031-Aayah Na Mafunzo: Nabiy Aadam ('Alayhis-Salaam) kufunzwa Majina Ya Vitu Vyote
Aayah Na Mafunzo
Al-Baqarah
Nabiy Aadam ('Alayhis-Salaam) kufunzwa Majina Ya Vitu Vyote
وَعَلَّمَ آدَمَ الْأَسْمَاءَ كُلَّهَا ثُمَّ عَرَضَهُمْ عَلَى الْمَلَائِكَةِ فَقَالَ أَنبِئُونِي بِأَسْمَاءِ هَـٰؤُلَاءِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٣١﴾
31. Na Akamfunza Aadam majina yote (ya kila kitu), kisha Akavionesha mbele ya Malaika; Akasema: “Niambieni majina ya hivi mkiwa ni wakweli.”
قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿٣٢﴾
32. Wakasema: Subhaanak Utakasifu ni Wako! Hatuna elimu isipokuwa Uliyotufunza; hakika Wewe Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote.
قَالَ يَا آدَمُ أَنبِئْهُم بِأَسْمَائِهِمْ ۖ فَلَمَّا أَنبَأَهُم بِأَسْمَائِهِمْ قَالَ أَلَمْ أَقُل لَّكُمْ إِنِّي أَعْلَمُ غَيْبَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَأَعْلَمُ مَا تُبْدُونَ وَمَا كُنتُمْ تَكْتُمُونَ ﴿٣٣﴾
33. Akasema: “Ee Aadam, wajulishe kwa majina yao.” Basi alipowatajia majina yao; (Allaah) Akasema: “Je, Sikuwaambieni kuwa hakika Mimi Najua ghaibu ya mbingu na ardhi na Najua mnayoyadhihirisha na mliyokuwa mkiyaficha.
Mafunzo:
Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Watakusanyika Waumini Siku ya Qiyaamah na Watasema: Lau tungetafuta kuombewa shafaa’ah kwa Rabb wetu! Watakwenda kwa Aadam na watasema: Wewe ndio baba wa watu, Amekuumba Allaah kwa Mkono Wake na Akaamrisha Malaika wakusujudie, na Akakufundisha majina ya vitu vyote, basi tuombee kwa Rabb wako ili Atupe faraja kutokana na sehemu yetu hii? Atasema: Mimi siwezi kufanya mnaloomba! Na atakumbuka makosa yake na ataona hayaa, atasema: Mfuateni Nuwh, hakika yeye ndiye Rasuli wa kwanza Aliyemtuma Allaah kwa watu ardhini. Watamfuata. Naye atasema: Siwezi kufanya mnaloomba! Na atakumbuka kumuomba kwake Allaah kwa jambo asilokuwa na ujuzi nalo. Naye ataona hayaa na atasema: Nendeni kwa Khaliylur-Rahmaan. Watakwenda kwa Ibraahiym. Naye atawaambia: Siwezi kufanya mnaloomba! Nendeni kwa Muwsaa mja ambaye Allaah Alizungumza naye na Akampa Tawraat. Muwsaa atasema: Siwezi kufanya mnaloomba! Atakumbuka kuwa aliwahi kumuua mtu bila ya haki na ataona hayaa kwa Rabb wake. Atasema: Nendeni kwa ‘Iysaa kwani ni mja wa Allaah na Rasuli Wake na neno Lake na Roho Yake. Naye atasema: Siwezi kufanya mnaloomba! Nendeni kwa Muhammad, ni mja aliyefutiwa makosa yaliyotangulia na yajayo. Watakuja kwangu na nitakwenda kwa Rabb wangu kumuomba idhini (ya maombi), nitapewa idhini. Nitakapomuona Rabb wangu nitasujudu na Ataniacha hivyo hivyo mpaka Atakavyo. Kisha itasemwa: Inua kichwa chako na omba utapewa! Na sema yatasikilizwa (uyasemayo)! Na omba shafaa‘ah utapewa! Nitainua kichwa changu na nitamhimidi kwa Himdi Zake Atakazonifundisha, kisha nitaomba na Atanikubalia idadi kubwa ya watu, nitawaingiza Jannah. Kisha nitarudi tena Kwake. Nitakapomuona Rabb wangu, nitafanya kama mara ya kwanza, kisha nitaomba na Atanikubalia idadi kubwa ya watu nitawaingiza Jannah. Kisha nitarejea mara ya tatu, kisha nitarudi mara ya nne kisha nitasema: Hakuna watu waliobakia motoni isipokuwa Qur-aan imewazuia na watawajibika kubakia humo.” [Al-Bukhaariy (4476)]