086-Aayah Na Mafunzo: Umuhimu Wa Maamkizi Ya Kiislam Na Baadhi Ya Fadhila Zake

Aayah Na Mafunzo

An-Nisaa

Umuhimu Wa Maamkizi Ya Kiislam Na Baadhi Ya Fadhila Zake

Alhidaaya.com

 

 

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَإِذَا حُيِّيتُم بِتَحِيَّةٍ فَحَيُّوا بِأَحْسَنَ مِنْهَا أَوْ رُدُّوهَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَسِيبًا ﴿٨٦﴾

Na mtapoamkiwa kwa maamkizi yoyote, basi itikieni kwa yaliyo mazuri zaidi kuliko hayo au yarudisheni hayo hayo. Hakika Allaah daima juu ya kila kitu ni Mwenye kuhesabu. [An-Nisaa: 86]

 

 

Mafunzo

 

'Imraan bin Al-Huswayn (رضي الله عنهما) amehadithia: Mtu mmoja alikuja kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamuamkia: "Assalaamu 'Alaykum." (Nabiy) akamrudishia salaam). Kisha yule mtu akaketi. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Kumi.” (kwa maana amepata thawabu kumi). Kisha akaja mtu mwengine, akasema: "Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaah." Naye akamrudishia, kisha yule mtu akaketi, Nabiy akasema: “Ishirini.” Kisha akaja mtu mwengine akasema: "Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh.” Naye akamrudishia kisha akasema: “Thelathini.” [Abuu Daawuwd na At-Trimidhiy na akasema Hadiyth Hasan].

 

Na maamkizi ya Kiislamu ni funguo za Jannah: Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hamtoingia Jannah hadi muamini, na wala hamuwezi kuamini hadi mpendane. Je, nikujulisheni jambo ambalo mtakapolifanya mtapendana? Toleaneni Salaam baina yenu.” [Muslim].

 

Pia katika khutbah yake ya mwanzo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipohajiri Madiynah alisema: “Enyi watu! Enezeni salaam, na lisheni chakula, na swalini watu wakiwa wamelala (Qiyaam), mtaingia Jannah kwa Amani.” [At-Tirmidhiy – Hadiyth Swahiyh].

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate faida tele:

 

Maamkizi Ya Kiislaam: Maamrisho Na Fadhila Zake

 

 

 

Share