230-Aayah Na Mafunzo: Haramisho La Kuhalalisha Ndoa Baada Ya Talaka Tatu

Aayah Na Mafunzo

Al-Baqarah

 

Haramisho La Kuhalalisha Ndoa Baada Ya Talaka Tatu

 

www.alhidaaya.com 

 

 

 فَإِن طَلَّقَهَا فَلَا تَحِلُّ لَهُ مِن بَعْدُ حَتَّىٰ تَنكِحَ زَوْجًا غَيْرَهُ ۗ فَإِن طَلَّقَهَا فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا أَن يَتَرَاجَعَا إِن ظَنَّا أَن يُقِيمَا حُدُودَ اللَّـهِ ۗ وَتِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ يُبَيِّنُهَا لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿٢٣٠﴾

230. Na akimtaliki (mara ya tatu) basi hatokuwa halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwengine. Akimtaliki (au akifariki) hapatokuwa dhambi juu yao wawili kurejeana wakidhani kwamba watasimamisha mipaka ya Allaah. Na hiyo ni mipaka ya Allaah Anaibainisha kwa watu wanaojua.

 

Mafunzo:

 

Haifai kufunga nikaah ya uongo kwa ajili kuhalalisha nikaah baada ya talaka tatu. Amelaaniwa afanyaye hivyo; Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amemlaani anayefanya tahliyl (mhalalishaji) na mhalalishiwa wale wanaokula ribaa na wanaotoa ribaa.” [At-Tirmidhiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah na Ahmad].

 

Faida nyengine:

 

‘Aaishah (رضي الله عنها) amehadithia: Mke wa Rifaa’ah Al-Qurdhwiy alikuja wakati mimi na Abuu Bakr tulikuwa na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: Nilikuwa mke wa Rifaa‘ah, lakini aliniacha na ilikuwa talaka isiyorejewa. Kisha niliolewa na ‘Abdur-Rahmaan bin Az-Zubayr lakini dhakari yake ilikuwa haina nguvu. Kisha akachukua ncha ya nguo yake akaonesha ulaini wa dhakari yake (kuwa mfano wa udogo wa dhakari). Khaalid bin Sa’iyd bin Al-‘Aasw ambaye alikuwa mlangoni akisubiri kuruhusiwa kuingia alisema: Yaa Abaa Bakr! Kwanini humzuii huyu mwanamke kusema wazi mbele ya Rasuli wa Allaah?  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akacheka, kisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamuuliza yule mwanamke: “Je, unataka kurudi kuolewa na Rifaa’ah? Basi, huwezi mpaka uonje ‘usaylah yake naye aonje ‘usaylah yako (yaani mjamiiane kikamlifu na mumeo wa sasa).” [Ahmad (6/34) na Al-Bukhaariy na Muslim na An-Nasaaiy walinukuu Hadiyth hii kwa maneno ya Muslim kuwa Rifaa’ah alimtaliki mkewe kwa talaka ya tatu na ya mwisho]. Maana ya ‘usaylah ni kitendo cha jimai kama ilivyo dalili ya Hadiyth: “Fahamu kuwa ‘usaylah ni kuingiliana kimwili.” [Ahmad (6/62)]

 

 

Share