083-Aayah Na Mafunzo: Matahadharisho Ya Kutangaza Khabari Bila Kuhakikisha
Aayah Na Mafunzo
An-Nisaa
Matahadharisho Ya Kutangaza Khabari Bila Kuhakikisha
Na Sababu Ya Kuteremshwa Aayah Hii
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَإِذَا جَاءَهُمْ أَمْرٌ مِّنَ الْأَمْنِ أَوِ الْخَوْفِ أَذَاعُوا بِهِ ۖ وَلَوْ رَدُّوهُ إِلَى الرَّسُولِ وَإِلَىٰ أُولِي الْأَمْرِ مِنْهُمْ لَعَلِمَهُ الَّذِينَ يَسْتَنبِطُونَهُ مِنْهُمْ ۗ وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ لَاتَّبَعْتُمُ الشَّيْطَانَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٣﴾
Na linapowafikia jambo lolote la amani au la khofu hulitangaza. Na lau wangelirudisha kwa Rasuli na kwa wenye madaraka kati yao, wangelijua wale wanaotafiti wakabainisha ya sahihi miongoni mwao. Na lau si fadhila ya Allaah juu yenu na rahmah Yake kwa yakini mngelimfuata shaytwaan ila wachache tu. [An-Nisaa: 83]
Mafunzo:
Matahadhirisho ya kutangaza khabari bila ya uhakikisho: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Inamtosheleza mtu kuwa ni muongo kwa kusema kila anachokisikia.” [Amehadithia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) ameipokea Muslim].
Na pia; Al-Mughiyrah bin Shu’bah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Nimemsikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: “Hakika Allaah Anachukia kwenu “qiylaa wa qaala” na kupoteza mali na kuuliza maswali mengi.” [Al-Bukhaariy na wengineo]. “Qiylaa wa qaal” kwa maana: “imesemwa na amesema” ni ibaarah inayokusudiwa uvumi, utesi, udaku, umbeya, usengenyaji n.k.
Sababun-Nuzuwl:
Aayah hii imeteremka kama alivyohadithia ‘Umar (رضي الله عنه) kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipojitenga mbali na wake zake, niliingia Masjid nikakuta watu wakipiga ardhi kwa changarawe wakisema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amewataliki wake zake! Na hivyo ni kabla ya kuamrishwa hijaab. ‘Umar akasema: Nitatambua hilo leo. Basi nikamwendea ‘Aaishah (رضي الله عنها) nikamwambia: Yaa bint Abiy Bakr! Je, hivi imekufikia kumuudhi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)? Akasema: Haijakuhusu jambo kwangu, nami hainihusu jambo kwako yaa bin Al-Khattwaab, juu yako kumuwaidhi (bint yako)! Nikamwendea Hafswah bint ‘Umar nikamwambia: Yaa Hafswah! Imenifikia (khabari) kwamba umemuudhi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na nimetambua kuwa hakupendi! Na lau ningekuwa (si baba yako) angekutaliki! Hafswah akalia sana. Nikamwambia: Yuko wapi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)? Akasema: Yuko chumba cha darini. Nikaenda nikamkuta Rabaah, mtumishi wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amekaa kitako kingoni mwa dirisha akinin’giniza miguu yake juu katika ufumbi wa shina la mtende ambalo likimsaidia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kupanda (chumba cha darini) na kuteremkia. Nikamwambia: Yaa Rabaah! Niombee idhini kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Rabaah akatazama chumbani kisha akanitazama mimi wala hakusema kitu. Kisha nikasema: Yaa Rabaah! Niombee idhini kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Rabaah akatazama chumbani kisha akanitazama mimi wala hakusema kitu. Kisha nikapandisha sauti yangu nikasema: Yaa Rabaah! Niombee idhini kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), mimi nadhani kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) anadhania kuwa nimekuja kwa ajili ya Hafswah! Wa-Allaahi kama Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ataniamrisha nimpige (nimkate) shingo yake nitampiga! Nikapandisha sauti yangu akaniashiria nipande (kuingia chumba cha darini). Nikaingia kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) nikamkuta amelalia jamvi.
