14-Shaykh ‘Abdullaah Al-Ghudayyaan: Kuwafunza Watoto Katika Ramadhwaan
Kuwafunza Watoto Katika Ramadhwaan
Shaykh ‘Abdullaah Al-Ghudayyaan
SWALI:
Watoto wengi wanapuuza mambo ya Dini yao. Upi umri ambao ni wajibu kwa wale wanaowafunza (hao watoto wanapaswa kuzingatia)? Na ipi nasiha yako kwa kuwapeleka watoto Masjid katika Ramadhwaan? Watoto ambao wako baina ya miaka 7 mpaka 13.
JIBU:
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Kila mmoja wenu ni mchunga na kila mmoja ataulizwa alichokichunga, kiongozi wa watu ni mchunga na ataulizwa kwa alichokichunga, mwanamme ni mchunga wa familia yake na ataulizwa kwa alichokichunga, mwanamke ni mchunga wa nyumba ya mume wake na watoto wake naye ataulizwa alichokichunga, na mtumwa ni mchunga wa mali ya bwana wake naye ataulizwa kuhusu uchungaji wake”.
Na Anasema Allaah (Jalla wa 'Alaa):
”Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto.” (66:6)
Na anasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi sallam):
”Kalamu imesimamishwa kwa watu aina tatu: akasema mmoja wao ni “mtoto mpaka abalehe.”
Kwa mwanamke mpaka abalehe. Na kwa mwanume (mara nyingi) hubalehe anapofikisha miaka 15, au anaota nywele za sehemu ya siri. (Mwanaume na mwanamke) wanapoanza kutokwa na manii, mwanamke anatofautiana na mwanamume, kwa kuwa yeye mwanamke hubalehe kwa hedhi. Hizi ndizo alama za kubalehe (kwa mwanaume na mwanamke).
Ama kabla ya kubalehe, si wajibu kwao Swalaah (na Swawm). Lakini waanze kufunzwa (na kupewa mazoezi), kama alivyosema Nabiy (Swaala Allaahu 'alayhi wa aalihi sallam). "Waamrisheni watoto wenu Swalaah wanapofika miaka 7, na wapigeni wakifikisha miaka 10 na watenganisheni kwenye vitanda". Kwa hiyo inatakiwa kwa baba ampeleke mtoto wake Masjid anapofikisha 7. Ama kabla ya kufikisha miaka hiyo anakuwa mtoto hana ile niyyah (hamu). Ama atapofikisha miaka 7, hapo anaponuia Swalaah, niyyah yake inakuwa Sahihi, na anaponuia Swawm niyyah yake inakuwa sahihi. Lakini mtoto kuweka niyyah kabla ya (kufikisha) miaka 7, mtoto halizingatii hili.
Katika msingi huu - mzazi amfunze mtoto wake sawa akiwa ni mwanaume au mwanamke. Na kama watoto hawana hamu ile ya kujifunza, ni vizuri awaletee jirani, au mtu kwenye Masjid ambaye anaweza kuwafunza watoto wake, (na kwa mama) kumleta mwanamke awafunze mabanati wake.