043-Asbaabun-Nuzuwl: An-Nisaa Aayah 043: يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ حَتَّىٰ تَعْلَمُوا مَا تَقُولُونَ
أسْبابُ النُّزُول
Asbaabun-Nuzuwl
Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya Aayaat Za Qur-aan)
Imekusanywa na: Alhidaaya.com
An-Nisaa 043- Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah na hali mmelewa….
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ حَتَّىٰ تَعْلَمُوا مَا تَقُولُونَ وَلَا جُنُبًا إِلَّا عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىٰ تَغْتَسِلُوا ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَفُوًّا غَفُورًا ﴿٤٣﴾
Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah na hali mmelewa mpaka mjue mnayoyasema, na wala mkiwa mna janaba isipokuwa mmo safarini mpaka muoge josho. Na mkiwa wagonjwa au safarini au mmoja wenu ametoka msalani au mmewagusa wanawake kisha hamkupata maji, basi ikusudieni ardhi safi ya mchanga (mtayammam), mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hakika Allaah daima Ni Mwingi wa Kusamehe, Mwingi wa Kughufuria [An-Nisaa (4:43)]
Sababun-Nuzuwl:
Sababu ya kuteremshwa hukmu ya tayammum:
Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) amehadithia: “Tulikwenda katika moja ya safari tukafika Al-Baydaa au Dhaatul-Jaysh ambako kidani changu kilivunjika (na kikapotea). Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akawa anakitafuta, kisha pia watu wengineo wakainuka kukitafuta. Hapakuweko na maji sehemu hiyo, basi watu wakamwendea Abuu Bakr Asw-Swiddiyq na kusema: Huoni alivyofanya ‘Aaishah? Kamfanya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) pamoja na watu wakae sehemu ambayo hakuna maji! Abuu Bakr akaja wakati Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa amelala akiwa amelaza kichwa chake mapajani mwangu. Akaniambia: Umemzuia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na watu sehemu ambako hakuna maji na wala hawana (akiba ya) maji. Basi akanigombesha na akasema Aliyomjaalia (Allaah) kusema kuhusu mimi na akanipiga ubavuni kwa mkono wake. Hakuna kilichonizuia kusogea (kutokana na maumivu) isipokuwa kwa vile Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa amelala mapajani mwangu. Hapo Allaah Akateremsha Aayah ya tayammum (4:43), basi wakatayammam. ‘Usayd bin Al-Hudhwayr akasema: Ee ahli ya Abuu Bakr! Hii si baraka ya kwanza kwenu. Kisha akaendeshwa ngamia ambaye nilikuwa nimempanda na tukakipata kidani chini yake.” [Al-Bukhaariy]
Sababun-Nuzuwl:
Uharamisho Wa Pombe:
Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ
43. Enyi walioamini! Msikaribie Swalaah na hali mmelewa
Ni kwamba, hatua ya kwanza kuhusu pombe imetahadharishwa katika Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):
يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ ۖ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا ۗ
Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na (baadhi ya) manufaa kwa watu. Na dhambi yake viwili hivyo ni kubwa kuliko manufaa yake[Al-Baqarah (2:219)]
Hii ni hatua ya pili ya kukatazwa pombe katika nyakati za Swalaah kwa sababu Maswahaba walikosea kusoma Qur-aan katika Swalaah kutokana na kulewa. Baada ya hapo ikafutwa hukmu hii na ikabakia pombe kuwa ni haramu nyakati zote kwa Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى) katika
Suwrat Al-Maaidah:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٩٠﴾
Enyi walioamini! Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli, ni najisi na chukizo kutokana na kazi ya shaytwaan. Basi jiepusheni navyo mpate kufaulu. (5:90):