043-Aayah Na Mafunzo: Nguzo Tano Za Kiislamu Umuhimu Wa Swalaah Na Zakaah
Aayah Na Mafunzo
Al-Baqarah
Nguzo Tano Za Kiislamu Umuhimu Wa Swalaah Na Zakaah
وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَارْكَعُوا مَعَ الرَّاكِعِينَ ﴿٤٣﴾
43. Na simamisheni Swalaah na toeni Zakaah na rukuuni pamoja na wanaorukuu (katika utiifu).
Mafunzo:
Nguzo tano za Uislamu zimetajwa katika Hadiyth ifuatayo:
Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: amesema: “Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano; Kushuhudia kwamba hapana Muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, na kwamba Muhammad ni Rasuli Wake, na kusimamisha Swalaah, na kutoa Zakaah, na kutekeleza Hajj, na kufunga Swiyaam Ramadhwaan.” [Al-Bukhaariy (8)]
Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amesisitiza mno katika Qur-aan nguzo mbili; Swalaah na kutoa Zakaah.
Miongoni mwa kusisitizwa Swalaah ni kwamba ni jambo la kwanza mja kuulizwa Siku ya Qiyaamah:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ َقَالَ سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ ((إِنَّ أَوَّلَ مَا يُحَاسَبُ بِهِ الْعَبْدُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مِنْ عَمَلِهِ صَلاتُهُ فَإِنْ صَلُحَتْ فَقَدْ أَفْلَحَ وَأَنْجَحَ وَإِنْ فَسَدَتْ فَقَدْ خَابَ وَخَسِرَ فَإِنْ انْتَقَصَ مِنْ فَرِيضَتِهِ شَيْءٌ قَالَ الرَّبُّ عَزَّ وَجَلَّ انْظُرُوا هَلْ لِعَبْدِي مِنْ تَطَوُّعٍ فَيُكَمَّلَ بِهَا مَا انْتَقَصَ مِنْ الْفَرِيضَةِ ثُمَّ يَكُونُ سَائِرُ عَمَلِهِ عَلَى ذَلِكَ)) الترمذي و أبوا داود والنسائي وابن ماجه وأحمد
Imepokelewa na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Kitu cha kwanza kinachohesabiwa katika ‘amali za mja wa Allaah Siku ya Qiyaamah ni Swalaah zake. Zikiwa zimetimia, hapo tena atakuwa kaneemeka na kafuzu, na zikiwa zina kasoro atakuwa kaanguka na kala khasara. Ikiwa pana upungufu katika Swalaah zake za fardhi Allaah (‘Azza wa Jalla) Atasema: “Tazama ikiwa mja wangu ana Swalaah zozote za Sunnah ambazo zinaweza kufidia zile zilizopungua, hapo tena ‘amali yake iliyobaki itaangaliwa hivyo hivyo)) [At-Tirmidhiy, Abuu Daawuwd, An-Nasaaiy, Ibn Maajah na Ahmad]
Na kuhusu Zakaah:
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayepewa mali kisha asitoe Zakaah yake, basi mali hiyo Siku ya Qiyaamah itageuzwa kuwa joka dume lenye upara, mwenye madoa mawili machoni (kutokana na wingi wa sumu aliyonayo), atajizungusha katika mwili wa mtu huyo, kisha atamkaba shingoni huku akimwambia: "Mimi ndiyo hazina yako uliyokuwa ukiikusanya, mimi ndiyo mali yako", kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaisoma Aayah hii:
وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُم ۖ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ ۖ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُوا بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ
180. Wala wasidhani kabisa wale wanaofanya ubakhili kwa yale Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kwamba hayo ni kheri kwao, bali ni shari kwao. Watafungwa kongwa yale waliyoyafanyia ubakhili Siku ya Qiyaamah. [Aal ‘Imraan 180 – Hadiyth katika Al-Bukhaariy na Muslim]