11-Kitaab At-Tawhiyd: Hapachinjwi Kwa Jina La Allaah Panapochinjwa Kwa Asiyekuwa Allaah

Mlango Wa 11

بَاب لَا يُذْبَحُ لِلَّهِ بِمَكَانٍ يُذْبَحُ فِيهِ لِغَيْرِ اَللَّهِ

Hapachinjwi Kwa Jina La Allaah Mahali Panapochinjwa Kwa Ajili Ya Asiyekuwa Allaah

 


 

وَقَوْلِ اَللَّهِ تَعَالَى:

Na kauli Yake Ta’aalaa:

 

لَا تَقُمْ فِيهِ أَبَدًا ۚ لَّمَسْجِدٌ أُسِّسَ عَلَى التَّقْوَىٰ مِنْ أَوَّلِ يَوْمٍ أَحَقُّ أَن تَقُومَ فِيهِ ۚ فِيهِ رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُوا ۚ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُطَّهِّرِينَ ﴿١٠٨﴾

((Usisimame (Msikitini) humo abadani.  Bila shaka Msikiti ulioasisiwa juu ya taqwa tokea siku ya kwanza unastahiki zaidi usimame humo. Humo mna watu wanaopenda kujitwaharisha. Na Allaah Anapenda wanaojitwaharisha)) [At-Tawbah (9: 108)]

 

عن ثابت بن الضَّحَّاك (رضي الله عنه) قال: نَذَر رجلٌ أن يَنحَرَ إبلا بِبُوانَةَ فسأل النبيَّ (صلى الله عليه وسلم) فقال: ((هَلْ كانَ فيِهَا وَثَنٌ مِن أوْثانِ الجاهِليَّة يُعْبَدُ؟)) قَالوا: لاَ، قال: ((فَهَلْ كَانَ فيِهَا عِيدٌ مِن أعْيادِهِم ؟)) قَالوا: لاَ. فقال رسول الله (صلى الله عليه وسلم): ((أوْفِ بِنَذْرِكَ فإنه لاَ وَفَاء لِنَذرٍ في مَعْصِيَةِ الله وَلا فيَمَا لا يَمْلِكُ ابْنُ آدم)) رواه أبو داود وإسناده على شرطهما  

Imepokelewa kutoka kwa Thaabit bin Adhw-Dhwahaak(رضي الله عنه)  amesema: Mtu mmoja aliweka nadhiri kuchinja ngamia katika mahali paitwapo Buwaanah. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akauliza: ((Je, hapo mahali palikuwa pana sanamu miongoni mwa sanamu ya jahiliya linaloabudiwa?)) Wakajibu: “Hapana.” Akauliza: ((Je, mahali hapo palikuwa panafanywa sherehe miongoni mwa sherehe za makafiri?)) Wakajibu: “Hapana.” Akasema Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Timiza nadhiri yako, kwani hakika hakuna kutimiza nadhiri katika kumuasi Allaah, au ambazo kutekelezwa kwake kuko nje ya uwezo wa bin Aadam)) [Imesimuliwa  na Abuu Daawuwd kwa sharti ya kuthibitishwa na Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Masuala Muhimu Yaliyomo:

 

1-Maelezo ya kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

لَا تَقُمْ فِيهِ أَبَدًا

((Usisimame (Msikitini) humo abadani)).

 

2-Maasi kumfanyia Allaah (سبحانه وتعالى) na kumtii huleta athari duniani.

 

3-Kurejesha suala lenye utata kwa lisilo na utata kwa ajili ya kuondoa utata.

 

4-Ruhusa kumuuliza Mufti atoe maelezo inapohitajika.  

 

5-Hakuna ubaya kuhusisha sehemu maalumu katika kufanya nadhiri, madamu hakuna makatazo ya Shariy’ah kufanya hivyo hapo.

 

6-Imekatazwa kuweka nadhiri mahali ambako kulikuwa na masanamu ya kijaahiliyyah, na hata kama yameshaondoshwa zamani.

 

7-Kukatazwa nadhiri mahali ambapo washirikina hupatumia kwa sherehe zao za ushirikina hata kama hawaendelei kupatumia mahali hapo.

 

8-Hairuhusiwi kutekeleza nadhiri mahali kama hapo kwa sababu hiyo ni nadhiri ya kumuasi Allaah (سبحانه وتعالى).

 

9-Onyo dhidi ya kujifananisha na washirikina katika sherehe zao, japo bila ya kukusudia.

 

10-Hakuna nadhiri katika maasi.

 

11-Haipasi kuweka nadhiri ambayo mtu hawezi kuitekeleza.  

 

Share