01-Imaam Bin Baaz: Kula Suhuwr (Daku) Wakati Muadhini Anaadhini
Kula Suhuwr (Daku) Wakati Muadhini Anaadhini
Imaam Bin Baaz (Rahimahu-Allaah)
SWALI:
Je, Unaruhusiwa kuendelea kula daku wakati Muadhini anaadhini adhaan ya pili au aache?
JIBU:
Hii ina maelezo.
Inategemea kama Muadhini anaadhini kwa ajili ya Alfajiri (anatoa Adhaan ya kuwa Alfajiri imeshaanza (Adhaan ya pili), basi lazima usimame kula na kunywa kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, ((Msisimamishe daku yenu mnaposikia adhaan ya Bilaal, kwani yeye anaadhini usiku, kwa hiyo kuleni na kunyweni mpaka Ibn Umm Maktuum aadhini)) Na hii ni kutokana na aya (ambayo inaleta maana hiyo)
“Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe (mapambazuko) wa Alfajiri kutokana na uzi mweusi (wa kiza cha usiku).” [Al-Baqarah: 2:187]
Vile vile ikijulikana kama Alfajiri imeingia kama mfano mtu akiwa kwenye jangwa basi aache kula na kunywa hata kama hakusikia adhaan (mahali ambapo adhana haisikiki).
Lakini kama Muadhini anaadhini mapema au kama kuna shaka na adhaan yake kama imewafikiana na Asubuhi au sio, basi unaweza kula na kunywa mpaka utakapokuwa na uhakika kuwa Alfajiri imeshaanza, ikiwa inajulikana hivyo kutokana na saa maarufu zinazothibitisha kuanza Alfajiri au kutokana na Muadhini mwenye kuaminika anayejulikana kuwa anaadhini wakati wa Alfajiri. Kwa hali hii (ikiwa adhaan imeadhiniwa mapema sana) unaweza kula wakati adhaan inaadhiniwa, ule au unywe kilichokuweko mkononi mwako kwa sababu hakuna hakika kama adhaan inaadhiniwa kwa wakati wake ulio sahihi, bali huenda kulikuwa tu ni kwa makisio na si kwa uhakika.
[Majmuw' Fataawa ash-Shaykh Ibn Baaz, mjalada 15, ukurasa 282].