033-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Maaidah Aayah 033: إِنَّمَا جَزَاءُ الَّذِينَ يُحَارِبُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَسْعَوْنَ فِي الْأَرْضِ فَسَادًا
أسْبابُ النُّزُول
Asbaabun-Nuzuwl
Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya Aayaat Za Qur-aan)
Imekusanywa na: Alhidaaya.com
Al-Maaidah 033-Hakika jazaa ya wale wanaompiga vita Allaah na Rasuli Wake na wakapania kufanya ufisadi...
إِنَّمَا جَزَاءُ الَّذِينَ يُحَارِبُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَسْعَوْنَ فِي الْأَرْضِ فَسَادًا أَن يُقَتَّلُوا أَوْ يُصَلَّبُوا أَوْ تُقَطَّعَ أَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم مِّنْ خِلَافٍ أَوْ يُنفَوْا مِنَ الْأَرْضِ ۚ ذَٰلِكَ لَهُمْ خِزْيٌ فِي الدُّنْيَا ۖ وَلَهُمْ فِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿٣٣﴾
Hakika jazaa ya wale wanaompiga vita Allaah na Rasuli Wake na wakapania kufanya ufisadi katika ardhi, wauawe au wasulubiwe au ikatwe mikono yao na miguu yao kwa kutofautisha au watolewe katika nchi. Hiyo ndiyo hizaya yao duniani. Na Aakhirah watapata adhabu kuu. (5:33)
Sababun-Nuzuwl:
Aayah hii imeteremshwa kama ifuatavyo:
Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Watu wanane toka ‘Ukal walikuja kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) wakampa Bay-‘a ya kuulinda Uislamu na kuwa Waislamu wema. Hali ya hewa (ya Madiynah) haikuwapenda wakaugua. Wakamlalamikia hilo Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Rasuli akawaambia: “Basi si ingekuwa vyema mkitoka na mchungaji wa ngamia wetu mkapata kunywa maziwa yao na mikojo yao?” Wakakubali na kutoka. Wakanywa maziwa na mikojo, na afya zao zikatengemaa vizuri. Walipokuwa hivyo, walimuuwa mchungaji na kutoroka na ngamia. Habari hiyo ikamfikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Akatuma watu kwenda kuwasaka, wakawapata na wakaletwa kwake. Akaamuru wakatwe mikono yao na miguu yao, na wapofuliwe macho (kwa kuwa walimpofua mchungaji). Kisha wakatelekezwa juani mpaka wakafa.
[Amehadithia Anas bin Maalik (رضي الله عنه) na imepokelewa na Abuu Daawuwd katika Kitaab Al-Huduwd]
Faida: Maana ya Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):
أَوْ تُقَطَّعَ أَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم مِّنْ خِلَافٍ
au ikatwe mikono yao na miguu yao kwa kutofautisha.
Ni kukatwa mikono ya kulia kwa miguu ya kushoto au miguu ya kushoto kwa mikono ya kulia.