140-Aayah Na Mafunzo: Kufanyia Istihzai Jambo La Dini Linamtoa Mtu Nje Ya Uislamu
Aayah Na Mafunzo
An-Nisaa
Kufanyia Istihzai Jambo La Dini Linamtoa Mtu Nje Ya Uislamu
وَقَدْ نَزَّلَ عَلَيْكُمْ فِي الْكِتَابِ أَنْ إِذَا سَمِعْتُمْ آيَاتِ اللَّـهِ يُكْفَرُ بِهَا وَيُسْتَهْزَأُ بِهَا فَلَا تَقْعُدُوا مَعَهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ ۚ إِنَّكُمْ إِذًا مِّثْلُهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ جَامِعُ الْمُنَافِقِينَ وَالْكَافِرِينَ فِي جَهَنَّمَ جَمِيعًا ﴿١٤٠﴾
140. Na kwa yakini Amekwishakuteremshieni katika Kitabu kwamba mnaposikia Aayaat za Allaah zinakanushwa na zinafanyiwa istihzai, basi msikae pamoja nao mpaka waingie katika mazungumzo mengineyo. Au sivyo mtakuwa kama wao. Hakika Allaah Atawakusanya wanafiki na makafiri wote pamoja katika Jahannam.
Mafunzo:
Miongoni mwa yanayomtoa mtu nje ya Uislamu ni kufanyia istihzai Maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى)! Ni kama ilivyotajwa katika Nawaaqidhw Al-Islaam: “Mwenye kufanyia istihzai (shere, dhihaka, masikhara) kwa chochote katika Dini ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) au akafanya utani katika thawabu au katika adhabu za Allaah, basi amekufuru.” [Muhammad bin ‘Abdil-Wahhaab, Nawaaqidhw Al-Islaam]
Ni tahadharisho kubwa kwa Waislamu kwani wengi katika mabaraza yao wakati wanaongea hupenda kufanya istihzai wakidhania kuwa ni jambo la kawaida ilhali hatari yake ni kubwa mno! Rejea At-Tawbah (9:64-66)