Nikakaa kitako akaivuta shuka yake na hakuwa na nyingine (isipokuwa hiyo tu) na jamvi hilo lilimfanyia alama ubavuni mwake. Nikatazama kwa macho yangu hicho kijichumba cha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) nikakuta shayiri kiasi kiasi cha kibaba kimoja na kiasi cha matawi ya mimosa yamewekwa pembeni mwa chumba na mkoba wa ngozi uliobadilishwa rangi. Nikatokwa na machozi (kuona maisha duni anayoishi).
Akasema: “Nini kinachokuliza yaa Ibn Al-Khattwaab?” Nikasema: Ee Nabiyy wa Allaah! Na kwanini nisilie na hali jamvi limekufanyia alama ubavuni mwako na sioni kitu chumbani mwako humu (isipokuwa vitu vichache mno); (Mfalme) Qayswar na Kisraa wanaishi maisha ya kifakhari lakini wewe Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ambaye Amekuteua (Allaah) hichii ndio kijichumba chako? Akasema: “Ee Ibn Al-Khattwaab! Hivi huridhiki kuwa sisi tuna Aakhirah nao wana dunia?” Nikasema: Ndio. Kisha nilipoingia kwanza niliona usoni mwake alama za ghadhabu, basi nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Unatatizwa nini na wanawake? Ungeliwataliki basi hakika Allaah Yuko pamoja nawe, na Malaika Wake na Jibriyl, na Mikaaiyl na mimi, na Abuu Bakr, na Waumini (wote) tuko nawe. Na kichache nilichosema (siku ile) na namhimidi Allaah, nilitaraji kwamba Allaah Atasadikisha kauli yangu. Basi ikateremka Aayah hii ya At-Takhyiyr (chaguo): “Ikiwa nyinyi wawili mtatubia kwa Allaah (ni khayr kwenu) kwani kwa hakika nyoyo zenu zimeelemea (kumchukiza Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم). Na mkisaidiana dhidi yake, basi hakika Allaah Ndiye Mlinzi (na Msaidizi) wake na Jibriyl na Waumini wema, na zaidi ya hayo, Malaika pia watasaidia. Akikutalikini, asaa Rabb Wake Akambadilishia wake bora kuliko nyinyi; Waislamu…” (66: 4- 5) Na walikuwa ni ‘Aaishah bint wa Abuu Bakr na Hafswah ambao walishikilia na kusaidiana (kudai mali) kuliko wake wote wengine wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Je, umewataliki? Akasema: “Hapana.” Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika niliingia Masjid nikakuta Waislamu wanacheza kwa vichangarawe (huku dhana zimewashughulisha) wakisema kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amewataliki wake zake. Je, niende kuwajulisha kuwa hukuwataliki? Akasema: “Naam ukipenda.” Nikaendelea kuongea naye mpaka (nikatanabahi) alama za ghadhabu zimepotea usoni mwake na mpaka (huzuni yake ikageuka kuwa ni furaha na hivyo) uso wake ukarudi kuwa na bashasha kama kawaida yake, akacheka na meno yake yalikuwa ya kupendeza mno kuliko watu wote! Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akateremka, nami nikateremka huku nikikamata shina la mtende, naye Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akateremka (kwa wepesi kabisa) bila ya kukamata chochote mkononi mwake (kujizuilia). Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Ulikuwa chumbani mwako siku ishirini na tisa. Akasema: (Mara nyingine) “Mwezi huwa ni siku ishirini na tisa.” Nikasimama mlangoni mwa Masjid nikaita kwa sauti yangu ya juu kabisa: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuwataliki wake zake! Hapo ikataremka Aayah hii: “Na linapowafikia jambo lolote la amani au la khofu hulitangaza. Na lau wangelirudisha kwa Rasuli na kwa wenye madaraka kati yao, wale wanaotafiti miongoni mwao wangelielewa… (4: 83). Ikawa ni mimi niliyetafiti jambo hilo. Na Allaah Akateremsha Aayah ya At-Takhyiyr (At-Tahriym 66: 4 – 5) [Al-Bukhaariy na Muslim].