034-Aayah Na Mafunzo: Fadhila Za Wanawake Wema Wanaotii Waume Zao Kwa Siri
Aayah Na Mafunzo
An-Nisaa
Fadhila Za Wanawake Wema Wanaotii Waume Zao Kwa Siri
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ ۚ وَاللَّاتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ ۖ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلَا تَبْغُوا عَلَيْهِنَّ سَبِيلًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا ﴿٣٤﴾
Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine na pia kwa ambayo wanatoa katika mali zao. Basi wanawake wema ni wale watiifu wenye kujihifadhi katika hali ya kutokuweko waume zao kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajihifadhi. Na wale ambao mnakhofu uasi wao wa ndoa, basi wanasihini na wahameni katika malazi na wapigeni (kipigo kisichodhuru). Wakikutiini, basi msitafute njia dhidi yao (ya kuwaudhi). Hakika Allaah daima ni Mwenye Uluwa, Mkubwa wa dhati, vitendo na sifa. [An-Nisaa: 34]
Mafunzo:
Kuhusu: “na wahameni katika malazi.” Imekusudiwa kutokulala nao na kutokujimai nao, kwa ujumla ni kuwagomea. Ama kuhusu: “na wapigeni.” Imekusudiwa kipigo kidogo kisichokuwa cha kumdhuru, wala haipasi kupigwa usoni. Hadiyth imethibitisha:
Jaabir (رضي الله عنه) amehadithia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema katika Hijja ya kuaga: “Mcheni Allaah kuhusu wanawake kwani wao ni wasaidizi wenu. Mnayo haki juu yao kuwa wasimruhusu mtu msiyempenda kukanyaga zulia lenu (kuingia katika nyumba) Lakini wakifanya hivyo, mnaruhusiwa kuwatia adabu ndogo. Wao wana haki kwenu kwamba muwatimizie matumizi yao na nguo kwa njia ya kuridhisha.” [Muslim]
Fadhila za mke mwema: “Mwanamke atakaposwali Swalaah zake tano, akahifadhi sehemu zake za siri (asifanye uzinifu), akamtii mume wake, ataingia Jannah kupitia mlango wowote autakao.” [Swahiyh At-Targhiyb (1932)].