233-Aayah Na Mafunzo: Faida Za Kumnyonyesha Mtoto
Aayah Na Mafunzo
Al-Baqarah
Faida Za Kumnyonyesha Mtoto
وَالْوَالِدَاتُ يُرْضِعْنَ أَوْلَادَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ ۖ لِمَنْ أَرَادَ أَن يُتِمَّ الرَّضَاعَةَ ۚ وَعَلَى الْمَوْلُودِ لَهُ رِزْقُهُنَّ وَكِسْوَتُهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۚ لَا تُكَلَّفُ نَفْسٌ إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَا تُضَارَّ وَالِدَةٌ بِوَلَدِهَا وَلَا مَوْلُودٌ لَّهُ بِوَلَدِهِ ۚ وَعَلَى الْوَارِثِ مِثْلُ ذَٰلِكَ ۗ فَإِنْ أَرَادَا فِصَالًا عَن تَرَاضٍ مِّنْهُمَا وَتَشَاوُرٍ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا ۗ وَإِنْ أَرَدتُّمْ أَن تَسْتَرْضِعُوا أَوْلَادَكُمْ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِذَا سَلَّمْتُم مَّا آتَيْتُم بِالْمَعْرُوفِ ۗ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٢٣٣﴾
233. Na wazazi wa kike wanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili, kwa mwenye kutaka kutimiza kunyonyesha. Na ni juu ya mzazi wa kiume kuwapatia chakula chao na nguo kwa mujibu wa ada. Hailazimishwi nafsi ila kwa iliwezalo. Asidhuriwe mzazi wa kike kwa ajili ya mwanawe, na wala mzazi wa kiume kwa ajili ya mwanawe. Na juu ya mrithi (wa baba) mfano wa hivyo. Watakapotaka kumwachisha kunyonya kwa maridhiano baina yao wawili na mashauriano basi hapana dhambi juu ya wawili hao. Na mtakapotaka kutafuta wa kuwayonyesha watoto wenu, basi si dhambi kwenu ikiwa mtalipa mlichoahidi kwa mujibu wa shariy’ah. Na mcheni Allaah na jueni kwamba hakika Allaah kwa myatendayo ni Mwenye kuona.
Mafunzo:
Faida Za Kunyonyesha:
Mama anafaa atambue kwamba kumnyonyesha mtoto ni jambo lenye kumpatia faida nyingi mtoto pamoja na mama yake, kwani ni jambo la asili Alilojaaliya Allaah (Subhanaahu wa Ta’aalaa) kwa rahma Yake kubwa na Hikma Yake na bila shaka faida zake hakuna anayezipinga kwani hata madaktari wametambua faida nyingi baada ya utafiti. Baadhi ya hizo faida ni:
Faida kwa mtoto
- Mtoto anakingika na maradhi mengi ya kila aina.
- Imepatikana asilimia ndogo ya vifo vya watoto wanaonyonyeshwa vifuani.
- Asilimia kubwa imeonekana kuwa watoto wanaonyonyeshwa huwa ni wenye akili kubwa (mahodari) na wenye utulivu zaidi.
- Maziwa ya mama ni chakula kamili anachokihitaji mtoto katika miezi yake ya mwanzo.
- Maziwa ya mama yako tayari wakati wowote na yako katika hali ya joto linalomfaa mtoto.
- Huenda maziwa ya kutengenezwa yakamfanyia mtoto mzio (allergy), ama maziwa ya kifuani hayana matatizo kama hayo.
- Hupata hamu ya kupenda kula zaidi (appetite).
Faida kwa mzazi
- Mama atapata himaya kutokana na maradhi ya saratani (cancer)
- Fuko la uzazi hurudi katika hali yake ya kawaida baada ya kunyonyesha.
- Mwili wa mama hupunguka uzito uliomzidi.
- Ni njia ya kupunguza masarifu ya hela kwa kununua badala yake maziwa ya sinai (ya kutengenezwa) na pia kuepukana na malipo ya hospitali kutokana na utafiti ulioonekana kwamba asilimia kubwa ya watoto wasionyonyeshwa hupata maradhi mara kwa mara.
- Kujipunguzia kazi za kutengeneza maziwa ya sinai (ya kutengenezwa) na kupata faida ya wakati zaidi, kwani ya kifuani yako tayari hayahitaji wakati wa kutengeneza, mbali pia kujiepusha na kazi za kukosha chupa na vifaa vya maziwa ya sinai.
- Wakati wowote, mahali popote yako tayari hana haja mama ya kubeba chupa za maziwa anapotoka nje au anapokuwa safarini.
Faida baina ya mama na mtoto
- Mtoto na mama wote kupata utulivu na kutulia nafsi.
- Huathiri mapenzi baina yao yakawa makubwa zaidi.
- Mama huridhika kuwa ameitumia Rahma na neema ya Allah (Subhaana wa Ta'aalah) na hutosheka kuwa ametimiza wajibu wake kwa mwanawe kwani wengi wanaoacha kunyonyesha huja kujuta baadaye.
[Imekusanywa na Alhidaaya.com]