171-Aayah Na Mafunzo: Nabiy ‘Iysaa Na Mama Yake Ni Waja Wa Allaah Si Washirika Wake

Aayah Na Mafunzo

An-Nisaa

Nabiy ‘Iysaa Na Mama Yake Ni Waja Wa Allaah Si Washirika Wake

Alhidaaya.com

 

 

 

يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لَا تَغْلُوا فِي دِينِكُمْ وَلَا تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ إِلَّا الْحَقَّ ۚ إِنَّمَا الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ رَسُولُ اللَّـهِ وَكَلِمَتُهُ أَلْقَاهَا إِلَىٰ مَرْيَمَ وَرُوحٌ مِّنْهُ ۖ فَآمِنُوا بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ ۖ وَلَا تَقُولُوا ثَلَاثَةٌ ۚ انتَهُوا خَيْرًا لَّكُمْ ۚ إِنَّمَا اللَّـهُ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖسُبْحَانَهُ أَن يَكُونَ لَهُ وَلَدٌ ۘ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ وَكِيلًا ﴿١٧١﴾

 

Enyi Watu wa Kitabu! Msipindukie mipaka katika dini yenu, wala msimzungumzie Allaah isipokuwa ukweli. Hakika Al-Masiyh ‘Iysaa mwana wa Maryam ni Rasuli wa Allaah na ni Neno Lake (la Kun!) Alompelekea Maryam na Ruwh (roho Aliyoumba kwa amrisho) kutoka Kwake. Basi mwaminini Allaah na Rusuli Wake; wala msiseme: ‘watatu’. Komeni, ni khayr kwenu. Hakika Allaah ni Mwabudiwa wa haki Mmoja Pekee, Utakasifu ni Wake kuwa ana mwana! Ni Vyake vyote vilivyomo mbinguni na vyote vilivyomo ardhini. Na Anatosheleza Allaah kuwa Ni Mtegemewa wa yote. [An-Nisaa (4:171)]

 

Mafunzo:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Amewakataza Watu wa Kitabu wasimfanye ‘Iysaa na Mama yake kuwa ni washirika wa Allaah bali hao ni waja wawili katika waja wema wa Allaah na si washirika Wake kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) Akimzungumzia ‘Iysaa (عليه السلام) katika Suwrat Maryam (19: 30-36) Na pia katika Suwratul-Maaidah (5: 17, 72-76). 

 

Pia ‘Ubaadah bin Asw-Swaamit (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mwenye kushuhudia kuwa laa ilaaha illa Allaah - hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Allaah Pekee, Hana mshirika na kwamba Muhammad ni mja wake na Rasuli Wake, na kwamba ‘Iysaa ni mja wa Allaah na Rasuli Wake, na Neno Lake (la Kun!) Aliloliweka kwa Maryam na roho ni kutoka Kwake (Ameiumba), na Jannah ni haki, na moto ni haki, Allaah Atamuingiza Jannah kwa amali zozote alizonazo." [Al-Bukhaariy]. Na katika riwaayah nyingine: “Ataingizwa Jannah katika milango minane ataingia katika wowote aupendao.” [Muslim].

 

Na pia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amekataza kutukuzwa kupindukia kiasi amesema: “Msinitukuze kama Manaswara walivyomtukuza Masiyh mwana wa Maryam, hakika mimi na mja kwa hiyo semeni mja wa Allaah na Rasuli Wake)) [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Share