05-Aayah Na Mafunzo: Haki Ya Allaah Kwa Waja Na Haki Ya Waja Kwa Allaah
Aayah Na Mafunzo
Al-Faatihah
Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada
Al-Faatihah Aayah 5:
إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ﴿٥﴾
5. Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.
Mafunzo:
Haki Ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni kumwabudu bila ya kumshirikisha na chochote.
عَنْ مُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ (رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: كُنْتُ رَدِيفَ اَلنَّبِيِّ (صَلَّى اَللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) عَلَى حِمَارٍ فَقَالَ لِي: ((يَا مُعَاذُ؟ أَتَدْرِي مَا حَقُّ اَللَّهِ عَلَى الْعِبَادِ، وَمَا حَقُّ الْعِبَادِ عَلَى اَللَّهِ؟)) قُلْتُ اَللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ، قَالَ: ((حَقُّ اَللَّهِ عَلَى الْعِبَادِ أَنْ يَعْبُدُوهُ، وَلاَ يُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا، وَحَقُّ الْعِبَادِ عَلَى اَللَّهِ أَنْ لاَ يُعَذِّبَ مَنْ لاَ يُشْرِكُ بِهِ شَيْئًا)) قُلْتُ يَا رَسُولَ اَللَّهِ أَفَلاَ أُبَشِّرُ اَلنَّاسَ؟ قَالَ: ((لاَ تُبَشِّرْهُمْ فَيَتَّكِلُوا)) أَخْرَجَاهُ فِي اَلصَّحِيحَيْنِ
Imepokelewa kutoka kwa Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nilikuwa nyuma ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya punda akasema: ((Ee Mu’aadh! Unajua nini haki ya Allaah kwa waja Wake, na nini haki ya waja kwa Allaah?)) Nikajibu: Allaah na Rasuli Wake wanajua zaidi: Akasema: ((Haki ya Allaah kwa waja wake ni kwamba wamwabudu na wasimshirikishe na chochote. Na haki ya waja kwa Allaah ni kwamba Hatomwadhibu yeyote ambaye hamshirikishi na chochote)). Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Niwabashirie watu? Akasema: ((Usiwabashirie wasije kuitegemea)) [wakaacha kufanya juhudi katika ‘ibaadah])) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Isti’aanah ni kuomba kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee katika ambayo hakuna mwenye uwezo nayo:
كُنْتُ خَلْفَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم يًوْماً، فقال: ((يا غُلامُ، إنِّي أُعَلِّمُكَ كلِماتٍ: احْفَظِ اللهَ يَحْفَظْكَ، احْفَظِ اللهَ تَجِدْهُ تُجاهَك، إذا سأَلْتَ فاسْأَلِ اللهَ، وإذا اسْتَعنْتَ فاسْتَعِنْ باللهِ، واعْلَمْ أنَّ الأُمَّة لَوِ اجْتَمَعَتْ على أَنْ يَنْفَعُـوكَ بِشَيءٍ لَمْ يَنْفَعُوكَ إلا بِشَيْءٍ قدْ كَتَبَهُ اللهُ لَكَ، وإن اجْتَمَعُوا على أن يَضُرَّوكَ بِشيءٍ لَمْ يَضُروكَ إلا بِشَيءٍ قَدْ كَتَبهُ اللهُ عَلَيْكَ، رُفِعَتِ الأقْلامُ وَجَفَّتِ الصُّحُفُ))
Siku moja nilikuwa nyuma ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia: “Ee kijana! nitakufundisha maneno (ya kufaa); Mhifadhi Allaah (fuata maamrisho Yake na chunga mipaka Yake) Atakuhifadhi. Muhifadhi Allaah utamkuta mbele yako. Ukiomba, muombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), ukitafuta msaada tafuta kwa Allaah. Tambua kwamba ikiwa ummah mzima utaungana kukunufaisha wewe kwa kitu, basi hutonufaika ila tu kwa kile Alichokwishakuandikia Allaah. Na wakikusanyika kukudhuru kwa chochote, hutodhurika ila tu kwa kile Allaah Alichokwishakukuandikia (kuwa kitakudhuru), kwani kalamu zimeshanyanyuliwa (kila kitu kishaandikwa) na swahifa zimeshakauka.” [At-Tirmidhiy, na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh]
Bonyeza kiungo upate faida zaidi:
18-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Isti’aanah (Kuomba Msaada) Kwa Asiyekuwa Allaah