفَ ذَلِكَ يَا رَسُولُ الله؟ قَالَ: ((مَرَّ رَجُلانِ علَى قَوْمٍ لَهُمْ صَنَمٌ لاَ يُجاوِزُهُ أحَدٌ حَتَّى يُقَرِّبَ لَهُ شَيْئاً، َقَالُوا ِلأَحَدِهِمَا: قَرِّبْ، قَالَ: لَيْسَ عِنْدِي شَيْءٌ أُقَرِّبَ، قَالُوا: قَرِّبْ وَلَوْ ذُباَبًا، فَقَرَّبَ ذُبَاباً، فَخَلُّوا سَبِيْلَهُ، فَدَخَلَ النَّارَ، وَقَالُوا لِلآخِر: قَرِّبْ، فَقَالَ: مَا كُنْتُ لأُقَرِّبَ لأحَدٍ شَيْئًا دُونَ الله عَزَّ وَجَلَّ. فَضَرَبُوا عُنُقَهُ، فَدَخَلَ الْجَنَّةَ))

Na kutoka kwa Twaariq bin Shihaab(رضي الله عنه)  kwamba Rasuli wa Allaah(صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ)  amesema: ((Mtu mmoja ameingia Jannah kwa ajili ya nzi, na ameingia motoni mtu mwengine kwa ajili ya nzi)).  Wakasema: Vipi hivyo ee Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Watu wawili walipitia mbele ya watu walikuwa na sanamu lao, hapiti mtu hadi mtu atolee mihanga na kafara. Wakamwambia mmoja wao: Litolee kafara! Akasema: Sina kitu cha kutolea kafara. Wakasema: Toa japo kwa nzi. Akapeleka nzi [kwa sanamu lao] Wakamwachia apite njia akaingia motoni. Wakamwambia mwengine: Litolee kafara!  Akasema:  Sikuwa natoa chochote kuwa kafara kwa ajili ya yeyote asiyekuwa Allaah ‘Azza wa Jalla.  Wakampiga shingo [wakamuua] akaingia Jannah)) [Ahmad]

 

 

Masuala Muhimu Yaliyomo:

 

1-Tafsiri ya Aayah:

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي

((Sema: “Hakika Swalaah yangu, na kuchinja kafara na ‘ibaadah zangu”)).

 

2-Tafsiri ya Aayah:

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾

((Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja kwa ajili Yake)).

 

3-Kuanza laana kwa anayechinja mnyama kwa ajili ya asiyekuwa Allaah.

 

4-Kumlaani anayewalaani wazazi wake, hii inajumuisha unapowalaani wazazi wa mtu na hivyo yeye kuwalaani wazazi wako.

 

5-Kumlaani mwenye kumpa hifadhi mkhalifu au mzushi kwa kuwa kamhami baada ya kuwa anastahiki hadd (adhabu katika Shariy’ah).

 

6-Kumlaani anayebadili mipaka ya ardhi, yaani mipaka inayotofautisha baina ya mali yako na majirani, hivyo anaibadili kwa kuzidisha au kupunguza.

 

7-Kutofautisha baina ya kumlaani mtu maalumu kwa ukhalifu maalumu na kuwalaani wakhalifu kwa ujumla. 

 

8-Kisa cha nzi na umuhimu wake.

 

9-Mtu ameingizwa motoni kwa sababu ya nzi ambaye hakumkusudia kumtoa kafara, bali alifanya hivyo kwa sababu ya kuepuka vitisho vya waabudu masanamu.

 

10-Kutambua kiwango cha kuchukia shirki katika nyoyo za Waumini, mmoja alikuwa na subira ya hali juu hadi alikuwa tayari kupoteza uhai wake lakini asimfanyie shirki Allaah (سبحانه وتعالى) hata kidogo. Hakukubaliana na maombi yao licha ya kuwa walichotaka kwake ni kitendo cha dhahiri.

 

11-Aliyeingia motoni alikuwa Muislamu, kwani angelikuwa kafiri, basi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) asingelisema: “Ameingia motoni kwa sababu tu ya nzi.”

 

12-Inathibitisha Hadiyth Swahiyh:

الْجَنَّةُ أَقْرَبُ إِلَى أَحَدِكُمْ مِنْ شِرَاكِ نَعْلِهِ وَالنَّارُ مِثْلُ ذَلِكَ

((Jannah iko karibu ya mmoja wenu kuliko kamba za viatu vyake, na moto kadhalika)) [Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Mas’uwd katika Al-Bukhaariy na Ahmad]

 

13-Kujua kuwa ‘amali za moyo ndio hitajio muhimu hata baina ya waabudu masanamu.

 

 

 

Share